You dont have javascript enabled! Please download Google Chrome!

NAMNA YA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MIFUGO KARIBU NA HIFADHI ZA WANYAMA AFRIKA MASHARIKI

Kwa karne nyingi wafugaji wamekuwa wakimudu mifugo yao na nyanda za malisho kwa kuhamahama kufuatana na majira, wakitunza maeneo ya malisho kwa msimu wa kiangazi, wakihifadhi aina fulani fulani za miti, na kujiepusha na maeneo yajulikanayo kuwa na maradhi. Utaratibu huu wa kimila wa mpango wa matumizi ya ardhi ulisaidia mifugo na wanyamapori kusitawi vizuri kwenye nyika za Umasaini, ambazo hadi sasa zina idadi kubwa ya mamalia wakubwa ulimwenguni.

Lakini katika miongo ya karibuni sera za serikali na kukua kwa ongezeko la watu vimesababisha kupungua kwa uhuru wa kuhamahama kwa wafugaji, ukiibana mifugo kwenye maeneo yenye nafasi ndogo.

Kupunguza uhuru  huo  kunahatarisha  vyanzo vya mapato na chakula kwa wafugaji, kusababisha migogoro, na kukua kwa “miingiliano” ya wanyamapori na mifugo. Katika hali hii, mifugo na wanyamapori wanashirikiana malisho, maji, na kuambukizana magonjwa.

Yawe yanatoka kwa wanyamapori au la, magonjwa ya mifugo yanaweza kusababisha hasara kubwa kwenye mifugo na mapato ya kaya. Wafugaji wengi wanapoteza sehemu kubwa ya mifugo yao na kutumia kiasi kikubwa cha mapato yao kudhibiti magonjwa kila mwaka. Baadhi ya vimelea hushambulia binadamu pia.

Kwa madhumuni ya kulinganisha: utafiti uliofanywa hivi karibuni kwenye wilaya ya Isinyi huko Kenya, umegundua kwamba asilimia 60 ya ndama na asilimia 50 ya ng’ombe waliokomaa walikadiriwa kuwa walipata magonjwa ndani ya mwaka mmoja, 2003-04 (Bedelian et al, 2006).

Kuwasaidia wafugaji waweze kumudu  afya  ya mifugo kunaweza  kuongeza kipato  kinachohitajika sana na kusaidia kudumisha afya za watu.

 

UMUHIMU WA SURA HII

Ugonjwa ni zaidi ya suala la vimelea. Viwango vya ugonjwa vinaongezeka au kupungua kutegemeana na sababu nyingi za kiekolojia na za kijamii. Kwa sasa, jamii na pia wanataaluma wamekwishaona kuwa magonjwa ya mifugo yanaongezeka kwenye maeneo ya wafugaji.

Magonjwa  ambayo   ni   mapya   katika   maeneo fulani fulani yanaibuka. Magonjwa ambayo yalikwishadhibitiwa huko nyuma yanarudi. Na mengine yanazidi kusambaa.

Watalamu wa mipango na wanajamii wanatakiwa kufahamu mienendo inayochangia kuleta magonjwa ya mifugo, kwa sababu magonjwa yanadhuru maisha ya jamii na mapato yao. Na shughuli za binadamu zinaweza kusaidia kudhibitiwa na hata kufuta kabisa magonjwa mengi.

Mambo yanayochangia ongezeko la magonjwa ya mifugo ni pamoja na ambayo yamejadiliwa kwenye kitini hiki (hasa Sura ya 1 na ya 2). Kwa ufupi ni:

 • Mabadiliko ya  tabianchi.  Joto  katika  Afrika

Mashariki, kama ilivyo katika sehemu nyingine nyingi ulimwenguni, linaongezeka taratibu. Licha ya hivyo, mgogoro wa hali ya hewa unasababisha ongezeko la  matukio ya hali mbaya ya hewa, ukame kutokea mara kwa mara zaidi, lakini pia mafuriko kutokea mara nyingi zaidi inaponyesha mvua. Mifugo inapodhoofika kwa kukosa malisho au maji, uwezo wa mifugo hiyo kustahimili magonjwa unapungua. Na, katika mzunguko huo wa matatizo, mifugo iliyodhoofishwa na magonjwa inapungukiwa na uwezo wa kustahimili ukame.

 • Wadudu wanaosambaza magonjwa wanaongezeka.

Joto linapoongezeka na mvuke hewani kubadilika, wadudu wasambazao magonjwa wanasambaa kwenye eneo kubwa zaidi na kusababisha mifugo kuugua katika maeneo ambayo hapo awali hayakuwa na magonjwa hayo.

 • Kupungua kwa ardhi. Kuibadili ardhi iliyokuwa

malisho kwa kuilima kunasababisha wafugaji kubanana kwenye maeneo madogo kuliko hapo awali, na kuwanyima uwezo waliokuwa nao wa kuhamahama kufuatana na majira ya mvua na malisho mazuri, na kuwaweka katika hali ambayo miingiliano na wanyamapori ni mikubwa.

 • Kupungua kwa huduma za afya kwa wanyama.

Kujitoa kwa serikali katika kutoa huduma za afya kwa wanyama kunakotokana na kuzidi kupungua kwa bajeti inayotengwa kwa huduma katika sekta

za jamii, upungufu wa wataalamu, miundombinu na vitendea kazi, mfumo dhaifu wa kupashana habari na pia ufuatiliaji, vyote hivyo vinaathiri uwezo wa utoaji huduma bora za kiwango cha juu katika maeneo ya wafugaji.

 

KUWAKUMBUKA NG’OMBE WAKATI WA KUPANGA MATUMIZI YA ARDHI

“watu wana wasiwasi kuwa tukitenganisha

wanyamapori na mifugo, itakuwa kama kuwa na hifadhi nyingine, na hawataki hali hii. ni muhimu zaidi kusisitiza kushirikiana kwenye ardhi. lakini wakati mwingine wanyama wanapaswa kutenganishwa kwa kipindi fulani. Kwa mfano, kuweka n’gombe mbali na mazalia ya nyumbu mpaka ndama wao wanapotimiza miezi mitatu. hii itazuia mifugo kupata ugonjwa wa nyumbu (Malignant catarrhal Fever).

lakini ili kufanya hivyo ni lazima kuwepo na sehemu nyingine iliyotengwa, ambapo ng’ombe watakuwa katika kipindi hicho. ni muhimu sana kulikumbuka hili wakati wa mchakato wa kupanga matumizi ya ardhi.

Moses Neselle, Mganga wa Mifugo na Mtaalamu wa Mipango ya Jamii

 

Habari njema  ni  kwamba  baadhi  ya  magonjwa yanaweza kuzuilika au kudhibitiwa kwa kupanga vizuri matumizi ya ardhi kwenye ngazi ya jamii (angalia sura ya 2). La muhimu  katika kupanga ni kuwa mwangalifu kuzingatia mahitaji ya wafugaji na  ujuzi walionao, ili mifugo yao  iwe  katika maeneo  yasiyokuwa na magonjwa na yana malisho wakati wa dharura.

Kwa kuongezea, mzigo uliyonayo jamii ya wafugaji utokanao na  magonjwa yanayohusiana na wanyamapori unaweza kufidiwa kwa kufungua fursa mpya, kama biashara zinazohusiana na asili. Nchi za Afrika Mashariki zinaruhusu jamii kunufaika na utalii, kufuga nyuki na biashara nyinginezo zinazohusiana na kuwepo kwa wanyamapori na misitu na mapori mazuri (angalia sura ya 3).

Si nia ya yafuatayo kuchukua nafasi ya muongozo wa matibabu ya mifugo ila, kwa ufupi, kutoa mwanga kwa masuala muhimu na maendeleo yaliyopatikana hivi karibuni juu ya magonjwa ya kawaida ya mifugo kwenye maeneo ya wafugaji yaliyo pembezoni mwa hifadhi za taifa.

MAGONJWA MAKUU YA MIFUGO NA MWENENDO WAKE KWENYE MAENEO YA WAFUGAJI

 

 1. Kimeta

(Maa: Engeeya Nairowa; Kiingereza: Anthrax)

 

Unayopaswa kujua

Ugonjwa wa Kimeta unawashika mifugo na pia mbogo, punda-milia, na wanyamapori wengine walao majani. Vimelea vya Kimeta vinaweza kuishi kwenye udongo kwa muda mrefu. Kuna uwezekano wanyama wakapata ugonjwa wa kimeta mwanzoni mwa majira ya mvua, wakati majani wanayokula yanapokuwa mafupi.

Kutokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi, ambayo yanaifanya  mifugo  na  wanyamapori kukaa  pamoja kwenye eneo dogo, matukio ya kimeta yanaongezeka.

Binadamu wanaweza pia kuupata ugonjwa huu, kwa kushika au kula nyama ya mifugo iliyoambukizwa.

 

Dalili za kimeta …

 • Kifo cha ghafla cha mfugo mwenye afya
 • Kuwa na uvimbe kwenye shingo, kifua, tumbo, na/au miguu ya mifugo inayougua lakini haifi.

 

Kuwa mwangalifu

Kama watu au wanyama walao mizoga wataupasua mzoga (na kuufanya utumbo kutoka) wa mnyama aliyekufa kwa kimeta, wanaweza kupelekea kuanza mlipuko wa kimeta kwa kusababisha vimelea kusambaa kwenye hewa na udongo. Ardhi ambayo itafikiwa na majimaji kutoka kwenye mzoga wa mnyama aliyeugua kimeta yaweza kuhifadhi vimelea vya ugonjwa huo hata kwa miaka ipatayo 60!

Kama unahisi mnyama amekufa kutokana na kimeta, linda mzoga au ufunike kwa miiba au mawe kuzuia wanyama walao mizoga wasiupasue.

Uchome mzoga baada ya kuunyunyizia mafuta ya taa au petroli. Au ufukie kwenye shimo la urefu wa mita mbili na kuumwagia majivu au chokaa.

 

Kuzuia na kudhibiti

Chanja kwa miezi kati ya tisa na kumi na mbili na chanjo hiyo bora iwe imehusisha juhudi ya jamii au serikali ikilenga kuwachanja ng’ombe wote.

Dawa dhidi ya bakteria (Antibiotics) zinaweza kuwa dawa sahihi iwapo matibabu yataanza mapema, ingawa ni bora kuzuia ambako pia gharama zake ni nafuu.

 

 1. Homa ya Bonde la Ufa

(Kiingereza: Rift Valley Fever)

 

Unayopaswa kujua

Watu wengi wanafikiri kuwa ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unatoka kwa wanyamapori, si hivyo.

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unaenezwa na panyanambu.Mbuwanang’atapanyawalioambukizwa, na  mbu  hao  wanaiambukiza mifugo ugonjwa huo wanapoing’ata.

Matukio ya ugonjwa yanaongezeka wakati wa kipindi cha mvua panapokuwa na mbu wengi hasa mvua nyingi zinaposababibisha madimbwi ya  maji ambayo ni mazalia ya mbu. Mbu wanaongezeka pia mwishoni mwa majira ya mvua, wakati idadi ya panya inapoongezeka.

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa ulikuwa haujawahi kusikika kwenye nyanda za  umasaini mpaka mwaka

1997, mlipuko ulipotokea kufuatia mvua kubwa za El Nino.  Baada  ya  hapo  ilionekana kudhibitiwa mpaka kipindi cha mvua kisichokuwa cha kawaida mwaka 2006, ambapo mlipuko ulisambaa kutoka mkoa wa Rift Valley nchini Kenya. Katika miaka ya 2006 na 2007, ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa uliua maelfu ya ng’ombe na zaidi ya watu 150 nchini Kenya na Tanzania.

Mabadiliko ya  tabianchi  yanaelekea kusababisha majira zaidi ya mvua nyingi au inayonyesha kwa vipindi virefu zaidi, kwa hivyo milipuko ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa inatarajiwa kuendelea kutokea.

 

Dalili …

Kwenye mifugo: Matukio mengi ya mimba kuharibika kwenye ng’ombe, mbuzi au kondoo.

Kwa binadamu: Dalili kama za mafua ikiwa ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa, na maumivu ya misuli na mgongo. Kama mwili umebadilika na kuwa wa  manjano na  unatapika, nenda  hospitali haraka la sivyo kupungukiwa damu, upofu au kifo vyaweza kutokea mara moja.

 

Kuwa mwangalifu

Binadamu  wanaweza kupata  ugonjwa wa  Homa ya Bonde la Ufa kutokana na kung’atwa na mbu, kuchinja mnyama mwenye ugonjwa huu bila kuchukua tahadhari au kula nyama ya mnyama mgonjwa bila kuiandaa vizuri, yawezekana kwa kunywa maziwa yasiyochemshwa vizuri, na pia hata kwa kuvuta hewa yenye virusi kutoka kwenye mzoga wa mnyama aliyeugua ugonjwa huu.

Ugonjwa huu huathiri vizazi vijavyo vya mifugo kwa sababu unaingilia uzaaji.

Kama patatokea mlipuko, wanyama kutoka kwenye eneo  linalohusika watapigwa  karantini.  Wakati  wa mlipuko na kipindi cha mwezi mmoja baada ya hapo, inazuiliwa kuuza mifugo (ng’ombe, kondoo au mbuzi), na mazao ya mifugo (maziwa, nyama au ngozi).

Ukiona uharibikaji mimba usio wa kawaida, toa taarifa mara moja kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji, au Ofisa ugani au bwana mifugo.

 

Kuzuia na kudhibiti

Kwa mifugo: kuchanja mifugo kila mwaka kunasaidia. Juhudi ya jamii au serikali kuchanja n’gombe wote ni mkakati sahihi zaidi.

Kwa binadamu:  tumia chandarua kuzuia kuumwa na mbu. Pia jiepushe kugusa mimba iliyotupwa. Jikinge kwa kuvaa mikononi glovu au mifuko ya plastiki. Zika mizoga kwenye shimo refu kiasi ambacho mbwa na wanyama wengine walao nyama hawawezi kufukua.

Mipango ya serikali inaweza kusaidia kwa kujiandaa kuchanja baada ya mvua nyingi. Kwa mafanikio mazuri muda wa kuchanja usirefushwe.

Hakuna matibabu ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la

Ufa yanayofahamika.

 

 1. Ugonjwa wa Miguu na Midomo (Maa: Oloroibi, English: Foot and Mouth Disease (FMD))

 

Unayopaswa kujua

Ugonjwa wa miguu na midomo unawashika ng’ombe, kondoo, mbuzi, mbogo, swala na  wakati mwingine tembo. Unasambaa haraka kwenye kundi ukiua ndama na kusababisha wanyama kupoteza uzito na uzalishaji wa wengine kupungua.

Ugonjwa wa miguu na midomo unaambukiza kwa kugusana kwa mnyama mmoja na mwingine. Unaweza vile vile kusambazwa na upepo kwenye umbali hata wa kilometa 250!

Ni nadra binadamu kupata ugonjwa huu.

Kwa muongo mmoja uliopita, kwa wastani ugonjwa huu  ulikuwa unashambulia kundi mara  moja  kwa mwaka. Kwa sasa, katika sehemu nyingi za  Afrika Mashariki, ugonjwa unatokea mara tatu kwa mwaka. Kwa kuongezea, jinsi hali ya hewa  inavyokuwa ya joto la juu, yanatokea matabaka mapya ya vimelea visababishavyo ugonjwa huu.

 

Dalili …

 • Kuwepo mifugo yenye  dalili  za   mafua,  na kuchechemea kwa wakati huo huo.
 • Ndama kufa kwa ghafla kutokana na ugonjwa wa moyo.

Kuwa mwangalifu

Ugonjwa wa miguu na midomo una madhara makubwa kiuchumi. Uzalishaji wa maziwa wa ng’ombe waweza kupungua kwa asilimia 75 kwa maisha yake yote. Kwa kuongezea, badala ya kuzaa kila mwaka au kwa vipindi kama hivyo, ng’ombe anaweza kuzaa kila baada ya miaka miwili au mitatu.

 

Kuzuia na kudhibiti

Chanjo inaweza kusaidia lakini gharama yake ni kubwa kwa sababu chanjo zinanunuliwa kutoka nchi za nje na lazima chanjo hiyo iwe ya kufanyakazi dhidi ya aina nyingi za vimelea. Jamii inaweza kupanga, na kununua chanjo kwa kushirikiana. Jamii chache kaskazini mwa Tanzania tayari wanafanya hivyo.

Serikali ina  jukumu la  kuzuia ugonjwa huu.  Kwa mfano, serikali ya Tanzania imeahidi kuchangia gharama za chanjo kwa ajili ya ng’ombe wapatao milioni mbili. Na kwa kuwa Tanzania ina ng’ombe wapatao milioni 20, wote wanaweza kunufaika na mchango wa serikali.

Ugonjwa wa miguu na midomo ni hatari, hasa pale ambapo mifugo inatumia ardhi ambayo pia inatumiwa na mbogo na nyumbu. Kwa hiyo, ugonjwa wa miguu na midomo, na gharama ya chanjo, ni vitu viwili kati ya sababu nyingi ambazo jamii zinapaswa kuzingatia zinapowazia kupanga matumizi ya ardhi na shughuli za  biashara  zihusianazo na  uhifadhi (angalia sura ya 2 na ya 3). Biashara kama hizo zinasaidia jamii kupunguza gharama wanazozipata kwa kuishi karibu na wanyamapori, wakipata kipato kutokana na kuwepo kwa wanyamapori hao.

 

4) Ugonjwa wa Nyumbu

(Maa: Iingati, Kiingereza: Malignant Catarrhal

Fever (MCF))

 

Unayopaswa kujua

Virusi aina mbili tofauti husababisha ugonjwa wa nyumbu kwenye ng’ombe. Aina moja ya virusi inasambazwa na kondoo na mbuzi wakati aina nyingine inasambazwa na nyumbu na pofu.

Aina ya  pili ni  tatizo  kubwa hasa wakati  na mahali ambapo nyumbu  wanazalia.  Virusi  vinawaachia  watoto wanyumbu wanapotimiza miezi mitatu baada ya kuzaliwa. Kwa karne nyingi, ugonjwa wa  nyumbu ulikuwa hauwaletei wafugaji madhara makubwa kwa sababu walikuwa wanahamisha mifugo yao kwenda sehemu nyinginezo kila mwaka katika kipindi ambacho nyumbu wanazaliana

Mpango  huu  wa  kimila wa  matumizi  ya  ardhi umesambaratika, ijapokuwa ni katika miongo michache iliyopita, kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya kutumia ardhi (hivyo mashindano) na hivyo ng’ombe na nyumbu kulazimika kupata malisho katika eneo moja hata katika vipindi nyeti ambapo nyumbu wanakuwa wanazaa.

Bila kuchukua hatua  za  tahadhari,  ng’ombe na nyumbu wataendelea kula katika eneo moja na hivyo uwezakano wa ugonjwa wa nyumbu kuongezeka pia.

 

Dalili …

Macho ya  ng’ombe yanakosa uwezo wa  kupitisha mwanga. Baada ya hapo mnyama anapofuka na kufa.

 

Kuzuia na kudhibiti

Kwa sasa hakuna chanjo wala tiba.

Udhibiti unawezekana kupitia matumizi mazuri ya ardhi. Mipango ya matumizi ya ardhi inabidi izingatie mahitaji ya wafugaji na uhamaji wa nyumbu na mazalia yao. Mipango inaweza kuweka eneo tofauti la malisho ya mifugo kwenye majira ya nyumbu kuzaa, ambayo kwa wastani yanaanza mwishoni mwa Februari hadi Mei (Angalia Sura ya 2 juu ya mpango shirikishi wa matumizi ya ardhi).

5) Ugonjwa wa Ndigana moto

(Maa: Engeeiya Nairowa, Kiingereza: Corridor

Disease (Theileriasis))

Ugonjwa wa Ndigana moto unahusisha magonjwa mabaya kadhaa ya ng’ombe, ambayo kati yake ndigana (East Coast Fever – ECF) ni ugonjwa ambao unafahamika na ambao ni maarufu.

Ndigana inasambazwa na kupe wa kahawia washambuliao masikio, ambao hushambulia mbogo. Mbogo hupendelea sehemu zenye vichaka – sehemu ambazo kwa hali ya kawaida ng’ombe hupata malisho wakati wa kiangazi.

 

Dalili …

Ugonjwa una dalili chache zinazoonekana, ingawa kwa kawaida vifo hutokana na matatizo ya kupumua.

 

Kuzuia na kudhibiti

Dawa za kutibu Ugonjwa wa Ndigana moto zipo lakini gharama yake ni kubwa; ni bora kuudhibiti.

Jamii na watumishi wa serikali wanaweza kuwa na majosho ya kuogeshea mifugo ili kusaidia kuua kupe, ambao ndio wasambazao ugonjwa. Kiutamaduni, wafugaji huchoma majani mara ufikapo mwisho wa majira ya mvua, yaani kinapoanza kipindi cha kiangazi (wakati wanyamapori wahamao kama mbogo huwa wanarudi kwenye hifadhi). Kuchoma kunafanywa pia kwa nia ya kuwezesha majani kuchipua kwa ajili ya malisho katika maeneo haya, hivyo faida ya kuchoma kuwa kubwa zaidi. Mpango wa matumizi ya ardhi ni suala muhimu. Inapopatikana   nafasi   kubwa   zaidi   kwa   mifugo na wanyamapori ndivyo uwezekano wa ng’ombe kuchanganyikana na mbogo na kukutana na kupe kunavyozidi kupungua.

6) Ndorobo

(Maa: Entorrobo, English: Trypanosomiasis)

 

Unayopaswa kujua

Ugonjwa wa ndorobo unawashambulia wanyamapori, mifugo na binadamu. Mbung’o ndio wanaoambukiza ugonjwa kutoka kwa mnyama au mtu mmoja ambaye amekwisha shambuliwa kwenda kwa mwingine. Ugonjwa huu unaposhambulia binadamu hujulikana kama “homa ya malale”.

Ugonjwa wa ndorobo nao unaongezeka. Katika miaka iliyopita, watuwalikuwawakikwepamaeneo yenyemapori ambapo kwa kawaida mbung’o huishi. Siku hizi wafugaji wanalazimika kwenda kwenye maeneo hayo kwa sababu ardhi inayofaa zaidi kwa kilimo inazidi kulimwa.

Ukiitwa “entorrobo” kwa Kimasaai, ugonjwa wa ndorobo ni mmoja kati ya magonjwa mabaya ya mifugo katika Afrika kwa sababu unashambulia mifugo mingi, unagharimu kuutibu, na unaweza kumshika mnyama huyo huyo kwa kurudia mara kadhaa. Unashambulia na kuua ng’ombe, kondoo, mbuzi, punda, na mbwa.

 

Kuwa mwangalifu

Baadhi ya wafugaji katika nchi za Afrika Mashariki wanatumia fedha nyingi kupambana na ndorobo kuliko wanavyotumia kwenye suala jinginelo lolote linalohusu ufugaji.

Utafiti mmoja uliofanyika hivi karibuni umebaini kuwa ng’ombe wanaofikia asilimia 15 sehemu za kusini mwa Kenya huambukizwa “entorrobo” kila mwezi.

Ugonjwa wa ndorobo (homa ya malale) ni hatari kwa binadamu pia. Wilaya za Tarangire na Babati kaskazini mwa Tanzania zinatambulika kuwa maeneo sugu ya ugonjwa wa ndorobo au homa ya malale.

 

Dalili

Homa zisizoisha, kuvimba, na kuharibika kwa mfumo wa mishipa ya fahamu. Ugonjwa husababisha kupungua sana uzito, damu kupungua mwilini, na kifo. Utambuzi kamili wa ugonjwa unafanywa kwenye maabara yenye vyombo maalum tu.

Kwa binadamu, ugonjwa wa homa ya malale unasababisha homa, kichwa kuuma, kuumwa viungo na mwili kuwasha. Hatua ya pili inahusisha mfumo wa mishipa ya fahamu, na unaweza kusababisha mawasiliano kati ya sehemu kadhaa za mwili kuharibika, kuchanganyikiwa, na hali isiyokuwa ya kawaida ya kusinzia. Ugonjwa unatibika lakini ni mbaya usipotibiwa.

 

Kuzuia na kudhibiti

Njia nzuri zaidi ya kudhibiti ugonjwa huu ni kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi unaowahakikishia wafugaji kuwa na  ardhi  ya  kutosha  isiyokuwa na mbung’o.

Maeneo yenye mbung’o mara nyingi yanakuwa na wanyamapori wengi, na hivyo kuwa maeneo yanayofaa kwa utalii na ambayo yanaweza kutumika kama maeneo ya malisho ya dharura wakati wa ukame.

Katika maeneo yaliyo na mbung’o, wenyeji wanawavuta na kuwaua kwa kutandaza kwenye miti au vichaka vipande vya nguo nyeusi, bluu au nyeupe, ambavyo vinakuwa vimetumbukizwa kwenye dawa.

Zipo dawa za kutibu ndorobo, lakini vimelea vya ugonjwa huo vinaweza kuwa sugu kwa dawa. Upangaji mzuri wa matumizi ya ardhi upewe kipaumbele kama namna ya kupambana na ugonjwa huu.

 

Mambo muhimu ya kukumbuka

1.. Mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya ardhi, magonjwa ya kawaida ya mifugo yanaongezeka kwenye maeneo ya wafugaji katika Afrika Mashariki. Kupungua kwa nyanda za malisho kunakokwenda sambamba na kuongezeka kutumia pamoja ardhi kati ya mifugo na wanyamapori, magonjwa yanakuwa mzigo ambao unabebwa na jamii ya wafugaji.

 1. Magonjwa ya mifugo yanaweza kupunguzwa kwa kupaga vizuri na kugawana matumizi ya ardhi, ikihakikishwa kuwa wafugaji hawasukumwi ili kufanya shughuli zao kwenye maeneo yanayosifika kwa kuwa na magonjwa. Wafugaji wanahitaji nafasi ya kutosha, kiasi cha uwezo wa kuhamahama na uwezo wa kufanya mabadiliko yanayoweza kuruhusu mifugo kubaki na afya inayostahili.
 2. Wakati wa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi, inapasa kuangalia kwa uangalifu maeneo ya wafugaji: mifugo itakuwa wapi, katika majira yapi? Ni maeneo yapi yenye magonjwa ya wanyamapori kwa wingi? Kama jamii inatumia ardhi ya vijiji jirani, kupanga kwa pamoja matumizi ya ardhi kunaweza kuwa kwa manufaa.
 3. Kwa kuongezea, inabidi kusisitiza biashara inayohusiana na uhifadhi, na mapato kuelekezwa kwenye jamii. Jamii ya wafugaji inaweza kunufaika sana kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato.
 4. Juhudi za kupunguza athari za matukio ya ukame yanayoongezeka zinaweza vilevile kusaidia, kwa mfano, kuvuna maji ya mvua na kukuza mabwawa ya asili na yaliyochimbwa.
 5. Serikali ina jukumu kubwa la kutekeleza katika kuzisaidia jamii kupata chanjo na mipango mingine ya kudhibiti magonjwa. Programu za ugani za wataalamu wa mifugo zinapashwa kuimarishwa na wahitimu wa tiba ya mifugo kutoka kwenye vyuo kama Emboreet, kwa mfano, waajiriwe kufanya kazi kwenye maeneo ya wafugaji na wakulima.

 

 

FAHARASA

Bedelian, C., Nkedianye, D., Herrero, M., 2007. “Maasai perception of the impact and incidence of malignant catarrhal fever (MCF) in southern Kenya,” Preventive Veterinary Medicine 78, 296-316.

Castro, J.J.  1997. Sustainable tick and tickborne disease control in livestock improvement in developing countries. Elsevier Science B.V. FAO. 1971. Reports of Joint FAO/OIE/CCTA Expert Panel on contagious bovine pleuropneumonia Rome.

Hall, S.A 1983. “The diagnosis of contagious bovine pleuropneumonia and other infections with mycoplasma mycoides subspecies mycoides,” Document No. EUR  8654 of the commission of the European Communities

Hudson, J.  R.  1971.  Contagious bovine pleuropneumonia. FAO, Agricultural Studies, No. 86.

Plowright, W. 1986. Malignant Catarrhal Fever. Revue Scientique et

Technique de le l’Office International des epizooties, 5, 897 – 918.

 

CHANZO NI  FAO

.

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!
%d bloggers like this: