KWA NINI UOGESHE MIFUGO YAKO?

Kwa nini uogeshe mifugo yako?JoshoKwa nini uogeshe mifugo yako?

“KINGA NI BORA KULIKO TIBA”

Huu ni usemi muhimu sana kwa wafugaji unaotufungulia makala yetu ya leo inayohusu kuogesha mifugo yetu. Lengo la kuogesha mifugo ni kuzuia magonjwa yanayoenezwa na kupe yasiwapate mifugo yetu. Unapomuona kupe kwenye mfugo wako anza kufikiria kuwa anaweza kuwa amebeba vimelea vya magonjwa yatakayo athiri mifugo yako. Lengo la kupe si kuleta vimelea vya magonjwa kwenye mifugo yako bali ni kujipatia chakula (damu) ili aweze kuishi na kwa bahati mbaya vimelea vya magonjwa navyo vinawatumia kupe ili viweze kumfikia myama mwenye mazingira mazuri kwa kuishi. Hivyo lengo la vimelea vya magonjwa navyo si kusababisha mnyama augue na kufa. La hasha maana vitakosa mahali pa kuishi, ni kwa bahati mbaya tu kuwa vimelea hivi vinapokuwa vinakuwa vinapata chakula au kuzaliana kwa namna moja au nyingine huathiri mifumo ya ufanyaji kazi wa mnyama jambo linalopelekea mnyama kuugua au hadi kupoteza uhai.

Kwa vile mfugo unamanufaa kwetu (kwa bahati mbaya nasi kwa wakati mmoja au mwingine huupotezea uhai hasa pale tunapohitaji kitoweo) hutulazimu kuutunza ili usipate magonjwa yatakayoathiri uzalishaji wake (maziwa, nyama, ngozi). Matunzo hayo ni pamoja na kumpa chakula, maji na kumkinga dhidi ya majanga kama magonjwa na ajali mbalimbali na kumpa hifadhi nzuri. Katika makala ya leo nitazungumzia namna ya kuukinga mfugo wako usipate magonjwa. Zipo njia kubwa mbili: kukinga mifugo kwa kutumia chanjo na kwa kuogesha mifugo. Makala hii itajikita kwenye uogeshaji wa mifugo kampeni inayoendelea nchi nzima ya Tanzania.

Swali la msingi ni kwa nini uogeshe mifugo yako? Wafugaji wengi wanajua sababu za msingi za kuogesha mifugo yao na wapo ambao wanajua ili wanazembea kwa makusudi au kwa kukosa miundo mbinu ya kuogeshea. Kama nilivyosema awali tunaogesha mifugo ili kuwakinga na kupe (ticks) wanaoeneza wadudu wa amgonjwa. Mbali na kueneza magonjwa kupe wenyewe huleta usumbufu kwa mifugo (muwasho), kuondoa nywele na kuharibu ngozi ya mifugo kunakopelekea maambukizi ya bakteria. Hivyo mifugo hukosa raha wawapo na kupe mwilini na tunalazimika kusaidia kuondoa kupe hao. Kupe wakishambulia kwa wingi mfugo wako hupelekea mfugo kupoteza damu nyingi (hunyonya damu) na hudhofisha mfugo. Zaidi ya hayo kupe husababisha uzalishaji wa mfugo kushuka. Kupe wa aina tofauti hupendelea kukaa maeneo tofauti ya mwili wa mnyama wakibeba vimelea vya magonjwa tofauti. Kupe utawaona maeneo yafuatayo ya mwili wa mnyama: masikioni, shingoni, kwapa za miguu ya mbele, unapoanzia mkia na maeneo ya mgongoni. Kupe hawa hubeba vimelea vya bakteria, virusi na protozoa na kuwaeneza toka kwa mfugo mmoja kwenda kwa mwingine wakati wanakunywa damu. Yapo magonjwa mengi sana yanayotokana na vimela vinavyoenezwa na hawa kupe kama ifuatavyo;

(i) Magonjwa ya protozoa-Ndigana kali/moto (East Coast Fever)- kupe wake hupatika kwenye masikio

-Ndigana maji moyo (Heartwater)

-Ndigana baridi (Anaplasimosis)

-Ndigana mkojo damu (Babesiosis)

(ii) Magonjwa ya bakteria- Ugonjwa wa Lyme

(iii) Magonjwa ya virusi- Ugonjwa wa kondoo Nairobi (Nairobi sheep disease), Homa ya Crimean-Congo  (Crimean-Congo hemorrhagic fever)

 

Magonjwa haya ya kupe nchini yamekadiriwa kusababaisha magonjwa kwa mifugo 5,000 kila mwaka (Gazeti la Mwanacnhi 2013). Idadi hii ni kubwa sana na ikikumbukwa kuwa ni makadirio tu, na ugonjwa wa ndigana kali ndio unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi vya mifugo nchini kwa mwaka. Hivyo jitahada za makusudi zinahitajika kukabiliana na magonjwa yanayoenezwa na kupe. Njia ya kuogesha mifugo ndiyo njia pekee iliyoonyesha ufanisi mkubwa kukabiliana na kupe na jitihada za kututengeneza chanjo zimekuwa na changamoto nyingi.

Serikali kwa kutambua hili ilianzaia majosho maeneo mengi nchini ili kusadia kupambana na magonjwa yaenezwayo na kupe tangu miaka baada ya kupata uhuru. Hata hivyo juhudi zimekuwa zikisuasua huku wakiachiwa wafugaji wenyewe washughulikie swala hilo ambalo halikuzaa matunda. Wengi wamekuwa wakitumia mabomba kunyuzia dawa mifugo yao, njia ambayo ufanisi wake ni mdogo maana si rahisi kumlowesha ng’ombe mwili mzima na hasa unapokuwa na mifugo mingi. Hivi karibuni serikali chini ya Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Joelson Mpina (Mb) imekuja na kampeni mpya ya kuogesha mifugo kwa njia ya majosho iliyozinduliwa tarehe 16-12-2018 wilayani Chato. Kwa kuanzia na kuboresha majosho yote nchini ambayo ni kati ya 1,400 na 1,500 na kuhakikisha majosho yote yanapata dawa ya kuogeshea toka serikalini bure.

MILIONI 300 ZANUNUA DAWA ZA MIFUGO – DKT. HEZROON NONGA

 

Leave a Reply