Na Kubota
Kuna maandiko mengi ya ufugaji Kuku wa Kienyeji! Nawasilisha kwenu mbinu ambazo kwa mikono yangu nimezitumia kutatua changamoto za kuku wa kienyeji! Nimeandika kuwalenga wajasiliamali ambao hawana nguvu kifedha kujenga mabanda ya kisasa, mashine kutotolesha vifaranga, kutibu magonjwa wala kujenga wigo (fence) n,k. Naomba mzijue mbinu hizi nisije kufa nazo, huu ni mchango wangu kwenu watanzania wenzangu wale ambao mtakuwa hamjawahi kuzisikia mbinu hizi. Mbinu hizi baadhi nilisoma vitabuni nikazijaribu na kuziboresha kwa mazingira yangu duni! Mbinu zingine niliziona kwa wakulima duni kama mimi nikazitumia na kuleta mafanikio makubwa, mbinu zingine nilizigundua mwenyewe na nikafanikiwa sana. Hizi mbinu hazijafanyiwa utafiti rasmi lakini nimeweza kufanikiwa kuwa na kundi kubwa la kuku kwa haraka sana kupitia ujanja huu!!
Mbinu hizi zitagusia zaidi: Utotoreshaji vifaranga vingi kwa mara moja bila kutumia mashine! Ukuzaji wa vifaranga vingi kwa njia rahisi na kwa haraka zaidi, ulinzi wa kuku dhidi ya wanyama maadui, kudhibiti kuku wasizurule, magonjwa niliyofanikiwa kuyadhibiti, ujenzi wa vibanda wenye kukidhi mahitaji mbali mbali. Ni utaalamu nilioupata kwa gharama kubwa na mahangaiko ya muda mrefu, nauleta kwenu ili sote tuendelee kukua pamoja kiujasiriamali.
Safari yangu ilianza baada ya kukutana na mhamasishaji aliyenitia chachu kwamba 10 x10 x 10 unakuwa millionea! Kwamba ukianza na kuku 10 kila mmoja akazaa 10 na hao watoto na mama zao wakazaa kila mmoja 10 unakuwa millionea! Ndugu zangu kuongea ni rahisi utekelezaji ukawa mgumu sana! Changamoto kuu aipatayo mfugaji wa kuku wa kienyeji ni kuzalisha vifaranga wengi na kuweza kuwakuza! Bila hivyo kundi haliwezi kukua na kukupa kipato cha uhakika!
Safari ya ufugaji niliianza kwa kununua mitetea 30 na jogoo watatu! Ilibidi nisubiri muda hadi kuku waanze kutaga! Muda ukafika kuku wakaanza kutaga kwa fujo sana! Nilikuwa na banda moja tu ambamo kuku wote walikuwa wakilala humo. Nilitengeneza viota vingi kwa ajili ya kuku kutagia. Asubuhi nilikuwa nawafungulia! Changamoto nilizoanza kupambana nazo kwanza kama mjuavyo kuku tofauti walikuwa wanataga kwenye kiota kimoja! Ilipofika wakati wa kuatamia ikawa kila kwenye kiota kimoja kuna kuku kadhaa wamebanana wanaatamia! Hali hii haipaswi kutokea kwani kuku mmoja anaweza kuwa amejilundikia mayai mengi ambayo hawezi kuyapa joto la kutosha na kuku mwingine anakuwa amekaa kando tu hana hata yai moja. Hii ilibadilika ikawa kero kubwa! Nilijua utotoaji unaweza kuathirika sana!
Ili utotoreshe vifaranga wengi kwa wakati mmoja badala ya kutumia kifaa cha kutotoleshea (incubator), tumia hao hao kuku. Wakianza kutaga kila siku okota mayai na kuyahifadhi mahali salama ili kuku wasiyatie joto! Kuku wengi wanapotaga kwa pamoja hufikia wakati mayai huishatumboni unakuta wamelala kwenye viota wakiwa wameatamia mayai yaliyopo au udongo tu! Kuku anaekuwa amefikia kuatamia utamjua kwani ukimshitua haondoki kwenye kiota. Kuku anaetaga ukimshitua hukimbia! Kwa hiyo kama nimepanga kutotolesha vifaranga 100 kwa mara moja nikishagundua kuwa kuna kuku 8 wameanza kuonesha dalili ya kuatamia hapo husubiri usiku ninawawekea mayai amabayo nilikuwa nimeyahifadhi. Ambapo mimi huwekea kila kuku mayai 15. Kwa hiyo kuku 8 hufanya jumla ya mayai 120. Kwa kuwa banda langu ni hilo moja tu kuku wengine wanaoendelea kutaga walikuwa wanaendelea kutagia kwenye viota ambavyo kuku wengine walikuwa wanaatamia! Hali hii ilikuwa inaleta tabu sana kwani ilikuwa si rahisi kutambua mayai mapya na yenye siku nyingi. Kuondoa shida hii nilinunua kalamu ya rangi (mfano MARKER PEN au rangi yeyote) na siku ya kuwawekea mayai kuku ili waatamie niliyachora mduara kuzunguka yai ili iwe rahisi kuyatambua mayai mapya. Huo mchoro hauwatishi kuku na hakuna dosari yoyote. Kwa hiyo kila siku jioni ninapokuja kuokota mayai yaliyotagwa nilikuwa pia nakagua kila kiota cha kuku walioatamia na kuondoa mayai mapya. Kumnyanyua kuku anaeatamia na kuondoa yai haileti shida yoyote!
Kuku akifikia wakati wa kuatamia ukamnyima mayai hawa wanatabia kuendelea kung’ang’ania kuatamia, hapo ilibidi kutengeneza JELA! Watu wengine wanambinu tofauti kumwachisha kuku asiatamie! Mbinu ya kumtia kuku stress inafanya kazi nzuri sana! Jela inaweza kuwa ni Tega, au Box kubwa au chumba kidogo kilichopo. Ukimfungia kuku JELA bila maji wala chakula kwa kutwa mbili siku ukimfungulia akili yake huwa ni kutafuta chakula tu hakumbuki kurudi kwenye kiota! Njia hii ilifanikiwa sana na ilifanya kuendesha shughuri zangu bila bughudha! Kuna wakati JELA ilikuwa na kuku kibao hivyo unapaswa kutengeneza kibanda cha JELA. Hawa kuku wakitoka JELA hutaga mapema sana amabapo bila hivyo wangekuwa wanaatamia. Pia kuku wakishaatamia kwa muda wa siku 10 nilikuwa nayapima mayai ili kubaini kama kuna mayai yasiyoweza kuanguliwa! Ni rahisi sana kama una Tochi! Ukimulika yai kwa kulizungushia vidole kiganjani kama ni yai zima linakuwa na giza kama ni yai bovu linapitisha mwanga kama yai lililotagwa siku hiyo! Jinsi ya kuzungushia vidole yai, tengeneza duara kwa vidole vyako na dole gumba kisha pachika yai katikati ya duara ili mwanga wa tochi upenye kwenye yai! Kwahiyo unaweka tochi inayowaka chini ya yai na hii ifanyike gizani au ndani ya chumba chenye mwaga mdogo. Kadri ya yai linavyokaribia kutotolewa ukilimulika huwa na giza zaidi! Ukimulika mayai toa mayai yasiyoweza kutotolewa maana hayo hutumia joto la Mama bure!
========
Mayai viza! Mayai yasiyototolewa kwangu ni hazina kubwa kwani huyatumia kuwawekea kuku ili wasubiriane! Yaani inaweza kutokea kuku wameanza kuonyesha dalili ya kuatamia ili aishituke akaahirisha kuatamia huwa namlundikia hayo mayai yasiyoweza kutotoleshwa! Hufanya hivi hadi idadi ya kuku ninaotaka waatamie ikitimia, siku hiyo huondoa mayai feki na kuwawekea siku moja kuku wote mayai halisi ya kuatamia! Hakika nilikuwa ninasisimka sana inapofikia siku ya siku kuku wote wanamwaga vifaranga kwa siku moja!!
Ufugaji huu wa kuharakisha kuwa na idadi kubwa ya kuku huendana na kutenganisha vifaraga na mama zao. Watu wa mjini hufanikisha kirahisi sana kwa kutumia taa za umeme kuwapatia joto vifaranga! Wengine wanaweza kutumia majiko ya mkaa! Ni wazi kwamba ukiwanyang’anya mapema vifaranga Mama zao ndani ya siku 10 huwa wanaanza kutaga mayai tena, ambapo bila hiyo angeendelea kulea vifaranga wake hadi miezi 3. Kwa kumnyang’anya vifaranga kuku hutotoa vifaranga wengi kwa mwaka! Sasa kazi ndiyo ipo hapa! Ukinyang’anya vifaranga mama zao halafu ukawarundika vifaranga wenye umri tofauti sehemu moja hapo ni balaa! Vifaranga wenye umri mkubwa huhakikisha vifaranga wadogo hawali! Vifo vingi vinavyosababishwa na lishe duni hutokea kwa vifaranga kutokana na ubabe unaotokea kwamba wale wenye umri mdogo hawashibi! Kwa hiyo ni muhimu kutotolesha vifaranga wote siku moja ili uwakuze pamoja!
Kwa mazingira yasiyokuwa na umeme nilifanikiwa kukuza vifaranga kwa kutumia mama zao! Kwenye kuatamisha kila kuku nilimpa aatamie mayai 15 baada ya kutotoa nilikuwa kila kuku mmoja ninamkabidhi vifaranga 30! Kuku alikuwa anatandaza mabawa yake na kuwafunika wote! Vifaranga wakirundikana ndani ya mabawa ya mama yao wanazalisha joto la kutosha na wala si kwamba wanategemea joto la mama yao tu! Kwa kufanya hivi vifaranga waliototolewa na kuku 8 walilelewa na kuku watatu au wanne tu! Kwa hiyo wale kuku wengine 4 au 5 walipelekwa JELA ili kuondoa usumbufu na baada ya kutoka JELA baada ya siku 10 wanaanza kutaga mayai!
======
Nilivyoendelea kufuga baada ya kuona kuwa kuku wanaoatamia wanapata usumbufu sana kutoka kwa kukuwanaoendelea kutaga, Banda langu la kuku nililigawa kukawa chumba na sebule! Nitaeleza wakati ukifika nilivyojenga mabanda yangu. Kwa hiyo chumbani niliweka viota na ndiko ambako nilikuwa nawaweka kuku wanaoatamia ili wasibughudhiwe kabisa na kuku wenzao, mlango wa kuingia chumbani nilitengeneza geti la mianzi iliyopigiliwa karibu karibu kuzuia kuku kupenya. Hapo sebuleni ndiko kuku wote watagao na wasiotaga walikuwa wanalala, kwa hiyo kulikuwa na viota vingi ambavyo juu yake nilikuwa naviwekea kizuizi kwa kutumia Mabanzi ya mbao ili usiku kuku wengine wanaposimama juu yake wasichafue kwa kinyesi chao kwenye viota. Viota hivi nilikuwa navitengeneza kwa kuweka vijivyumba (partitions) kwa kutumia tofari za tope, zenye saizi kama ya matofali ya kuchoma. Kwa hiyo kwa kuambaa ukuta nilikuwa nalaza tofari nne chini kwenda juu, nilifanya hivyo kila baada ya upana wa futi moja, juu ya hizo tofali ndiyo niliweka Banzi! Ndani ya hivyo vijivyumba nilitifua umbo kama kijibeseni na kuweka Majani laini ili mayai yatulie yasisambae. Huko chumbani wakati wote kulikuwa na chombo chenye chakula na chenye maji! Hakuna kuku kutoka na hakuna kuku wa kuwaingilia! Ilikuwa ni incubator TOSHA! Nilikuwa nawaona kuku kama wananishukuru kwa kuwatengenezea mazingira safi maana walikuwa hawabughudhiwi na walikuwa wanashiba chakula vizuri tu! Nitaeleza siku nyingine juu ya harakati zangu za kutengeneza chakula na changamoto nilizokutana nazo! Huko chumbani nilikuwa nimetandaza carpet la nyasi; kando kando ya kuta zote kulikuwa na viota ambavyo nilivizamisha ndani ya hilo kapeti la nyasi nadhani mtanielewa! Ninaposema carpet la nyasi, ni nyasi tu nilizisambaza kwa unene wa kama sm 15 au nchi sita! Kwa hiyo kipindi hawa kuku wanapokuwa wanaatamia nilikuwa nazuia wengine wasiatamie hadi hawa watakapo totoa! Kwa hiyo mayai yanayopatikana wakati hawa wengine wanaatamia nilikuwa ninakula na mengine kuuza maana mpango wangu ilikuwa kutotolesha mara moja tu kuku mia kwa mwezi! Hii ndiyo Incubator yangu ambayo nilikuwa ninatotolesha vifaranga 100 kwa siku moja!! Kwa kuwa nilikuwa ninajukumu pia la kulea kuku utotoleshaji nilikuwa ninaudhibiti uendane na miundombinu yangu ya kulea kuku na vifaranga.
========
Masimulizi yangu hapo yamegusia kuwa nilikuwa nina banda kubwa lenye chumba na sebule, pia nilikuwa nina JELA ambapo mwanzoni nilitumia matenga au maboksi! Baada ya kuanza kutotolesha vifaranga, ilibidi nijenge kibanda cha kukuzia vifaranga (Nursery)! Kilikuwa kibanda kidogo kidogo tu mfano wa kigorofa hivi.
Mara baada ya kutotolewa kwenye banda kubwa vifaranga na mama zao niliwahamishia kwenye hii nursery. Kila chumba niliweka chakula na maji ya kutosha siku nzima kila siku asubuhi. Kuku walikuzwa humo kwa muda wa mwezi mmoja ambapo baada ya vifaranga kuota manyoya mwili mzima ndipo mama zao niliwatoa. Kisha hawa vifaranga wakubwa ambao nitakuwa nawaita VINYOYA niliwasambaza wote kwenye vyumba vingine vitano na nilibakisha chumba kimoja tu ambacho ndiyo hicho nilikitumia kama JELA! Nimeshaelezea tayari juu ya matumizi ya hii Jela.
Hao VINYOYA baada ya kuwatengenisha na mama zao niliwaacha wiki moja kisha nao nikawa nawafungulia waanze kuokoteza chakula na kuchunga. Wakati huu kwenye banda kubwa kulikuwa na kuku wanaoatamia ambao niliwawekea mayai siku 10 baada ya kutotolewa hawa VINYOYA! Kwa hiyo kwa kujua kuwa kuna vifaranga ambao wangetumia hii nursery hapo baadae, ilibidi nijenge banda lingine kwa ajili ya kuwakuzia hawa Vinyoya. Baada ya kuwahamishia hawa vinyoya kwenye banda lao nilikuwa ninawaaacha hadi miezi miwili au zaidi kabla ya kuwahamishia kwenye banda kubwa.
Hadi kufikia hapo mzunguko wangu wa mabanda ya kuku ukawa umekamilika! Yaani nilikuwa na banda kubwa sebuleni kwa ajili ya kulala na kutaga kuku wakubwa, chumbani kwa ajili ya kuatamia na kutotoleshea, banda la kukuzia vifaranga (nursery) na banda la kukuzia vinyoya.