Unaweza kufikiria ni mzaha lakini wafugaji wanafanya haya na kuona Mafanikio kwa kiasi kikubwa sana. Miezi michache iliyopita tulipotembelea wakulima huko Njombetulikutana na utafiti huu ambao wakulima wamefanya na kujaribu wenyewe na kisha kuona mafanikio.
Utafiti huu unahusisha mmea mdogo sana ambao bado hatujaweza kufahamu jina leke kitaalamu au kwa Kiswahili sahihi, lakini kwa lugha ya Kibena unafahamika kama Muyeheyehe. Muyeheyehe kwa Kibena ni mmea ambao una vijitawi vidogovidogo ambavyo ni kama mfagio (dhaifu) ndio maana wakaita muyeheyehe. Unapokomaa unabaki na vijitawi na vijinundu vidogo-vidogo. Mmea huu hustawi sehemu ambayo haina rutuba au iliyolimwa kwa muda mrefu.
Wafugaji wa eneo hili wanaeleza kuwa baada ya kuona hauna jina linalotambulika na ni mmea ambao ulikuwa unadharauliwa sana waliamua kuupa jina hilo. Mmmea huu unasaidia kuku kutaga mayai mengi zaidi ya ilivyokuwa kawaida.
Namna ya kuandaa
Ng`oa mimea hiyo upate ya kutosha. Twanga na kuanika sehemu yenye kivuli hadi ukauke ili kupunguza kupotea kwa virutubisho kwa njia ya hewa. Rudia tena kutwanga ili kupata unga ambao utautunza kwa muda mrefu.
Namna ya kutumia
- Changanya kijiko kimoja kikubwa cha chakula kwenye maji lita 5 ya kunywa kuku.
- Wape kuku kwa muda wa wiki moja mfululizo. Baada ya hapo wape kuku mara mbili kwa wiki, na kuendelea.
Njia nyingine
Chemsha maji kisha chukua majani nusu kilo, weka hiyo dawa kwenye ndoo ya lita kumi na ujaze maji ya moto na kufunika. Acha kwa saa 12-24 inakuwa tayari. Changanya maji kwa uwiano wa 1:2 Dawa lita moja maji ya kawaida lita 2 utachanganya kulingana na idadi ya kuku wako na kiasi cha maji wanachohitaji kwa siku.
Wape maji hayo kama ilivyo kwenye matumizi ya unga. Wakati mwingine ili dawa hii ifanye kazi vizuri zaidi unaweza kuchanganya na unga wa majani ya lusina, calliandra, alfa alfa na chokaa, mchanganyiko huu ni kwa uwiano wa muyeheyehe lita 1 kwa robo tatu lita ya mchanganyiko wa lusina ,calliandra alfa alfa na chokaa.
Pia dawa hii inasaidia kuwakinga kuku dhidi ya magonjwa ya kideri. Kwa kutizama picha, hiyo unaweza kuutambua mmea huu kutoka katika eneo lako na ukajaribu kuutumia. Ni vizuriwakulima/wafugaji wa kujaribu njia za asili na rahisi huku wakiwashirikisha watafiti na wataalamu ili waweze kuwa na mafanikio zaidi.