Na Walter Riwa 0756264580 DSM (imehaririwa)

Vifaranga wa bata mzinga ni tofauti na wa kuku kwani vifaranga wa kuku hutotolewa wakiwa tayari wanajua kujifunza kula na kunywa maji wakati wale wa bata mzinga huzubaa kwa siku kama 4 ndipo wajue kula vizuri. Hivyo wana hitaji uangalizi wa karibu na wa hali ya juu sana.

Hukaa kwenye bruda (brooder) kwa muda wa wiki 4 wakiwa watahitaji joto la kutosha muda wote. Wiki ya kwanza wanahitaji nyuzi joto 38 na wiki ya pili unapunguza nyuzi joto 5 na kila wiki utaendelea kupunguza nyuzi joto 5. Wanakua kwa haraka hivyo wanahitaji sehemu kubwa ya kuwatunzia, yaani sentimita 20×20 kwa kila kifaranga kwenye wiki ya pili hadi ya tatu. Wanahitaji chakula chenye protini nyingi 28% kwa wiki 8 za mwanzo, hivyo ni bora kuwapa broiler starter kwa muda wa miezi miwili.

Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye uleaji wa vifaranga vya bata

  1. Hakikisha unaweka matandiko (brooder) sehemu ya kuwalelea vifaranga kiasi cha kutosha (kina cha inchi 3) ili kuweka hali ya joto. Matandiko yaweza kuwa maranda ya mbao, nyasi au pumba za mpunga.
  2. Wape joto kwa vyanzo vya joto ulivyo navyo kama taa za umeme 100w au 200w, jiko la mkaa, taa ya chemli au kandiri au tumia njia za asili. Njia nzuri na isio na gharama kubwa yakutengeza joto ni kwakutumia jiko la mkaa liwashe nje likisha waka vizuri liingize kwenye chumba chao. Ni rahisi kutambua kama joto linawatosheleza ama la. Joto linapokua kali utawaona vifaranga wakiachama midomo kama vile afanyavyo mbwa pia hutanua mbawa zao na kuachiana nafasi. Ukiona hivyo fungua madirisha kwa muda mpaka wawe kwenye hali ya kawaida kisha funga tena madirisha ili kuhifadhi joto kuokoa matumizi ya mkaa mara kwa mara. Joto linapopungua vifaranga hukusanyana hapo tambua kwamba wanasikia baridi hivyo ingiza jiko ndani. Njia hii yakutumia jiko ni rahisi kwani kama utawasha jiko usiku saa mbili hutaweka tena mpaka asubuhi cha msingi chumba kisiwe na upotevu wa joto.

 

  1. Weka vyombo vya chakula na kunywea maji kabla hujawaingiza vifaranga hao.
  2. Weka vitu vya kung’aa katika chakula na maji ili kuwavutia kujifunza kula. Vitu vya kung’aa yaweza kuwa gololi zile za kuchezea watoto unatumbukiza kwenye maji hivyo zile rangi zitawavutia kusogea pale na kudonoa donoa. Au waweza kuweka maji ya mchele kama maji yao ya kunywa ili ile rangi nyeupe iwavutie kusogelea maji. Pia unaweza kuamua kuwachanganya na vifaranga wa kuku watajifunza kula kupitia vifaranga wa kuku. Hii ni namna ya kuwafunza kula.
  3. Wape chakula muda wote na wape majani wiki ya pili maana asilimia 50 ya chakula chao ni majani ya mbogamboga mbichi.

Chanjo na madawa

Chanjo: Kama ilivyo kwa kuku bata mzinga wanahitaji dawa na chajo.

Wiki ya kwanza: Wape chanjo ya Mdondo/kideri (Newcastle), Ndui (Fowl pox) na Mbande (Gumboro).

Wiki ya sita: Rudia chanjo ya Mdondo, kila baada ya miezi mitatu

Madawa: Madawa hasa antibiotic pindi unapoona viranga vinaonesha dalili za kuumwa na tatizo kubwa kwa vifaranga ni ugonjwa wa chorera (Magonjwa ya matumbo). Magonjwa mengi ya matumbo hutibiwa kwa antibiotic hasa OTC 20% pia ni vema ukafika kwa mtaalumu wa mifugo kama uko jirani ili upate matibabu sahihi kwa bata wako.

Wape vitamini na madini ktk chakula chao na vitamini nzuri ni ile yenye mchanganyiko wa vitamini nyingi (Multivitamin). Multivitamin inaweza kutumika wakati wote kwani husaidia kuwapa vifaranga vitamini pia huviongezea nguvu.

Chakula: Ikifika wiki ya 8 unaweza kuanza kuwatoa nje wajifunze mazingira ya nje na kujitafutia maana bata mzinga ni watafutaji wazuri wa chakula kama kuku wa kienyeji japo hupenda sana majani. Ni vizuri kuwapa lusina mbichi hufanya vizuri katika bata mzinga. Wape vifaranga vyakula venye mchanganyiko maalumu walau kwa miezi miwili. Vyakula hivi vinauzwa madukani lakini pia kama unaweza na kuelewa mchanganyiko huo unaweza fanya mwenyewe.

Utagaji wa mayai: Wiki ya 24 hadi 28 wanakuwa tayari wana kilo 8 hadi 12 hivyo wanaanza kutaga wachanganye na maduma katika ratio ya 1:5 yani dume 1 majike 5 hii ni kama bado hawajawa wazito sana kama wameshakuwa wazito au kuanza kuwa wavivu kuzeeka wawekee ratio ya 1:3 yani dume 1 majike 3.

Bata mzinga hutaga kwa msimu kama walivyo kanga na hulalia siku 28 kama kanga na wanauwezo wakulalia mayai yao 10 hadi 15 lakini hutaga mengi zaidi hivyo ni vizuri ukatumia mashine ya kutotolesha au kama una kuku wa kienyeji anapo lalia unamuwekea mayai 6 ya bata mzinga. Hivyo wakati huo bata anaendelea kutaga huku wanalalia mayai yao. Hivyo ni njia nzuri maana bata mzinga wanatabia ya kususa mayai yao kama mtu ukiyashika na marashi au yakipata harufu ambayo sio yao.

Soko: Soko la bata mzinga lipo mpaka sasa wanunuzi wanakuja kununua shambani kwako kwa sh 12,000/= kwa kilo moja ya bata mzinga na bata mzinga wakubwa wana zaidi ya kilo 15 kila mmoja.

 

 

JINSI YA KUTUNZA WATOTO WA BATA MZINGA (TURKEY)

‎Na Aaron Magembe‎ 

Ni takribani miaka 7 sasa tangu nimekuwa nikijishighulisha na ufugaji wa Bata Mzinga, japo ni kwa kiwango kidogo. Nimeona si vibaya, kutoa uzoefu wangu juu ya kukuza vifaranga wa Bata mzinga.

Kumekuwa na mawazo au kasumba kwamba ufugaji wa bata mzinga, hasa kukuza vifaranga ni mgumu sana ukilinganisha na kuku. Ni kwa nini? Baadhi ya watu huchukulia bata mzinga kama vile kuku – hapa nikimaanisha pindi anapototoa unaweza kumuachia vifaranga na akaweza kutembea navyo na kuvikuza mwenyewe atakavyo – LA HASHA! Bata mzinga ni mzembe kwa kiasi Fulani katika kuangalia au kutunza vifaranga wake hasa wakiwa wadogo ukilinganisha na Kuku.

Hizi ni baadhi ya mbinu au taratibu ninazozitumia kukuza vifaranga wa bata mzinga.

  1. MAYAI – Bata mzinga ana uwezo wa kutaga mayai mengi ili mradi uwe unayatoa mayai pale anapotaga na kuyahifadhi. Binafsi hutumia incubator kutotoresha mayai ya Bata Mzinga – lakini bata mzinga vile vile ana uwezo wa kuatamia mayai kati ya 15 mpaka 20 (inategemea na umbile lake). Mayai yanapotagwa huyaifadhi kwenye tray (sehemu ya wazi) kwa muda wa siku 10-12 Maximum na kuyaweka kwenye machine. Vifaranga huanguliwa baada ya siku 28.
  2. UTUNZAJI – Vifaranga hawa huwa nawaweka kwenye brooder maalumu ambayo huhifandhi joto. Vifaranga wa bata mzinga huhitaji joto la kutosha hasa katika wiki ya kwanza huhitaji nyuzi joto 95 – 100 (degrees) na unaweza kuwapunguzia nyuzi joto 5 wiki ya pili na kuendelea mpaka watakapo ota manyoya kati ya wiki 5-6. Hata wakiota manyoya ni vizuri kuendela kuwawekea taa ya mwanga wa kawaida hasa wakati wa usiku ndio muda ambao wanapenda kupata chakula na kucheza.
  3. CHAKULA – Vifanga wa bata mzinga hupendelea chakula chenye PROTEIN kwa wingi ukilinganisha na Kuku. Katika mchanganyiko wa Chakula kiwango cha virutubisho vya Protein ninachoweka ni asilimia ishirini na nane (28%). Mara nyingi mimi natumia unga wa samaki aina ya FURU au dagaa au UDUVI (hawa ni worms ambao huvuliwa pamoja na dagaa – ziwa Victoria) – kama sehemu ya Protein. Kwa ujumla chakula cha vifaranga wa Bata mzinga (Starter) kinatakiwa kiwe chenye muonekano wa unga unga (punje ndogo ndogo sana) ili kisiwakwame kooni wanapokula. Chakula kinapowakwama utengeneza madonda kooni hivyo kifaranga hudhoofika kwa kuacha kula. Ni vizuri vile vile kuchanganya vifaranga wa bata mzinga na wa kuku ili waweze kuwachangamsha hasa wakati wa kula chakula.
  4. MAGONJWA – Kama hautakuwa makini kwa kuzingatia joto hasa wiki ya kwanza – Vifaranga wa bata mzinga hushambuliwa na ugonjwa wa Nimonia na huathiri mfumo wa kupumua na hatimaye kifo. Magonjwa kama concidiocise, fow cholera, ndui (fow pox) n.k huwashambulia sana vifanga wa bata mzinga.
  5. KINGA/TIBA – Baada ya siku 7 vifaranga wa bata mzinga wapewe chanjo ya kinga ya kideri na wiki inayofuata wapewe chanjo ya Gumboro. Baada ya wiki ya 5 wapewe chanjo ya kinga ya Ndui. Vile vile mimi hutumia dawa za asili hasa vitunguu swaumu kwa ajili ya kinga ya Mangonjwa kuanzia wiki ya kwanza mpaka ya tano huwawekea vitunguu swaumu kwenye maji ya kunywa nikichanganya na vitamin – hii husaidia sana kuwapa kinga ya bacteria wanaoweza kushambulia miili ya vifaranga hao.

 

Leave a Reply