UMUHIMU WA KUPIMA UZITO NGURUWE WAKO

*MIZANI NA UPIMAJI UZITO*
_By ARBO Pigs Farm_
Katika *Ufugaji wa Nguruwe Kisasa na kwa Tija/Kibiashara*, Mizani na Upimaji Uzito ni Nyenzo muhimu kabisa kwa Mfugaji wa Nguruwe kwenye shughuli zake za kila siku na katika kujipima/kujitathmini kama yupo katika mstari sahihi kufikia malengo aliyojiwekea. *Bila Mzani ni vigumu sana kufanya Ufugaji wa Tija.* Hapa tutaongelea Upimaji Uzito wa Mnyama, Nyama na Chakula. Kutokana na uzefu katika ARBO Pigs Farm, hapa chini tunawashirikisheni:
*FAIDA 3 ZA MZANI NA UPIMAJI UZITO*
1️⃣ *KUJUA UZITO WA NGURUWE*
🐖 *Wakati wa kununua*
➖ Katika zama hizi za kuzingatia BioSecurity, huwezi kwenda kumwona Nguruwe kabla ya kununua, sana sana utaoneshwa picha/video tu. Hivyo ni muhimu ukafahamishwa uzito na umri wa Nguruwe unayetaka kununua ili ujiridhishe kama anafikia kiwango unachotaka au la, na hivyo ufanye uamuzi sahihi wa kununua au la. Baada ya kununua na kumfikisha shambani kwako, unaweza kujithibitishia (kama unao mzani) kuwa uzito wake ni/si sawa na ule ulioahidiwa. Hapo utajipatia Nguruwe wa thamani halisi ya pesa uliyolipa (value for money).
➖ Fahamu kwamba ukinunua Nguruwe ambaye hajafikia kiwango fulani – mfano, mtoto (weaner) wa wiki 12, awe na uzito wa kilo 35 – 40 (kwa viwango vyetu; vinginevyo unaweza kurejea viwango vya Kampuni ya PIC Growth Curve – hivi vipo juu sana!). Chini ya hapo, utakuwa na kazi ya ziada na utaingia gharama kubwa kumlea (kama ni jike) ili afikishe walau kilo 120 wakati wa kupandwa; na inawezekana hata asifikishe uzito huo unaoshauriwa.
➖ *Hivyo wakati wa kununua, hata kama ni Mbegu Bora (hybrid),* usipofuata viwango sahihi vya uzito, inakula kwako! Hata hawa hybrid wasipotunzwa vizuri, hawawezi kuleta matokeo tarajiwa – iwe kwenye Nguruwe wa Nyama au wa Mbegu.
Watoto Wanapoachishwa Kunyonya katika umri wa siku 20 – 35 uzito (weaning weight) unaoshauriwa ni walau kilo 7-8. Chini ya hapo unaweza kufanya maamuzi kadri ya viwango ulivyojiwekea – mfano, kama uzito ni chini ya kilo 6, kutoendelea nao kwa sababu watakusumbua na kugharimu sana kuwafuga ili wakue katika viwango vinavyotakiwa.
🐖 *Majike Wanaopandishwa Mara ya Kwanza.* Uzito unaoshauriwa ni walau kilo 120. Hapo jike anakuwa amejengeka vizuri mfumo wake wa uzazi na mifupa. Jike mwenye kiwango hicho:
➖ Atakuletea matokeo mazuri katika maisha yake yote ya uzaaji hapo baadae.
➖ Ataweza kuhimili kupandwa hata na dume mkubwa, yaani mwenye kilo 200+.
🐖 *Katika Rika Mbalimbali*. Mara nyingi hatua mbalimbali za ukuaji wa Nguruwe au ubadilishaji wa Lishe yao, hutenganishwa kwa uzito. Mfano, Weaner atakula Starter mpaka afikishe uzito wa kilo 25. Baada ya hapo anakuwa Grower mpaka atakofikisha kilo 45, halafu anaingia kwenye hatua ya Finisher mpaka kilo 95-105. Mizani itakuwezesha kupambanua hatua hizo mbali mbali na kuwalisha Lishe sahihi.
Unapofuga Nguruwe wa Nyama: Utauza kwa Tija na kadri ya malengo yako kama utapima uzito wa nyama baada ya kuchinja, badala ya kukadiria tu uzito. Hybrid huwa na mwonekano wa umbo dogo, lakini ukimweka kwenye mzani utashangaa uzito mkubwa alio nao.
🐖 *Wakati wa kutibu*. Dawa zote hutolewa kwa kufuata uzito wa mnyama. Ukifahamu uzito wa Nguruwe wako, utawapatia dozi na hivyo matibabu sahihi.
2️⃣ *KUPIMA CHAKULA*
Wakati wa Kuchanganya Chakula unahitaji kupima uzito wa makundi mbali mbali ya viinilishe (ingredients) ili utengeneze mlo kamili (balanced ration) kwa usahihi.
Wakati wa Kulisha.
➖ Tunaona, kwa mfano, Jike anayenyonyesha inatakiwa alishwe kilo 2.5 – 3 kwa siku kwa ajili ya mwili wake, na kilo 0.4 kwa kila mtoto. Hivyo Jike mwenye watoto 10 atalishwa jumla ya kilo 7. Hapa pia, Mzani utafanikisha mahesabu yako.
3️⃣ *KUJIWEKEA MALENGO, VIWANGO NA KUJIPIMA/ TATHMINI*
🐖 *Malengo na Viwango vya Ukuaji*. Kwa kurejea viwango (Growth Curve) vya makampuni makubwa, kama PIC, unaweza kujitengezea (customize) Malengo na Viwango vya Ukuaji wa Nguruwe wako katika rika mbalimbali – kwani si rahisi sana kufikia, kama vilivyo, viwango vya PIC.
🐖 *Malengo vya Uzalishaji Nyama*
➖ Uzalishe kilo/tani ngapi kwa mwaka.
➖Hapa ni lazima ujiwekee lengo. Mfano, Nguruwe wa Nyama afikishe kilo 120 katika umri wa wiki 28 ili ukimchinja upate walau kilo 80 (wataalamu wakishatoa kichwa, miguu na utumbo) . Ili ufikie lengo hilo lazima ufuatilie (monitoring) ukuaji wa Nguruwe wako kwa kujipima kama inavyoelezewa hapo chini.
🐖 *Viwango Mbalimbali* Mfano:
➖ Ili Jike apandwe mara ya kwanza lazima awe amefikisha walau uzito wa kilo 120.
➖ Watoto wanao achishwa kunyonya katika umri wa siku 28-35 wawe na uzito walau kilo 7-8; chini ya uzito wa kilo 6 waondolewe kwa sababu huko mbeleni hawataweza kukua katika kasi na viwango ulivyojiwekea na hivyo kuleta hasara.
➖ Kuchinja Nguruwe katika umri wa wiki 28 akiwa amefikisha walau uzito wa kilo 120
3️⃣ *KUJIPIMA/KUTATHIMINI UFANISI KATIKA UFUGAJI WAKO*
Baada ya kujiwekea Malengo na Viwango mbalimbali, hasa katika Ukuaji (Growth Curve), utaweza Kujipima/Kujitathmini kwa kupima Nguruwe wako kila baada ya muda fulani, labda kila baada ya wiki moja au mbili, ili kuona kama wanafikia malengo na viwango vyako. Kama hawafikii, utatafuta sababu (kama ni Lishe duni au matunzo kwa ujumla) na kurekebisha mapungufu mpaka ufikie viwango vyako na hatimaye kupata Tija uliyokusudia.
*Hivyo basi, utaweza Kufuga kwa Tija au Kibiashara na kwa Ueledi ukiwa na MIZANI !*

Leave a Reply