Wapiganapo fahari wawili ziumiazo ni nyasi unaweza kusema kutokana na mauaji ya kikatili ya ng’ombe wilayani Mvomero. Pia unaweza kusema ni kupima upepo wa Waziri mpya wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwiguru Nchemba maana yameibuka siku ya kuapishwa kwake.
Historia ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji wilayani Mvomero umeanza muda mrefu na jitihada za kuutatua mgogoro huo hazijawahi kuzaa matunda. Chini ya kauli mbiu ya ‘HAPA KAZI TU’ na nia ya dhati ya rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli pamoja na serikali yake huenda ikaja na suluhisho ya kudumu ya migogoro ya wakulima na wafugaji nchini. Migogoro ya wakulima na wafugaji ni swala tanzu ambalo mikakati ya kuleta suluhu linatakiwa kufanywa kwa ushirika na wizara ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi na Wizara ya maji na umwagiliaji.
Katika mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyotokea siku ya Jumamosi tarehe 12/12/2015 katika kijiji cha Dihinda kata ya Kanga wilayani Mvomero yalisababisha mtu mmoja kufariki dunia na wengine kujeruhiwa vibaya.
Mapigano haya yameleta hasara kubwa sana kwa wafugaji kwa ng’ombe takribani 79 kuuawa na wengine 71 kujeruhiwa kwa kukatwa na mapanga. Ilikuwa ni simanzi kubwa sana kwa wafugaji na wale wote walioshuhudia ng’ombe wakifa na wengine kushindwa kusimama kwa majeruhi ya miguuni na wengine kwa majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
Mapigano haya yalimlazimisha Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwiguru Nchemba kuingilia kati na kuweka mikakati ya haraka ya kukabiliana na kuibuka kwa migogoro mipya baina ya wakulima na wafugaji. Nchemba alimwagiza Mkuu wa wilaya Mvomero, Beth Mkwasa kuunda kamati ya Ulinzi na Usalama katika wilaya ya Mvomero ili kamati ihusike maeneo yote ya Nchi yetu ili kuhakikisha wanaimarisha ulinzi maeneo yote yenye migogoro, pia wahakikishe waliosababisha maafa
Aidha Mheshimiwa waziri alikutana na wananchi husani wakulima na wafugaji na kuwaambia haya, nanukuu, “Natoa rai kwa Wananchi hususani wa jamii ya Wafugaji na Wakulima, kuwa hakuna ardhi au Mnyama mwenye thamani sawa na Maisha ya Mwanadamu yeyote yule, njia bora na salama ya kutatua migogoro hii inayohusisha wakuliama na wafugaji ni kufuata taratibu za kuonana na Uongozi wa Serikali wa eneo husika hatua kwa hatua, Nawaomba wananchi waache kujichukulia sheria mikononi, tunakwenda kuunda kamati za usuruhishi wa migogoro hii kwa kila kijiji zitakazohusisha pande zote mbili ili kubaini wavamizi wa maeneo na kuwachukulia hatua za kisheria.”
SIKILIZA KISA CHA MAPIGANO HAYO NA MAELEZO YA KINA HAPA CHINI