Serikali itafute suluhisho la kudumu migogoro ya wakulima na wafugaji

ByChengula

Sep 24, 2015

 

 

Katika siku za karibuni kumeibuka tena taarifa za vurugu kati ya wakulima na wafugaji katika wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Hivi karibuni kulikuwa na taarifa za kuuawa ng’ombe 68 na kujeruhi 108 ikiwa mwendelezo wa mapambano kati ya wakulima na wafugaji kwenye eneo hilo.

Kujirudia kwa vurugu hizi ni jambo la kusikitisha kwani linazua maswali mengi kuhusu utendaji wa viongozi wa vyombo vya dola kwenye eneo hilo.

Ugomvi kati ya wakulima na wafugaji kwenye eneo hilo ni wa miaka mingi lakini katika hali ya kushangaza hakuna ufumbuzi wa kudumu juu ya tatizo hilo.

Suala hili limeongelewa sana kwenye duru za serikali na hata vikao vya Bunge lakini katika hali ya kushangaza kumekuwa hakuna ufumbuzi wa mgogoro huu.

Mgogoro huu wa Mvomero haujaanza leo,  ni wa miaka mingi, lakini jambo linalosikitisha ni kuwa suala hili limekuwa likichukuliwa kisiasa zaidi. Imetokea kila mara katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu viongozi wanakuja na ahadi nyingi za kutatua mgogoro huo kati ya wakulima na wafugaji.

Hata hivyo, viongozi hao wanapopewa dhamana husahau ahadi zao za kumaliza mvutano na badala yake damu imekuwa ikiendelea kumwagika kwenye eneo hilo.

Mgogoro wa Mvomero siyo pekee hapa nchini, kwani kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji kwenye maeneo mengine mbalimbali.

Mathalani, katika wilaya ya Kilosa ambayo iko mkoani Morogoro na pia Kiteto, mkoani Manyara na Handeni mkoani Tanga.

Kushindwa kupatiwa ufumbuzi kwa migogoro hii kunadhihirisha jambo moja tu kuwa kuna udhaifu mkubwa wa kiutendaji miongoni mwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza maeneo hayo.  Haiwezekani eneo lenye mkuu wa mkoa au wilaya, makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya na watendaji wa kuajiriwa wa serikali wanashindwa kupata dawa ya matatizo hayo.

Jambo moja ambalo linafanya watu wajiulize maswali mengi ni kuwa, serikali haina dhamira ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo haya au ni uzembe wa utendaji wa viongozi wa maeneo hayo. Ifike wakati sasa kwa viongozi wa kisiasa na serikali kuhakikisha wanakuja na majibu ya kutatua matatizo hayo.

Serikali inapaswa kuja na sera inayoeleweka juu ya masuala ya ardhi na hasa sheria na kanuni za kuendesha sekta za kilimo na ufugaji. Lazima kuwapo na sheria za kulinda wakulima na mazao yao, lakini pia kwa upande wa wafugaji pawekwe taratibu za kuwaongoza. Kwa mfano, suala la wafugaji kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kutafuta malisho ya mifugo linapaswa kuwekewa utaratibu wa kitaifa.

Kitu kikubwa kinachokwamisha ni kuwa viongozi wachache wenye tamaa wamekuwa wakinufaika na migogoro hii aidha kwa kushirikiana na wakulima au wafugaji.

Bila kuwekwa kwa utaratibu ni ndoto kwa migogoro hii kumalizika na badala yake damu itaendelea kumwagika kwa kuwa hakuna ufumbuzi.

Ni fedheha kubwa kwa nchi kama Tanzania inayojivunia kuwa ina amani na utulivu wakati kuna wananchi wake wanauana kwa migogoro ya ardhi.

Serikali lazima ije na ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hii ili kuhakikisha kuwa maeneo yenye vurugu watu wake wanaishi kwa amani na kuendesha shughuli zao na hili litafanikiwa ikiwa viongozi na vyombo vya dola vitatimiza wajibu wao ipasavyo.

CHANZO: NIPASHE, 23rd September 2015

Leave a Reply