Je wajua kwa nini ugonjwa wa kimeta unajitokeza mara kwa mara ukanda wa kasikazini mwa tanzania?

PAKUA APP YA UFUGAJI HAPA KAMA BADO

Ndugu msomaji na mfuatiliaji wa makala za tovuti yako pendwa ya Ufugaji, leo nakuletea Makala muhimu sana inayohusu ugonjwa wa kimeta (Anthrax). Fuatana nami upate kujua ugonjwa wa kimeta unasababishwa na nini, dalili zake ni zipi, je kuna kinga na kwa nini umejikiita hasa maeneo ya kasikazini.

Ugonjwa kimeta unasababishwa na nini?
Ugonjwa wa kimeta unasababishwa na vimelea vya Bakteria wanaojulikana kisayansi kama “Bacillus anthracis”.

Nani hupata ugonjwa huu?

Ugonjwa wa kimeta kwa kawaida ni wa wanyama wanaocheua na binadamu lakini wanyama wengine pia huupata. Wanayama hao ni pamoja na ng’ombe, mbuzi, kondoo, mbwa, ngamia, farasi na wanyama pori kama swala, sungura, mbawala/paa na nyumbu pamoja na binadamu. Ng’ombe na kondoo huupata ugonjwa kirahisi wakifuatiwa na mbuzi, mbwa na farasi.

Wanyama na mifugo huupataje?

Hugonjwa wa kimeta hauenei moja kwa moja toka kwa mnyama mmoja kwenda kwa mwingine wala toka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. Hivyo ueneaji wake upo namna hii; vimelea vya ugonjwa vinatoka kwa mnyama mwenye ugonjwa kwenda kwenye mazingira na kubadilika umbo na kuwa viiniyoga (spores) na umbo hili huwezesha bakteria kukaa kwenye udongo kwa muda mrefu. Bakteria huyu akiwa kwenye umbo la kiiniyoga huweza kuhimili mazingira magumu kama joto, baridi, pH na kemikali na huweza kukaa kwa miaka hata 200. Hii ndiyo inayowezesha kujitokeza kwa milipuko ya ugonjwa huu hata baada ya miaka mingi kupita bila ya kuwa na ugonjwa.

Wanyama huupata ugonjwa huu wanapo kula nyasi/majani au kuvuta hewa yenye viiniyoga. Binadamu huupata ugonjwa huu kwa njia ya kugusa/kushika wanyama wenye ugonjwa, hewa yenye viiniyoga, kula nyama mbichi au ambayo haijaiva vizuri, kunywa maziwa yasiyochemshwa vizuri au kushika mazao ya mifugo yenye ugonjwa.

 

Madhara yake ni yapi?

Ugonjwa huu husababisha vifo kwa kiasi kikubwa kwa wanyama na binadamu. Ugonjwa kimeta umekuwepo nchi tangu miaka ya 1962 ukisabisha magonjwa na vifo kwa wanyama pori, mifugo na binadamu.

 

Mikoa ipi Tanzania inaongoza kwa kukumbwa na Kimeta na kwa nini?

Katika kutafuta jibu la swali hili nikakutana na chapisho la hivi karibuni la Dr. Elibariki R. Mwakapeje na wenzake (soma hapa) linalotupa jibu la swali hili. Katika chapisho hili la kimataifa kwenye jarida la “Royal Society Open Science” linaonyesha kuwa Arusha na Kilimanjaro ndiyo mikoa inayoongoza kwa kuwa na matukio mengi ya Kimeta kwa kuangalia kati yam waka 2006 hadi 2016.

Sababu za Kimeta kujitokeza mara kwa mara kanda ya kasikazini ni pamoja na;

  • Mikoa hii kuwa karibu na hifadhi ya Serengeti na Ngorogoro ambapo kuna mwingiliano mkubwa kati ya wakazi na wanyama pori. Hivyo wanashirikiana maeneo muhimu ya maji na malisho ya mifugo yao.
  • Mikoa hii ina maeneo yenye mabonde na udongo wenye unyevu kalsiamu kwa wingi, vipindi virefu vya joto na ukavu, pamoja na pH kubwa (alkali), vitu ambavyo husaidia vimelea wa Kimeta kushamili.
  • Kwa upade wa binadamu tabia ya watu wa maeneo haya kula nyama mbichi au isiyoiva vizuri, kula nyama ya mnyama aliyekufa bila kujua sababu ya kifo chake pamoja na mazao ya wanyama kama damu mbichi na maziwa yasiyochemshwa.

 

Dalili za Kimeta ni zipi?

Kwa wanyama

Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni vifo vya ghafla vya ndani ya saa 2 au 3 kwa mnyama aliyekuwa mzima wa afya. Hadi sasa hii ndiyo dalili kuu kwa ugonjwa huu kwa wanyama. Mara chache mnyama anaweza kuonyesha dalili kama kutetemeka, joto kubwa, kupumua kwa shida, kupoteza fahamu na kuzimia kabla ya kufa. Na hii mara nyingi inatokea ndani ya saa 24.

Mnyama aliyekufa hutoa damu ambayo haigandi kwenye maeneo yote ya mwili yaliyowazi ikiwa ni pamoja na mdomoni, pua, uwazi wa kutolea haja kubwa na ndogo.

Kwa binadamu

Dalili zinaweza kujitokeza kuanzia siku moja hadi miezi miwili baada ya kupata maambukizi. Kwa binadamu kimeta hujitokeza katika aina tatu kutegemea na njia ya uambukizwaji; (i) kimeta cha ngozi, (ii) kimeta cha mfumo wa upumuaji na (iii) kimeta cha mfumo wa chakula. Dalili hizo zinaweza kuonekana kulingana na umbo la ugonjwa wenyewe.

Kimeta cha ngozi: kutakuwa na lengelenge dogo lililozungukwa na uvimbe mara nyingi hubadilika na kuwa kidonda chenye weusi katikati.

Kimeta cha mfumo wa upumuaji: Umbo hili hujitambulisha kwa homa, maumivu ya kifua, na kukosa pumzi.

Kimeta cha mfumo wa chakula: Hii huambatana na kuharisha kunakoweza kuwa na damu, maumivu ya tumbo, kichefu chef una kutapika.

 

Matibabu

Kwa wanyama: Mara nyingi huwa ni vigumu kwa namna ambavyo ugonjwa hutokea kwa ghafla na kuua wanyama kwa haraka kabla ya kumwita daktari wa mifugo. Pale inapowezekana basi dozi kubwa ya penicillin imesaidia.

 

Kwa binadamu: Madawa ya aina mbalimbali yanaweza kutumika ikiwa ni pamoja na penicillin, doxycycline na ciprofloxacin. Kwa kimta cha mfumo wa upumuaji, mchanganyiko wa zaidi ya dawa moja unaweza kutumika kwa njia ya sindano kupitia mirija ya damu.

 

Kinga dhidi ya kimeta

Kinga ni bora kuliko tiba

Kimeta kwa asili ni ugonjwa wa wanyama wanaokula nyasi, na uzuiaji wake kwa wanyama na binadamu unategemea sana kuzuia kwa wanyama hasa ng’ombe, kondoo, mbuzi na farasi. Kwa binadamu kunategemea sana njia nzuri za kujihusisha na wanyama walio kufana kimeta pamoja na kuwahi kutumia dawa wanapopata maambukizi.

Kwa wanyama chanjo dhidi ya ugonjwa inapatikana nchini kwenye wizara ya Maendeleo ya Mifugo na uvuvi. Hivyo ni vyema kuchanja wanyama wetu dhidi ya ugonjwa huu maana madhara yake ni makubwa kwa wanyama na binadamu.

Pale ugonjwa unapotokea au unapoona dalili zinazoashiria kimeta, epuka kushika mzoga wowote ule bila tahadhari na wala usijaribu kuupasua mzogoa au mnyama aliyekufa ghafla akiwa na dalili za kimeta. Toa taarifa haraka kwa afisa mifugo aliyekaribu nawe ili ujiridhishe na hatua stahiki zichukuliwe.

Kama imegundulika ng’ombe mmojawapo amekufa kwa kimeta mkiwa machungani basi mifugo mingine iondolewe mara moja eneo hilo. Kisha endelea kuwachunguza mifugo hao angalau mara tatu kila siku ili kubaini dalili za awali zilitajwa hapo juu kwa muda wa wiki mbili (hasa upumuaji wa haraka na kupanda kwa joto, kujaa maji maeneo ya chini ya mwili). Wanyama wowote watakao onyesha dalili hizo watengwe toka kwenye wanyama wengine kwa ajili ya matibabu. Na njia bora zaidi ni kuwapa dawa inayofanya kazi kwa muda mrefu angalau kwa saa 72, maana kuangalia kila siku inaweza ikashindikana au umakini ukakosekana. Uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi wanyama hasa ng’ombe wakitibiwa hupona hata kama wamezidiwa sana.

 

Kwenye mlipuko wa kimeta, mizoga yoyote isipasuliwe kwa wadudu wakipata hewa tu hubadilika umbo kuwa viiniyoga ambao wanasambaa kwenye mazingira na hata kuleta maambukizi kwa binadamu kwa njia ya hewa na kwa wanyama kwenye mazingira. Hivyo mizoga itupwe kwa kufuata utaratibu mzuri.

Maeneo yenye mlipuko yawekewe zuio la kutoa au kuingiza mifugo mingine hadi pale watakapopewa chanjo. Wanyama wagonjwa watibiwe kwanza kisha wapewe chanjo baada ya siku 8-12 hasa kama umetibu na dawa zinazofanya kazi muda mrefu.

 

Namna ya kuteketeza mizoga ya ugonjwa wa Kimeta

Kwa kuwa vimelea kubadilika umbo kwenda umbo la viiniyoga linalokuwa hatari kwa maambukizi kwa wanyama na binadamu, ni muhimu wakati wa kuangamiza mizoga kusiruhusu vimelea kupata hewa ya oksijeni. Njia zinazoweza kuzuia hili ni pamoja na kuchoma mzoga kwa kumwagia mafuta ya taa na kufukia kwenye shimo. Mzuga uchomwe au kuzikwa kwenye eneo ulipo kuepusha kusambaza vimelea vya kimeta maeneo mengine. Wakati wa kuzika mzoga unaweza kumwagiwa kemikali kama fomalini kuzuia kuoza kwa mzoga wakati huo huo kuzuia vimelea vya kimeta. Ikiwezekana ni vema mzoga ukazikwa ukiwa umeviringishwa karatasi ya naironi maana imetokea maeneo mengine baada ya miaka mingi vimelea vilitoka nje na kusababisha milipuko.

Shimo pia lafaa kuwa refu kuzuia mbwa na wanyama wengine kuweza kufukua na kuutoa mzoga nje kutakako pelekea kusambaa kwa viiniyoga. Matumizi ya chokaa kama ilivyokuwa siku za nyuma kwa sasa haishauriwi. Nimesema hapo mwanzo kuwa vimelea wa kimeta wanapendele maeneo yenye udongo wenye alkali kubwa (pH kubwa). Sasa chokaa imeonekana haiui vimelea vya kimeta bali husaidia vistamili vyema.

Kwa kuhitimisha njia inayofaa ni ya kuchoma mizoga, lakini kwa sababu ya gharama na hasa wanyama wapokuwa wengi basi njia ya kuzika itumike kwa kuchimba shimo ref una ikiwezekana mizogo iviringishwe kwenye karatasi ya naironi.

 

SOMA ZAIDI KUHUSU KIMETA KWENYE KITABU HIKI ANTHRAX 4TH EDITION

 

Leave a Reply