Mageuzi ya Kilimo na Mifugo yanawezekana

 

Imeandikwa na mhariri wa Habari Leo

IMECHAPISHWA: 07 AGOSTI 216

MAONESHO ya wakulima ya Nanenane yaliyoanza wiki iliyopita, yanatarajiwa kufikia kilele chake kesho katika Kanda mbalimbali nchini, huku yale ya kitaifa yakifanyika kwenye Viwanja vya Ngongo, nje kidogo ya mji wa Lindi.

Ni maonesho muhimu yenye lengo la kuonesha fursa zilizopo katika sekta ya Kilimo na kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, ili shughuli zao ziweze kuwa na tija. Pia yanalenga kuwaonesha Watanzania kwamba, kilimo ni zaidi ya biashara badala ya kubaki na dhana kwamba kilimo ni kwa ajili ya chakula tu.

Aidha, yanasisitiza umuhimu wa kuacha kulima kwa mazoea na badala yake wanapaswa kulima mazao yenye soko na mwisho ni kuhakikisha baada ya kazi ngumu ya shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi, mazao hayo yawe na thamani katika soko.

Ndiyo maana tunasema, haya ni maonesho muhimu mno kwa ustawi wa uchumi wa nchi hasa ikizingatiwa asilimia 80 ya Watanzania wanategemea zaidi sekta ya kilimo.

Ni kutokana na umuhimu huo, tunapenda kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuyatambua maonesho haya, lakini pia kamati husika za maandalizi, wakulima, wafanyabiashara, idara na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi zikiwemo za fedha, nazo zinastahili pongezi kwa kushiriki katika kusogeza fursa mbalimbali karibu zaidi na wakulima.

Kutokana na sekta zote muhimu kuwapo katika viwanja vya maonesho ya Nanenane, hakika ni fursa nzuri kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuweza kujifunza mengi juu ya kufanya mabadiliko katika shughuli zao, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali hasa ikizingatiwa kuwa, kwa muda mrefu sekta ya kilimo na ufugaji imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kutozingatia kanuni bora na za kisasa za kilimo na Ufugaji.

Mbali ya kukutana na wataalamu katika sekta hizo, maonesho hayo hukusanya wataalamu wa teknolojia katika sekta ya kilimo, watafiti, wataalamu wa ushauri wa masuala ya fedha masoko na kadhalika.

Hivyo tunaamini, mkulima, mfugaji au mvuvi aliyehudhuria maonesho hayo, kamwe hawezi kutoka bila kuzaliwa upya au kuongeza maarifa juu ya kuboresha shughuli zake, hivyo kumsaidia kuongeza uzalishaji utakaomwinua mkulima kiuchumi, lakini pia uchumi wa taifa.

Kwamba, maonesho haya kwa kiasi kikubwa yanakuwa na majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima, wafugaji na wavuvi katika nchi hii.

Mathalani, wafugaji watakuwa wamenufaika na mbinu za kuboresha mazao yao ikiwa ni pamoja na jinsi ya kunenepesha mifugo kwa muda mfupi na kuiuza kwa bei nzuri zaidi, kuboresha magulio ya mifugo na mazao yake, kuhamasishaji uwekezaji wa viwanda vya mazao mbalimbali ya mifugo kama vile ngozi na maziwa ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.

Kwa wakulima, watajifunza juu ya matumizi ya mbegu bora, uchunguzi wa udongo na aina ya pembejejeo inayofaa, matumizi ya kilimo cha umwagiliaji kwa teknolojia za kisasa, lakini pia jinsi ya kuzitumia taasisi za fedha na nyinginezo katika kuinua shughuli zao.

Ni dhahiri kwamba, mapinduzi katika sekta hizo yanasaidia kuongeza ajira, kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara, lakini pia kupaisha uchumi wa nchi kwa kasi kupitia mauzo ya ziada ya mazao na malighafi nje ya nchi.

Huko ndiko tunakopaswa kuupeleka uchumi wa nchi yetu, kutoka kilimo cha mazoea hadi chenye tija ikiwa na maana kuleta mapinduzi makubwa katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji.

Ndiyo maana tunasema, maonesho haya yakitumika vizuri, kuna uwe uwezekano mkubwa wa kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.

Hivyo, shime tuyatumie vyema badala ya kushiriki kwa kuwa kalenda inaonesha kila ifikapo Agosti 8 ni kilele cha Maonesho ya Wakulima ya Nanenane

Leave a Reply