Na Augustino Chengula
Ugonjwa wa homa ya nguruwe unaojulikana kwa kitaalamu kama African Swine fever (ASF) unasababishwa na virusi vijulikanao kwa kitaalamu kama African Swine fever virus. Homa ya nguruwe ni ugonjwa unaoambukizwa kutoka nguruwe mmoja kwenda mwingine kwa kasi kubwa sana. Mbali na kuwa ugonjwa huu hujitokeza kwa nguruwe wanaofugwa, nguruwe pori pia hutunza vimelea vya ugonjwa bila wao kuugua. Nguruwe pori hawa wanauwezo wa kueneza vimelea vya ugonjwa huu kwa nguruwe wa kufugwa kwa njia ya kupe laini wajulikanao kitaalam kwa jina la Ornithodoros moubata na kusababisha mlipuko wa ugonjwa. Kupe humeza virusi wanaponyoonya damu na kueneza kwa nguruwe wa kufugwa wanaponyonya damu. Nguruwe wanaozurula hovyo ni chanzo cha kuumwa na kupe walioanguka toka kwa nguruwe pori. Ugonjwa huu umekuwa ukijitokeza mara nyingi hapa nchini hasa ukianzia maeneo ya Mbeya, Rukwa, Iringa na Morogoro. Mara hii ugonjwa huu umeibukia kanda ya ziwa katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza. Ugonjwa huu mkoani Mwanza tayari umeshathibitishwa na Maabara ya chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Serikali imekwisha kutoa tangazo lake la uwepo wa ugonjwa huu na namna ya kukabiliana nao (kiambatanisho hapa chini). Maelezo ya kina ya dalili za ugonjwa huu na historia yake hapa nchini pia yapo hapa chini.
Usambaaji wa ugonjwa
Mara nyingi nguruwe hupata maambukizi kwa kugusana na nguruwe mwenye maambukizi au kwa kula mabaki ya vyakula yenye vimelea vya ugonjwa hasa mabaki ya mazao ya nguruwe mfano mautumbo ya nguruwe au chakula chochote kilichochanganyika na vimelea vya ugonjwa. Wadudu wengine wanaoweza kuuma nguruwe kama nzi na kupe wanauwezo wa kueneza ugonjwa kwa nguruwe wengine.
Je, ugonjwa wa homa ya nguruwe unaweza kumpata binadamu?
La hasha, ugonjwa wa homa ya nguruwe hauambukizwi kwa binadamu hata kidogo. Hivyo si tishio kwa binadamu, madhara makubwa ni kuteketeza nguruwe kwa muda mfupi na kumpa hasara kubwa sana mfugaji.
Dalili za ugonjwa wa homa ya nguruwe
Dalili hizi zaweza kujionyesha dhahili au zisijionyeshe wazi wazi wakati huo ugonjwa ukiwa unasambazwa. Dalili ku inayoambatana na ugonjwa huu ni kuvuja na kusambaa kwa damu kwenye viungo vingi vya mwili wa mnyama. Dalili nyingine ni kama ifuatavyo;
- Homa kali sana
- Nguruwe kupoteza hamu ya kula
- Muonekano wa damu mithili ya vinuka kwenye ngozi hasa masikioni, tumboni na miguuni
- Muonekano wa damu kwenye viuongo mbalimbali vya ndani ya nguruwe baada ya kumpasua
- Kupumua kwa shida
- Kutapika
- Kutoka damu puani na sehemu ya haja kubwa na mara chache kuharisha
- Kutupa mimba mara nyingi huwa ni kiashiria cha kwanza kuonekana kama kuna nguruwe wenye mimba
- Vifo kwa nguruwe ndani ya siku 2-10
- Nguruwe wote wanaweza kufa kwa ugonjwa huu
Dalili nyingine kwa nguruwe wanaokaa na ugonjwa muda mrefu ni kupoteza uzito, homa za mara kwa mara, dalili za mfumo wa upumuaji na vidonda sugu kwenye ngozi na kwenye maungio mfano magoti.
Utambuzi wa ugonjwa huu
Utambuzi wa awali unaweza kufanywa kwa kutumia dalili za ugonjwa wenyewe na kisha sampuli kupelekwa kwenye maabara ili kuuthibitisha kwa kutumia njia mbalimbali za kitaalamu.
Kukabiliana na ugonjwa
Madhara yake kwa nguruwe yanaweza kuwa makubwa au madogo yasiyoweza kuonekana kwa macho. Homa ya nguruwe haina tiba maalumu wala chanjo inayofaa na hivyo uzuiaji wa ugonjwa huu unategemea sana utambuzi wa ugonjwa mapema na kisha kuzuia utembeaji wa holela wa nguruwe (karantini). Maonyo yamekuwa yakitolewa kupitia mikutano ya hadhara na vyombo vya habari kama magazeti ya kuzuia kutembea kwa mifugo ovyo pamoja na kuzuia kula nyama ya nguruwe kwa kuhofia kusambaa kwa ugonjwa.
Historia ya ugonjwa Tanzania
Ugonjwa huu umekuwa ukitokea mara kwa mara katika nchi yetu na kuathiri mifugo na soko la nguruwe kwa ujumla. Ugonjwa huu uliripotiwa kwa mara ya kwanza Tanzania mwaka 1914 ukifuatiwa na mlipuko mwingine mwaka ya 1962. Mlipuko mkubwa wa ugonjwa huu ulilipotiwa na Tasisi ya utafiti ya wanyama (ADRI), Dar es Salaam miaka ya 1987 an 1988 na kusababisha hasara kubwa sana kijamii na kiuchumi katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Kilimanjaro. Tafiti zilizo fanywa na wataalamu wa magonjwa ya virusi (Misinzo na wenzake, 2011) kwa kutumia sampuli kutoka Chunya, Ileje, Kyela, Loliondo, Ludewa, Temeke and Tukuyu zilizokusanywa kati ya mwaka 2010 na 2011 wakati wa mlipuko zilionyesha kuwepo kwa ugonjwa maeneo hayo. Ugonjwa huu kwa nchi yetu umekuwa ukiripotiwa kama mlipuko ukianzia maeneo ya Mbeya ambako unaaminika kutoka nchi ya jirani ya Malawi. Mwezi may 2011, mlipuko wa ugonjwa pia ulilipotiwa Dar es Salaam nah ii inatokana na sababu kwamba Dar es Salaam sasa imekuwa na wafugaji wengi wa nguruwe kwa vile ufugaji wa nguruwe unaonekana kuwa na faida kubwa kwa mfugaji.