Utunzaji bora wa kuku wa kisasa

Kuku wa kisasa ni kuku maalum ambao wamezalishwa kwa madhumuni ya nyama au kutaga mayai. Ufugaji wa kuku wa kisasa unahitaji utaalamu maalumu.

Uzalishaji wa kuku hawa-huweza kufanywa na mfugaji mwenyewe kwa kutotolesha vifaranga au kununua vifaranga kutoka kwenye kituo au mashamba ya kutotolea vifaranga.

UTOTOAJI WA VIFARANGA
Utotoaji wa vifaranga hufanywa na kuku, au mashine maalum za kutotolea vifaranga.
Kuna aina mbili za mashine zinazotumika zaidi, nazo ni:-

Mashine Inayofanana na Meza
Mashine zilizo kama meza kwa kawaida ni ndogo na zina uwezo wa kuchukua mayai machache kuanzia hamsini hadi mia tano. Mashine hizi huitwa “Flat table incubators” na zina sahani kubwa za mraba ambamo huwekwa maji. Pia hutumia maji ya moto au hewa yenyejoto. Kati ya rnashine hizo, zipo zinazotumia umome au mafuta ya taa.

Mashine za Aina ya Masanduku au Makabati Makubwa ya Chuma au Mbao
Mashine zinazofanana na masanduku au makabati hutumia umeme. Mashine hizi ambazo huchukua mayai mia tano au zaidi huitwa “Cabinet machines” na hutumia mapanga boi katika kuingiza na kutolea hewa. Zina namna ya kuangalia joto sahihi na kugeuza mayai, na hujirekebisha zenyewe.
Mayai huwekwa kwenye chano za kuatamia, upande mpana huelekea juu na ule uliochongoka huelekea chini. Kugeuzwa kwa mayai hufanyika kwa kuzilaza upande kidogo chano zenye mayai hayo.

Chumba Chenye Mashine za Uanguaji
Chumba cha kuwekea mashine kijengwe kwa matofali ya saruji na vile vile kisiribwe kwa saruji ili kuzuia kubadilika kwa hali ya joto.

Mayai Yanayofaa kwa Kuanguliwa na Mashine
Mayai hayo yatokane na kuku wazazi waliopimwa damu na kuthibitishwa kuwa hawana magonjwa yanayoweza kurithiwa na vifaranga. Mayai yawe safi na yenye uzito kati ya gramu hamsini hadi gramu sabini. Vile vile yasiwe na nyufa, mchongoko mkali au ya mviringo.
Baada ya kukusanya mayai yaache yapoe kwa usiku mmoja yakiwa juu ya chano za mayai. Baadaye yahifadhi kwenye chumba kisichopitisha upepo, chenye nyuzijoto kati ya 12.8 hadi 15.6 za Sentigredi, unyevunyevu wenye asilimia 75 hadi 80 na kisichopitisha upepo. Mayai yanayokusudiwa kuhifadhiwa zaidi ya juma moja yawekwe kwenye chano sehemu zilizochongoka zikielekea chini. Mayai yaliyowekwa katika hali hiyo, hayahitaji kugeuzwa.

Uendeshaji na Utunzaji wa Mashine
Mashine itumike kufuatana na maagizo ya mtengenezaji. Washa mashine kwa saa 12 hadi 24 kabla hujaweka mayai. Baada ya kuwasha mashine hakikisha kuwa vifaa vyote vinafanya kazi sawasawa. Weka mayai kwenye mashine sehemu pana ikielekea juu.
Kama unatumia mashine inayofanana na meza, anza kuyageuza mayai saa 24 baada ya kuyaweka kwenye mashine. Mayai yageuzwe mara tatu kwa siku hadi kufikia siku ya tisa. Katika mashine inayofanana na sanduku au kabati mayai hayahitaji kugeuzwa kwa mkono. Utambuaji wa mayai yasiyofaa kuanguliwa ufanyike baada ya siku tisa na ya kumi na tano katika mashine inayofanana na meza. Katika mashine inayofanana na kabati, utambuaji ufanyike baada ya siku kumi na nane.
Mayai ya kuanguliwa yakichunguzwa kwenye mwanga baada ya siku tisa yataonyesha mishipa ya damu kando ya kiini. Hali hiyo hujitokeza zaidi baada ya siku kumi na tano na kumi na sita.
Mayai yasiguswe wala mashine kufunguliwa siku tatu kabla ya kuanguliwa. Baada ya siku ishirini vifaranga hao watolewe kwa uangalifu ili wasipigwe na baridi wakati wa kuwahamishia kwenye sehemu ya kulelea. Vifaranga wote dhaifu na waliochelewa kutotolewa hawafai kukuzwa.
Vifaranga wapelekwe kwenye chumba maalum kwa ajili ya kukaguliwa ili kuondoa walio na vilema, wasiokauka vitovu na manyoya Vifaranga kwa ajili ya mayai watenganishwe na vijogoo na wapatiwe chanjo.
Baada ya hapo wawekwe kwenye makasha tayari kwa kuuzwa au kupelekwa kwenye sehemu ya kukuzia. Kabla ya kuweka mayai mengine ya kuanguliwa katika mashine, ni lazima kusafisha vyano na mashine na kufukiza dawa inayopendekezwa kama vile “Potassium permanganate” au Formalin 40%.

MATAYARISHO KABLA YA VIFARANGA KUWASILI
Chumba
Vifaranga walelewe katika chumba maalum hadi umri wa majuma manne. Chumba kitayarishwe siku kumi na nane kabla ya vifaranga kuwasili. Matundu yote yaliyo kwenye sakafu, dari, madirisha na ukuta yazibwe. Kama chumba hicho kina sakafu ya saruji, kisafishwe kwa maji ya moto na baadaye kinyunyizie dawa kama vile Rhino au Dettol ya kuua wadudu Ikiwa chumba hicho hakina sakafu ya saruji, toa takataka kisha mwagia chokaa. Ili kuyaweka mazingira katika hali ya usafi na kuzuia wadudu waharibifu yasafishe hadi kufikia upana wa mita mbili au zaidi kuzunguka banda.
Katika chumba watakamofikia vifaranga tengeneza sehemu maalum ya kulelea. Sehemu hiyo maalum inatakiwa iwe na umbile la duara, itengenezwe kwa kutumia karatasi gumu, waya wenye matundu madogo au majamvi. Mduara huhifadhi joto, huzuia upepo na huzuia vifaranga wasiende mbali na chanzo cha joto.

 yumba ya kuku1

Mduara wa Kulelea Vifaranga

Kama chumba ni kidogo unaweza kuweka vizuizi kwenye kona za chumba hicho ili vifaranga wasijikusanye katika sehemu hizo Tandaza makapi ya mazao mbali mbali, maranda au nyasi kavu katika kina cha sentimita 7 hadi 10. Funika na karatasi ili kuzuia vifaranga wasile makapi na wasipate vumbi. Tabaka hili linasaidia kuhifadhi joto, kuzuia harufu mbaya, kunyonya unyevunyevu na kupunguza uwezekano wa vifaranga kupatwa na magonjwa.

Vifaa vya Joto
Vifaranga wanaweza kupatiwa joto kwa kutumia vyombo vya umeme, taa za chemli au jiko la mkaa.

Taa ya Umeme
Njia nzuri na rahisi ya kulea vifaranga ni kwa kutumia taa kubwa nyekundu za umeme (wati 200 au 275) au tumia kipasha joto (Heater) Taa moja ya umome inatosha kulea vifaranga mia moja thelathini katika sehemu za joto na vifaranga mia moja katika sehemu za baridi. Mwanzoni taa iwekwe umbali wa kati ya sentimita 35 hadi 37 kutoka sakafuni Unavyeza kurekebishajoto kwa kupandisha au kushusha taa. Unapaswa kuwa na jiko la mkaa au taa ya chemli kwa tahadhari ya umeme kukatika.

Jiko la Mkaa
Unapotumia jiko la mkaa ni lazima uhakikishe kwamba mkaa unaotumia hautoi moshi na chumba kina hewa safi na ya kutosha Weka jiko juu ya matofali ili kuzuia vifaranga wasiliguse.

Taa ya Chemli
Kama utatumia taa ya chemli, iweke juu ya matofali ma izungushiwe waya ili kuzuia vifaranga wasiiguse. Taa moja inatosha kutoajoto kwa vifaranga hamsini. Hakikisha kwamba taa hiyo haivuji na unayo akiba ya mafuta ya kutosha. Usitie mafuta mengi kwenye taa ili kuepuka kulipuka kwa taa.
Vifaa vya joto vianze kufanya kazisaa tatu au zaidi kabla ya vifaranga kuwasili ili chumba kipate joto la kutosha. Vile vile ni muhimu kutayarisha madawa na chakula siku moja kabla ya kuwasili vifaranga.

UAGIZAJI WA VIFARANGA
Ni muhimu mfugaji ufahamu mahali pa kupata vifaranga wa mayai au wa nyama wenye sifa zifuatazo:
· Wawe na nguvu na afya nzuri
· Wawe wamekauka vizuri baada ya kuanguliwa
· Wawe wamepata chanjo kuzuia magonjwa mbali mbali
· Wasiwe na vilema au magonjwa yoyote.
Agiza vifaranga kutoka katika mashamba au vituo vya kutotolea vifaranga vinavyotambulika kama vile, Interchick Co. Ltd. (Dar es Salaam), Pol Italia (Dar es Salaam), Kazmin (Dar – es Salaam), Kibo Poultry (Moshi), Arusha Poultry Farms (Usa River Arusha) na Marungu Farms (Tanga).

Mapokezi ya Vifaranga
Baada ya vifaranga kuwasili kutoka kwenye vituo vya kutotolea, wapelekwe moja kwa moja hadi kwenye sehemu maalum ya kulelea. Mara tu vifaranga wakiwasili, masanduku yaingizwe ndani na yawekwe moja moja na siyo moja juu ya lingine Vifaranga wakaguliwe, wahesabiwe na kisha wawekwe katika sehemu maalum ya kulelea.
Vifaranga wapewe maji safi, endapo watakuwa wamechoka wapewe maji yaliyochanganywa na sukari laini au glukosi kiasi cha vijiko viwili vya chakula katika lita tano za maji. Vile vile ongeza mchanganyiko wa vitamini kama vile Vitox.

 

ULISHAJI
Baada ya saa tatu hadi nne wapewe chakula maalum cha kuning’inizwa kwa kamba ili kuwapatia vitamini, madini na protini, na kuzuia tabia ya kudonoana.
Hakikisha chumba ni kisafi na hakina unyevunyevu wakati wote. Unyevu husababisha ugonjwa wa baridi ambao hufanya vifaranga wajikunyate na kutetemeka na wanaweza kufa ghafla.

JOTO
Joto ni muhimu katika uhai wa vifaranga. Katika juma la kwanza joto lihalostahili katika sehemu ya kulelea ni nyuzi joto 35 za Sentigredi. Joto hili hupimwa kwa kutumia kipima joto ambacho huwekwa Sentimita nne hadi tano kutoka kwenye mduara. Kiasi hiki kipunguzwe kwa nyuzi joto mbili za Sentigredi kwa kila juma hadi kufikia nyuzi joto 27 za Sentigredi katika juma la tano. Angalia jedwali namba 2:

Jedwali Na. 2

Juma

Joto
1 35°C
2 33°C
3 31°C
4 29°C
5 27°C

Ikiwa huria kipimajoto, unashauriwa uangalie tabia na mwenendo wa vifaranga.
Kama vifaranga wakichangamka wakinywa maji vizuri na kutawanyika sehemu zote, joto hilo linatosha.

 Joto la kuku

Joto linalotakiwa

Kama joto halitoshi, vifaranga hujikusanya karibu na taa au hujirundika katika sehemu moja. Hivyo unashauriwa kuongeza joto kwa kuongeza idadi ya vifaa au nguvu ya joto kwa mfano umeme.

 Joto dogo

Joto Kidogo

Ikiwa joto ni kali sana utaona vifaranga wanakaa mbali na taa, wakipanua mabawa yao na wakihema haraka haraka. Hali hii ikizidi huleta ugonjwa wajotojingi, ambao husababisha vifaranga kuanguka chini Hali hiyo ikitokea unashauriwa kupunguza idadi ya vyombo vya joto na kuwapa maji mengi ya kunywa.

 Joto kali

Joto Kali

Baada ya majuma manne, vifaranga watolewe kwenye sehemu maalum ya kukuzia na kupelekwa kwenye banda la kufugia. Kabla ya kuwahamisha tenganisha vijogoo kutoka kwenye kundi la vifaranga ikiwa vifaranga hivyo ni kwa ajili ya kuku wa mayai.

MALEZI YA MITEMBA NA MITETEA


Mitemba
Vifaranga wenye umri wa kuanzia majuma manne huitwa mitemba. Kuku wa umri huu wanahitaji chakula maalum cha kukuzia. Chakula hicho hupatikana katika vituo vinavyouza vyakula vya kuku, ikiwa huwezi kupata vyakula nivyo, tengeneza mwenyewe kwa kutumia aina mbali mbali za vyakula. Pamoja na kuwapa chakula, hakikisha pia unawapa maji safi na ya kutosha.
Kila kuku wanne hadi watano wanahitaji eneo la mraba wa mita moja. Epuka msongamano wa kuku wengi katika eneo dogo. Msongamano husababisha vifo kwa kukosa hewa. Vile vile husababisha kuku kudumaa, kudonoana na kuchafuka kwa nyasi zinazotandikwa ndani.
Mitemba ikifikia umri wa majuma kumi na sita wawekewe viota.

Mitetea
Mitemba ikishafikia umri wa majuma kumi na nane huitwa Mitetea. Mitetea waliodumaa na majogoo waondolewe katika kundi la mitetea bora.
Zuia viroboto, chawa na utitiri kwa kutumia dawa zinazoshauriwa na wataalamu.
Ni muhimu kupunguza midomo ya mitetea ili wasidonoane. Mitetea hudonoana kutokana na upungufu wa protini, msongamano, mwanga mwingi na kukosa mazoezi. Ili kupunguza kudonoana ongeza protini ya asili ya nyama, ning’iniza majani mabichi, wawekee bembea ndani ya banda na ongeza nafasi ya banda kulingana na idadi ya kuku. Kama tabia ya kudonoana aendelea punguza midomo ya juu kwa kutumia mkasi, kisu, panga au kifaa maalum. Kisu au panga liwe la moto

 Debeaking
Jinsi ya kupunguza mdomo wa kuku kwa kutumia mkasiKulisha
Kuku wanapokaribia kutaga wanatakiwa wabadilishiwe chakula na kupewa chakula cha kutagia (Layers mash), badala ya chakula cha kukuzia (Growers mash). Mabadiliko hayo ya chakula yasifanyike ghafla. Changanya chakula cha kukuzia na kutaga katika uwiano ufuatao:

Juma Chakula cha kukuzia Chakula cha kutagia
18 Sehemu 3 Sehemu 1
19 Sehemu 2 Sehemu 2
20 Sehemu 1 Sehemu 3
21 Sehemu 0 Sehemu 4

Sehemu hizo zinaweza kuwa katika vipimo kama kopo, karai, sahani kubwa, ndoo au debe. Mfuko wa kilo 50 wa chakula cha kutagia unaweza kutumika kwa kuwalisha kuku 100 kwa siku nne. Kuku mmoja wa mayai anahitaji kilo 50 za chakula katika maisha yake yote. Hakikisha kuwa kuna maji safi ya kutosha wakati wote.
Wasipewe chakula kingi kupita kiasi kwa sababu watanenepa na hawatataga mayai ya kutosha. Chakula kidogo husababisha kuku wasitage vizuri. Inashauriwa kuongeza majani mabichi ambayo ni laini ili kuku wapate vitamini, madini na protini ya kutosha.

Utagaji na Ukusanyaji wa Mayai
Kwa kawaida kuku huanza kutaga wanapofikia umri wa majuma ishirini na mbili. Kuku wa mayai aliyetunzwa vizuri anaweza kutaga mayai zaidi ya 250 kwa mwaka, na Kuku wa mayai ana nwezo wa kutaga vizuri kwa muda wa mwaka mmoja hadi mmoja na nusu tangu anapoanza kutaga. Mfugaji achunguze kuku mara kwa mara na kuwaondoa wasiotaga.

Dalili za Kuku Wasiotaga
– Ukiingia kwenye banda kuku huruka na kukimbia ovyo. Ukimshika ni mwepesi sana.
– Upanga wake umekauka na kupauka.
– Sehemu yake ya kutagia huwa kavu
– Kuku asiyetaga vidole vitatu haviingii kwenye nafasi iliyoko kati ya mifupa miwili ya sehemu ya kutagia.

 Uchunguzi
Jinsi ya kukagua kuku asiyetaga vizuri

Ukusanyaji wa mayai ufanyike mara tatu au zaidi kwa siku ili kuzuia mayai yasichafuke, yasipasuke na kuzuia baadhi ya kuku wasiatamie na kula mayai. Baada ya kipindi cha kutaga kuisha, kuku wauzwe au kutumika kwa chakula kwani utagaji wao hupungua na hula chakula kingi.

MATUNZO YA KUKU WAZAZI
Kuku wazazi ni wale wanaotaga mayai kwa ajili ya kutotolea vifaranga. Misingi ya matunzo ya kuku hawa haitofautiani sana na ile ya kuku wa mayai isipokuwa:-
– Hulishwa chakula kwa kiwango maalumu kila siku au kila baada ya siku moja tangu wakiwa wadogo.
– Kuna utaratibu wa kuwapima uzito kila baada ya muda wa wiki mbili hadi tatu ili wasizidi uzito unaotakiwa.
Katika juma la kumi na nane kuku wazazi walishwe chakula cha kuku wazazi (Breeders mash) kama inavyoonyeshwa katika jedwali lifuatalo:-

Juma Chakula cha Kukuzia Chakula cha Kuku Wazazi
18 Sehemu 3 Sehemu 1
19 Sehemu 2 Sehemu 2
20 Sehemu 1 Sehemu 3
21 Sehemu 0 Sehemu 4

– Majogoo wanafugwa sehemu tofauti na mitetea, lakini wanachanganywa na mitetea wanapofikia umri wa kuweza kupanda.
– Uwezo wao wa kutaga mayai ni mdogo, ni chini ya mayai 200 kwa mwaka.
– Jogoo mmoja anaweza kupanda mitetea saba hadi kumi kwa wakati mmoja. Katika kundi la mitetea 7 hadi 10, kuwe na jogoo mmoja.
Tunza majogoo ya ziada ili yatumike endapo baadhi ya majogoo wanaotumika watapatwa na matatizo. Ni muhimu kufuata maagizo ya uzalishaji.
Gharama ya kununua kifaranga cha kuku wazazi ni kubwa zaidi ya vifaranga wa mayai ya biashara.

UTUNZAJI BORA WA KUKU WA NYAMA
Kuku wa nyama wana uwezo wa kukua haraka. Huwa tayari kuuzwa au kuchinjwa baada ya muda wa majuma saba hadi nane. Kuku hao huwa na uzito wa nyama usiopungua kilo moja kwa muda mfupi kuliko kuku wengine.
Matunzo ya kuku wa nyama yanafanana na ya kuku wa mayai, tofauti ni hizi zifuatazo:
· Majogoo na majike hawatenganishwi.
· Huhitaji nafasi ndogo kuliko kuku wa mayai.
· Wanalishwa chakula cha kunenepesha toka siku ya kwanza.
· Wanakula chakula usiku na mchana.
· Mifuko 8 hadi 10 inatosbeleza kuku 100 kwa majuma nane.

 

Leave a Reply