Pakua App ya Ufugaji HAPA

Na Augustino Chengula

Makala hii inampa msomaji uelewa wa kina wa nini kinatokea wakati wa baridi au joto kali hadi kupelekea kuku wake kupunguza utagaji wa mayai na nini mfugaji wa kuku wa mayai anatakiwa kufanya katika nyakati hizo mbili.

Msimu wa joto na baridi huathiri sana utagaji wa mayai. Watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa kuku wao wamepunuza utagaji wa mayai alkini wasijue nini cha kufanya wanapokutana na hali hiyo ili kuboresha utagaji wa mayai nyakati kama hizo.

Wakati wa baridi

Nyakati za baridi kuku wanapoteza joto jingi linalozalishwa mwilini mwao kwenda kwenye mazingira kulingana na kiasi cha baridi kilichopo. Ili kukabiliana na hali hiyo ya kupoteza joto la mwili kutokana na baridi kuku huongeza joto la mwili wao kwa kutetemeka. Kutetemeka husababisha misuli yao ikunjamane kitendo ambacho kinatumia nishati inayopelekea kuzalisha joto mwilini. Kwa kufanya hivyo kuku hufanya joto la mwili wake libaki la kawaida. Ili wapate nishati hiyo wanayotumia kutengeneza joto la mwili wao, kuku wakati wa baridi hula chakula kingi.

Hivyo mfugaji wa kuku wa mayai atawasaidia kuku wake kwa kufanya yafuatayo: (i) kuwaongezea kiasi cha chakula wakati wa baridi zaidi ya kile alichozoea kuwapa siku za kawaida. Hii itawafanya pia kuku wako waendelea kutaga mayai vizuri japo wanaweza wasifikie utagaji wa kawaida. Muhimu hap ani kuwaongezea chakula. (ii) Kujenga nyumba inayoweza kuwakinga kuku na baridi (ii) Wawekee kuku wako vyanzo vya joto kama taa na chemli n.k

Wakati wa joto

Kama tulivyoona kuwa wakati wa baridi kuku hupunguza kutaga mayai, vivyo hivyo wakati wa joto kati kuku hupunguza kutaga mayai. Tofauti na wakati wa baridi, wakati wa joto kuku hupunguza kula chakula. Kuku anapokula kula chakula hutumia pia nishati kukisafirisha chakula kwenda tumboni ambapo nishati hii huambatana na uzalishwaji wa joto mwilini. Kwa kuwa joto la nje ni kubwa na ndani joto linazalishwa kuku hushindwa kukabiliana na ongezeko la joto la nje hivyo ubongo huhisi ongezeko hili na kuamua kupunguza joto linalozalishwa ndani ya mwili linalotokana na ulaji na usafirishaji wa chakula kwenda tumboni kwa kupunguza ulaji wa chakula. Hivyo mfugaji wakati wa joto kali ataona kuku wake wamepunguza kula chakula.

Utagaji wa mayai pia hutumia nishati inayoambatana na utoaji wa joto, hivyo kuku pia hupunguza utagaji wa mayai ili kupunguza ongezeko la joto la ndani ya mwili. Aidha kupungua kwa utagaji wa mayai pia kunatokana na kuku kupunguza kula chakula kunakopelekea pia maganda ya mayai kuwa laini. Hii inatokana na kuku kutopata Kalsiamu ya kutosha kutoka kwenye chakula.

Mfugaji wa kuku wa mayai anaweza kumsaidia kuku wake ili aweze kutaga mayai mengi na yenye ubora kwa kufanya yafuatayo: (i) Kumpa kuku maji ya baridi wakati huu wa joto; (ii) Kujenga banda linaruhusu hewa kupita wakati huu wa joto; (iii) Kuwaongezea kuku wao Kalsiamu mfano DCP au vyanzo vingine vya Kalsiamu kama unga wa maganda ya mayai na mifupa na (iv) ukiweza unaweza kuwanyunyizia kuku wako na michirizi ya maji baridi kwa njia ya mabomba.

Leave a Reply