- Kunyonyoka manyoya kwa kuku ni nini?
Ni mchakato wa asili na muhimu kwa kuku kupoteza/kujinyonyoa manyoya ya zamani/yaliyochoka/yaliyovunjika ili kupata/kuota manyoya mapya.
- Kwa nini kuku wananyonyoka manyoya?
* Sababu kuu ni kuku kumaliza mzunguko wake wa utagaji.
* Sababu ndogo ndogo ni:
– Ukosefu wa chakula bora
– Ukosefu wa maji
– Joto kali sana
– Stress/ msongo wa kimwili, mfano majogoo kupanda jike moja mara nyingi
- Kuku hunyonyoka manyoya wakati gani?
* Vifaranga wanapototolewa wanakuwa wamefunikwa na vimanyoya kama hariri. Katika ukuaji wao hupitia kunyonyoka manyoya mara 4 mpaka wanapokuwa wakubwa, na hivyo kupata manyoya kamili. Vipindi hivyo ni wakiwa na umri wa wiki 1 – 6, wiki 7 – 9, wiki 12 – 13 na wiki 20 – 22.
* Kuku wakubwa wananyonyoka manyoya angalau mara moja kwa mwaka. Na itamchukua kuku muda wa miezi 2 – 4 kumaliza mchakato wa kunyonyoka manyoya hadi kuota.
- Mchakato wenyewe wa unyonyokaji manyoya.
Manyoya yanayoota huyasukuma manyoya ya zamani kwa nje na kudondoka. Kuku huanza kunyonyoka kuanzia kichwani, kwenye mabawa, mwilini hadi mkiani.
- Aina za unyonyokaji manyoya.
* Unyonyokaji mgumu: Ambapo kuku hunyonyoka manyoya haraka, na humchukua muda mrefu kuota manyoya mapya.
* Unyonyokaji laini: Ambapo kuku hunyonyoka manyoya huku manyoya mapya yakiota baada ya muda mfupi.
- Utegemee nini kipindi cha kuku kunyonyoka manyoya?
* Kuku hupunguza kutaga au kuacha kabisa. Hii hutokana na kwamba 80-85% ya manyoya ni protein na 13% ya mayai ni protein, hivyo kuku hufanya uchaguzi wa kuitumia protein anayokula kwenye chakula katika ukuaji wa manyoya mapya na kupunguza protein kwenye kutengeneza mayai.
* Manyoya mengi kunyonyoka.
* Kuku wanaweza kuonekana kama wanaumwa na kupungua uzito.
* Kuku wanaweza kuwa wakorofi na wakali.
* Kuku wengine kwenye banda wanaweza kumdonoa ngozi kuku anayeota manyoya na kusababisha kutoka damu.
- Nini cha kufanya kuku wanaponyonyoka manyoya?
* Walishe chakula chenye protein nyingi. Kwa kawaida chakula cha kuku wanaotaga huwa na protein 16%, kipindi cha kuku kunyonyoka manyoya ongeza protein ifike 20-25%.
* Hakikisha kuku wana chakula na maji muda wote.
* Hakikisha kuku hawasumbuliwi na kupata stress. Mfano, epuka kuleta kuku mgeni bandani.
* Epuka kuwabeba au kuwashika kuku kipindi hiki, kwani itawaumiza na kuwaongezea stress.
* Hakikisha kuku anayeota manyoya hadonolewi na wenzake.
MUHIMU: Majogoo na mitetea yote hupitia unyonyokaji wa manyoya.
Imeandaliwa na
Aquinus Poultry Farm.
0655347932