Kwa nini tunahitaji dhana ya “afya moja” kwa binadamu, wanyama na mazingira?

PAKUA APP YA UFUGAJI HAPA

Leo nakuletea Makala itakayojibu swali la kwanini tunahitaji dhana ya “Afya Moja” kama nchi ili kukabiliana na magonjwa yanayo mpata binadamu na Wanyama. Haijalishi wewe ni mfugaji au si mfugaji au ni mtaalamu wa fani fulani, kwenye afya moja kila mmoja ni mdau muhimu sana.

“Kwa pamoja tunaweza kutokomeza magonjwa ya binadmu na mifugo pamoja na kutunza mazingira tunamoishi”.

Fuatilia Makala hii hadi mwisho ili kujua wewe unahusikaje kwenye dhana ya afya moja inayohusisha afya ya wanyama binadamu na mazingira.

 

Dhana ya ‘Afya Moja’ ni nini?

Dhana ya “Afya Moja” ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000. Dhana ya “Afya Moja” ni mtazamo wa kukabiliana na magonjwa yanayoambukizwa kwa binadamu toka kwa wanyama kwa mfumo wa pamoja wa wataalamu na wadau mbalimbali wanaojihusisha na mifugo, wanyama pori na mazingira. Katika mkitadha wa Afya Moja, kuna ukweli usiyopingika kuwa binadamu na wanyama wanaunganishwa na mazingira yanayowazunguka. Binadamu, wanyama na mazingira ni viungo muhimu vya vimelea vya wadudu wa magonjwa yanayoweza kumpata binadamu na wanyama. Hivyo ni ukweli kuwa kuna uwezekano mkubwa wa binadamu kupata magonjwa toka wanyama na mazingira na wanyama kupata magonjwa toka kwa binadamu na mazingira. Na mazingira ni kiunganishi kikubwa sana cha wanyama, binadamu na vimelea vya magonjwa. Kwa kuongezea, binadamu akiwa anafanya kazi zake kwenye mazingira mara nyingi kwa kujua au kwa kutokujua husambaza kemikali kwenye mazingira zinazopelekea madhara kwa wanyama na binadamu mwenyewe. Hivyo binadamu, wanyama na mazingira hutegemeana kwa hali ya juu sana ili usitawi kiafya wa kila mmoja udumu. Hapa ndipo umuhimu wa dhana ya afya moja unapokuja.

Dhana ya ‘afya moja’ ni swala mtambuka linalojumuisha/leta pamoja watalaamu wa aina mbalimbali toka sekta tofauti kukabiliana na ugonjwa unahusisha wanyama, binadamu na wakati mwingine mazingira. Wakati huo huo wataalamu wanapokabiliana na janga linalohitaji afya moja wadau mbalimbali wasiokuwa wafugaji hushirikishwa kwa karibu zaidi. Shirika la kimataifa la kupambana na magonjwa ya mifugo na binadmu duniani (OIE) linatekeleza dhana hii kama kama mbinu ya kimataifa ya ushirikiano wa kuhakikisha afya ya binadmu na wanyama (wakiwemo wanyama pori) pamoja na afya ya mazingira kwa ujumla zinalindwa.

Chapisho la OIE linaoonyesha kuwa asilimia 60 ya magonjwa ya binadamu yanatokana na maambukizi toka kwa wanyama (wafugwao na waporini). Na asilimia 75 ya magonjwa ya kuambukizwa yanayojitokeza kwa kasi mfano Ebola na mengine yanye asili ya kutoka kwa wanyama hata kama magonjwa hayaonekani kwa wanyama. Mara nyingi wanyama hasa wa porini wamekuwa wabebaji wa vimelea vya magonjwa bila wao wenyewe kupata madhara. Hivyo tuishi na wanyama tukijua kuwa wanaweza kuwa wamebeba vimelea vya magonjwa hatari kwetu na tutumie njia za kuzuia vimelea visiwapate wanyama tunaofuga.

 

Kwanini Tanzania tunahitaji dhana ya Afya Moja?

Kama nilivyokwisha tangulia kusema hapomwanzo kuwa vimelea vingi vya magonjwa vinavyo wapata wanyama humpata pia binadmu kwa kula mazao ya wanyama (nyama, maziwa, damu), kumgusa mnyama mwenye vimelea vya ugonjwa au kupitia kwa wadudu wanao kunywa damu ya wanyama na binadamu. Kwa muktadha huu jitihada za sekta moja kuzuia au kutokomeza tatizo huwa haiwezekani. Kwa mfano ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa kwa binadamu unazuiwa kwa ukamilifu kwa kulenga chanzo cha kirusi kwa kuwachanja Mbwa. Mbwa asipochanjwa na akapata virusi vya kichaa cha mbwa na kwa bahati mbaya akamuuma binadamu, wataalamu toka sekta ya mifugo na binadamu wanatakiwa kuja pamoja kutafuta suluhu.

Upatikanaji wa taarifa ya virusi vya ugonjwa influenza kuwapo kwa wanyama ni muhimu sana kwa ajili ya utengenezaji wa chanjo kwa ajili ya binadamu. Kwa kifupi magonjwa mengi kama tulivyoona hapo awali huanzia kwa wanyama kwenda kwa binadamu, hivyo wataalamu wa mifugo wana mchango mkubwa wa kuhakikisha wanazuia vimelea vya magonjwa visiwapate wanyama. Vimelea vya magonjwa vinapovuka mipaka kwenda kwa binadamu wataalamu wa binadamu lazima nao wawe na uelewa wa magonjwa yanyotoka kwa wanyama. Hivyo dhana ya afya moja hapa inakuwa muhimu sana ili kupambana na magonjwa ya namna hiii.

Tukirudi kwenye swali la msingi, je Tanzania tunahitaji afya moja? Bila shaka jibu utakuwa umeshalipata toka kwenye maelezo hapo juu kuwa tunahitji sana. Siku za nyuma dhana ya afya moja haikupewa kipao mbele sana na imepelekea kupoteza kwa watu wengi sana kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama. Kila sekta ilijifungia kivyake katika kushughulikia magonjwa mtambuka hasa yale yasi ya mlipuko. Magonjwa kama kichaa cha mbwa, mafua makali ya ndege na homa ya bonde la ufa yalitumia dhana hii ya afya moja siku za nyuma bila ya kuwa na mpango mkakati na kuonyesha mafanikio. Ni kwa kuona umuhimu huo wa dhana ya afya moja nchini, Serikali ilikuja na “Mpango Mkakati wa Afya Moja 2015-2015” kwa mara ya kwanza ukiratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Mpango mkakati huu umeainisha kazi zote kwa kila mdau wa dhana ya afya moja. Lengo likiwa ni kuhakikisha ushiriki hai kati ya sekta kwa ajili ya kuzia na kupambana na magonjwa yanayo mpata binadamu toka kwa wanyama kwa wakati na kwa ushirikiano wa hali ya juu. Ili kutimiza adhima hii Serikali ilianzisha kitengo maalumu cha kuratibu mipango ya Afya Moja (Kitengo cha Kuratibu Kitaifa).

Tanzania tuna magonjwa mengi sana yanayo mpata binadamu toka kwa wanyama na kufanya dhana ya afya moja kuwa muhimu sana Tanzania. Magonjwa haya yamegawanywa kwa makundi kulingana na aina ya kimelea: magonjwa yanayoenezwa na virusi (Kichaa cha mbwa, mafua makali ya ndege na homa ya bonde la ufa) na bakteria (kimeta na homa ya vipindi) na magonjwa mengine yanayoenezwa na minyoo na protozoa.

Pasi na shaka hadi hapo umeelewa dhana ya afya moja na umuhimu wake kwetu kama nchi. Endelea kufuatilia makala hizi zinakujia kupitia tovuti hii ya Ufugaji pamoja na app yake ya Ufugaji iliyopo google play store.

MPANGO MKAKATI WA AFYA MOJA 2015-1021

 

Makala hii imeletwa kwako na Dr. Augustino Chengula

Leave a Reply