Na Augustino Chengula
Kwa asili kuku wanapenda sana kudonoa kila kitu wanachokiona kinawavutia chenye mfanano na chakula. Kwa bahati mbaya tabia ya kudonoa haiishii tu kwa vitu bali huenda mbali kudonoa kuku wenzao. Hivyo kuku kudonoana ni tabia asili (si ugonjwa) inayoonekana kwa kuku kudonoa manyoa (feather pecking) ya kuku mwenzake hasa ya mkia na kichwani. Wakati mwingine huwa ni tabia asili ya kuku kutaka kuonyesha nani mkubwa ndani ya banda. Tabia hii ikizidi sana hupelekea kuku kudona ngozi kupelekea damu kutoka, hatua mbaya inayo pelekea kifo cha kuku. Kitendo cha kuku kudonoa kuku mwenzake kwa makusudi hadi kusababisha damu kutoka na hata kupelekea kifo kinajulikana kama kuku kulana (cannibalism) Ni vizuri kutatua tatizo hili mapema uonapo kuku wanaanza kudonoana manyoya.
Nini kinasababisha?
Sababu kuu zinasababisha hili tatizo ni jinsi kuku wanavyofugwa na kupewa matunzo kama nilivyofafanua hapa chini.
Upunugu wa mahitaji ya msingi: Kuku watadonoana na kulana endapo chakula au maji ndani ya banda haviwatoshi, vyombo vya kulishia na kunyweshea vipo karibu karibu sana au vifaa vya kutagia na sehemu za kulala haziwatoshi. Kuku wakipewa chakula au maji kidogo hupigana ili wakipate. Lakini pia upungufu wa madini unasababisha kuku wadonoane.
Kuku wengi-Kuku wakiwa wengi ndani ya banda pamoja na maeneo machache ya kutagia mayai husababisha wadonoane na kupigana. Lakini pia kufuga kuku wa aina tofauti (kisasa na kienyeji), umri tofauti (wadogo na wakubwa),rangi tofauti na maumbile tofauti ambao hawajakua pamoja husabisha wengine kuonewa. Kuku wagonjwa, wenye vidonda husababisha waonewe na wenzao kwa kudonolewa.
Joto kubwa kupita kiasi-Joto kali huwakasirisha kuku na kumaliza hasira zao kwa kuwadonoa wengine. Hivyo hakikisha joto ni lile linalowafaa kuku kwa umri husika. Hii inaendana sambamba na mwanga mkali hauwafai kuku hasa wakubwa hukasirishwa nao sana, hivyo wapewe mwanga stahili tu.
Sababu nyingine: Kufuga kuku wa aina, umri, umbile na rangi tofauti sehemu moja, upungufu wa madini kama chumvi, kuchanganya kuku wadhaifu, wagonjwa na wenye vidonda pamoja na wazima.
Dalili za kudonoana na kulana
Dalili za mwanzo za kuku kudonoana zinajumuisha kudonoa vidole vya vifaranga, kudonoa manyoya ya kuku wakubwa, kichwani na mkiani.
Kudonoa vidole: Tabia hii huonekana zaidi kwa kuku wadogo (vifaranga), na hutokana na nafasi ndogo ya vyombo vya kulishia au kifaranga kutopata chakula. Tabia hii hujitokeza kwa vifaranga wakakamavu kwa kudonoa vidole vyao au vya vifaranga wengine na mara nyingi kwao haina madhara, madhara huonekana zaidi kwa kuku wakubwa.
Kudonoa manyoya: Tabia hii huanza taratibu kwa kuku wakubwa tena na mmoja au zaidi na kuenea kwa kuku wote ndani ya banda. Yaweza kujitokeza kwa kuku wanaofugiwa kwenye keji au wale wanaofugiwa ndani sakafuni inayopelekea kuku kukosa mazoezi. Kudonoa manyoya kwa kuku ni sawa na kudonoa chakula na mara nyingi hufanyika mgongoni, mkiani na kichwani, na unapokuwa ni udonoaji wenye shari na wa kuendelea huwa ni tabia mbaya (si ya kawaida). Hii inaweza kupelekea kwenye muonekano mbaya wa manyoya ya kuku au kupoteza manyoya kabisa. Kuku akipoteza manyoya (hatua mbaya) ngozi huachwa wazi ambapo kuku anaweza kupata majeraha kwa urahisi inayopelekea kupoteza damu na kuku kulana.
Ni vigumu sana kutofautisha kudonoana kwa kawaida na kule kutakako pelekea kulana kunakosababisha madhara makubwa kwa kuku. Ni vema kuwaangalia kuku wako mara kwa mara ili kujua mapema kama kuna tabia ya kudonoana inaanza kujengeka ili kutatua tatizo mapema kabla halijafikia hatua ya kudonoana.
Kudonoa kichwa: Tabia hii hujitokeza kwa kuku waliojazana na kuku wadogo ambapo hudonoana undu wa jogoo (comb) na upanga/ndevu za jogoo (wattles).
Kudonoa mkia (sehemu ya nyuma): Hii ndiyo hatua mbaya ya kuku kudonoana na kulana, inayoonekana mara nyingi kwenye kuku wanaofugwa kwa ajili ya mayai na kuku wadogo wanao karibia kupevuka wenye uzito mkubwa. Na eneo wanalopenda kudonoana ni mkiani na hasa pale ambapo mayai yamepasukia wakati akitaga.
Je, tabia hii inaweza kusambaa ndani ya banda?
Jibu la haraka ni ndiyo, tabia mbaya ya kudonoana linaweza kuenea katika banda au kuku wote ndani ya banda. Ingawa tabia ya kudonoana mwanzoni huanza kama tendo la kawaida isiyo na madhara kwa kuku wa aina zote na umri wowote, lakini inaweza kukua na kuongezeka kwa haraka na kuwa tabia yenye madhara makubwa na hasa kama juhudi mahusi za kuzuia tatizzo hazija chukuliwa kwa haraka kabla ya kufikia hatua ya kualana.
Nini kifanyike kama tabia imeshaanza?
Kwa vile kuna sababu nyingi zinapelekea kwenye tabia hii, mara nyingi huwa ngumu kujua sababu ya tatizo. Lakini ukigundua mapema tabia ya kudonoana manyoa inapoanza na kuchukua hatua mahususi za kuzuia, husaidia wasifikie tabia mbaya ya kulana inayopelekea vifo. Tabia inaweza kuanza na kuku mmoja, kama hajadhibitiwa na kuku wengine huiga tabia hiyo.
Tenga kuku wanaoonyesha kuwa ndo vinara wa kudonoa au kula wenzao, pia wale wenye vidonda wawekwe kando. Waweza pia ning’iniza mboga za kijani ndani ya banda kwa urefu utakao muwezesha kuku kurukia na kula, hakikisha unaweka sehemu nyingi ili kupunguza kuku kujaa sehemu moja na kuanza kupigana.
Kuku wenye vidona, nyunyiza/pulizia dawa ya kuzuia wadudu kama bacteria (antibiotics) maeneo yenye vidonda.
Kukata midomo (beak trimming): Kuku wanaodonoa wenzao wanaweza kukatwa midomo yao upande wa juu (tazama picha) ili kuzuia wasidonoe wenzao. Ukataji unaweza kufanywa na wembe mkali au kisu kilichochomwa na moto, uwe makini usimchome kuku au wewe mwenye. Kwa kuku wadogo ili wasijedonoana baadaye, midomo ikatwe wakiwa na siku 10 na au wiki 10 – 12. Njia hii haishauriwi kwa kuku wadogo hasa kama njia nyingine za kuzuia zinaweza kufanywa na mfugaji. Hivyo ni vema ukakinga kuku wako kwa kuwapa chakula na maji kwa nafasi.
Nini kifanyike kuzuia tabia ya kudonoana na kulana?
Njia nzuri ya kuzuia tabia ya kudonoana na kulana ni kufuga kuku wa aina moja, umri unaofanana, umbile sawa na afya zinazofanana. Kuku yeyote mwenye afya dhaifu au mgonjwa huwa ndo chanzo cha kudonolewa na kuku wengine, hivyo ni vema wakatengwa mapema iwezekanavyo kupunguza tatizo la kudonoana. Ikiwezekana kuku wa aina hiyo waondolewe kwa kuwauza au kuliwa na familia. Kuku wapewe eneo zuri la kuishilenye nafasi ya kutosha ili kuku wasibanane, viota view na nafasi ya kutosha, na pia liwe na hewa nzuri ili kupunguza joto. Kuku pia wapewe chakula na maji ya kutosha na kuwe na vifaa vya kutosha ili kuku wasianze kufukuzana ili kupata chakula au maji. Kama unatumia taa za umeme hakikisha mwanga wake unakuwa si mkali ili usiwaudhi kuku na kuanza kudonoana. Hakikisha unatibu magonjwa hasa ya ngozi mapema iwezekanavyo (viroboto, chawa, utitiri visiwepo kwa kuku) ili kupunguza hasira ya kuku.