Watu wengi wamekuwa wakianzisha miradi ya ufugaji wa kuku bila kuzingatia kanuni bora za utekelezaji wa mradi huo. Moja ya mambo ambayo wafugaji mara nyingi husahau kuzingatia ni utoaji wa chanjo sahihi na kwa muda muafaka.

Kuku akichanjwa na chanjo ya matone inayodondoshewa kwenye macho: Ni njia rahisi kwa mfugaji mwenyewe kuchanja.
   

Ni muhimu kufahamu mambo unayotakiwa kuzingatia katika kuwapatia kuku chanjo. Wakati wa kutayarisha mpango wa kuchanja kuku kwa ajili ya kinga dhidi ya magonjwa, kuna vipengele vikuu sita ambavyo unatakiwa uvifahamu na kuvizingatia kama ifuatavyo:

 1. Vifaranga vinavyoanguliwa kwa pamoja: Iwapo una kundi zaidi ya moja la vifaranga wanaoanguliwa, weka utaratibu wa chanjo ambao utapunguza uwezekano wa magonjwa kuenea shambani.
 1. Umri wa kuchanja kuku: Kwa kuku ambao wanatarajiwa kutaga mayai au kuwa kuku wazazi, chanjo nyingi hutolewa si zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kuku kuanza kutaga.
 1. Magonjwa makuu katika eneo husika: Ni muhimu sana kuelewa magonjwa ya kuku yaliyopo katika eneo lako kabla ya kuandaa program ya uchanjaji, kwa magonjwa ambayo chanjo zenye vimelea hai hutumika.
 1. Hali ya kiafya ya kuku watakaochanjwa: Usiwape chanjo kuku ambao wanaonesha dalili za kuathirika kwa mfumo wa hewa au wanaonesha kuwa na minyoo au wadudu wengine. Kwa kuku walio na dalili hizi chanjo zinaweza kuleta madhara.
 1. Aina ya kuku watakaochanjwa: Kuku wanaofugwa kwa ajili ya nyama wanahitaji kinga ya muda mfupi, hivyo basi chanjo moja inaweza kutosha. Lakini kuku wa mayai na kuku wazazi wanahitaji mpango wa chanjo ambayo itawakinga na magonjwa kwa kipindi chote wanapokua na kutaga.
 1. Historia ya magonjwa katika shamba: Kabla ya kuandaa mpango wa chanjo, lazima ufahamu ni magonjwa gani yaliyoenea katika shamba.
 • Kama unataka kuingiza kuku wapya kutoka mahali ambako ugonjwa umeshawahi kutokea, kuku hao wachanjwe wiki 3 kabla ya kuwaingiza shambani.
 • Iwapo utatumia chanjo yenye vimelea hai, hakikisha kwamba magonjwa hayo yameshawahi kutokea katika shamba husika. Usitumie chanjo hizi katika shamba ambalo ugonjwa huo haujawahi kutokea au kutambuliwa.
 • Wasiliana na mashamba jirani kufahamu iwapo wanatumia chanjo zenye vimelea hai.

Mambo muhimu ya kuzingatia

 • Hakikisha unazingatia kwa makini masharti ya mtengenezaji wa chanjo: Jinsi ya kuhifadhi, kutayarisha na njia inayotumika kumchanja kuku. Wakati wote zingatia masharti ya mtengenezaji kuhusu uhifadhi wa chanjo ili isipoteze nguvu.
 • Fuata ushauri wa daktari wa mifugo unapoandaa mpango wa chanjo
 • Watumie wataalamu waliopatiwa mafunzo ya utoaji chanjo
 • Chagua aina ya chanjo kulingana na umri na hali ya kiafya ya kuku
 • Fanya usafi wa mara kwa mara katika mabanda ili kupunguza wingi wa vimelea kwenye mazingira
 • Tumia maji ambayo hayajawekwa dawa au kemikali kwa ajili ya kuchanganyia chanjo, kwa mfano maji ya kisima, mvua na kadhalika. Maji ya kuchanganyia chanjo yawe na ubaridi, yasiwe moto.
 • Changanya chanjo kabla ya kutumia na iwekwe mbali na kuku.
 • Pata ushauri wa daktari wa mifugo kabla ya kuchanja kuku wagonjwa au wale ambao hawako katika muonekano mzuri.
 • Siku ya chanjo, usiwape kuku maji kwa masaa 3 – 4 ili waweze kunywa maji yaliyowekwa chanjo kwa haraka.
 • Zoezi la uchanjaji lifanyike haraka ili kupunguza usumbufu kwa kuku.
 • Tenganisha kuku waliochanjwa na wale ambao hawajachanjwa.
 • Baada ya kuchanjwa, kuku wawekwe kwenye banda linalopitisha hewa vizuri.
 • Baada ya kila zoezi la kuchanja, wafanyakazi wabadilishe mavazi, viatu/buti zisafishwe na kuwekwa dawa, na vifaa vilivyotumika viwekwe dawa ya kuua vimelea.
 • Fuata utaratibu uliowekwa wa kuharibu/kusafisha vifaa vilivyotumika kuchanja.
 • Weka kumbukumbu za uchanjaji.

AINA ZA CHANJO

 

 

 

CHANZO: Mkulima Mbunifu

Leave a Reply