Ufugaji wa samaki hatua kwa hatua: hatua ya pili

Farida Mkongwe  Na Farida Mkongwe     

HATUA YA 2: UCHIMBAJI WA BWAWA

Katika hatua hii ya 2 ambayo ni uchimbaji wa bwawa, jambo la kwanza la kuangalia ni vipimo. Kimsingi kwa mujibu wa Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Wanyama iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dr. Berno Mnembuka ambaye pia ni mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji hakuna vipimo maalum vya ukubwa wa bwawa maana ukubwa wa bwawa unategemea eneo na malengo. Kwa mfanyabiashara bwawa kubwa litakuwa ni bora zaidi kwake ili aweze kuvuna samaki wengi zaidi ukilinganisha na mtu anayefuga kwa ajili ya chakula.

Jambo la pili ni kuwa unapochimba bwawa unatakiwa kuchimba upande mmoja uwe na kina au umbali wa  mita 1.5 (mita moja na nusu) na upande mwingine mita 1 na sentimita 20 kwenda chini. Hii ni kwa sababu mianya ya jua ambayo inapeleka mwanga ardhini haiwezi kupenya kwenda chini zaidi ya mita 1.5 na hivyo ukizidisha zaidi ya hapo utakuwa umepoteza nguvu zako bure na ukipunguza utakuwa umeathiri ustawi wa samaki.

bwawa

Mtaalamu huyu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka anasema kuwa umbo la bwawa la kufugia samaki ni vizuri likawa la mstatiri ili kurahisisha shughuli za uvunaji kwa kuwa hata wavu utakaotumika kuvunia na idadi ya watu watakaohitajika katika shughuli za uvunaji watakuwa ni wachache ukilinganisha na maumbo mengine,  pia kama unatumia mashine umbo la mstatiri ni zuri zaidi kwa sababu hata gharama yake ya uchimbaji inakuwa ni ndogo tofauti na maumbo mengine.

Sambamba na hilo katika uchimbaji kitako cha bwawa hakitakiwi kiwe tambarare kinapaswa kiwe na mwinuko upande mmoja ili kukusaidia kuweza kutoa maji kwa urahisi pale unapokuwa huyahitaji.

Vile vile kingo za bwawa zinatakiwa ziwe zimechongwa kuegemea nje ili kukinga bwawa lisibomoke wakati wa kujaza maji. Pia iwapo kingo hizo za bwawa zitakuwa zimechongwa kuegemea nje itakusaidia uweze kuingia bwawani kwa urahisi tofauti na kingo zikiwa zimesimama.

Bwawa linaweza kuchimbwa kwa mikono au kwa mashine, njia hizo zote mbili ni sahihi isipokuwa kama bwawa ni kubwa au kama unakusudia kufuga kibiashara ni vema ukatumia mashine kwa sababu mashine inafanya kazi kwa haraka na hivyo kumaliza mapema, pia ufanisi wake unakuwa ni mkubwa ukilinganisha na ufanisi wa bwawa linalochimbwa kwa mikono.

Kwa kuhitimisha hatua hii ya 2 ya uchimbaji wa bwawa la kufugia samaki inasisitizwa kuwa ni vizuri ukazingatia maelezo ya kitaalamu katika uchimbaji wa bwawa ili uweze kufanikiwa katika  kazi hii ya ufugaji wa samaki.

Usikose kufuatilia hatua ya 3 ya ufugaji wa samaki ambayo itazungumzia uandaaji na upandikizaji wa vifaranga au mbegu za samaki katika bwawa lako.

 

CHANZO: SUAMEDIA

Leave a Reply