Ufugaji wa mbuzi wa maziwa: mwanzo – mwisho

Aina za Mbuzi wa Maziwa

Aina ya mbuzi anayepatikana sehemu nyingi nchini ni Small East African Goat na hutoa kiwango kidogo sana cha maziwa. Hata hivyo mbuzi hawa wanaweza kuzalishwa na mbuzi wa kigeni ili kupata mbuzi wa aina ya hali ya juu wanaotoa maziwa mengi na wenye uwezo wa kustahimili magonjwa na hali ya hewa ya hapa nchini.

Aina ya mbuzi wa kigeni wanaopatikana nchini ni kama vile:

 • Toggenburg, Boer, Saanen, British Alpine, German Alpine, Anglo Nubian, Angora na Oberhauzen.
 • Aina hizi zote za mbuzi hustahimili aina tofauti ya hali ya hewa na huhitaji mazingira tofauti ya ya kuwafuga.

Ikiwa unataka kufuga mbuzi wa maziwa ni bora kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wa mifugo katika eneo lako ili wakufahamishe aina nzuri ya mbuzi wanaopatikana na mbinu nzuri za kuwazalisha zinazopatikana nchini.

Jinsi ya kuwalisha Mbuzi wa Maziwa

Ni muhimu kufahamu kuwa chakula unachomlisha mbuzi wako ndicho kitakachotengeneza maziwa hivyo basi ni muhimu:

 • Kumpa mbuzi chakula katika mazingira ya usafi kwa sababu:
  o     Mbuzi hula kila aina ya chakula hivyo usiwaruhusu kula chakula kilicho na mchanga
  o     Hali hii huwazuia kuambukizwa minyoo wanaopatikana kwenye mchanga
 • Mbuzi wa maziwa kwa mara nyingi hufugiwa kwenye zero grazing hivyo basi kumbuka kuwatengezea mahali pa kulia chakula na kunywea maji ambapo panahitajika kuwa juu na mbali na nyumba za kulala ili wasikanyage,au kuchafua chakula
 • Mbuzi mwenye uzani wa wastani huhitaji takribani kilo 500 za chakula chenye virutubisho muhimu ama nyasi zilizokaushwa kwa mwaka huku kiwango cha kila siku kikiwa asilimia 5-7 ya uzito wake
 • Majani ya mahindi au mtama, mboga zisizotumiwa na majani ya viazi yanapaswa kukatwakatwa ili kurahisisha ulaji wake.
 • Ondoa chakula ambacho hakijatumiwa kutoka bandani mara mbili kwa siku. Ikiwa mbuzi wako hubakiza chakula kingi hii ni ishara ya kuwa chakula ni duni, ama kupewa chakula kingi kupita kiasi, ama mbuzi wako hawana hamu ya kula chakula kwa sababu wana tatizo kama vile la minyoo
 • Wape maji safi ya kumywa kwa wingi kama lita 5 kwa kila mbuzi wa maziwa kwa siku
 • Waweza kuwapa mbuzi nafaka kama njia ya kubadilisha na chakula cha kawaida lakini kumbuka kubadilisha polepole wala si mara moja ili kuwaruhusu mbuzi kuzoea chakula kipya bila kuwadhuru. Lakini jihadhari usiwape mbuzi nafaka tupu kwani zaweza kusababisha matatizo ya tumbo
 • Waweza kuwanyweesha mbuzi maziwa ya ng’ombe katika kiwango cha nusu lita kwa mbuzi asiyekamuliwa na lita moja kwa mbuzi wa kukamuliwa
 • Walishe mbuzi madini muhimu kulingana na kiwango cha maziwa wanachotoa

 

Magonjwa yanayowakabili Mbuzi wa Maziwa

Hakikisha unawachunguza mbuzi wako mara kwa mara na kuwapa chanjo ili kuwakinga dhidi ya magonjwa, wadudu hatari na kuwalisha vyakula bora viliyvo na madini muhimu.

Baadhi ya magonjwa yanayowakabili mbuzi ni kama vile:

 • Ugonjwa wa maji moyo (Heart Water)
  o  Huu ni ugonjwa wa bakteria unaosababishwa na kupe
  o  Hata mbuzi wanaofanyiwa zero grazing wanaweza kupatwa na ugonjwa huu.
  o  Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kufa kwa mbuzi wengi haswa wachanga, kupoteza hamu ya kula chakula, matatizo ya kupumua,na mara nyingi mbuzi huwa mnyonge.
  o  Ukiona dalili kama hizi mwite dakatari wa mifugo mara moja
  o  Waoshe mbuzi wako mara kwa mara ili kuwakinga dhidi ya kupe
 • Homa ya Mapafu (Contagious Caprine Pleuropneumonia, CCPP)
  o  Ni ugonjwa wa kuambukiza mbuzi wakati mbuzi wenye afya nzuri wanapokaribiana na wale wagonjwa
  o  Dalili za nyumonia ni kama vile ongezeko la joto mwilini na matatizo ya kupumua na vifo kwa wingi haswa katika maeneo ambao ugonjwa huu umeenea
  o  Ukiona dalili hizi mwone daktari wa mifugo
  o  Wape chanjo mbuzi wako mara kwa mara
  o  Zingatia marufuku ya kusafirisha mifugo yako na uhakikishe kuwa wanyama wamechunguzwa kabla ya kuwasafirisha ama kuhamishwa
 • Ugonjwa wa Kiwele (Mastitis)
  o Kiwele au matiti huvimba na kuwa na maumivu na maziwa huwa na damu
  o Ugonjwa huu waweza kuzuiliwa kupitia kudumisha usafi haswa wakati wa kukamua maziwa
  o Madaktari wa mifugo watakupa dawa ya kupaka katika sehemu zilizoathiriwa. Endapo mbuzi wako huambukizwa ugonjwa huu mara kwa mara ni vizuri umpe matibabu ya kutosha kulingana na ushauri wa daktari
 • Homa ya bonde la Ufa (Rift Valley Fever)
  o  Huu ni ugonjwa wa unaosababishwa na virusi vinavyosambazwa na mbu na hutokea sana sana wakati wa mvua nyingi wakati mbu wanapozaana kwa wingi.
  o  Watu na mifugo wanaweza kuambukizwa kwa kukanyaga kinyesi ama mkojo wa wanyama wagonjwa na kupitia kula ama kukanyaga nyama mbichi
  o  Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa ya ghafla, kukosa hamu ya kula, kutoka kwa makamasi yaliyo na usaha puani,kutokwa na jasho jingi, kuhara, vifo visivyo vya kawaida kwa wanyama wachanga na kutoka/kuharibika kwa mimba
  o  Dalili hizi za ugonjwa huu hufanana na zile za magonjwa mengine na unapaswa kumwita daktari wa mifugo ili akuthibitishie
  o  Ugonjwa huu unaweza kuzuilika kupitia chanjo na kuwazuia mbu
 • Minyoo
  o Hawa ni wadudu wanaokaa kwenye tumbo la mbuzi
  o Huathiri uchangamufu wa mbuzi hususan wale wadogo ambao hufa ikiwa minyoo watakuwa wengi
  o Wakati minyoo wanapozaliana na kuwa wengi henda kwenye mapafu na wanaweza kusababisha matatizo ya kupumua
  o Minyoo wanaweza kuzuiliwa kwa kuwapa mbuzi dawa ya kuua minyoo mara kwa mar ana vema ifanyike kila baada ya miezi mitatu. Lakini ni muhimu kupata ushauri wa daktari wa mifugo kabla ya kuwapa dawa kwani dawa zingine huua aina nyingi ya minyoo huku zingine zikiangamiza aina moja pekee.
 • Kupe, Chawa, Viroboto
  o Kupe huambukiza mbuzi magonjwa na ni vyema kuyazuia magonjwa haya
  o Wadudu kama vile viroboto, chawa hufyonza damu na kuwasumbua mbuzi na kuwaathiri
  o Tafuta ushauri kutoka kwa daktari wa mifugo kuhusu dawa unayopaswa kutumia kuwaua kupe, chaw ana au viroboto katika eneo lako

 

Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye ufugaji wa mbuzi wa maziwa

 • Maziwa ya mbuzi ni mazuri na yana madini muhimu kwenye mwili hivyo basi kila mmoja apaswa kuyatumia.
 • Ufugaji wa mbuzi wa maziwa ni uwekezaji mzuri haswa kwa wakulima wenye mashamba madogo.
 • Maziwa ni chakula muhimu chenye madini muhimu mwilini na pia ndiyo njia mojawapo ambayo watu huambukizwa magonjwa haswa kwa kupuuza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatia.
 • Ukulima ni sawa na biashara na biashara nzuri lazima iwe na mpangilio mzuri haswa kwa matumizi ya pesa zinazopatikana. Ikiwa hutakuwa na matumizi mazuri ya pesa hizo inaweza kukuwia vigumu kununua vitu muhimu ili kuendeleza biashara hiyo. Hivyo kumbuka kuweka rekodi ili kujua ikiwa unapata faida au hasara na ili kuweza kubaini matatizo yanayoikumba biashara yako.
 • Kupitia kwa kuunda makundi ya wakulima, wakulima hao watafaidika na kupigania kupata bei nzuri ya bidhaa zao pamoja na uimarishaji wa sera za mifugo ili kuwawezesha kufanya biashara yao chini ya usaidizi mzuri toka serikalini
 • Tanzania ni mojawapo ya mataiafa yaliyo na watumishi wa umma waliohitimu mafunzo ya mifugo na kupata elimu nzuri lakini wafugaji wengi huwa hawawatumii wataalamu hawa ipasavo. Utafanikiwa kufuga mbuzi wako vizuri na kupata matokeo chanya endapo utabadili namna unavyofuga kwa kuwashirikisha wataalamu hawa walio kwenye eneo lako.

Matatizo yanayowakumba wafugaji wa Mbuzi wa maziwa nchini

Watanzania wengi hufuga mbuzi kwa ajili ya nyama na kwa sababu za mila na tamaduni hivyo basi kufanya ufugaji wa mbuzi wa maziwa kubaki nyuma.

Ufugaji huu wa mbuzi hukabiliwa na vizuizi vingi vya utamaduni ambavyo lazima viepukwe ili ufugaji huu uweze kuwa na tija.

Baadhi ya matatizo yanayokumba ufugaji wa mbuzi wa maziwa ni kama vile:

 • Baadhi ya mila na tamaduni za jamii fulani kupinga unywaji ama utumiaji wa maziwa ya mbuzi
 • Kufuga mbuzi ndani ya nyumba ni mbinu ya kilimo inayohitaji pesa nyingi na hivyo basi kufanya bidhaa za mbuzi kuhitaji soko lililo tayari na lenye bei nzuri ili kumnufaisha mkulima
 • Huwalazimu wakulima wenye eneo dogo la shamba kuwatafutia mbuzi malisho na kununua vyakula vinavyouzwa madukani badala ya kuwafanyia zero grazing jambo linalofanya ufugaji huu kuwa mgumu
 • Mbuzi huzaliana kwa njia ya kawaida hivyo basi kuwepo kwa ongezeko la mbuzi hao kuambukizana magonjwa kama vile ugonjwa wa brucella ambao unaweza kuangamiza mbuzi wako.
 • Aina nyingi ya mbuzi huwa wa asili ya maeneo yaliyo na baridi na yale yenye joto kadiri na hivyo basi kuwa vigumu kwa mbuzi hawa kufugwa katika maeneo kame na yenye joto jingi.
 • Licha ya matatizo mengi yanayokumba ufugaji wa mbuzi wa maziwa, wakulima wanaotaka kufuga mbuzi lazima washirikiane kueneza elimu ya umuhimu wa maziwa ya mbuzi na kuyafanya yatambulike.

 

Mbinu za kueneza elimu ya umuhimu wa maziwa ya mbuzi

 • Kuelimisha watu kuhusu umuhimu wa maziwa ya mbuzi na iwapo umefuga mbuzi washauri wenzako kuonja na kutumia maziwa haya
 • Watafute wenzako wanaofuga mbuzi wa maziwa na muungane kubuni chama ama kikundi ya kutetea haki zenu kama wakulima ili kuimarisha ufugaji huu kama vile kupigania kulipwa bei nzuri ya maziwa, kuundwa kwa soko bora la bidhaa hii, ama njia bora za kuboresha ufugaji huu.
 • Mkiwa kwenye vikundi hivi piganieni kwa pamoja kubuniwa kwa soko ama kiwanda cha maziwa ya mbuzi kama vile mnaweza kuzungumza na kiwanda cha kinachonunua maziwa ya ng’ombe ili pia kianze kununua maziwa ya mbuzi au mbuniwe kiwanda chenu cha maziwa hayo.
 • Tafuta ushauri ama msaada kutoka kwa taasisi za utafiti wa mifugo kuhusu uwezekano wa kupata chakula cha mbuzi kizuri kwa bei nafuu pamoja na mbinu nzuri na za kisasa za kufuga mbuzi wa maziwa.
 • Weka mpangilio bora wa kuwachunguza mbuzi wako mara kwa mara ili kutambua wagonjwa kwa urahisi na kuyatokomeza.
 • Wazalishe mbuzi wa maziwa wa kienyeji na wale wa kizungu ili kupata aina nzuri ya mbuzi wanoweza kustahimili aina mbali mbali ya hali ya hew ana magonjwa.

 

Nyumba ya Mbuzi

Unaweza kufuga mbuzi ndani ya nyumba au zero grazing endapo huna shamba kubwa, lakini ikiwa una eneo kubwa la shamba waweza kuwaruhusu wajitafutie nyasi wenyewe (ufugaji huria).

Chumba cha mbuzi mmoja kinaweza kujengwa kwa kutumia mbao na kinapaswa kuwa na kipimo cha upana wa futi 4 na urefu wa futi 6 na kwenda juu futi 12 na kumbuka kuacha eneo la futi 6 mraba kwa mbuzi kufanyia mazoezi na kumbuka kuweka vijisanduku/vyombo viwili kimoja cha kulia chakula na kingine cha kunywea maji.

Ni bora kuhakikisha kuwa mlango wa nyumba ama banda hautazamani moja kwa moja na mahali upepo unakotokea ili kuwakinga dhidi ya magonjwa yaambukizwayo kwa njia ya hewa.

 

Umuhimu wa afya ya umma kwa Wafugaji wa Mbuzi wa maziwa

Maziwa ya mbuzi kama ilivyo kwa ng’ombe wa maziwa kinaweza kuwa chanzo cha magonjwa ya kuambukizwa kwenda kwa binadamu.  Baadhi ya madhara yanayotokana na utumiaji wa maziwa ni kama vile.

Magonjwa

 • Magonjwa kama vile brucellosis na kifua kikuu yanaweza kuambukizwa kupitia maziwa ambayo hayajachemshwa vizuri.
 • Watu wanaweza kuambukizwa magonjwa kupitia kugusa mkojo ama nyama za mnyama aliye mgonjwa ama maji na mchanga wenye vimelea vinavyoweza kuambukiza magonjwa. Watu wanapaswa kuwa waangalifu wanapogusa mimba za mifugo zilizoharibika kwani nazo zinaweza kuwa na vimelea vya magonjwa.
 • Magonjwa kama vile homa ya matumbo, kuhara damu na kuendesha yanaweza kuambukizwa kwa kula nyama ambayo haijapikwa vizuri na maziwa yaliyo na bakteria na virusi vinavyoambukiza magonjwa.
 • Ugonjwa wa kimeta (anthrax) ni ugonjwa hatari unaoambukiza binadamu kupitia hewa, kugusa mzoga wa mnyama aliyekufa ama kula nyama ya mnyama anayeugua ugonjwa huo. Vimelea vya ugonjwa vyaweza kuishi mchangani kwa miaka mingi na havifi kwa urahisi hata ikiwa nyama itachemshwa kwa muda mrefu.
 • Sumu kuvu au fangasi hupatikana katika nafaka zilizooza. Mifugo ikipewa aina hii ya nafaka, sumu huingia mwilini na inaweza kuambukizwa kwa binadamu anapokunywa au kula nyama ya huyo mnyama. Hivyo basi si vyema kuwapatia mifigo nafaka zilizooza.
 • Kumbuka kuwa:
  o  Viwango vya dawa inayotuka kwa mifugo kuuwa kupe, chawa na viroboto kinapaswa kuwa kile kilichoandikwa kwenye dawa wala hupaswi kuzidisha.
  o  Ukizidisha kiwango, dawa hii hupenya na kuingia ndani ya ngozi.
  o  Matititi na chuchu za mnyama zinapaswa kuoshwa vizuri kabla ya kuanza kukamua maziwa baada ya mifugo kutibiwa.
  o  Dawa za mifugo kama vile za kuua minyoo na za kutibu magonjwa zinafaa kupewa wanyama kwa kunywesha au kuwachoma sindano.
  o  Mbuzi wanafaa kulishwa masalio ya mboga na mimea mingine baada ya kuvuna
  o  Zingatia maagizo ya matumizi yaliyo kwenye chupa na pakiti za dawa.
 • Dawa za antibiotic zinazoingia kwenye maziwa ni hatari na zinaweza kusababisha
  o Allergy ya mara kwa mara
  o Kuongeza kiwango cha allergy kwa mwili wako
  o Kusababisha dawa kukataa kufanya kazi ama kutibu magonjwa na hatimaye kusababisha kukosekana kwa dawa za kutibu magonjwa hayo.

 

Uzalishaji wa Mbuzi

Kumbuka ili kuwa na aina nzuri ya mbuzi wanaotoa maziwa mengi hutokana na usimamizi bora na uwezo wake wa kimaumbile. Mbuzi hawa wa kigeni huathiriwa sana na mbadiliko ya hali ya hewa na magonjwa yanayopatikana katika eneo wanalofugiwa na chakula kinachopatikana ikiwa yatatofautiana na pale wanapotoka.

 

Mambo muhimu unayopaswa kufahamu kabla ya kuwazalisha mbuzi wako.

 • Mbuzi wa kike huwa tayari kushika mimba katika muda wa miezi sita hadi mwaka mmoja kulingana na aina ya mbuzi na chakula wanachokula
 • Mbuzi wa kike ambaye hajazaa huwa tayari kushika mimba kila baada ya siku 21
 • Mbuzi mmoja dume ana uwezo wa kuwazalisha mbuzi 30 majike.
 • Kufuga mbuzi mmoja dume kwa minajili ya kuzalisha kundi la mbuzi majike huenda kuongezea gharama kwa mkulima hivyo ni vema mfugaji kutafuta mbuzi dume kwingine au kwa jirani.
 • Katika hali hii mfugaji anapaswa kuweka rekodi ama kumbukumbu za kuonyesha jinsi mbuzi wake huuzaliana ili kubaini wakati mbuzi wako yupo tayari kushika mimba na wakati wa kuwaweka pamoja na madume ili waweze kuzaana.
 • Mbuzi jike walio na kasoro ama matatizo ya kiafya hawapaswi kuruhusiwa kuzaana. Mbuzi ambao hawapaswi kuruhusiwa kuzaa ni kama vile:-
  o     Walio na matiti-kiwele kilicholemaa
  o     Mbuzi ambao wamekuwa tasa kwa zaidi ya misimu miwili hawapaswi kuzalishwa
  o     Walio na matatizo ya kuharibika kwa mimba
  o     Mbuzi walio wakongwe/waliozeeka
  o     Walio na kiwango kidogo cha maziwa ama wasio na uwezo wa kuwalea mbuzi wachanga.
 • Mbuzi wa kiume walio na ulemavu wanapaswa kutengwa na wa kike wala hawapaswi kuwazalisha wa kike. Mbuzi hawa ni kama wale walio na;
  o     Ulemavu wa mwili
  o     Walio na historia ya magonjwa ya kuambukiza kwani huuenda wazae mbuzi walio na matatizo haya
  o     Mbuzi wasio na maziwa wala kuweza kustahimili magonjwao
 • Mbuzi wa kiume hapaswi kuruhusiwa kuzalisha kwa zaidi ya miaka miwili. Ili asiende akazalishe mwanawe.

Ni vyema kuhifadhi kumbukumbu ama rekodi za mbuzi wako wa maziwa ili kutambua wakati wa kuwatenga wale wasiofaa katika kundi.

 

Chanzo: The beehives

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!