Utajuaje kama mayai ya kuku yataanguliwa?

Na Augustino Chengula

 

Ni jambo jema kufahamu kama mayai yanayo atamiwa na kuku wako yataanguliwa yote au mangapi hayataanguliwa. Na kwa wanaototoresha vifaranga ni muhimu zaidi kwao kujua hali ya mayai inavyoendelea ndani ya incubeta na kama kuna tatizo linatokea linalosababisha kifaranga ndani ya yai kufa. Lakini pia yale ambayo hayatapelekea kutotoa kifaranga kuyaondoa. Kujua hili lazima uyachunguze mayai kila siku.

 

Na makala hii imelenga kukujuza namna ya kuchunguza mayai hayo na kujua kama (a) yana kifaranga hai (b) kifaranga kimekufa (yai viza) na (c) kama yai halina kifaranga. Kuku anaweza kutaga mayai kukiwepo na jogoo au bila hata kuwepo na jogoo. Kazai ya jogoo ni kurutubisha mayai ili yaweza kuwa na kifaranga ndani. Hivyo yale yatakayorubishwa na jogoo yatakuwa na kifaranga ndani wakti yale ambayo hayajarutubishwa na jogoo hayatakuwa na kifaranga. Hii ni pointi muhimu ya kuzingatia maana tutaitmia huko hapo baadaye kadiri tunavyoendelea.

 

 

Kutotolesha mayai kwa njia ya asili (kuku)

Mayai yanayototoreshwa na kuku hayana vitu vingi vya kuzingatia maana ni kuku mwenyewe anayeyapatia joto mayai ili yaje kuangua vifaranga. Unaweza kuchagua kuku mwenye uwezo mzuri wa kutamia na kukupatia vifaranga na akaatamia mayai ya wale kuku wasio na uweezo wa kuatamia. Lakini kuku huyu pia awe na sifa nyingine ya kulea vifaranga mara baada ya kuangua. Kuku wa aina hii watakuwa kama mashine ya kuangua vifaranga ndani ya shamba lako. Hivyo watahitaji matundo ikiwa ni pamoja nav iota vizuri vya kuangulia, yaani sehemu salama kwa kuku kuatamia mayai kwa siku 21.

 

Kuku anayeatamia vizuri atakaa kwenye mayai usiku na mchana, akitoka nje mara moja kula au kutafuta chakula, kunywa maji na kunya kinyesi. Ukitaka kumtoa kwenye mayai bila ridhaa yake huwa mkali na anaweza kukufukuza kwa hasira. Kiota chake kikiwekwa mahali pautulivu, kuku huyu atageuza mayai mara 12 hadi 14 kutoka upande yalipolalia kwenye kiota. Mara kadha atakuwa akiyatawanya manyoya yake ya kifua ili joto lake la mwili liyafikie mayai na kuyafanya yabaki kuwa ya joto lile linalohitajika (nyuzi joto 37 za sentigredi). Lakini pia manyoya ya kuku hukifanya kiota chote kiendelee kuwa na joto.

 

Kutotolesha mayai kwa njia ya mashine (Incubeta)

Utotoleshaji wa mayai kwa njia ya mashine unafuata kanuni zinazotumiwa na njia ya asili (kuku). Incubeta imetengenezwa kufuata mahitaji yanayotolewa na kuku anayeatamia. Tumesema kuku ataatamia mayai kwa siku 21, atageuza mayai mara kwa mara, atayapa mayai joto (nyuzi joto 37 digirii za sentigredi) na unyevu nyevu. Hivyo hivi vyote lazima incubeta itemize yaani igeuze mayai, joto stahiki liwepo, unyevunyevu, na mayai yakae kwa siku 21.

 

 

Mayai yanayowekwa kwenye incubeta lazima yawe masafi na ambayo hayajapasuka.

 

Hivyo kama kuna mayai machafu, yamechafuliwa na kinyesi cha kuku yasafishwe vizuri na kitambaa/spongi safi. Kuepuka mayai kuchafuliwa na kinyesi ni bora ukusanye mayai mapema. Unaweza kukusanya mayai mara mbili kwa siku.

 

Uchunguzaji wa mayai yanayoatamiwa au yaliyopo kwenye mashine ya kuangulia vifaranga

Kuchunguza maendeleo ya mayai yanayoatamiwa au yaliyopo kwenye mashine ni muhimu sana. Hii itakusaidia kubaini kama mayai yako yana vifaranga, hayana vifaranga au vifaranga vimekufa. Hivyo utaondoa mayai yale ambayo hayataanguliwa.

 

Njia inayotumika inajulikana kama candling. Wagunduzi wa mwanzo walitumia mshumaa kubaini hayo niliyosema. Lakini sasa vipo vifaa vingi kuanzia vile vya kisasa hadi vile vya kawaida ambavyo vinapatikana mazingira yetu kirahisi mfano tochi. Utofauti uliopo ni kuwa vile vya kisasa mionzi yake inakusanywa pamoja kumulika eneo moja inaypenya kirahisi kuona ndani ya yai wakati mwanga kama wa torchi unatawanyika.

 

Kwa nini ufanye candling ya mayai?

Candling ni sehemu muhimu sana katika ufugaji wa kuku hasa unapofanya uchunguzi wa ukuaji wa kifaranga ndani ya yai. Hivyo candling ya mayai inakusaidia kuona nini kinaendelea ndani ya yai katika kila hatua ya ukuaji wa kifaranga. Mwanga mulika yai kwenye eneo lenye giza unaweza kuona baadhi ya vitu ndani ya yai.

 

Nini utaona wakati wa candling

Kwa yai hai lililorutubishwa utaona mishipa ya damu, kifaranga kikichezacheza na uwazi upande ule mkubwa.

Kwa yai ambalo kifaranga kimekufa (yai viza) huwezi kuona mishipa ya damu, utaona kifaranga ila hakichezichezi na huwezi kuona uwazi wa hewa upande mkubwa wa yai.

Kwa yai ambalo halikurutubishwa huwezi kuona chochote (mishipa ya damu, kifaranga).

Candling inatakiwa ifanyike kila siku hasa kwa wanaotumia mashine ili kubaini kama kuna tatizo lolote linalotokana na mashine na kulirekebisha. Chunguza yai moja baada ya jingine na hakikisha yai halikai nje ya incubeta zaidi ya nusu saa.

 

Candling ya mayai hatua kwa hatua

 

Hatua ya 1: Andaa eneo la giza kama unafanya candling wakati wa mchana hasa kwa utotoleshaji wa asili ukitegea kuku akiwa ameondoka kwenda kula. Tumia box au kitu chochote kutengeneza giza. Kwa utotoleshaji wa incubeta candling ni vizuri ikafanyika wakati wa usiku ambapo taa zitazimwa kuruhusu giza kuwepo.

Hatua ya 2: Chukua yai moja moja kwa uangalifu kutoka kwenye kiota au incubeta na liweke upande mkubwa umulikwe na mwanga. Yaani upande mdogo uwe juu na mkubwa chini unakotoka mwanga. Lishike yai upande ule mdogo kwa kidole gumba na kidole cha kati.

 

Hatua ya 3: Taratibu zungusha yai huku ukiliinamisha kidogo upande mmoja hadi pale unapoona vizuri.

 

Hatua ya 4: Tazama mayai kama yananyufa na  mipasukoili yaondolewe na weka alama eneo la hewa (uwazi upande ule mkubwa) ukitumia penseli zungusha mstari eneo hilo ili ikusaidie kulinganisha ukubwa kadiri siku zinavyoenda. Hatua ni pale unapofanya candling mwanzoni kabisa.

 

Hatua ya 5: Yape namba mayai kwa kutumia penseli tu wala si peni maana wino unaweza kupenya na kudhuru yai. Nayo hii inafanyika mwanzoni.

 

Hatua ya 6: Anza kufanya candling kila siku kuona maendeleo ya mayai. Toa yai na kurudisha kwenye incubeta au kiota kwa umakini ili usivunje. Hakikisha mikono yako ni misafi wakati wa candling. Andika matokeo ya candling kwa kila yai kwenye daftari la kumbukumbu.

MUHIMU: Unaweza kufanya candling kila siku tangu siku ya 1 hadi 16 au 17. Wengine hu candle siku ya 1, 7, 14 na 16.

 

Nini unapaswa kuona kwa siku unapofanya candling

 

Siku ya 1: Huwezi kuona chochote, japo candling siku ya kwanza ni muhimu ili kubaini kuwa mayai yote yanayowekwa kwenye incubator ni mazima, hayana mipasuko. Mipasukuko itaruhusu bakteria lakini pia kifaranga hakitatengenezwa, hivyo yasitumike.

 

Siku ya 4: Hapa utaona mishipa ya damu ikisambaa kwenye yai na itaonekana kama nywele. Kama hujaona chochote siku hii subiri siku ya saba kuna mayai mengine huchelewa kidogo.

Siku ya 7: Siku unatakiwa kuona mishipa ya damu vizuri na ule upande mkubwa utaanza kuona eneo la uwazi la hewa likijitokeza. Hewa hii itatumiwa na kifaranga.

 

Siku ya 10:  Hapa utaanza kuona kifaranga na kwa kiasi kinacheza cheza. Eneo la hewa sasa limetanuka na kuwa kubwa unaliona vizuri. Utaona pia kidoti cheusi kinachoonekana vizuri ambalo ni jicho la kifaranga. Hakikisha kufikia siku hii uwe ume candle mayai yote.

Siku ya 17:  Kufikia siku hii kila kitu huonekana kusimama n ahata hupelekea wafugaji wengi kupaniki wakidhani Vifaranga vimekufa kwasababu hawaoni chochote (giza tupu). Lakini hali hii ni ya kawaida kwasababu kifaranga kimejaa karibu yai lote na kifaranga sasa kinaelekea kuanguliwa. Usijaribu kuchezesha yai sana wakati huu kwani kifaranga kinajiandaa kutoka.

 

Siku ya 18:  Usiendelee na candling siku hii. Sasa ni wakati wa kuacha uchunguzi na tamaa ya kujua nini kinaendelea kwenye mayai kwani vifaranga wako wataanza kutotolewa muda wowote. Ni muhumu sana wakati huu kutokufungua incubator yako tena kwani joto na unyevu vinapaswa visishuke ndani ya incubata.

 

Siku ya 21:  Hii ni siku ya kuanguliwa vifaranga. Hapa kifaranga kwa kutumia mdomo wake hugonga gonga yai ili kitoke. Hapa kuna maajabu hutokea, yai hutembea kwasababu ya kuongwa gongwa na kifaranga kilichopo ndani. Kunakuwa na kelele za kugonga gamba la yai na wakati kifaranga kikijaribu kutoka kwneye yai. Baada ya jitihada za kutoka mwisho kifaranga hifanikiwa kutoka kikiwa kibichi na kimechoka.

Kuna baadhi yenu watakuwa wamesha ona namna kifaranga kinavyovurukuta kutoka kwenye yai. Kitendo cha kifaranga kuanguliwa  kinafurahisha na kinafundisha hasa ukitaka kujifunza.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Reply