Ufugaji wa kuku wa mayai hatua kwa hatua: hatua ya tano

Utunzaji wa kuku wanao taga (Wiki 20-120)

Kama tulivyoona kwenye hatua ya nne ya ufugaji wa kuku wa mayai, kuku wa mayai wanaweza kuanza kutaga yai moja moja na wakati mwingine likiwa na umbo dogo kuanzia wiki ya 18. Lakini kwa kawaida utagaji halisi huanza kuku wa mayai wanapofikisha umri wa wiki 20, na hapa ndipo matumizi ya kuku wa mayai linatakiwa lianze kutumiwa.

Kuku wakiwa kwenye umri huu wanatakiwa wawe wamekwisha hamishiwa kwenye nyumba ya kutagia mayai kama ni ufugaji wa sakafuni au kwenye vizimba. Tumeona kwenye hatua ya nne ya ufugaji wa kuku wa mayai kuwa kuku wanatakiwa wahamishiwe kwenye nyumba ya kuku wa mayai wakifikisha umri wa wiki 18 ambapo utagaji huanza kujitokeza.

Hakikisha unawaondoa kuku wote wenye dalili za ugonjwa au wale ambao ukuaji wao sio mzuri yaani ni wa taratibu.

Mahitaji ya kuku wanaotaga

  1. Chakula chenye mchanganyiko wa protini asimia 18, na maji yawepo muda wote. Epuka kubadilisha ghafla fomula ya chakula cha kuku wa mayai kwani itapelekea kupunguza utagaji. Hakikisha vyombo vya chakula na maji vinakuwa safi muda wote kuepusha maambukizi ya magonjwa.
  1. Wakati huu wa utagaji kuku wa mayai wanahitaji mwanga kwa muda wa masaa 14 mfululizo. Kwa kawaida mwanga wa asili ni kati ya masaa 10-12, hivyo inakulazimu kuongeza masaa 2-4 ya mwanga usio wa asili (umeme au chemli) kulingana na kipindi cha mwaka. Kuna msimu mchana unakuwa mrefu kuliko usiku na kuna wakati usiku unakuwa mrefu kuliko mchana.

Ni lazima masaa 14 ya mwanga vipindi vyote hivi yatimie. Kama unatumia balbu za umeme kwa ajili ya mwanga, basi tumia balbu moja ya wati 50 kwa kila kuku 100. Kama nilivyoeleza kwenye hatua ya nne, mwanga ni muhimu kuwafanya kuku wako waanze kutaga au watagie vizuri na pia kuruhusu kuku wako wawe na muda mwingi wa kula chakula. Hivyo mwanga si swala la kupuuza hata kidogo kwa ufugaji wa kuku wa mayai.

  1. Kelele si rafiki kwa kuku kwani hupelekea kushuka kwa utagaji, kelele huwapa msongo wa mawazo. Hivyo ni vema jitihada za maksudi zikachukuliwa kuhakikisha kelele zilizopitiliza haziwafikii kuku wako. Hili linapaswa kuzingatiwa tangu mwanzo wa utafutaji wa eneo la kufugia kuku wako wa mayai. Nyumba ya kuku wa mayai ni vizuri ikawa eneo lenye utulivu.
  2. Kama unafanya ufugaji wa sakafuni, hakikisha una eneo la kutosha kwa ajili ya kutagia mayai. Hili si tatizo kwa kuku wa mayai walio kwenye vizimba maana vizimba vina eneo maalumu la kudondoshea mayai punde kuku atagapo. Eneo lenye ukubwa wa nchi 2 x 6 kwa kila kuku 100 linatosha kukishi mahitaji ya kuku wa mayai.

Hakikisha unakusanya mayai mara mbili kwa siku, mara moja asubuhi na nyingine jioni. Mayai yatunzwe eneo la ubaridi kama hayatauzwa au kutumiwa siku moja baada ya kukusanywa.

Mbolea na damu kwenye maganda ya mayai yanaweza kuoshwa na maji. Ni vema mara baada ya kuyaosha mayai yawekwe kwenye friji ili kuzuia maambukizi ya vimelea vya magonjwa kama Salmonela.

  1. Kuku wa mayai wanahitaji nafasi ya kutosha kwenye nyumba yao, angalau mita za mraba 0.6 kwa kila kuku zinatosha. Kwa mfano kama una kuku 500 wa mayai watahitaji mita za mraba 300. Hapa unazidisha 0.6 kwa idadi ya kuku wa mayai ulionao unapata eneo watakalo hitaji. Hakikisha nyumba ya kuku hairuhusu maji kuingia hasa wakati wa mvua. Unaweza pia kuwa unawaruhusu kuku wako kukaa nje ya nyumba yao muda mwingi hasa wakati wa mchana. Lakini eneo hilo linaweza kuzungushiwa fenzi ya waya au tofali na juu ikawa na nyavu kuzuia ndege wasiwadhuru.
  2. Kuku wa mayai wanaweza kuondolewa kwenye mzunguko wakati wowote ule. Kuku wasiotaga vizuri wanaweza kuondolewa maana watakuingizia gharama kubwa bila sababu. Baadhi ya dalili za kuku wasiotaga vizuri ni pamoja na kusinyaa kwa undu (comb)/ufito (wattle), mwili mwembamba na uliokonda na kutokuwa na uchangamfu. Hivyo ni vizuri kuwachunguza kuku wako kila siku ili kubaini ni wapi si watagaji wazuri waweze kuondolewa.

Zingatia: Unapoona kumekuwa na kuku wengi wanaohitaji kuondolewa ni dalalili tosha kuwa kuna tatizo kwenye kuku wako linalohitaji uangalizi wa karibu na mtaalamu wa mifugo na linalohitaji utatuzi wa haraka.

Leave a Reply