Na Mbega Mnyama
Halima ni mtoto wa darasa la tano. Alihama kutoka Dar es Salaam kwenda shule ya Msingi Mtanana. Shule hiyo iko katika Wilaya ya Mpwapwa kama kilometa arobaini kutoka Kongwa. Hapa ni mahali panapofugwa ng’ombe kwa wingi. Halima alipowaona ng’ombe wengi namna hiyo alimwomba mwalimu amweleze zaidi juu ya ufugaji wa ng’ombe. Mwalimu Sadiki alifurahishwa sana na ombi hili la Halima. Akaahidi kumweleza Halima juu ya ufugaji wa ng’ombe kesho yake.
Siku hiyo ilipowadia mwalimu Sadiki alianza hivi: “Ng’ombe ni wanyama tunaowafuga vijijini mwetu.
Zamani sana walikuwa wanyama wa porini. Waliishi huko kama mbogo na pofu. Baadaye binadamu wakaanza kuwafuga. Tunawafuga wanyama hawa kwa ajili ya faida nyingi. Kwanza wanatupatia maziwa ambayo ni chakula bora sana. Tunapowachinja tunapata nyama inayofaa sana kujenga miili yetu. Baada ya kuwachinja ngozi zao zinafaa pia. Ngozi hutengenezwa viatu, mifuko, masanduku, mikanda, pia tunawambia ngoma zetu. Kinyesi cha ng’ombe hufaa sana kwa mbolea mashambani mwetu. Kwato pia hufaa kutengenezea gundi.
“Ng’ombe hutusaidia kulima kwa plau. Wanaweza kulima sehemu kubwa kwa muda mfupi. Kwa njia hiyo tunaweza kupata mashamba zaidi na mazao mengi. Mazao mengi huongeza uchumi wetu. Tunapohitaji fedha, tunaweza kuwauza ng’ombe ili kupata mahitaji yetu.”
Baada ya maelezo hayo Halima akasema, “Tafadhali mwalimu naomba unieleze zaidi habari za maziwa.” Mwalimu akajibu, “Hebu kwanza tumchunguze mzee Mazengo tuone jinsi anavyopata maziwa. Kila siku asubuhi mzee Mazengo huamka mapema sana kwenda kukama ng’ombe wake. Ng’ombe wengine hawataki kumamuliwa mpaka watoto wao wanyonye kwanza. Hivyo mzee Mazengo huwaachia ndama wanyonye kwanza kabla ya kuanza kuwakama mama zao. Ng’ombe wenye matata huweza kuwapiga mateke wakamuaji. Hivyo mzee Mazengo huanza kwa kuwafunga kamba za miguu. Kisha husafisha mikono yake kwa maji safi. Halafu huziosha chuchu za ng’ombe kabla ya kuanza kukama. Huchukua buyu au ndoo au debe la kukamulia maziwa. Baada ya hapo shughuli za kuwakama ng’ombe huanza. Amalizapo kuwakama ng’ombe wote huyajaza maziwa katika chupa. Hubakiza chupa chache kwa matumizi ya jamaa yake. Kisha huziweka chupa zilizosalia katika sanduku lililo wazi na kuzipeleka kwenye kituo cha kuuzia maziwa.” Alipokwisha kusema hivi Halima aliuliza tena, “Je, mzee Mazengo huyatumiaje maziwa yanayobaki?” Mwalimu akajibu, “Jamaa yam zee Mazengo hupenda sana kunywa maziwa. Wakati mwingine hupenda kunywa maziwa yaliyoganda na kutiwa sukari. Maziwa yakiwa mengi mkewe hutengeneza mafuta ya siagi.” Hapo Halima akamuuliza mwalimu, “,Je, mafuta ya siagi hutengenezwaje?”
Mwalimu Sadiki akamjibu, ‘Iwapo mzee Mazengo anataka kupata siagi basi hugandisha maziwa kwanza. Sehemu ile ya juu iliyoganda huenguliwa na kutiwa katika kibuyu safi. Kitu hiki kilichoenguliwa twakiita siagi. Siagi inapokaribia kujaa katika kibuyu hicho mzee Mazengo hukifunga kwa kamba na kukitundika. Kisha mkewe huanza kukitikisa kibuyu kile kwa muda mrefu mpaka siagi ile ishikamane vizuri. Ili kuifanya siagi hiyo ishikamane vizuri huongeza maji. Baadaye siagi hiyo huondolewa.
“Iwapo anataka kupata jibini ataiacha siagi hiyo igande vivyo hivyo kwa muda mrefu katika chombo. Lakini iwapo anataka samli, basi siagi hiyo ataipika katika chungu au sufuria na kuiacha ichemke pole pole kwa muda mrefu. Halafu hitia katika chupa au debe. Hiyo ndiyo samli safi. Mafuta ya samli hufaa kwa kupikia na kukaangia vyakula. Kwa hiyo kutokana na maziwa twaweza kupata vitu vingine kama siagi, jibini, samli na mtindi.” Halima akauliza, “Je, mwalimu, mtindi ni nini?” Mwalimu akajibu, “Mtindi ni maziwa yale yaliyobaki baada ya kutolewa siagi.”
Mwalimu Sadiki alipomaliza kutoa maelezo yake Halima aliendelea kuuliza akisema, “Kweli mwalimu, ng’ombe wana faida nyingi sana kwetu. Sasa nitawezaje kuwaangalia vizuri na kuwatunza?” Mwalimu akaendelea kumweleza, “Jambo la kwanza la lazima kwa viumbe wote ni chakula. Huna budi kuangalia kuwa ng’ombe wako wanashiba sawasawa. Chakuka cha ng’ombe ni majani. Lakini inawezekana kuwalisha vyakula vilivyotengenezwa kwa nafaka mbalimbali. Kama unawalisha ng’ombe wako vizuri kila siku na kuwapa maji ya kutosha watanawiri na kutoa maziwa mengi. Pia unapowachinja huwa na nyama nyingi na nzuri. Vile vile ng’ombe wanahitaji nyumba nzuri. Nyumba yao inaweza kuwa boma imara. Ndani yake lazima pawe na sehemu ya kivuli cha kuzuia jua na mvua. Ukavu wa nyumba yao ni jambo muhimu sana. Kuifanya nyumba hiyo iwe kavu, sakafu ya zizi inabidi iwe ya mtelemko ili mkojo uweze kutiririka kwa urahisi.”
Baada ya kulijibu swali la Halima, mwalimu aliendelea, “Ng’ombe ni viumbe hai kwa hiyo nao huweza kuugua. Kwa hiyo waogeshe ng’ombe wako kwenye josho ili kuwaepusha na magonjwa.” Baadaye Halima akauliza, “Kama ng’ombe wangu ni wagonjwa nitafanya nini?” Mwalimu akamwambia, “Kila mara uombe msaada kwa wakuu wa Idara ya Wanyama. Watakupa mashauri hata kabla ya ugonjwa kutokea. Ikiwa kwa bahati mbaya wamepatwa na ugonjwa kabla ya wao kujua wape taarifa upesi. Wao watapambana na ugonjwa huo.”
Mwishoni mwalimu alimaliza kwa kusema, “Yatubidi kuwaangalia sana wanyama wetu katika hali ya uzima na ugonjwa. Tunapotaka kuwachinja tutumie visu vikali ili wasipate maumivu makali. Tena tusichinje walio na mimba. Tunapowapeleka malishoni tusiwakimbize, wala tusiwapige. Ng’ombe pamoja na wanyama wengine ni viumbe wanaotuhifadhi sana katika maisha yetu. Tukiwatunza vema tutapata faida nyingi, nasi tunaendeleza uchumi wa nchi yetu.”
Halima alimshukuru mwalimu kwa yote aliyomweleza.

Leave a Reply