Farida Mkongwe Ufugaji wa samaki hatua kwa hatua: Hatua ya tano   Na Farida Mkongwe 

HATUA YA 6: MASOKO

Katika hatua ya 5 ya mfululizo wa  makala hii ya ufugaji wa samaki tulizungumzia uvunaji, usindikaji na uhifadhi wa samaki.

Katika uvunaji tuliona kuwa mfugaji anaweza kupunguza maji kwenye bwawa ili samaki waweze kuvuliwa kwa urahisi lakini pia kutokana na uhaba wa maji mfugaji anaweza asipunguze maji badala yake akavua samaki kwa kutumia nyavu yenye macho yanayokubalika kitaalamu. Kwa upande wa usindikaji na uhifadhi tuliona kuwa samaki wanaweza kuhifadhiwa kwa kutumia chumvi, moshi, kuwakaanga kwenye mafuta na kuwagandisha kwenye barafu.

Katika hatua hii ya 6 tunaangalia suala la masoko ya samaki. Hapa Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ambaye pia ni mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Berno Mnembuka anaeleza kuwa mfugaji anaweza kunufaika na masoko ya aina 3.

Aina ya kwanza ya soko la samaki ni soko la awali, hili ni soko la moja kwa moja kutoka kwa muuzaji ambaye ni mfugaji kwenda kwa mlaji, soko hili linahusisha majirani na vituo mbalimbali ambavyo vinanunua samaki au kubadilishana samaki na bidhaa nyingine kwa lengo la kuwatumia samaki hao na siyo kuwauza.

Soko la pili ni soko la kati, katika soko hili kwa kawaida kunakuwa na mtu wa kati ambaye ananunua samaki kwa mfugaji kwa lengo la kwenda kuwauzia walaji. Mtu huyu wa kati ambaye si mlaji hununua samaki na kwenda kuwauza kwa bei ya juu ukilinganisha na ile aliyonunulia ili aweze kupata faida.

Aina ya tatu ya soko ni soko la kimataifa, hili ni soko linalofanyika nje ya nchi (baina ya nchi moja na nchi nyingine). Mfugaji akifikia hatua hii ni wazi kuwa atakuwa mfanyabiashara mkubwa na hivyo atakuwa na uwezo wa kupata faida zaidi ukimlinganisha na mfanyabiashara mdogo.

Changamoto kubwa iliyopo kwenye masoko na hasa soko la kati ni wanunuzi kuungana pamoja na kumpangia bei mkulima hali ambayo inaathiri mapato ya mkulima. Kutokana na hali hiyo Dr. Mnembuka anawashauri wafugaji kuunda chama chao ambacho kitakuwa na uwezo wa kupanga bei na hivyo kutokubali bei watakayopangiwa na watu wa kati, ushauri mwingine ni kwa wafugaji kusindika samaki wao ili wasiharibike kiurahisi kwani kwa kufanya hivyo kutawaondolea hofu ya samaki wao kuharibika na hivyo kuwauza wakati wowote kwa bei wanayoipanga wenyewe.

Hadi hapo ndiyo tunafikia ya tamati hatua hii ya 6 ya ufugaji wa samaki hatua kwa hatua, usikose kufuatilia hatua ya 7 ambayo itakuwa ikizungumzia vyakula na ulishaji wa samaki wafugwao.

 

CHANZO: SUAMEDIA

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!