Ormilo (coenurus cerebralis), ugonjwa unaosumbua wafugaji wa mbuzi na kondoo nchini

Ormilo ni jina la Kimaasai lenye maana ya ugonjwa unaoshambulia kichwa na kufanya Mbuzi na Kondoo wazunguke zunguke na kuanguka (kizunguzungu). Ni ugonjwa ambao umeibuka na kuwa tatizo kubwa sana kwa wafugaji wa Mbuzi na Kondoo nchini. Ugonjwa huu umekuwepo miongoni mwa wafugaji hasa afugaji wa kabila la Kimaasai kwa muda mrefu sasa. Kila Mmaasai ukimuliza tatizo kubwa kwenye ufugaji wake hatakosa kuutaja ugonjwa huu wa Ormilo. Inakadiliwa kuwa kati ya Mbuzi 100 wanaougua ugonjwa huu 20 hufa. Ugonjwa umekuwa ukijitokeza sana hasa kwa mbuzi na kondoo wenye umri kati ya mwaka mmoja hadi miaka mitatu. Ugonjwa hujitokeza wakati wowote wa mwaka. Ugonjwa huu unaenea kwa njia ya kulisha mbwa vichwa vya Mbuzi na kondoo.

 

Kisababishi cha ugonjwa (Coenurus cerebralis)

Ormilo inasababishwa na lava wa minyoo bapa (Taenia multiceps) ambao huvamia mfumo wa fahamu kwenye ubongo wa wanyama wakiwemo Mbuzi, kondoo, ng’ombe, Nyati, Nguruwe, swala, farasi, ngamia. Wanyama hawa hupata maambukizi kwa kula chakula chenye mayai ya mnyoo bapa (Taenia multiceps). Mayai hayo huwa yametoka kwenye kinyesi cha mbwa na wanyama wengine jamii ya mbwa kama bweha.

Umbwa wakiwa eneo la kuchinjia mbuzi na wanaweza kuokota ubongo au kupewa kichwa cha mbuzi na kisha kuwapata lava wa ugonjwa.

Ugonjwa huu pia humpata binadamu akila vyakula hasa mboga ambazo zimechanganyika na kinyesi cha mbwa. Makao ya minyoo ya ugonjwa huu ni kwenye utumbo mdogo wa mbwa au mbweha.

Dalili za Ormilo

Ugonjwa huu unaweza kujitokeza katika maumbo ya aina mbili: ugonjwa mkali unaoua haraka (acute) na ugonjwa mpole wa kudumu(chronic).

Acute form: Huu hujitokeza kwa kondoo wa wiki 6 hadi 8. Baada ya siku 4 hadi 5 tangu kujitokeza kwa dalili ikiwemo homa, uchomvu, kujipigiza kichwa na kutetemeka, vifo hutokea.

Chronic form: Hii hujitokeza kwa Wanyama wenye umri kati ya miezi 6 hadi 18. Kitendo cha lava kwenda kwenye mfumo wa fahamu (ubongo) kwenda kwenye mfumo wa fahamu huchukua miezi kadhaa. Lava anayeshambulia mfumo wa fahamu akifika kwenye ubongo hutengeneza uvimbe angavu ukiwa na maji (cyst) wenye ukubwa wa kipenyo cha sm 0.3 hadi sm 9.5.

Cyst ikiwa imeshikiliwa na kilole ni angavu na yenye majimaji ndani

Dalili zinazosababishwa na cyst huyo hutofautiana kulingana na eneno cyst ilipo, ukubwa wa cyst yenyewe na mgandamizo wa cyst kwenye ubongo. Mwanzoni cyst husababisha kuta za ubongo kuvimba inayopelekea mfumo wa fahamu kuzorota au kushingwa kufanya kazi kunakopelekea kifo cha mnyama.

Dalili kubwa za ugonjwa huu ambazo huonekana ndani ya miezi 2-8 ya mwanzo baada ya kumeza mayai ya mnyoo huu hujumuisha mfumo wa kutembea.

Kutokana na mgandamizo wa cyst kwenye mfumo wa fahamu (ubongo) mnyama hupinda shingo kuelekea upande cyst ilipo, hutembea kwa kuzunguka (mduara), na kugonga kichwa chake kwenye vitu vyovyote vilivyo karibu naye.

Dalili nyingine ni pamoja na kukosa uzani (balanzi), kizunguzungu, kupooza, kunyonga shingo, kutafuna meno, upofu, kupoteza fahamu na ubongo kupungua ukubwa.

 

 

 

TAZAMA VIDEO YA HATUA YA MZUNGUKO WA MAISHA YA ORMILO HAPA

 

 

 

 

 

.

Leave a Reply