Mbuzi na kondoo wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu na kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na ng’ombe. Kutokana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia wanaweza kuhudumiwa na familia yenye nguvukazi na kipato kidogo. Uzao wa muda mfupi unamwezesha mfugaji kupata mbuzi/kondoo wengi kwa kipindi kifupi.

Wanyama hao hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, sufu na mazao mengine kwa matumizi ya familia na kuongeza kipato. Ufugaji bora wa mbuzi na kondoo uzingatie kanuni zifuatazo:-

 1. Wafugwe kwenye banda au zizi bora,
 2. Wachaguliwe kutokana na sifa za koo/aina na lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au sufu),
 3. Wapatiwe lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili,
 4.  Kuzingatia mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo,
 5. Kuweka na kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji; na
 6. Kuzalisha nyama, maziwa au sufu yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko

 

Zizi au Banda la Mbuzi/Kondoo

Mbuzi/kondoo wanaweza kufugwa katika mifumo ya huria, shadidi na kwa kutumia njia zote mbili. Zizi hutumika katika mfumo huria ambapo mbuzi/kondoo huchungwa wakati wa mchana na kurejeshwa zizini wakati wa usiku. Zizi bora ni lile lenye sifa zifuatazo:-

 • Lililo imara linaloweza kumkinga mbuzi/kondoo dhidi ya wanyama hatari na wezi,
 • Lililojengwa mahali pa mwinuko pasiporuhusu maji kutuama,
 • Ukubwa wa zizi uzingatie idadi na umri wa mifugo. Ni vema mbuzi/kondoo watengwe kulingana na umri wao; na
 • Liruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.

Pale ambapo mbuzi/kondoo wanafugwa kwa mfumo wa shadidi hufugwa katika banda wakati wote. Banda bora la mbuzi/kondoo linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-

 • Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama

hatari,

 • Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi,
 • Lijengwe sehemu isiyoruhusu maji kutuama na liwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu. Pia ujenzi uzingatie mwelekeo wa upepo ili hewa

kutoka bandani isiende kwenye makazi,

 • Liwe na sakafu ya kichanja chenye urefu wa mita 1 kutoka ardhini (Kwa banda la mbuzi),
 • Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji na mahali pa kuweka jiwe la chumvichumvi; na
 • Liwe na vyumba tofauti kwa ajili ya majike na vitoto, mbuzi/kondoo wanaokua, wanaonenepeshwa na wanaougua.

 

Vifaa vya Kujengea na Vipimo vya Banda

Inashauriwa banda la mbuzi/kondoo lijengwe kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika eneo husika. Ukubwa wa banda utategemea idadi yabuzi/kondoo wanaofugwa humo na ukubwa wa umbo

 • Paa lijengwe kwa kutumia vifaa kama miti, mbao, na kuezekwa kwa nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati au hata vigae kwa kutegemea uwezo wa mfugaji,
 • Kuta zijengwe kwa kutumia mabanzi, mbao, nguzo, wavu wa waya, fito na matofali. Kuta ziwe imara zinazoruhusu hewa na mwanga wa kutosha.
 • Mlango uwe na ukubwa wa sentimita 60 x 150,
 • Sakafu inaweza kuwa ya udongo au zege.
 • Sakafu ya kichanja inaweza kujengwa kwa kutumia miti, fito, mianzi, mbao au mabanzi na iweze kuruhusu kinyesi na mkojo kupita.
 • Chumba cha majike na vitoto kiwe na nafasi ya sentimita 1.25 kati ya papi na papi, fito na fito au mti hadi mti.
 • Chumba cha mbuzi/kondoo wakubwa iwe sentimita 1.9 kati ya mbao na mbao.

 

Uchaguzi wa Mbuzi/Kondoo wa Kufuga

Madhumuni ya kuchagua mbuzi au kondoo wa kufuga ni kuboresha uzalishaji na kuendeleza kizazi bora. Kuna aina nyingi za mbuzi/kondoo wanaoweza kufugwa kulingana na mazingira na mahitaji ya mfugaji. Uchaguzi hufanyika kwa kuangalia umbile, uzalishaji na kumbukumbu za wazazi kama vile umbo kubwa, ukuaji wa haraka, uwezo wa kutunza vitoto na kutoa maziwa mengi.

Mbuzi wanaofaa kwa ajili ya maziwa ni aina ya Saanen, Norwegian na Toggenburg pamoja na chotara wao.

Mbuzi wanaofaa kwa ajili ya nyama ni Boer na chotara wao, mbuzi wa asili kama vile Pare white, Newala na Ujiji. Mbuzi aina ya Malya (Blended) wanafaa kwa ajili ya nyama na maziwa.

Aidha, kondoo aina ya Black Head Persian (BHP), Masai red, Suffolk na Hampshire wanafaa kufugwa kwa ajili ya nyama. Merino na Lincoln hufugwa kwa ajili ya sufu, wakati Corriedale na Romney hufugwa kwa ajili ya nyama na sufu. Hapa Tanzania kondoo wanaopatikana kwa wingi ni Black Head Persian, Masai Red Dopper na kondoo wengine wa asili.

 

Sifa za jike

Mbuzi/kondoo jike wanaofaa kwa ajili ya kuzalisha maziwa na nyama wawe na sifa zifuatazo:-

 • Historia ya kukua upesi, kuzaa (ikiwezekana mapacha) na kutunza vitoto vizuri,
 • Umbo la mstatili linaloashiria utoaji wa nyama nyingi; na
 • Asiwe na ulemavu wa aina yoyote

Sifa za Ziada kwa Mbuzi wa Maziwa

 • Awe na miguu ya nyuma iliyo imara na iliyonyooka na yenye nafasi kwa ajili ya kiwele; na
 • Awe na kiwele kikubwa na chuchu ndefu zilizokaa vizuri

 

Sifa za Dume

Dume bora awe na sifa zifuatazo:-

 • Miguu iliyonyooka, imara na yenye nguvu,
 • Asiwe na ulemavu wa aina yoyote,
 • Mwenye uwezo na nguvu ya kupanda; na
 • Mwenye kokwa mbili zilizo kaa vizuri na zinazolingana

Angalizo: Dume lichaguliwe kwa makini kwa sababu “dume ni nusu ya kundi”.

 

Utunzaji wa Vitoto vya Mbuzi/Kondooa

Utunzaji huanza mara tu baada ya kuzaliwa.

Mfugaji ahakikishe:-

 • Kitoto cha mbuzi/kondoo kinapata maziwa ya mwanzo (dang’a) ndani ya masaa 24 tangu kuzaliwa na kwa muda wa siku 3,
 • Kama kinanyweshwa maziwa, kipewe lita 0.7- 0.9 kwa siku. Maziwa haya, ni muhimu kwani yana viinilishe na kinga dhidi ya magonjwa,
 • Iwapo mama hatoi maziwa au amekufa, inashauriwa kutengeneza dang’a mbadala au kama kuna mbuzi/kondoo mwingine aliyezaa anaweza kusaidia kukinyonyesha kitoto hicho,
 • Kitoto cha mbuzi/kondoo kiendelee kunyonya kwa wiki 12 – 16. Wiki 2 baada ya kuzaliwa, pamoja na maziwa, kianze kupewa vyakula vingine kama nyasi laini na chakula cha ziada ili kusaidia kukua kwa tumbo. Aidha, kipewe maji wakati wote,
 • Vyombo vinavyotumika kulishia vinakuwa safi muda wote,
 • Kitoto cha mbuzi/kondoo kiachishwe kunyonya kikiwa na umri wa miezi 3 hadi 4 kutegemea afya yake; na
 • Vitoto vipatiwe kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.

 

Matunzo Mengine

Utambuzi

Mbuzi huwekewa alama ili atambulike kwa urahisi na kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu zake. Shughuli hii hufanyika kwa mbuzi/kondoo akiwa na umri wa siku 3 – 14. Njia zitumikazo ni pamoja na:

 • Kuweka alama sikioni kwa kukata sehemu ndogo ya sikio,
 • Kumpa jina kwa wafugaji wenye mbuzi wachache,
 • Kumvisha hereni ya chuma au plastiki yenye namba kwenye sikio,
 • Kumvalisha mkanda wenye namba shingoni; na Kuweka namba kwa kuunguza sehemu ya ngozi ya mbuzi. Pale mfugaji anapotumia njia hii inashauriwa aweke alama kwenye eneo ambalo halitaathiri ubora wa ngozi

 

Kuondoa vishina vya pembe

Mbuzi/kondoo aondolewe vishina vya pembe akiwa na umri kati ya siku 3 hadi 14.

Visipoondelewa hukua na kusababisha kuumizana na kuhitaji nafasi kubwa kwenye banda. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.

 

Kuhasi

Vitoto vya mbuzi/kondoo ambavyo havitatumika kwa ajili ya kuendeleza kizazi vihasiwe kabla ya kufikia umri wa miezi 3. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.

 

Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo wa Miezi 4 – 8

Mbuzi wa miezi 4 mpaka 8 ni wale ambao wameacha kunyonya mpaka umri wa kupandishwa kwa mara ya kwanza. Mbuzi wa umri huu wana uwezo wa kula aina mbalimbali za malisho kama nyasi, mikunde, miti malisho na mabaki ya mazao wakati kondoo hupendelea zaidi nyasi fupi. Wakati wa kiangazi huhitaji kupatiwa chakula cha ziada au kupewa pumba za nafaka mbalimbali, mashudu ya alizeti,

pamba na dengu, majani ya mikunde yaliyokaushwa, madini na vitamini. Katika ufugaji huria ni vema kuzingatia idadi ya mbuzi/kondoo inayoweza

kuchungwa katika eneo, aina na hali ya malisho. Ili mbuzi/kondoo aweze kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa/kupevuka mapema, mfugaji anapaswa kufuata kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-

 • Kumpatia vyakula vya ziada kwa muda wa miezi 2 mfululizo kiasi cha kilo 0.2 – 0.7 kwa siku kuanzia anapoachishwa kunyonya,
 • Kumpatia dawa ya kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3 na kutoa kinga za magonjwa mengine kama itakavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo, Kuchanja na kuogesha ili kuzuia magonjwa mbalimbali,
 • Kukata kwato mara zinapokuwa ndefu; na
 • Kuhasi madume yasiyotumika kuzalisha.

 

Umri wa Kupandisha Mbuzi/Kondoo

Mbuzi/kondoo wakitunzwa vizuri wanaweza kupandishwa wakiwa na umri wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili kutegemea afya yake. Hata hivyo, inashauriwa wapandishwe wanapofikia uzito wa kilo 12 au zaidi na wasipandishwe mbuzi/kondoo wa ukoo mmoja.

 

Dalili za joto

Mfugaji anashauriwa asimpandishe jike kabla hajafikisha umri wa kupandwa wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili hata kama ataonyesha dalili ya kuhitaji dume. Mbuzi/kondoo aliyezaa anaweza kupandishwa siku 30-60 baada ya kuzaa. Mbuzi/kondoo aliyeko kwenye joto huonyesha dalili zifuatazo:-

 • Hutingisha/huchezesha mkia,
 • Hupanda na kukubali kupandwa na wengine,
 • Hutoa ute mweupe ukeni,
 • Huhangaika mara kwa mara na kupiga kelele,
 • Hufuata madume,
 • Hamu ya kula hupungua,
 • Hukojoa mara kwa mara,
 • Uke huvimba na huwa mwekundu kuliko ilivyo kawaida; na
 • Kwa mbuzi anayekamuliwa hupunguza kiwango cha maziwa

Mbuzi/kondoo apelekwe kwa dume mara tu dalili za joto zinapoonekana kwani joto hudumu kwa wastani wa siku 2 (saa 48). Chunguza tena dalili za joto baada ya siku 19 hadi 21 na kama dalili hazitaonekana tena kuna uwezekano mkubwakuwa mbuzi/kondoo amepata mimba. Mfugaji apange msimu mzuri wa mbuzi/kondoo kuzaa. Msimu mzuri ni mara baada ya mvua.

 

Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo Mwenye Mimba

Kwa kawaida mbuzi/kondoo hubeba mimba kwa muda wa miezi 5. Utunzaji wa mbuzi/kondoo mwenye mimba ni muhimu kwani ndiyo chanzo cha kupata vitoto vyenye afya bora. Mfugaji anashauriwa kufuata kanuni zifuatazo:

 • Apatiwe vyakula vya ziada kilo 0.2 – 0.7 kwa siku ili kutosheleza mahitaji yake na kitoto kinachokua tumboni,
 • Apatiwe nyasi, miti malisho na mikunde mchanganyiko kilo 1.8 – 2.5 kwa siku.

 

Dalili za Mbuzi/Kondoo Anayekaribia Kuzaa

 • Huhangaika kwa kulala na kuamka mara kwa mara,
 • Sehemu ya nje ya uke hulegea,
 • Hujitenga na kundi na hutafuta sehemu kavu na yenye kivuli,
 • Hupiga kelele; na
 • Hutokwa na ute mzito ukeni.

Mfugaji akiona dalili hizi anashauriwa asimruhusu mbuzi/kondoo kwenda machungani, bali amtenge kwenye chumba maalum, ampatie maji ya kutosha na kumuandalia sehemu ya kuzalia.

 

Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo Anayenyonyesha

Mbuzi/kondoo anayenyonyesha huhitaji chakula kingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya mwili na kuzalisha maziwa kwa ajili ya kitoto/vitoto. Pamoja na nyasi, mikunde na majani ya miti malisho kilo 1.8 – 2.5 kwa siku ni muhimu apewe chakula cha nyongeza kilo 0.3 – 0.8 kwa kila lita ya maziwa inayoongezeka baada ya lita 2 na maji safi, salama na ya kutosha wakati wote.

 

Taratibu za Kuzingatia Katika Ukamuaji wa Mbuzi wa Maziwa

Lengo la ufugaji wa mbuzi/kondoo wa maziwa ni kupata maziwa mengi, safi nasalama pamoja na mazao yatokanayo na maziwa. Mambo muhimu ya kuzingatia ni:-

 • Sehemu ya kukamulia iwe safi na yenye utulivu,
 • Mbuzi/kondoo awe na afya nzuri, msafi, na kiwele kioshwe kwa maji safi ya uvuguvugu,
 • Mkamuaji asibadilishwe badilishwe awe msafi, mwenye kucha fupi na asiwe na magonjwa ya kuambukiza,
 • Vyombo vya kukamulia viwe safi; na
 • Maziwa ya mwanzo kutoka kila chuchu yakamuliwe kwenye chombo maalum (strip cup) ili kuchunguza ugonjwa wa kiwele.

 

Utunzaji wa Dume Bora la Mbegu

Dume bora la mbegu ni muhimu litunzwe ili liwe na uwezo wa kutoa mbegu bora, kupanda na kuzalisha. Dume bora huanza kupanda akiwa na umri kati ya miezi.8 – 10 kwa mbuzi walioboreshwa. Katika msimu wa kupandisha dume moja liruhusiwe kupanda majike 40 hadi 50. Aidha, inashauriwa madume wenye umri wa miezi 8 – 9 waruhusiwe kupanda majike ambao ndio mara ya kwanza kupandwa.

Dume apatiwe:-

 • Malisho ya kutosha na vyakula vya ziada kiasi kisichopungua kilo 0.2 – 0.7 kwa siku na maji ya kutosha,
 • Majani ya miti malisho, mikunde na nyasi mchanganyiko na mabaki ya mazao; na
 • Kilo 0.45 hadi 0.9 za chakula cha ziada za nyongeza kwa siku kulingana na uzito wake na wingi wa majike anayopanda.wiki 2 kabla na baada ya kuanza kupanda.

 

 

Chanzo: Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi

 

Leave a Reply