Ugonjwa wa Ndui kwa Kuku (Fowlpox)

ByChengula

Nov 3, 2015 , ,
Ugonjwa wa ndui kwa kuku (fowlpox)FpUgonjwa wa ndui kwa kuku (fowlpox)

Na Mwandishi Wetu

Augustino Chengula

Ndui ya kuku ni nini?

Ndui ya kuku ni ugonjwa unaowapata kuku na bata ukienezwa na virusi wajulikanao kwa jina la kisayansi kama fowl pox virus walioko kwenye familia ya poxviridae. Ugonjwa huu unapatikana dunia nzima ukiwa na sifa ya kusambaa taratibu uikishambulia ngozi na maeneo ya juu ya mfumo wa chakula na upumuaji wa kuku. Hivyo ugonjwa huu hujitokeza katika maumbo ya aina tatu kulinga na eneo linaloshambuliwa: ugonjwa wa mfumo wa ngozi, ugonjwa wa mfumo wa chakula na upumuaji (hewa) na ugonjwa wa mifumo mingi ya mwili.

Dalili zake ni zipi?

Ugonjwa wa ngozi hujitambulisha kwa uwepo wa vinundu (viuvimbe) maeneo yasiyo na manyoya au yenye manyoya machache. Vinundu hivi baada ya muda huwa vigumu.

FP3
Vinundu vinavyoonekana ni dalili halisi za ugonjwa ndui, vingine vimepasuka na kutengeneza vinundu vigumu.

Ugonjwa wa mfumo wa chakula na hewa huwa na vidonda hasa kwenye membrini za mdomoni na mfumo wa juu wa upumuaji.

Wakati ugonjwa unaposhambulia mifumi mbalimbali ya mwili wa kuku au bata, hujulikana kama ugonjwa wa mifumo mingi.

FP6
Vidonda kwenye mfumo wa hewa na chakula (angalia mishale)

Ugonjwa wa ndui unaoshambulia mfumo wa chakula na upumuaji pamoja na ule wa mifumo mingi hutokea mara chache sana. Lakini pale unapotokea husababisha vifo vingi sana vya kuku. Ugonjwa wa ngozi ndio unaojitokeza mara nyingi sana, lakini mara chache sana hupelekea vifo vya kuku.

FP4
Hili ni umbile la ndui inayoshambulia mifumo mingi na hapa ni mfano mmoja wa namna ndui ilivyosambaa na kwenda maeneo ya tumboni.

Madhara yake kwa kuku ni yapi?

Maambukizi ya virusi wa ugonjwaa wa ndui kwa kuku husababisha kuku kuwa na ukuaji mbovu, chakula kutofanya kazi mwilini na kushuka kwa kiasi kikubwa cha utagaji wa mayai. Ugonjwa wan dui huwapata kuku wa umri wowote, na hasa kipindi cha miezi ya joto ya mwaka.

Ugonjwa wa ndui unaeneaje?

Kirusi cha ugonjwa huu kinaweza kusambazwa kwa njia ya kuku kugusana na kuku mwenzake mwenye ugonjwa au vijimelea vya ugonjwa au kwa kuumwa na mbu mwenye vimelea vya ugonjwa.

Utautambuaje ugonjwa wa ndui?

Ugonjwa wa ndui ni rahisi sana kuutambua kwa kupata historia ya ugonjwa, uwepo wa vidona/vinundu vya ugonjwa na wakatim fulani darubini inaweza kutumika kuangalia nyama za maeneo yenye ugonjwa na unaweza kuwakuza virusi kwenye chembe hai au mayai ya kuku.

Je ugonjwa ndui una tiba na kinga?

Ndui haina tiba yeyote. Njia pekee ya kupambana na kuzuia ugonjwa huu ni kwa kutmia chanjo inayochomwa kwenye ubawa. Chanjo zipo madukani (pox au pigeon pox vaccine). Chanjo itolewe kwa kuku wote wakiwa na umri wa wiki 12 hadi 16.

Leave a Reply