Na: Farida Mkongwe
“Kimsingi hakuna tofauti kubwa wala athari kubwa sana za ufugaji wa samaki wakati wa kiangazi ukilinganisha na wakati wa masika, tofauti zilizopo ni ndogo ndogo ambazo kitaalamu hazina madhara makubwa kwa mfugaji”, hivi ndivyo anavyoanza kusema Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Wanyama iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dr. Berno Mnembuka ambaye pia ni mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji.
Watu wengi wamekuwa wakijiuliza swali hilo la tofauti za kiufugaji wakati wa kiangazi na wakati wa masika wakihusisha na shughuli za kilimo ambazo ufanisi wake umekuwa na tofauti kubwa katika misimu hiyo miwili.
Mtaalamu huyu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka anaweka bayana tofauti ndogo zilizopo ambapo anasema tofauti ya kwanza ni “ulaji wa chakula wa samaki na ukuaji wao”. Kimsingi ujoto wa maji katika bwawa unapelekea ongezeko la uchangamfu wa samaki na hamu ya ulaji wa chakula, kama ilivyo kwa viumbehai wengine, ulaji wa chakula kwa samaki humuwezesha kupata viinilishe vinavyomsaidia kukua na kuzaliana, hivyo basi hali ya ubaridi uliopo msimu wa mvua unapunguza kwa kiasi fulani ulaji wa samaki na hivyo kumpunguzia ukuaji kwa kiasi kidogo.
Tofauti ya pili ni “uwezekano wa magonjwa na matatizo mengine ya kiafya kwa samaki”. Hali ya ubaridi uliyokithiri wakati wa mvua unaweza kupelekea kujitokeza kwa mashambulizi ya vimelea vya kuvu au fangasi na mara nyingi mashambulizi haya huleta athari za nje kwa samaki na kupelekea usumbufu tofauti na kipindi cha kiangazi, hata hivyo mashambulizi haya hayapunguzi sana ukuaji na uzalishaji wa samaki.
Upatikanaji wa maji na ubora wake ni jambo la msingi hapa. Ni dhahiri kuwa msimu wa mvua maji huwa mengi hivyo mfugaji ana uwezo wa kuyaboresha kwa ufanisi zaidi kwa mfano kuyaruhusu yatoke kwenye bwawa na kujaza mengine na pia upotevu wa maji ardhini unakuwa ni mdogo ukilinganisha na wakati wa kiangazi.
Tofauti nyingine ndogo iliyopo ni “uchafuzi wa maji yanayoingia kwenye mabwawa ya kufugia” anaeleza Dr. Mnembuka. Wakati wa mvua kunakuwa na mtiririko wa maji chini na juu ya ardhi. Wakati mwingine maji yanayotiririka chini ya ardhi yanaweza kuwa chanzo cha uchafuzi wa maji yaliyopo kwenye mabwawa, uchafuzi huu unaweza usiwe tatizo kama kutakuwa na zoezi endelevu la ukaguzi wa ubora wa maji katika mabwawa, kuna uwezekano wa kufuatilia na kuondoa tatizo.
Kwa kuhitimisha makala hii naweza kusema kuwa kwa kuzingatia tofauti za kimazingira za kufugia na tofauti za kibaiolojia ya samaki ni kweli zipo tofauti za ufanisi wa ufugaji kati ya msimu wa masika na msimu wa kiangazi lakini kwa kutumia ushauri wa wataalamu mbalimbali wakiwemo wale wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA mfugaji anaweza kuboresha huduma zake na kuondoa tofauti hizo na hivyo kumuwezesha kupata faida katika misimu yote.
Na huu ndiyo mwisho wa sehemu ya pili ya makala hii, endelea kufuatilia makala zinazofuatia za ufugaji wa samaki zenye kichwa “ufugaji wa samaki hatua kwa hatua”.
CHANZO: SUAMEDIA