PASIPO CHAKULA BORA HAIWEZEKANI KUPATA FAIDA KUBWA KATIKA UFUGAJI WA KISASA

Pasipo chakula bora haiwezekani kupata faida kubwa katika ufugaji wa kisasaChakulaPasipo chakula bora haiwezekani kupata faida kubwa katika ufugaji wa kisasa

Imeandikwa na: Katabaro, Mugyabuso G (0689494521)

UTANGULIZI
Vyakula ni muhimu sana hasa unapofikiria ufugaji wa kisasa na kibiashara. Vyakula huchangia kuanzia asilimia hamsini (50%) hadi sabini (70%) ya gharama za uendeshaji wa shughuli za ufugaji. Hii ina maana kwamba faida ya ufugaji wako itategemea sana na namna unavyoweza kusimamia ulishaji wa mifugo yako.
Kumbuka huwezi kupunguza gharama ya vyakula kwa kupunguza kiasi kitakiwacho kwa ajili ya wanyama husika, na si maana yangu kuandika haya.
Mchanganyiko wa chakula usio sahihi huongeza gharama kwa maana kwamba wanyama watakula lakini uzaishaji wao hautakuwa sawa na kiwango walacho.
Chakula chenye mchanganyiko ulio sahihi hupunguza gharama kwani kile kiwango cha chakula wapatacho wanyama huzalisha sawasawa. Hivyo mapato yako yataongezeka kwa sababu uzalishaji huongezeka pia.
Wengi hudhani wanapunguza gharama kwa kulisha chakula kisichochanganywa vizuri. Kumbe wanapata hasara kwa uzalishaji mdogo ndani ya muda mrefu.
Kutokana na bei kubwa ya vyakula vitengenezwavyo viwandani wafugaji wengi hasa wadogo na wanaoanza hushindwa kupata ufanisi katika ufugaji wao. Lengo la andiko hili ni kuwasaidia wafugaji njia sahihi ya kutengeza vyakula kwa ajili ya mifugo yao.

TAARIFA MUHIMU UNAZOTAKIWA KUWA NAZO KABLA YA KUANZA ZOEZI
i. Mahitaji ya virutubisho ya mnyama husika. Wanyama huwa na mahitaji tofauti tofauti. Mfano katika kuku kuna mahitaji kwa ajili ya kuku wanaokua, vifaranga, wa-nyama na wanaotaga.
ii. Orodha ya vyakula vyote vinavyopatikana kwa urahisi na vifaavyo kwa ajili ya kulisha Wanyama (angalia; mapungufu, bei na virutubisho ndani yake. Je chakula kinafaa na ghalama yake ni sawa kwa matumizi yaliyopangwa)
iii. Hali ya chakula na utayari wa wanyama kukitumia. Epuka kutumia vyakula ambavyo unajua wanyama hawapedelei sana kuvitumia. Endapo utavitumia usitegemee matokeo mazuri katika uzalishaji.
iv. Uwepo wa vitu vinavyoweza kudhuru afya ama uzalishaji wa wanyama (angalia viwango vya ubora kwa vyakula husika)
v. Matazamio ya ulaji wa wanyama. Hii husaidia kujua kwa kipindi fulani cha ufugaji utahitaji chakula kiasi gani. Kufahamu hii inahitaji kuwasiliana na wataalamu wa sayansi ya wanyama.

MAKUNDI MUHIMU YA VIRUTUBISHO YANAYOHITAJIKA
1. WANGA
2. PROTINI
3. MADINI
4. MAFUTA
5. WANGA
Hivi ni vyakula muhimu kwa wanyama na hutengeneza sehemu kubwa ya mchanganyiko wa chakula. Hutoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa wanyama (mayai, maziwa, nyama na mengineyo). Kazi ya wanga ni kutia nguvu mwilini. Vyakula hivi ni pamoja na mahindi, pumba za mahindi au ngano, mtama, uwele na mihogo na pumba ya mchele. Vyote hivi hufanya kazi moja lakini vyote pia hutofautiana katika ubora wa virutubisho ndani yake. Hivyo katika kuchanganya vyakula unashauriwa kuchanganya zaidi ya kimoja kulingana na urahisi wa upatikanaji wake lakini bila kusahau kwamba kiasi chake katika mchanganyiko kina ukomo kutokana na uwepo wa vitu vinavyoweza kudhuru wanyama. Mfano kama unachanganya kilo mia moja fuata malekezo haya (hasa kwa wanyama wenye tumbo moja kama kuku na nguruwe);
Mahindi yawe kati ya kilo 15 hadi 55 katika mchanganyiko wako (yabalazwe mashineni kwanza)
Pumba ya mahindi kilo 10 hadi 35
Pumba ya mchele isizidi kilo 15
Ngano chini ya kilo 5
Vyakula vinginevyo katika kundi hili la wanga havitakiwi kuzidi kilo kumi kila kimoja endapo vitatumika.

Lengo la kuchanganya ni:
i. Kuhakikisha mapungufu kwenye chakula kimoja yanazibwa na uzuri uliomo kwenye kingine.
ii. Kupunguza ghalama za mchanganyiko. Changanya kwa kuzingatia bei za vyakula husika ili mwisho wa siku tuwe na mchanganyiko uliokamili kwa bei ndogo.
Vyakula vya wanga kwa ujumla vinatakiwa kutengeneza kilo sabini hadi sabini na tano (70-75) za mchanganyiko mzima wa kilo mia moja.

Mfano wa mchannyiko wa wanga:
mahindi kilo 22+pumba mahindi kilo 35+pumba za mchele kilo15= kilo 72

PROTINI
Hivi ni vyakula ambavyo kazi yake ni kujenga mwili na kurekebisha ama kukarabati mwili. Kutokana na kazi yake vyakula hivi huitajika kwa wingi katika mchanganyiko wanyama wanapokuwa katika ukuaji na huitajika kwa viwango vya kawaida ama chini wanyama wanapokuwa wakubwa. Kukosekana kabisa kwa vyakula hivi kwa wanyama wanaokua huweza kuathiri ukuaji na kusababisha wanyama kudumaa na kwa wanyama wakubwa husababisha kudhoofika kwa afya ya wanyama maana hakuna ukarabati katika mwili. Kwa kawaida vyakula hivi ni ghali sana lakini ni muhimu pia. Vyakula hivi ni pamoja na; dagaa, damu ya wanyama, mashudu ya pamba au alizeti, soya, kunde, karanga na korosho. Katika mchanganyilo wako wa kilo mia moja fuata maelekezo haya;
Soya isizidi kilo 25
Mashudu ya pamba yasizidi kilo 20
Mashudu ya alizeti yasizidi kilo 25
Dagaa zisizidi kilo 10
Damu ya wanyama iwe chini ya kilo 5
Ukitumia karanga ama korosho zisizidi kilo 10
Mashudu yasagwe kwanza
Katika mchanganyiko wa kilo mia moja (100) vyakula vya protini inatakiwa viwe kati ya kilo ishirini na ishirini na tano (20-25). Unaweza fanya mchananyiko kufuatana na urahisi na bei ya vyakula husika kwa kuzingatia viwango tajwa hapo juu. Sio lazima viwepo vyote ila waweza pata viwili au hata kimoja ila nasisitiza ZINGATIA VIWANGO NILIVYOTAJA HAPO JUU.

Mfano wa mchanganyiko:
mashudu ya pamba kilo 15+gadaa kilo 5+mashudu ya alizeti kilo 5=kilo 25

MAFUTA
Kazi ya vyakula hivi ni kutia joto na nguvu mwilini. Hivi ni pamoja na mashudu ya alizeti, pamba na karanga. Mchanganyiko wake tayari ulikwisha kutajwa hapo juu hivyo zingatia maelekezo kama yalivyotolewa.

MADINI NA VITAMINI
Kazi ya madini na vitamini ni kubwa na muhimu sana mwilini japo vyenyewe huhitajika kwa kiwango kidogo tu katika mchanganyiko wako. Madini hujenga mifupa, husaidia mmeng’enyo wa chakula, huimarisha mayai na mifumo ya fahamu kwa wanyama. Vitamini husaidia kulinda na kupambana dhidi ya magonjwa katika mifugo. Katika mchangako wa kilo mia moja tumia kilo mbili (2) za madini na vitamin (za viwandani). Lakini pia waweza tumia vyanzo asilia kwa ajili ya wanyama wako. Hivi ni pamoja na;
Dengu, chokaa, mifupa
Majani mabichi ya mipapai, kunde michicha na mengineyo

CHUMVI
Hii ni muhimu lakini haitakiwi kuzidi nusu kilo (0.5) katika mchanganyiko wa kilo mia moja. Ni muhimu kuwa makini maana ukizidisha kiwango huweza kuleta madhara makubwa katika uzalishaji wa mifugo yako.

MFANO WA JUMLA:
wanga kilo 72+protini kilo 25+madini kilo 2+chumvi kilo 0.5=99.5kg

JINSI YA KUCHANGANYA
Tafuta sehemu nzuri (isiwe kwenye mchanga ama udongo) yaweza kuwa kwenye karatasi kubwa ama sakafuni. Kabla ya kuchanganya vyakula vyako hakikisha vimekauka vizuri kwa kuanikwa juani. Unapochanganya anza kwa kutandaza wanga chini alafu protini ifuate na mwisho madini juu. Changanya kwa ukamilifu na uhakikishe hilo.

HITIMISHO
Kama nilivyosema mwanzo lengo la kuwa na mchanyanyiko wa vyakula ni kutumia gharama ndogo katika chakula lakini uwe na uzalishaji wa hali ya juu. Na kabla hujaanza kutengeneza cahakula cha mifugo yako ni lazima kuorodhesha vyakula vyote vipatikanavyo katika mazingira yako pamoja na bei yake ili unapoanza uchague kutumia vyakula ambavyo vina bei nafuu na vinapatikana kwa urahisi kama nilivyoeleza huko juu.
Mchanganyiko ulio sahihi utaongeza uzalishaji wa mifugo na hivyo kuongeza faida kwa kiwango cha juu kabisa.

PASIPO CHAKULA BORA HAIWEZEKANI KUPATA FAIDA KUBWA KATIKA UFUGAJI WA KISASA.

Leave a Reply