Uchanganyaji wa chakula cha kuku na ulishaji wake

 

 LISHE YA KUKU

Ili kuku waweze kuishi, kukua vizuri, kunenepa na kutaga mayai mengi ni lazima wale chakula kingi na chenye ubora unaotakiwa. Uwingi na ubora wa lishe ya kuku unaweza kuainishwa katika makundi ya vyakula kama ifuatavyo:

 1. Vyakula vya kutia nguvu
 2. Vyakula vya kujenga mwili
 3. Vyakula vya kuimarisha mifupa
 4. Vyakula vya kulinda mwili
 5. Maji.

 

Makundi ya vyakula

 

 1. Vyakula vya kutia nguvu

Vyakula vya mifugo vifuatavyo vinawekwa katika kundi hili;

 1. Pumba za mahindi, pumba laini za mpunga, na, pumba laini za ngano.
 2. Nafaka kama vile mtama , chenga za mahindi ,chenga za mchele, uwele , na ulezi
 3. Mimea ya mizizi kama vile muhogo, viazi vitamu na magimbi. Kabla ya kulisha kuku hakikisha mizizi hiyo inalowekwa kwa muda wa saa moja au kupikwa kabla ya kukausha ili kuondoa sumu ambayo kwa asili imo katika vyakula vya aina hii.Inashauriwa kuwa  mizizi hiyo ilishwe kwa kiasi cha asilimia 10% ya chakula chote anacholishwa kuku.

Katika kundi hili la kutia nguvu ,vyakula vya mafuta kama vile mafuta ya kutoka kwenye vyakula vya mafuta kama mashudu ya mimea ya mafuta, mafuta ya samaki husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini. Vyakula vya kutia nishati huchangia asilimia 60-70 ya mchanganyiko wote wa chakula.

 

 1. Vyakula vya kujenga mwili

Ø  Mashudu :Haya ni makapi ya mbegu za mimea aina ya mikunde na vyakula v vinavyotoa mafuta kama vile alizeti, mawese, karanga, soya ,korosho, na ufuta .

Ø  Damu ya wanyama iliyokaushwa (waliochinjwa na kukaguliwa), hii inafanywa ili kuepusha uwezekano wa kuku kupata magonjwa ya kuambukiza .

Ø  Mabaki ya samaki ya samaki/dagaa na nyama.

Ø  Vyakula asilia kama vile minyoo, mayai ya mchwa, Masalia ya nyama toka kwenye ngozi/mifupa, wadudu walioteshwa kutokana na damu au nyama iliyooza na vyakula vya aina nyingine.

Ø  Vyakula hivi huchangia asilimia 20 hadi 30% ya mchanganyiko wote wa chakula cha kuku.

 

 1. Vyakula vya kuimarisha mifupa(madini)

a)      Hivi ni vyakula vya madini ambavyo huhitajika kwa ajili ya kujenga mifupa, maganda ya mayai, kukua na kuuweka mwili wa ndege (kuku) katika hali ya afya njema kwa ujumla.

b)      Madini ya muhimu ni madini ya chokaa (calcium) na fosiforasi (phosphorus). Ili kuku watage mayai yenye ganda gumu ni lazima wapate madini ya chokaa maganda ya konokono na mayai yaliyosagwa vizuri. Lakini inapendekezwa kwamba unapoongeza madini ya fosforasi inakubidi uongeze pia madini ya chokaa kadri inavyopasa ,kwasababu kiwango cha aina moja kikizidi kuliko cha aina nyingine husababisha upungufu wa kile kidogo

Viinilishe vya madini vinavyotakiwa ni pamoja na;

Ø  Majivu ya mifupa yaliyosagwa vizuri, unga uliosagwa wa magamba ya konokono wa baharini, konokono wa nchi kavu na maganda ya mayai yaliyochomwa . Kabla maganda ya mayai na nyumba za konokono havijatumika inashauriwa yachomwe moto mkali au yachemshwe ili kuua vijidudu vya maradhi.

Ø  Chumvi ya jikoni

Ø  Madini yaliyotengenezwa viwandani kama vile Di-calcium phosphate

Ø  Magadi (kilambo).

 

 1. Vyakula vya kulinda mwili

Kundi hili linajumuisha vyakula vya mbogamboga kama vile;

Ø  Mchicha, samadi ya ng’ombe ambayo haijakaa muda mrefu baada ya kunyewa, mchicha pori, Chinese kabeji n.k.

Ø  na Mchanganyiko wa vitamini uliotengenezwa na viwanda vya madawa (vitamin premix).

Ø  Jua ni muhimu katika kuhakikisha vitamini A na D zinatumika vizuri mwilini, kwahiyo banda ni lazima lijengwe kwa mtindo ambao unaruhusu mwanga kupita hasa nyakati za asubuhi na jioni.

Ø  Chakula cha kuku wanaofugwa ndani ni lazima kichanganywe na vitamini zinazotayarishwa viwandani.

 

 KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU

Njia za kuchanganya chakula cha kuku;

Kuna njia kuu mbili za kuchanganya chakula cha kuku, nazo ni;

Ø  Kuchanganya chakula kwa mashine;

o   Njia hii hutumika viwandani kuchanganya chakula kwa ajili ya kuku wanaofugwa katika mashamba makubwa.

Ø  Kuchanganya chakula majumbani (home made ration): Hii ni njia inayotumika kuchanganya chakula kwa ajili ya kulisha kundi dogo la kuku na njia ambayo inaweza kutumiwa na wafugaji wadogowadogo.

VIFAA; Beleshi /koleo(spade), Turubai/sakafu safi, Viinilishe , Viroba/Magunia kwa ajili ya kuhifadhia chakula kilichochanganywa.

Chakula kilichochanganywa kinaweza kuwekwa katika uzani wa kilo 25-kilo 50, au kilo 100.

 

MCHANGANUO WA VIINILISHE VYA CHAKULA CHA KUKU

 

Aina ya chakula                                                                           kiasi

 1. Vyakula vya kutia nguvu mwilini

Pumba za mahindi                                                                            kilo   48

Pumba laini za mpunga                                                                   kilo   26

 Jumla                                                                                          kilo 74

 

 1. Vyakula cha kujenga mwili                                    

Mashudu ya alizeti                                                                  kilo 18

Damu ya wanyama                                                                     kilo   1

Mabaki ya samaki /dagaa                                                        kilo   3

    Jumla                                                                                kilo  22

 

iii. Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini)

 1. chumvi ya jikoni                                                                 kilo ½
 2. chokaa(dicalciumphosphate)…                                       kilo 2
 3. poultry premix/                                                                 kilo ½
 4.  unga wa mifupa                                                                kilo 1

          Jumla                                                                             kilo 4

  

Mahitaji halisi ya viinilishe kwa muhtasari:

Ø  Vyakula kutia nguvu mwilini                                              kilo 74

Ø  Vyakula vya kujenga mwili                                                  kilo 22

Ø  Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini)                        kilo 4

  JUMLA                                                                             100

 

Jumla ya mchanganyiko wa vyakula usizidi       kilo 100 

 

 

HATUA ZA KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU

 

Hatua ya kwanza

Katika hatua ya kwanza utaanza kuchanganya vyakula vya madini

Changanya , chokaa, chumvi na majivu ya mifupa pig mix vizuri – huu utauita mchanganyo Na.1

 

Hatua ya pili

Changanya mchanganyo huo na damu pamoja na samaki waliosagwa – huu utauita mchanganyo Na. 2

 

Hatua ya tatu

Mchanganyo Na.2 uchanganye na mashudu vizuri ambao utauita mchanganyo Na.3.

 

Hatua ya nne

Mchanganyo Na.3 umwage juu ya rundo la pumba iliyochanganywa (pumba ya mahindi na pumba laini ya mpunga).

o   Chukua beleshi /koleo safi lililo kavu na kulitumia kuchanganya rundo la chakula ili kusambaza viinilishe vizuri.

 

Mambo ya kuzingatia katika kulisha na kutunza chakula cha kuku

 1. Baada ya kuchanganya chakula kitawekwa kwenye viroba au magunia na kutunzwa ghalani (stoo) hadi pale kitakapohitajika kwa ajili ya kulisha kuku.
 2. Hakikisha kuku wanapata lishe kadri inavyopendekezwa na wataalamu.
 3. Chakula kilichochanganywa ni lazima kiwekwe sehemu kavu ili kisiharibiwe na unyevunyevu kama vile kwenye chaga mabanzi yaliyotandazwa juu ya mawe yalipangwa vizuri
 4. Chakula kilichoharibika hakifai kulisha kuku kwani kinaweza kusababisha matatizo ya afya.
 5. Chakula kilichochanganywa kinatakiwa kisikae muda mrefu baada ya kutayarishwa.

 

Vyakula vya ziada

Ili kuhakikisha kwamba kuku wanapata viinilishe vya kutosha kuku wanaweza kupewa mchwa na mafunza.

Vilevile vitu mbadala aina ya nafaka vinavyopatikana hutegemea sana aina ya mazao yanayolimwa katika eneo husika.

 

Mbinu za kuotesha mchwa na funza

Funza na mchwa ni chakula kizuri na rahisi chenye viinilishe aina ya protini kwa kuku wanaofugwa kwa mfumo huria unaoboreshwa. Hata hivyo vyanzo hivi vya chakula cha protini huchangia tu vile ambavyo kuku wanatakiwa kupewa.

 1. Inashauriwa uwape vifaranga hao funza na mchwa kwa sababu ndio wanaohitaji protini kwa kiasi kikubwa na cha kuaminika. Funza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa njia rahisi na kutumika kuboresha chakula cha vifaranga.
 2. Mafunza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa kutumia damu, viungo vya ndani ya tumbo la ng’ombe pamoja na samadi ya ng’ombe.
 3. Chungu kijazwe maji theluthi moja ya ujazo wake, inzi watakuja na kutaga mayai katika mchanganyiko ambao mafunza walioteshwa wataanza kula mchanganyiko huo.
 4. Baada ya hapo vitu hivi vyote vitachanganywa pamoja katika chungu kimoja kikubwa ambacho kitaachwa wazi wakati wa mchana na kufunikwa wakati wa usiku.
 5. Siku tano baadaye maji yatajazwa kwenye mtungi huo na mafunza yatakusanywa wakiwa wanaelea juu. Baada ya kukusanya waoshe vizuri na maji halafu lisha kuku moja kwa moja.
 6. Kumbuka kuweka chungu kinachooteshwa mafunza kuweka mbali na maeneo ya watu ili kuepuka harufu inayoweza kusumbua watu.

 

                                                  KULISHA KUKU
 

Makadirio ya chakula cha kuwalisha vifaranga 100/siku moja

 

Umri (wiki baada ya kuzaliwa) Idadi ya

vifaranga

Kiasi kinachotakiwa kwa siku moja(kilo)
1 100 1
2 100 1
3 100 2
4 100 3
5 100 4
6 100 5

 

 

Maelezo kwa ufupi  kuhusu kulisha kuku

 

 • Ni vigumu kukadiria mahitaji ya chakula cha kuku wanaojitafutia chakula, lakini inakadiriwa kuwa kuku mmoja mkubwa wa uzito wa kilo 1-2 anahitaji chakula chenye uzani wa gramu 80-160 kwa siku kwa kuku wanofugwa ndani lakini wale kuku wanafugwa kwa mfumo wa huria nusu huria mahitaji yanakadiriwa kupungua hadi kufikia gramu 30-50 kwa siku .
 • Ifahamike pia kuwa kiasi cha chakula hutegemea mahitaji kutokana na uzito na uzalishaji, mfano kuku anayetaga na anayekua wanahitaji chakula kingi zaidi ya wale ambao hawatagi au wamekoma kukua.
 • Hakikisha kuku wanawekewa chakula na maji safi kwenye vyombo safi na kubadilisha kila vitakapoisha.

 

BLOGU: FUGA KUKU KWA NJIA YA KISASA na Majumbeni

 

                                                            KWA MAWASILIANO

 

                                                                   TUPIGIE

 

                                                                0768 – 625660 

 

 

Leave a Reply