Heifer yapania kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini

Na THEDDY CHALLE

“INGAWA Tanzania kuna ng’ombe wengi upungufu wa maziwa ni mkubwa kwa sababu idadi kubwa ya wafugaji bado wanafuga ng’ombe wa asili ambao hutoa kiasi kidogo cha maziwa,” anasema, Mark Tsoxo.

Mark Tsoxo ambaye ni Meneja Mradi wa Shirika la Kimataifa la Heifer anasema Tanzania kuna ng’ombe milioni 22.8 kati yao ng’ombe wa maziwa ni 720,000 sawa na asilimia tatu. Takwimu hizo zinaonesha kuwa kiwango cha ng’ombe wa maziwa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya maziwa yanayohitajika nchini jambo linalosababisha Watanzania kutegemea maziwa yanayoagizwa kutoka nchi ya nchi.

Licha ya kuwa na upungufu wa maziwa, bado wafugaji wengi wa Kitanzania wanapendelea kufuga ng’ombe wa asili ambao hutoa maziwa kidogo ikilinganishwa na ngombe wa kisasa. “Ng’ombe wa asili hutoa maziwa kati ya nusu lita hadi lita moja kwa siku wakati ng’ombe wa kisasa hutoa lita 12 hadi 28 kwa siku hivyo….Watanzania wanapaswa kubadilika na kuwekeza katika ufugaji wa ng’ombe wa kisasa,” Tsoxo anahimiza.

Ufugaji wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa kunasaidia kuongeza pato la mfugaji na kuchangia uchumi wa taifa kwa ujumla. Hata hivyo bado kuna changamoto kwa kuwa hivi sasa hivi sasa asilimia 70 ya maziwa yanatokana na kwa ng’ombe wa asili na asilimia 30 pekee ndio yanayotokana na ng’ombe wa kisasa kwa kuwa wafugaji bado wameshikilia ufugaji wa jadi.

Uzalishaji duni wa maziwa nchini unasababisha masoko makubwa kutawaliwa na bidhaa toka nje na zinaongezeka kila siku na kufanya watu wengi kunywa maziwa ya nje zaidi na hivyo kuwanufaisha wafugaji wa nje badala ya wafugaji.

Tsoxo anasema ili kukabiliana na tatizo hilo, Shirika la Heifer International limeanzisha Mradi wa uendelezaji sekta ya maziwa Afrika kwa kutumia mfumo wa kitovu cha maziwa (Dairy Hub), ili kuwainua wafugaji wadogo nchini na kuongeza thamani ya mnyororo wa sekta ya maziwa.

Anasema mradi wa kitovu cha maziwa ni sehemu ya Mradi wa miaka mitano ya uendelezaji sekta ya maziwa Afrika Mashariki (EADD) ambao ulianza kutekelezwa kwa awamu ya pili katika nchi za Kenya Uganda na Tanzania kuanzia mwaka 2013 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018.

Hivi sasa mradi wa kitovu cha maziwa unatekelezwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe ambapo wafugaji wanafundishwa mbinu mbalimbali za kuboresha ufugaji, kuzalisha maziwa na jinsi ya kutafuta masoko.

Mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya Heifer International, Shirika la Marekani lisilo la Kiserikali Technoserve (TNS), Shirika la Usimamizi wa Ubora wa Mazao na Huduma za Mifugo Afrika (ABS –TCM) , Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa kilimo misitu (ICRAF).

Katika ubia huo washirika wamegawana majukumu ambapo Shirika la Heifer International ni msimamizi mkuu wa mradi wa kuongeza uzalishaji maziwa, Tecnoserve wanashughulikia biashara na masoko ya maziwa, ABS inashughulikia uboreshaji wa koosafu za ng’ombe wa maziwa, ICRAF inashughulikia uboreshaji wa lishe na malisho ya mifugo wakati ILRI inayojishughulisha na utafiti na mafunzo ili kuongeza ufanisi .

Anasema kitovu cha biashara ya maziwa ni kituo cha kisasa kinachosimamia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ununuzi, uuzaji na usambazaji wa maziwa ili kuboresha sekta ya maziwa na kuifanya kuwa biashara. Kitovu hicho cha biashara ya maziwa inamilikiwa na wafugaji wanaojikita kwenye biashara ya maziwa ili kuzalisha faida kuimarisha uchumi miongoni mwa wafugaji.

Katika kituo hicho wafugaji mbalimbali hukusanya maziwa sehemu moja kuyauza kwa jumla au rejareja na kinawasaidia kumiliki biashara zenye faida. Kituo hicho kinasaidia kufungua njia za uchumi vijijini, kuwavutia wawekezaji maeneo ya vijijini hasa uwezekano wa kuvutia wawekezaji binafsi na kuwa na sehemu moja ya kukusanyia mazao kwa ajili ya wasindikaji.

Heifer International ni shirika la mitamba Tanzania na ni taasisi isiyo ya kiserikali ya huduma za kibinadamu iliyojitoa kumaliza njaa na umasikini duniani na kutunza ardhi kwa kugawa mifugo, miti, mafunzo na rasilimali kusaidia familia masikini ulimwenguni kuweza kujitegemea na kuinua kiwango cha maisha.

Shirika hilo ilianzishwa mwaka 1944 nchini Marekani mara baada ya vita kuu ya pili ya dunia, ambapo muasisi wake alikuwa muinjilisti Dan West ambapo kazi zake nyingi zimefanyika katika nchi 125 duniani na majimbo 38 ya Marekani. Mwaka 1974 Heifer International iliamua kuingia Afrika ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuanzisha na kutekeleza miradi ya Heifer.

Uamuzi wa kuingia Tanzania ulifuatia mwaliko uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kuboresha maisha ya wakulima walioko vijijini kwa kugawa mitamba katika vijiji vya ujamaa wakati vinaanzishwa , lakini baadaye waliona kuwa uwezekano wa kulifikia lengo utakuwepo iwapo tu italengwa familia moja moja badala ya jamii kwa ujumla.

Nchini Tanzania imekuwa inatekeleza miradi ya kukuza na kutoa aina mbalimbali za wanyama ikiwemo ng’ombe na mbuzi wa maziwa,mbuzi wanyama, nguruwe, kuku wa asili, punda na ngamia. Miradi mingine ni ya ufugaji wa kuku, ufugaji wa samaki na utunzaji wa mazingira.

Mwaka 1981, Heifer International – Marekani ilishauriana na serikali kuanzisha utaratibu mpya wa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo ambao ndio walio wengi kwa kutumia mfumo na falsafa ya Heifer ya dhamana ya ‘Kopa ng’ombe lipa ng’ombe’, ikilenga kuboresha maisha ya familia moja moja zenye kipato cha chini.

Tsoxo anasema kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo kuwa ni pamoja na ukosefu wa ng’ombe bora wa maziwa na ukosefu wa vituko vya ukusanyaji wa maziwa.

Anasema mifugo iliyoko haizalishi maziwa kwa wingi hivyo kuna haja ya kutafuta mbegu bora za ng;ombe wa kisasa ili kupata maziwa mengi. Pia kuna haya ya kutengeneza matanki ya kuhifadhia maziwa katika maeneo ya wafugaji ili waweze kupata mahali pa kuhifadhia maziwa katika hali ya usafi na salama zaidi.

Anazitaja changamoto nyingine kuwa ni gharama kubwa za usindikaji wa maziwa, unywaji mdogo wa maziwa unaosababisha soko la maziwa kuwa chini jambo ambalo linapelekea msindikaji au mfugaji kutoona umuhimu wa kuzalisha maziwa kwa wingi. Changamoto nyingine inayowakabili wafugaji na wafanyabiashara wa maziwa ni kodi kubwa ya bidhaa za maziwa na uwezo mdogo wa kusindika maziwa.

Hivi sasa maziwa yanayosindikwa kwa siku ni lita 417,000 sawa na na asilimia 34. Asilimia 66 ya maziwa yanabaki bila kusindikwa hivyo kutumika kutengeneza mtindi na maziwa yaliyochachushwa ambayo hayawezi kudumu sokoni kwa muda mrefu.

Tsoxo ameiomba serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kuangalia upya viwango vya tozo na kodi mbalimbali zinazotozwa katika sekta ya maziwa ili kushawishi ukuaji wa sekta ya maziwa na mazingira bora ya uwekezaji badala ya kuhamasisha soko la nje. Anawahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kunywa maziwa yanayozalishwa Tanzania ili kujenga uchumi wa Taifa.

 

Chanzo: Gazeti la Habari leo

Leave a Reply