Upotevu wa kijusi (fetus au foetus) wakati wa kuchinja mifugo unapunguza kasi ya kuongezeka kwa mifugo nchini

 

A. Upotevu wa kijusi kwa ng’ombe

Imeeandikwa na Mhadhiri Dr. H. E. Nonga wa Chuo cha Sayansi ya Tiba ya Wanyama na Binadamu, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kilichopo Morogoro na kuchapishwa kwenye jarida (journal) la Livestock Research for Rural Development toleo la 27 (12) kwa lugha ya kiingereza

 

Kwa Ufupi: Tanzania ni nchi ya tatu yenye ng’ombe wengi barani Afrika baada ya Ethiopia na Sudan. Tanzania inajumla ya ng’ombe wapatao milioni 21 ambao zaidi ya asilimia 95 ni ng’ombe wajulikano kama Zebu (wana sifa ya kuwa na pembe fupi).

Uchinjaji wa ng’ombe jike na mitamba wenye mimba limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa nchi nyingi zinazoendelea husani zilizopo barani Afrika. Jambo hili linapunguza kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya mifugo na lipo kinyume kabisa na sharia za usitawi wa wanyama na pia hupelekea kupunuza ubora wa nyama kwa mlaji. Uchinjaji wa ng’ombe wenye mimba hupelekea kupoteza kijusi na kuathiri ukuaji wa ufugaji wa ng’ombe kwa siku za usoni.

Katika utafiti huu uliofanywa na Dr. Nonga umebaini kuwa asilimia 15.6 ya ng’ombe jike waliochinjwa katika machinjio ya Manispaa ya Bukoba na asilimia 46 katika machinjio iliyopo Manispaa ya Dodoma walikuwa na mimba. Wastani wa juu ulionyesha kuwa kwa kila ng’ombe wawili majike wanaochinjwa mmoja alikuwa na mimba. Na wastani wa chini ulionyesha kuwa kwa kila ng’ombe sita majike wanaochinjwa mmoja alikuwa na mimba. Hii inaonyesha kuwa kiwango cha ng’ombe jike wanaochinjwa wakiwa na mimba nchini Tanzania ni kikubwa sana kinachotishia sekta ya mifugo na hivyo kufifisha juhudi zote zinazofanywa na serikali za kuongeza upatikanaji wa chakula kutoka kwenye mifugo. Aidha uchinjaji wa ng’ombe wenye mimba unakwenda kinyume na sheria ya ustawi wa wanyama ya mwaka 2008. Kutokana na utafiti huu, upo umuhimu mkubwa wa kuweka nguvu za ziada katika utoaji elimu pamoja na matumizi ya wataalamu wa utambuzi wa ng’ombe wenye mimba ili kubaini na kupunguza uchinjaji wa ng’’ombe wenye mimba nchini Tanzania.

Chapisho zima:  Kwa lugha ya kiingereza lipo hapa 

 

B. Upotevu wa kijusi kwa mbuzi na kondoo

Imeeandikwa na na watafiti E.S.Swai, H. Ayubu and B S Mhina kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyopo Dar es Salaam na kuchapishwa kwenye jarida (journal) la Livestock Research for Rural Development toleo la 27 (10) la mwaka 2015 kwa lugha ya kiingereza

 

Kwa Ufupi: Mbuzi na kondoo wanashika nafasi ya pili kwa uwingi mara baada ya ng’ombe nchini Tanzania. Ufugaji wa mbuzi na kondoo kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazoendelea hufanyika maeneo mbalimbali ndani ya nchi husika. Tanzania ina jumla ya mbuzi na kondoo milioni 15.9 ikiwa ni wastani wa mbuzi na/au kondoo 8 hadi 9 kwa kila kaya inayofuga. Kulingana na sensa ya Serikali ya mwaka 2012 ilikadiriwa kuwa kaya 1,732,863 hufuga mbuzi.

Utafiti huu wa kuangalia upotevu wa kijusi kwa mbuzi na kondoo ulifanywa kwenye machinjio yaliyopo Tanga kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba 2014. Jumla ya mbuzi waliochinjwa kwa kipindi hicho walikuwa 1,072 ikiwa ni wastani wa mbuzi 357 kwa mwezi na 12 kila siku. Wakati jumla ya kondoo 403 ikiwa ni sawa na wastani wa kondoo 134 kwa mwezi na 4.5 kila siku. Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa mbuzi na kondoo wengi majike walichinjwa (860 sawa na asilimia 57.12) kuliko madume (615 sawa na asilimia 42.88). Asilimia 38.5 ya majike kwa kondoo na mbuzi waliochinjwa walipatikana kuwa na mimba na kati ya hao asilimia 77.8 walikuwa na mimba kubwa zaidi ya miezi miwili. Aidha kulingana na matokeo haya, kwa kila mbuzi au kondoo watatu wanaochinjwa kila siku alipatikana na mimba ya kijusi kimoja au mapacha au zaidi na hakukuwa na tofauti yeyote kwa miezi yote mitatu.

Matokeo haya yameonesha kwamba kuna upotevu mkubwa wa vijusi kwenye machinjio ya mbuzi/kondoo kutokana na kuchinja mbuzi/kondoo wenye mimba mkoani Tanga. Hii inapunguza upatikani wa protini na ukuaji wa ufugaji wa mbuzi/kondoo mkoani Tanga. Hivyo watafiti wanashauri hatua za kisheria za kuzuia uchinjaji wa mbuzi/kondoo wenye mimba kuwepo. Pia elimu ya kubaini mbuzi/kondoo wenye mimba kutolewa kwa wahusika wa uchinjaji ili kupunguza uchinjaji wa mbuzi wenye mimba.

Chapisho zima:  Kwa lugha ya kiingereza lipo hapa

Leave a Reply