Ufugaji wa mbuzi wa nyama

PAKUA APP YA TOVUTI HII YA UFUGAJI HAPA

 

Na Daniel Mbega

BINAFSI nimezaliwa katika jamii ya wafugaji ambayo ulaji wa nyama, hasa ya mbuzi, ni sehemu ya maisha. Nakumbuka tangu nikiwa mdogo wakati tunaishi kwenye maboma porini mwanzoni mwa Vijiji vya Ujamaa, haikuwahi kupita siku tatu kabla baba yangu hajachinja mbuzi ambaye tulimbanika huku tukimtafuna wakati baba akitusimulia hadithi.

Ingawa tulikuwa na kundi kubwa la ng’ombe zaidi ya 1,000, lakini mbuzi walikuwa ni wengi pia pamoja na kondoo ambao sisi watoto tuliwachunga pamoja na ndama. Ilikuwa nadra sana kukuta baba yetu akimchinja kondoo, kwa sababu huyo alikuwa kwa nyakati maalum, hasa pale vijana wanapokwenda jando ambapo walikunywa mafuta yake.

 

Lakini kwa mbuzi, nyama ilikuwa kitu cha kawaida hasa tunapokosa mawindo ya nyamapori. Wakati mwingine watoto watukutu waliweza kumjeruhi mbuzi mkorofi kwa makusudi ili kumshawishi mzee amchinje. Unajua mbuzi wa asili ni wakorofi sana na wanaweza kukimbilia kwenye mashamba ya watu wakati wewe ukihangaika na ndama.

Hata hivyo, ufugaji wa wakati ule ulikuwa ni wa asili na mazowea. Hakuna aliyefuga mbuzi kwa ajili ya biashara, labda kama kulikuwa na mahitaji kidogo nyumbani ambapo mzee angewachukua kadhaa na kuwapeleka mnadani kwa ajili ya fedha za matumizi kama nguo na kadhalika. Usiulize kuhusu masuala ya hospitali, kwa sababu wengi tulitumia mitishamba tu.

Lakini kwa kadiri maendeleo yalivyoongezeka, misitu imepungua ya kumfanya mtu kuwa na kundi kubwa la ng’ombe huku watu wakitafuta ardhi kwa ajili ya kilimo. Ni changamoto kubwa sana huku ikichangiwa na mabadiliko ya tabianchi. Ufugaji wa mbuzi nao umepungua pia huku serikali ikihimiza wananchi kufuga kisasa kwa kuangalia uchumi.

Mbuzi wana soko kubwa kila mahali. Hapo ulipo au katika miji mikubwa, lakini si watu wengi wanaofuga mbuzi, tena kibiashara.

Kwa hiyo basi, ni vizuri tukajifunza namna nzuri ya kufuga mbuzi wa nyama kisasa. Kama unao tayari, elimu hii itakusaidia kuboresha, lakini kama bado, unaweza kushawishika kuanzisha mradi wa ufugaji mbuzi hata hapo ulipo.

Mbuzi ni tofauti na ng’ombe kwa sababu ni wastahimilivu sana dhidi ya ukame. Wanakula nyasi pia wanakula majani na magome ya miti. Kama nyasi zimekwisha au kukauka wataendelea kuishi na kuzaliana kwa kula majani ya miti.

Kwa ujumla, ufugaji wa mbuzi wa nyama ni fursa muhimu kwa wananchi wengi kujipatia maendeleo hasa ukiongeza thamani kwa kuwafuga kisasa ili kupata soko zuri. Kama utazingatia kanuni za ufugaji, hakika mbuzi anaweza kukupatia faida kubwa na kupunguza umaskini.

Ikiwa umevutiwa, basi tunaweza kuendelea na mjadala wetu.

Jambo la msingi kabisa ni kwamba lazima uwe na eneo la kufugia, walau shamba lenye ukubwa wa ekari moja. Ni ndani ya shamba hili ambako mbuzi wanatakiwa wajengewe banda bora na wapate eneo la malisho.

Mbuzi wanapenda kulala kwenye banda kavu, lililoinuliwa na kuezekwa vizuri ili kuwakinga na jua na mvua, lakini pia lililozungushiwa kuta (za udongo, mbao au mabati) kuwakinga na upepo mkali. Mwanga na hewa ya kutosha ni vitu muhimu sana. Banda la mbuzi siyo ghali, kwani linaweza kujengwa kwa rasilimali zinazopatikana mahali ulipo – miti, mabanzi, nyasi.

Ukiamua kufuga mbuzi kwa lengo la kibiashara unaweza kupata faida kubwa kwa sababu kwa kawaida mbuzi anazaa mara mbili kwa mwaka. Anabeba mimba kwa miezi mitano (yaani siku 145 hadi 155) na wananyonyesha kwa miezi miwili.

Wapo mbuzi ambao wanazaa mapacha, na kwa hiyo unaweza kuongeza kundi lako katika muda mfupi.

Kwa kawaida, mbuzi anakuwa tayari kuzaa anapofikisha miezi 7 hadi 8. Hata kama mbuzi wako siyo wa kuzaa mapacha, lakini kama wanazaa mara mbili kwa mwaka, ukianza na mbuzi 20, una uhakika kwamba kwa mwaka mmoja utakuwa umeongeza mbuzi 40, ambao kwa mwaka unaofuata – ikiwa majike watakuwa 20 kati ya watoto hao, basi utaongeza mbuzi 120 na katika mwaka wa tatu utakuwa umeongeza mbuzi wengine 240, hivyo jumla unaweza kuwa na kundi la mbuzi 320 ndani ya miaka mitatu.

Kama unataka kuzalisha zaidi, basi unaweza kuamua kuwauza madume na kubakiwa na majike ambayo yataendelea kuzaa na kuongeza kundi lako.

Faida za mbuzi ni nyingi sana, lakini mbali ya kuwauza wakiwa hai, ukiwachinja utapa nyama, ngozi, kwato na pembe ambazo ni rasilimali nyingine zinazoweza kuuzwa kwenye viwanda ili kuzalisha bidhaa nyingine za ngozi na nta.

Katika nchi nyingi, nyama ya mbuzi inapendwa sana kwa sababu ni tamu na haina lehemu (cholesterol) wala mafuta mengi kulinganisha na nyama nyingine.

 

Aina ya mbuzi wa nyama

Inawezekana umesikia aina mbalimbali ya mbuzi, lakini hujajua ni wepi wanaofaa kufugwa kwa ajili ya nyama. Ukumbuke kwamba, wapo mbuzi wanaofugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, na nyuzi.

Sasa hapa tunazungumzia mbuzi wa nyama tu na kidogo mbuzi wanaofugwa kwa ajili ya nyuzi, makala nyingine zinaelezea kwa kina mbuzi wa maziwa na aina zake.

 

Boer (Mbuzi Kaburu)

Mbuzi wanaofaa zaidi kwa nyama hasa unapofuga kibiashara ni jamii ya Boer (maarufu kama Mbuzi Kaburu), ambao ni chotara wanaokua kwa haraka, wana umbo kubwa, nyama yao ni ya kiwango cha juu.

Mbuzi hawa wana rangi nyeupe, kichwa chenye rangi ya udongo au nyekundu, masikio makubwa na pembe ambazo zimepinda kwa nyuma na chini.

Mbuzi jike mkubwa wa jamii ya Boer ana uzito wa kilogramu kuanzia 68 hadi 102, wakati beberu mkubwa ana uzito wa kilogramu 80 hadi 150.

Unaweza kuona ni kwa jinsi gani mbuzi hao wanavyokuwa wakubwa na uzito mkubwa sana.

 

Kiko

Kiko ni jamii ya mbuzi inayokuja kasi baada ya Boer hata katika utoaji wa nyama. Wana uwezo wa kula nyasi na kuzibadili kuwa nyama, hivyo wananenepa haraka. Mbuzi hawa wanaweza kuwa na rangi tofauti, ingawa wengi wao ni weupe. Pembe za beberu ni ndefu zilizojiviringa wakati pembe za jike ni fupi. Jike ana uzito wa kilogramu 45 na beberu ana uzito wa kilogramu 80.

 

Pygmy (Mbuzi Mbilikimo)

Mbuzi jamii ya Pygmy ni wadogo kwa umbo lakini wenye miili imara na minene iliyojaa minofu; miili yao ni mipana. Mbuzi hawa wana manyoya marefu. Mbuzi jike mkubwa ana uzito wa kati ya kilogramu 16 hadi 23, na beberu mkubwa ana kilogramu kati ya 20 hadi 32.

Pamoja na udogo wake, lakini mbuzi aina ya Pygmy wanatoa kiwango sawa cha maziwa kama mbuzi jamii ya Nigerian Dwarf ingawa Pygmy huwa hawakamuliwi mara kwa mara kutokana na udogo wa matiti yao.

 

Spanish

Kabla mbuzi jamii ya Boer na Kiko hawajawa maarufu, hususan Marekani, mbuzi wengi waliofugwa kwa ajili ya nyama walikuwa wakiachwa kujitafutia wenyewe chakula kwenye mabonde na vichakani Kusini na Kusini Magharibi mwa Marekani ili kusafisha mashamba yasiwe na vichaka na nyasi – kama ilivyo kwa mbuzi wetu wa asili hapa Tanzania.

Mbuzi hao huko Marekani waliitwa Spanish kwa sababu walipelekwa kwa mara ya kwanza na wapelelezi wa Kihispania na wakaachwa huko ili wawafae kwa kitoweo wakati mwingine watakaporejea tena.

Kwa vile mbuzi hao wanatofautiana kwa maumbo na rangi, kwa hiyo jina la Spanish halimaanishi aina moja ya mbuzi. Mbuzi jike mkubwa ana uzito wa kilogramu kati ya 30 hadi 60 wakati beberu ana uzito wa kati ya kilogramu 36 na 91.

 

San Clemente

Katika miaka ya 1500, mbuzi wa Kihispania waliachwa kwenye Kisiwa cha San Clemente, kutoka Pwani ya California jirani na San Diego. Mbuzi hao walizaliana na wameendelea kuzaliana huko hivyo kupewa jina la San Clemente. Wakati fulani mbuzi walikuwa wengi mno kisiwani humo kiasi kwamba walikaribia kuharibu mazingira ya kisiwa, hivyo ikabidi wapunguzwe.

Mbuzi wa jamii hii ni wadogo na wana nyama nzuri kuliko jamii nyingine ya mbuzi kutoka Hispania, na pembe zao zinakuwa ndefu kwa kwenda juu.

Mbuzi hawa wana rangi tofauti na mabaka ya rangi ya udongo au nyeusi. Mbuzi jike mkubwa ana uzito wa kati ya kilogramu 15 na 32 wakati bebeeru lina uzito kati ya kilogramu 18 na 36.

 

Myotonic

Hawa ni jamii ya mbuzi ambao hawapatikani sana ingawa wanafugwa kwa ajili ya nyama. Ni mbuzi ambao mara nyingi wanaitwa ‘mbuzi wa kuzimia’ kwa sababu wanakuwa na ulemavu fulani ambao kitaalam unaitwa myotonia. Mbuzi mwenye ulemavu wa aina hiyo ambao hutokana na ulemavu wa jeni mara nyingi hukumbwa na hofu wanaposikia kelele, misuli hukakamaa na miguu hufa kazi. Kama mbuzi huyo atapata na mshtuko huo kwa ghafla, anaweza kudondoka na hawezi kuinuka mpaka misuli ya miguu ilegee.

Kwa mfugaji mwenye mbuzi hao, ambaye kila mara atakuwa akiwaminya misuli kwenye miguu, huwafanya mbozi hao kuwa na minofu mingi kwenye mapaja, hivyo kuwa wanyama bora kwa nyama.

Kutokana na ulemavu huo, ambao hauna madhara kwa kula nyama yake, huwafanya mbuzi hao wasiwe wasumbufu na kuwa watulivu daima.
Hata hivyo, nchini Tanzania kuna mbuzi wengine chotara walioboreshwa ambao waliwahi kugawiwa kwa wafugaji katika mradi maalum. Wasiliana na ofisa mifugo aliye jirani ili akuelekeze vyema ni aina gani ya mbuzi wanaofaa kufugwa katika eneo lako na hasa hao walioboreshwa na namna ya kuwapata. Mbuzi walioboreshwa mara nyingi huzaa pacha.

 

Kwa mawasiliano nipigie au nitumie ujumbe wa whatsapp kupitia namba 0656-331974, au niandikie barua pepe: maendeleovijijini@gmail.com

Leave a Reply