Ufugaji wa kuku wa mayai hatua kwa hatua: utangulizi

Utunzaji wa kuku wa mayai wanaokaribia na wanaoanza kutaga (Wiki ya 12-20)

Umri huu ni wa kuku wanaojulikana kama matetea vijana ( “pullets “) walioko kwenye kipindi cha mpito cha ukuaji kuelekea umri wa kuku wanaotaga. Katika umri huu matetea vijana yanahitaji kupewa chakula na maji na nafasi ya kutosha kulingana na maumbile yao kuongezeka. Wapewe chakula na maji ya kutosha ili wawe watagaji wazuri wa mayai wafikiapo umri wa kutaga. Epuka kuweka kuku wengi katika eneo dogo.

Anza kuchunguza uzito wa kuku wako kwa kuwapima baadhi ya kuku ndani ya nyumba yao. Hii inaweza kufanywa kwa kuwanyua matetea yako kwa mikono ili kuona uzito wao unaendeleaje. Uzito wa kuku ni muhimu sana kwenye utagaji wa mayai.

Kuku wanapofikia umri wa wiki 16 wahamishiwe kwenye vizimba au nyumba ya kulelea kuku wa mayai. Matetea vijana wanaweza kuanza kutaga yai moja moja kuanzia wiki ya kumi 18. Mayai haya mara nyingi huwa madogo na wengi wamekuwa wakidhani yametagwa na jogoo kitu ambacho si kweli.

NB: Ni muhimu kuwatunza matetea vijana hasa kwa kuangalia swala la chakula na mwanga  kwani huathiri kiasi na ubora wa mayai yatakayotagwa hapo baadaye wakishaanza kutaga.

Mwanga

Ukiona matetea vijana yanaanza kutaga, taratibu ongezea muda wa mwanga hadi kufikia muda wa saa 14 kwa siku. Hii husaidia kuwaingiza kuku wako kwenye utagaji. Muda wa mwanga utaongezeka kufikia saa 16 wakishafikisha umri wa utagaji ili kusaidia utagaji. Mwanga ni muhimu sana kwa kuku wa mayai kwani husaidia waingie kwenye utagaji na waendelee na utagaji muda wote hasa mchana unapoonekana kuwa mrefu. Na huu unaweza kuongezwa kwa kutumia mwanga wa taa za umeme au chemli pale giza linapoingia ili masaa ya mwanga yanayohitajika yaweze kufikiwa. Kwa ufugaji mdogo balbu ya wati 60 inatosha na unaweza kuongeza idadi kulingana na uwingi wa kuku wako.

Chakula

Kuku ili anahitaji mlo kamili kama ilivyo kwa binadamu na wanyama wengine. Chakula hiki unaweza kukinunua dukani kilichotengeneza kwa mchanganyiko maalumu kufanya mlo kamili au ukachanganya mwenyewe kwa kutumia kanuni uliyoitengeneza mwenyewe au uliyotengenezewa. Kwa aina yoyote utayochangua zingatia ubora wa chakula maana hata cha dukani wakati mwingine hakifanyi vizuri kulingana na watengenezaji wengine kutokuzingatia ubora wa chakula wanachotengeneza. Upungufu wa virutubisho kwenye chakula utaathiri ukuaji wa matetea yako na utagaji wa mayai huko mbeleni. Wanapoanza kutaga na wanapotaga kalsiamu huwa muhimu sana kwenye chakula kwa ajili ya kuimarisha maganda ya mayai.

Natumai ndugu mfuatilia wa elimu hii ya ufugaji wa kuku wa mayai hatua kwa hatua umenufaika na hatu hii ya nne. Endelea kufuatilia hatua ya tano ya ufugaji wa kuku wa mayai itakoyohusu utunzaji wa kuku wanaotaga.

Leave a Reply