KinengunenguKinengunengu

-Usafirishaji na upokeaji wa vifaranga

Endapo unanunua vifaranga hakikisha una namba sahihi na kwamba vifaranga wanauwiano sawa, wapo hai na wachangamfu na hawana matatizo yeyote na kitovu hakina dalili za ugonjwa. Vifaranga wasafirishwe kwenye gari lenye hewa lisiloruhusu jua au mvua. Maboksi yatakayotumika kuwekea vifaranga lazima yaruhusu hewa kupita.

Vifaranga wasafirishwe toka ulipowanunua moja kwa moja kwenda shambani au eneo unalotaka kufugia bila kusimama pasipo na sababu. Wafikapo shambani au kwenye nyumba ya vifaranga, vifaranga wakiwa kwenye maboksi washushwe kutoka kwenye gari au chombo cha usafiri hadi kwenye nyumba yao.

Vifaranga watolewe kwenye maboksi kwenda eneo la kulelea (kinengunengu/kizimba). Kwa uhalisia vifaranga wanatakiwa wafikishwe kwenye nyumba ya kulelea (kinengunengu) kati ya massa 6 hadi 12 baada ya kuanguliwa ili kupunguza madhara kwa vifaranga.

Utunzaji wa vifaranga wa kuku wa mayai (Siku ya 1 hadi wiki 6 au 8)

Matunzo ya vifaranga huanza mapema sana mara baada ya kupokelewa kwenye nyumba yao. Hatua hii ya utunzaji wa vifaranga wakiwa wadogo inajulikana kwa jina la kiingereza kama “Brooding” ikiwa na maana vifaranga wanalelewa kwenye eneo lao maalumu liitwalo ‘brooder’ au kinengunengu au kwenye vizimba (cages). Matunzo haya huanza siku ya kwanza baada ya kuanguliwa hadi wiki ya sita au nane.

Eneo la kulelea vifaranga lazima liwe na nafasi ya kutosha kwa idadi ya vifaranga utakavyo weka (wasizidi 25 kwa mita moja ya mraba) kuepuka msongamano. Vifaranga waruhusiwe kusambaa nyumba yote baada ya wiki tatu (3) tangu kuanguliwa.

Maji

Vifaranga wakiwa kwenye eneo la kulelea wapewe maji ya kunywa muda wote. Inashauriwa kuongeza Glukosi na vitamini kwenye maji ya kunywa ili kuwaongezea nguvu na kusaidia kukabiliana na msongo unaotokana na safari. Pia unaweza kuchanganya mafuta ya taa kidogo kwenye maji ili kusaidia kinyesi kipite vizuri. Osha vyombo vya maji kila siku kwa maji safi, sabuni na dawa ya kuulia vimelea vya magonjwa. Hakikisha vyombo vimejazwa maji mara baada ya kuonshwa na hakikisha maji yanapatikana muda wote. Hata siku moja usiache vyombo vikiwa havina maji.

Chakula

Hakikisha unanunua chakula toka kwa wauzaji wenye uhakika wa ubora wa chakula muda wote. Epuka kuchanganya chakula toka kwa wauzaji tofauti tofati. Katika masaa 48 ya kwanza, chakula kisambazwe vizuri kwenye karatasi au kwenye vyombo vya kulishia (trei au mifuniko) ambavyo huwekwa maeneo tofauti tofauti ya eneo la kulelea vifaranga. Hii hufanya chakula kipatikane kwa urahisi kwa vifaranga wote. Angalau trei au mfuniko mmoja unaweza kutosha vifaranga 50. Wakati huu wa ukuaji (hadi wiki ya 8), vifaranga wapewe chakula cha vifaranga (“Chick mash”)

Joto

Wakati huu wa kulea vifaranga ni muhimu kuhakikisha kuwa joto linalostahili kwa vifaranga lipo muda wote kulingana na umri wao. Jedwali hapa chini linonyesha na joto linalotakiwa ndani ya nyumba nae neo la kulelea vifaranga.

Umri (Wiki) Joto (ºC) ndani ya kinengunengu Joto (ºC) ndani ya nyumba
1 33-35 30-32
2 30-32 27-29
3 27-29 24-26
4 24-26 21-23

Joto lazima litazamwe mara kwa mara kuona kama lipo sawa kwa kutumia vifaa vya kupimia joto vilivyowekwa kwenye eneo la kulelea vifaranga. Kielelezo hapa chini kitakusaidia kujua kama joto lipo sawa au la ndani ya kilelea vifaranga.

Joto sahihi           Joto kali mno         Joto halitoshi (Baridi)

Kukiwa na joto ambalo si sahihi kwa vifaranga, utasikia keleleze nyingi kuonyesha kuwa haviridhisshwi na hali ya joto iliyopo. Na mara nyingi unaweza kuona baadhi ya dalili zifuatazo endapo joto halipo sawa:

-Joto dogo

  • Vifaranga watanyongeka na baridi na kukusanyika pamoja ili ktafuta joto
  • Kinyesi chao kitakuwa cha majimaji na hugandamana maeneo ya karibu na kutolea kinyesi

-Joto kali

  • Vifaranga hunyong’onyea wakiwa wamelala vichwa na shingo zao zimenyooka
  • Vifaranga huhema kwa haraka na huonekana kuishiwa pumzi
  • Hunywa maji mengi yanayopelekea kujaa kwa tumbo na maji ya ziada
  • Vifaranga hukaa mbali na chanzo cha joto na hutafuta sehemu ambazo zinaunafuu wa joto
  • Mara nyingine husogea na kugusa vyombo vya maji
  • Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha joto la kuku linalotakiwa lipo muda wote kuondoa msongo joto unaopelekea ongezeko la vifo, ukuaji duni unaopelekea utofauti wa ukuaji na matatizo ya maji kujaa tumboni.

 

Hewa

Muda wote wa uleaji vifaranga hakikisha mzunguko wa hewa safi upo kwenye nyumba na eneo la kulelea vifaranga. Mzunguko wa hewa husaidia kuondoa ammonia kutoka ndani ya nyumba na kuhakikisha malalio ni makavu na hivyo kupunguza uwezekano wa maambukizi ya maonjwa. Lakini pia hewa safi husaidia vifaranga wako wakue vizuri’

Mwanga

Mwanga ni muhimu kwa uleaji wa vifaranga lakini si tishio kwa vifaranga ukikosekana. Maeneo yasiyo na umeme vyanzo vingine vya mwanga kama taa ya mafuta au chemli vinaweza kutumika. Kuku wa mayai wanakuwa makini na mabadiliko ya masaa ya mwanga na kuathiri muda wao wa kuanza utagaji na ulaji wa chakula.

Muda mrefu wa mwanga husaidia kuku wale sana na kuongeza ukuaji wao. Hivyo inashauriwa kuwapunguzia mwanga wat aa taratibu hasa wiki saba za mwanzo kabla ya kuwaacha na mwanga wa asili. Fuata kielelezo hiki hapa chini kwa swala la mwanga kwa vifaranga wako.

Umri (wiki) Masaa ya mwanga
1-2 23 kwa siku 2-3 kisha masaa 22
3 22
4 20
5 18
6 16
7 14

Leave a Reply