Mambo muhimu ya kuzingatia ili kupunguza magonjwa ya mifugo shambani mwako

ByChengula

Oct 1, 2015

Na Mwandishi wetu

Augustino Chengula

Maswali mengi sana ambayo nimekuwa nikiyapata toka kwa wafugaji wengi wa mifugo ya aina mbalimbali inahusu namna ya kutibu magonjwa. Wengi wa wauliza maswali ni wafugaji wa kuku, wanataka kujua namna ya kutibu aina fulani ugonjwa kwa kadiri ya dalili wanazoziona. Kuku wangu au mfugo wangu una daalili hizi na hizi ni ugonjwa gani na nitumie dawa gani kuku au mifugo yangu iipone. Baada ya kupokea maswali mengi ya wafugaji wengi nimebaini magonjwa mengi ni yale yanaweza kuzuiwa yasitokee kwa mfugaji. Nimebaini pia kuwa wafugaji wengi wanaingia kwenye ufugajji wakiwa na elimu kidogo waliopata toka kwa wafugaji wenzao au ndani ya familia yake ambao pia wanafuga tu kwa mazoea. Na wengine huanza kufuga wakiwa hawana elimu ya ufugaji kabisa, hawatafuti kujifunza kidogo kabla ya kuanza. Wote wana nia nzuri ya kutaka kujiongezea kipato na kujikwamua na ugumu wa maisha. Katika kuingia kwao kwenye ufugaji bila kuwa naa elimu ufugaji, wengi wamekutana na matatizo ya vifo vya mifugo yao kwa magonjwa. Hata wale wanaofanikiwa kwa kiasi fulani wamekumbana na uzalishaji duni usio mletea faida mfugaji. Wengi pia wameishia kujutia kwa nini waliamua kuingia kwenye ufugaji. Mara nyingi wameishia kuwakatisha tamaa na wengine wenye tamaa ya kutaka kuingia kwenye ufugaji.

Ukweli una bakia pale pale tu kuwa ufugaji unalipa sana ukiamua kuufanya kwa kufuata kanuni za ufugaaji bora. Leo nimeona ni vema nikakupa elimu ya namna ya kuzuia magonjwa na kuongeza uzalishaji wa mifugo yako. Mambo haya muhimu ya kuzingatia yanahusu mfugaji yeyote anayefuga aina yeyote ile ya mfugo. Hivyo mfugaji yeyote kabla ya kuanza ufugaji wake ni vizuri akafahamu haya na akatengeza utaratibu wake utakao msaidia kuona anafuatilia mambo haya hatua kwa hatua. Mpango mkakati wako wa ufugaji lazima uzingatie mambo haya muhimu.

 

JAMBO LA KWANZA: Chaguo la nini unataka kufuga

Kila jambo unalofaanya katika maisha ni lazima liwe na kusudi fulani linalo kusukuma kulifanya. Hivyo kitu cha kwanza cha kujiuliza kabla ya kuingia kwenye ufugaji lazima ujiulize nataka kufuga ili iweje? Na je msukumo unatoka ndani ya moyo wako au ni wan je tu uliochagizwa na wafugaji wengine? Ufugaji si jambo la kukurupuka, chukua muda kutathmini na kuona upo tayari kufanya ufugaji. Wengi wameingia kwenye ufugaji kufuata mkumbo tu na mwisho wa siku hawaweki jitihada kwenye ufugaji na wameishia kushindwa. Wengi pia wanafuga lakini hawaweki jitihada na muda wao kwenye ufugaji wakitegemea kufanikiwa. Huwezi kufanikiwa kwa namna hiyo. Chaguo la aina ya mfugo litatofautiana kati ya mtu na mtu na eneo ufugaji unatarajiwa kufanyika. Wengi huchagua aina fulani ya mfugo kwa sababu soko lake lipo na la uhakika na wachache hufuga kwa kupunda aina ya mfugo wenyewe. Chagua mfugo kwa kuangalia uwezo wa kumtunza katika eneo husika na muda wa upatikanaji wa faida. Ukishajua aina ya mfugo itakusaidia kuanza kujifunza namna ya kumfuga hata kabla ya kuanza.

 

JAMBO LA PILI: Eneo la ufugaji

Uuchaguzi wa eneo la kufugia ni muhimu sana kwa kwa kupambana na magonjwa ya mifugo yako, hivyo ni muhimu kulifanyia upembuzi wa kina kubaini vitu vitakaoweza kuathiiri ufugaji wako. Hii itakupa uchaguzi sahihi wa kuendelea kulitumia huku ukijua tahadhari zaa kuchukua au uchague eneo linguine. Chunguza kama kuna mfugaji/wafugaji kwenye hilo unalotaka kufugia ambao wanafuga mifugo unayotaka kufuga. Shamba lako ni vizuri likawa mbali na mashamba mengine kuepusha mifugo yako kupata magonjwa toka kwa jirani zako. Ni vizuri pia kama una mifugo ya umri tofauti tofauti mfano kuku wakakaa kwenye eneo (banda) moja kuepusha magonjwa kutoka kwa kuku wakubwa kwenda kwa kuku wadogo. Mara nyingi kuku au wanyama wadogo ndo wanao athirika zaidi na magonjwa. Lakini pia kama unafanya ufugaji mkubwa ni vizuri ukawa na eneo kubwa na ukawa mifugo yako ili ugonjwa usiipate mifugo yako yote kwa wakati mmoja.

 

JAMBO LA TATU: Ramani ya banda au shamba la kufugia

Baada ya kuchagua eneo hatua inayofuata ni kujua ramani shamba au banda lako ikaaje ili kupunguza maambuki ya magpnjwa. Shamba lako lazima lizungushiwe uzio ili kuzuia mifugo na watu kuongea shambani mwako kiholela. Mabanda yako yatengenezwe kiasi cha kuwa rafiki kwa wanaofanya usafi na yasiwe na uwezo wa kutuamisha maji. Usafi ndani ya Nyumba ya kulala mifugo ni hatua muhimu sana katika kupambana na magonjwa mengi yanayosababishwa na vimelea jamii ya bakteria, virusi na minyoo. Hivyo hakikisha banda au Nyumba ya mifugo wako inakuuwa safi wakati wote. Mabanda ya kuku sehemu za uwazi ziwekwe nyavu kuzuia ndege wengine na wadudu kuingia na kuwadhuru kuku wako. Andaa banda lako vizuri tayari kwa kupokea wanyama wapya.

 

HATUA YA NNE: Uchaguzi na uletaji wa wanyama wapya

Kitu kikubwa cha kuzingatia wakati wa kutafuta wanyama wa kufuga ni ubora wa chanzo watakako toka wanyama unaotaka kuanza kuwafuga. Hatua hii nayo ni muhimu sana, chukua muda kidogo kuafanya upelelezi kwa watu mbalmbali na hasa wataalamu wa mfugo. Ukishapata chanzo kizuri kiwe cha kuku, ng’ombe, mbuzi, kondoo, samaki n.k ukifika pale jiridhishe mwenyewe kuwa ni aina ya wanyama unaowahitaji. Mambo ya kuangalia na au kuuliza ni afya ya wanyama alionao kwa ujumla, uliza utaratibu wa chanjo alio nao na namna anavyopambana na magonjwa. Uliza wanyama unaonunua kama wamepata chanjo yeyote na zamu nyingine itakuwa lini. Ratiba ya uchangaji hasa kwa vifaranga wa kuku ni muhimu sana maana kama hachanji kuna uwezekano ukanunua vifaranga wenye ugonjwa na punde utakapo wapeleka kwenye banda lako wakaanza kufa. Lakini pia kama unaleta wanayama wapya na kuwachanganya na wenyama waliopo unaweza kuleta ugonjwa kwenye wanyama wako ambao hawakuwa nao. Hii inaweza kukupelekea kupata hasara kubwa sana nap engine ni mnyama mmoja tu akasababisha kuuawa kwa wanyama wako wote. Hivyo kuwa makini sana na wanyama wapya unaoleta. Ikiwezekana usiwachanganye na wanyama wako wa zamani hadi pale utakapojiridhisha kuwa hawana ugonjwa wowote. Unaweza kuumuita mtaalamu ukajiridhisha kabla ya kuchanganya na mifugo yako.

 

HATUA YA TANO: Taratibu za kuendesha shughuli za za shamba

Shamba lako lazima liwe na utaratibu unaoeleweka wa kuliwezesha lilete matunda unayotarajia kuyapata kulingana na uwekezaji wake. Hakuna miujiza hapa, kile unachopanda ndicho utakacho   vuna. Hivyo ni lazzima uwekeze kuanzia muda hadi rasilimali. Mpango kazi uliandaliwa vema utazaa matunda mema maana utawawezesha wewe na wasaidizi wako kuwa kitu kimoja hasa kila mmoja akiujua na kuufuata kisawa sawa. Mambo ya kuwekea mpango kazi ni kama yafuatayomchanganyo wa chakula na ratiba ya ulishaji, upatikanaji wa maji na ratiba ya usafi wa banda, vyombo na mzaingira yake, utaratibu wa watu kuingia ndani ya shamba, utaratibu wa wafanyakazi kuingia banda moja baada ya jingine, ratiba ya chanjo kwa mifugo yako na utunzji kumbukumbu wa shughuli zote za shamba.

Mpangalio wa mifugo

Mifugo itenganishwe kwa aina na umri, wanyama wa aina moja wakae kwenye banda moja na umri wao ufanane. Mfano usichanganye kuku na bata au njiwa, bata wanaweza kuwa na vijidudu vya magonjwa ambavyo havimdhuru lakini vijidudu hivyo hivyo vinaweza kumdhuru kuku. Hali kadhalika kwa umri, kuku wakubwa wanaweza wasidhurike na vijidudu fulani lakini wadogo wakadhurika. Lakini pia kuku wakubwa wanaweza wadhuru kuku wadogo kwa kuwaparua au kuwadonoa.

Maji na chakula

Chanzo cha maji na chakula kinapaswa kiwe cha uhakika kwa upatikanaji lakini pia kutokuwepo na vijimelea vya magonjwa. Mifugo inahitaji maji kwa wingi kila siku ili iweze kuleta matunda mazuri na ikinyimwa uzalishaji wake hupungua. Mchanganyiko wa chakula lazima uwe ni ule uliopendekezwa na wataalamu hasa uwe na viinilishe vyote vinavyotakiwa kwa myama waa aina na umri wake. Ukilisha mifugo yako bila kufuata utaratibu itashndwa kutoa mazao bora, inaweza kukonda mithili ya kuwa na ugonjwa fulani. Wafugaji wengi wamekuwa wakilalamika na kukimbilia kwenye matibabu kumbe tatizo ni lishe tu. Hana utaratibu mzuri wa ulishaji na kama mifugo ni shemu ya ziada tu na wanakula kile kitakacho patikana siku hiyo. Huo sio ufugaji unakuwa umevamia tu na huna nia ya kufuga. Kwa Maneno mengine ni unyanyasaji wa wanyama na sharia yake ipo. Watu wanafuga mbwa lakini chakula chao ni mabaki tu ya siku na wakati mwingine kisipo baki mbwa analala njaa. Wapo pia wanaofuga nguruwe, wamekuwa wakisumbuliwa na nguruwe kutoka nje kwasababu ya njaa. Kwa nini ufuge kama huwezi kumpa chakula?  Fikiria upya kama ni mfugaji wa aina hii. Vyakula vipo madukani na unaweza kutengeneza mwenyewe kwa kutumia mazao yanayopatikana eneo ulipo. Pitia tovuti ya ufugaji (ufugaji.co.tz) ujifunze namna ya kutengeneza chakula wewe mwenyewe. Ratiba ya ulishaji lazima ijulikane na ifuatwe kikamilifu. Walishaji lazima waanze na wanyama wadogo na kumalizia na wanyama wakubwa.

Vyombo na vifaa

Hakikisha kuwa vyombo vyako vinafanyiwa usafi kila mara unapomaliza kuvitumia kwa kutumia dawa ya      kuua vijidudu vya magonjwa ili kuepusha wadudu wa magonjwa kuweka makazi. Vyombo viwe ni rafiki wakati wa kuvisafisha. Hakikisha huchanganyi vyombo vya kazi tofauti tofauti, mfano vyombo vya kukusanyia mayai na vile vya chakula. Lakini pia vyombo vya banda moja na jingine au wanyama wa aina moja na nyingine. Ii itasaidia kuzuia maambukizi kusambaa kwenye mabanda yaako.

Utaratibu wa watu kuingia ndani ya shamba na banda

Watu wanaokuja ndani ya shamba lako au wanaotembelea ndani ya banda lako laweza kuwa chanzo cha uingiaji wa vimelea vya magonjwa. Hivyo kusipokuwa na utaratibu mzuri huwa ni hatari kubwa kwa ueneaji  wa magonjwa ya mifugo. Kusiwe na uingiaji usio wa lazima ndani ya shamba na mabanda yako watu wasio husika. Ni muhimu kuweka maji yenye dawa mlangoni mwa shamba lako ili watu waingiapo waoshe viatu vyao na kabla ya kuingia kwenye banda. Maeneo mengi utakuta mnunuzi anaingia ndani ya banda kuchagua kuku huku akishika huyu na yule akifanya hivyo kwa mabanda tofauti bila ya kunawa mikono yake. Hii ni hatari kwa mifugo yako maana anaweza kukuletea ugonjwa au akaondoka na ugonjwa kwenda shamba jingine. Wafugaji wengi hushindwa kuhusianisha mambo haya wakitafuta mchawi wa vifo vya mifugo yao. Hata wafanyakazi wako lazima wazingatie kanuni hii maana wengine pia wanafuga majumbani kwao hivyo wasipofuata taratibu hizi bado mifugo yako inaweza kupata magonjwa.

Ratiba ya chanjo kwa mifugo yako

Baada ya kupambana na magonjwa kwa njia ya usafi na lishe bora kwa mifugo yako hatua nyingine muhimu ni kuchanja mifugo yako dhidi ya magonjwa mbalimbali kulinga na ratiba inayopendekezwa. Kila aina ya mfugo ina utaratibu wake wa chanjo uliopendekezwa na wataalamu wa mifugo. Hivyo lazima uwe na ratiba ya chanjo kwa magonjwa muhimu kulinga na mapendekezo ya wataamu wa mifugo. Ratiba hiyo lazima iwe imeandikwa kulingana na aina na umri wa wanyama ulionao. Watalaamu wa mifugo watakusaidia kutengeneza ratiba hii na hakikisha inafutwa kama ilivyo ili kuzuia kujitokeza kwa magonjwa kwenye mifugo yako. Wafugaji wengi wamekuwa wakiuliza chanjo mara baada ya mifugo yao kuugua na wengine wamekuwa wakichanja kuku wenye magonjwa. Anza kupata taarifa za chanjo kwa mifugo yako wakati unaanza kufuga na tengeza ratiba yako. Usichange kuku wako kama tayari wanaugonjwa utasababisha vifo vingi zaidi.

Kutunza kumbukumbu

Kumbukumbu ni muhimu sana kwa kazi yeyote ile kwani itasaidia kujua yote unayoyafanya na kulinganisha kuona kama kazi yako inamanufaa. Wengi wanapuuzia sana utunzaji kumbukumbu wa kazi zao, na bado utasikia wanasema wanapata faida au hasara. Utunzaji wa kumbuukumbu utakusaidia kujua matumizi yako na mapato kwa mifugo yako na hatimaye kujua kama unatengeneza faida au hasara. Itakusaaidia pia kujua matibabu gani yalifanyika na lini kwa ugonjwa gani. Hivyo hakikisha unatunza kumbukumbu ya kila unachokitumia shambani mwako na kila unachokipata kutokana na ufugaji wako ili ikusaidie kujua mwishoni kama unatengeneza faida.

Mfano wa baadhi ya kumbkumbu za kutunza:

  • Tarehe za kuzaliwa mifugo yako
  • Umri ambapo mfugo ulipata chanjo
  • Ni chanjo ya aina gani
  • Magonjwa ambayo yamewahi kushuambulia shamba lako, na dawa ulizotumia katika matibabu.
  • ldadi na aina ya wanyama wanaokufa
  • Kukadiria kiasi cha chakula ambacho mifugo yako watahitaji kwa muda fulani na aina ya chakula
  • Kujua kila siku mazao yanazalishwa na mifugo yako mfano kuku wametaga mayai mangapi, ng’ombe, mbuzi au kondoo wametoa lita ngapi n.k
  • Kujua utahitaji muda gani kutunza mfugo wako toka mdogo mpaka anapofikia kuuzwa.

Ili uweze kufahamu mambo haya yote unahitaji kutunza kumbukumbu

Leave a Reply