Vipi tunaweza kujikinga na homa ya mafua ya ndege
Homa ya mafua makali inaweza kumpata binadamu na ina uwezo wa kukufanya ukawa mgonjwa sana au hata kukuua. Njia rahisi ya kujikinga usipate homa hiyo ni kujiepusha na kushikashika kuku/bata au ndege au kinyesi chao, kunawa mikono kwa kutumia jivu au sabuni na maji mara tu kabla au baada ya kushika kuku/bata au ndege, na kwa kupika kuku/bata/ndege na mayai vizuri kabla ya kula. Ifuatayo ni taarifa mahususi:-
Usafi wa jumla
- Nawa mikono kwa sabuni au jivu na maji kabla au baada ya kushika chakula.
- Vaa barakoa wakati wa kusafisha shamba
- Tumia vifaa vingine vya kujihifadhi ikiwa utagusana na kuku/bata au ndege wengine
- Ikiwezekana, badili nguo zako ikiwa unahudumia kuku nyumbani kwako kabla ya kwenda kazini
Jiepushe na kukaribia au kugusa ndege wa aina yoyote
- Ikiwa unafuga kuku/bata inabidi wawekwe ndani, basi waweke katika eneo maalum mbali na pale ambapo familia inalala na kula
- Usiache kuku/bata kuingia ndani ya nyumba
- Waweke watoto mbali na ndege na ikiwezekana wasiachiwe kuokota mayai – hii ni pamoja na ndege wa kufuga, ikiwa wanaachiwa kutoka nje.
Ukiona ndege aliyekufa au mgonjwa, usimguse kama hujavaa glavu
- Kama kuna ndege wagonjwa au waliokufa, toa taarifa kwa viongozi mara moja
- Aina zote za ndege zinaweza kupata homa ya mafua ya ndege – kuku, bata, kanga, bata mzinga, njiwa, ndege mwitu na hata wale wanaofugwa
- Baadhi ya ndege kama bata wanaweza kuwa wameambukizwa japokuwa hawaonekani wagonjwa
- Ukijisikia mgonjwa baada ya kugusa ndege wagonjwa au waliokufa, pata matibabu haraka.
Hakikisha kuwa nyama ya kuku/bata/ndege na mayai vinapikwa vizuri
- Mapishi ya kawaida (nyuzi joto 70C au zaidi kwa sehemu zote za chakula) yanaua virusi vya homa ya mafua ya ndege.
- Virusi vya homa ya mafua ya ndege, kama vimo katika nyama ya kuku/bata havifi kwa kuwekwa kwenye friji au kwa kugandisha katika barafu.
- Usile yai linalochuruzika au nyama ya kuku/bata ambayo haikuiva vizuri na usinywe damu ya bata isiyochemshwa.
- Mayai yasiyopikwa yasitumiwe katika vyakula ambavyo havipikwi.
- Mayai yanaweza kuwa na virusi vya homa ya mafua ya ndege nje (kwenye gamba) au ndani (kwenye ute na kiini), kwa hivyo pamoja na kuyapika vizuri, ni muhimu kunawa mikono baada ya kushika mayai.
Usichinje au kutayarisha kuku/bata waliokufa au wagonjwa kwa ajili ya chakula
- Njia kuu ya kuambukizwa homa ya mafua ya ndege ni kwa kushikashika au kuchinja kuku/bata hai walioambukizwa
- Usafi ni muhimu wakati wa kuchinja na baada ya kuchinja ili kuepuka maambukizo kwa kushika nyama mbichi ya kuku/bata au kuchafuka kwa chakula, maeneo au vifaa vya kutayarishia chakula kutokana na kuku/bata..
- Nyama mbichi, kuku/bata, samaki na majimaji yao yatengwe na vyakula vingine.
- Baada ya kukatakata nyama, nawa mikono, osha kibao cha kukatia, kisu na kaunta kwa maji ya moto yenye sabuni, na ikiwezekana tumia blichi.
Chukua tahadhari ikiwa unatembelea mashamba au maeneo mengine wanapofugwa kuku/bata na ndege
- Ukitembelea shamba au ambako wamewekwa kuku/bata, nawa mikono yako kwa jivu au sabuni na maji kabla kuingia na baada ya kutoka.
- Pangusa na weka dawa kwenye nguo, viatu matairi ya baiskeli, pikipiki, n.k. baada ya kuondoka, hasa kama utaingia ndani ya nyumba.
Ikiwa utagusana kwa bahati mbaya na kuku/bata katika eneo lenye maambukizo (kama vile kuugusa mwili wa ndege au kinyesi chake, au kukanyaga udongo wenye kinyesi cha kuku/bata/ndege):
- Nawa mikono vizuri kwa maji na sabuni au jivu kila ukigusa
- Vua viatu vyako nje ya nyumba na visafishe kuondoa uchafu wote
- Ukisikia mwili una joto kali, nenda kwa daktari au kwenye kituo cha afya kilicho karibu haraka.
Anzisha majadiliano na marafiki, familia, majirani na jamii kwa ujumla kuhusu mikakati ya kuzuia kuenea kwa mafua ya ndege katika mtaa wenu
- Mafua ya ndege ni ugonjwa wa ndege wa porini ambao huambukiza kuku/bata/ndege wanaofugwa, aidha kwa kupitia maji au udongo ambao umepata kinyesi cha ndege wagonjwa. Ni rahisi ugonjwa huu kusambaa kwa kuku wanaofugwa. Kuku wote wanaoambukizwa hufa baada ya siku mbili.
- Ni vigumu kwa mwanadamu kupata ugonjwa huu, endapo atazingatia kanuni za usafi. Lakini, endapo mwanadamu atagusana na kuku wagonjwa, ugonjwa huu unaua haraka haswa kwa watoto wadogo. Athari kubwa iko katika mabanda ya kuku yaliyo karibu na makazi ya kuishi.
- Familia nyingi zina kibanda cha kuku nyumbani kwa ajili ya kitoweo au mayai ya kienyeji kwa wanafamilia. Chukua tahadhari hasa kama kuku hufunguliwa asubuhi na kuachwa huru, na kufungiwa tena jioni. Ugonjwa wa “Newcastle” na magonwa mengine ya kuku yanafanana sana na ugonjwa wa mafua ya ndege.
- Ni vizuri ukatoa taarifa kwa viongozi wa mitaa endapo kuku/bata/ndege wataonyesha dalili zozote za kuumwa.