Na Edson Kamukara
Ule usemi kuwa penye miti hakuna wajenzi, unaonekana kwenda tofauti kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera, wakazi hawa wana Ziwa Victoria, Burigi na visiwa vidogo 25 lakini wana tatizo la upatikanaji wa samaki. Wao wana miti (ziwa) lakini hawapati wajenzi (samaki) ambao sasa wamekuwa bidhaa ya anasa kwa watu wa kipato cha chini. Ni jambo la kushangaza kidogo kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera uliozungukwa na Ziwa Victoria, Burigi na visiwa vingine vidogo 25 kuanza kufuga samaki. Wamefikia hatua hiyo baada ya kitoweo cha uhakika na nafuu walichokizoea miaka nenda rudi kuonyesha dalili ya kupungua kama si kutoweka kabisa. Wakazi wengi mkoani Kagera mbali na shughuli za kilimo pia uvuvi ni sehemu ya maisha yao kwa lengo la kupata kitoweo na kujiingizia kipato. Kadiri siku zinavyosonga mbele, idadi ya watu inaongezeka, mahitaji ya samaki yanakuwa makubwa, si kwa wakazi wa mkoa huo pekee bali kwa masoko ya ndani na nje ya nchi. Ni jambo la kawaida kusikia vilio vya wavuvi, walaji na wafanyabiashara wakilalamikia uadimu wa samaki sambamba na kuongezeka kwa gharama za kumpata. Hali hiyo inachangiwa na teknolojia ya uvuaji wake kuwa tofauti na ile ya awali ya kutegemea zana duni za nyavu na mitumbi. Leo uvuvi huu unatumia pia boti za kisasa na meli kubwa. Hapa ndipo ujanja unaingia kwa wavuvi wakongwe, kubuni mbinu ya kujipatia samaki zaidi ili kukabiliana na hitaji la soko la walaji. Ni katika ubunifu huo, sasa Mkoa wa Kagera uliodhaniwa kuwa na neema ya samaki milele, sasa tumaini hilo linaelekea kufutika. Njia pekee ya kuhakikisha kitoweo cha samaki kinaendelea kuwepo na kupatikana kwa unafuu ni kuwafuga majumbani kwao. Katika utafiti uliofanywa na Tanzania Daima mkoani Kagera hivi karibuni kubaini umasikinishwaji wa wakazi hao, umebaini kuwepo uhitaji wa haraka wa nguvu za serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi nchini. Nguvu hizo pia zisisahaulike kuwekezwa kwenye ufugaji wa samaki ambao unaonekana ndiyo tumaini jipya kwa watu. Mradi wa kisasa wa ufugaji wa samaki mkoani Kagera ni wa kwanza na wa aina yake nchini, lakini bado Wizara ya Uvuvi na Mifugo haijatoa kipaumbele kuufanya uwe endelevu hasa katika mikoa isiyo na uwezekano wa kuvua. Wakazi wawili, wa Kijiji cha Ruhanga, Kata ya Ruhanga Tarafa ya Kamachumu, wilayani Muleba, Julius Onesmo na Bashiri Rashid, ni wavuvi wa muda mrefu ambao sasa wamejielekeza katika mradi mkubwa wa kisasa wa ufugaji samaki. Hivi sasa wanamiliki kituo kijulikanacho kama J&B Ruhanga Fish Culture Co. Ltd, ambacho serikali imekiteua kiwe cha utafiti wa ufugaji wa Samaki. Eneo hili ni maarufu sana mkoani Kagera, kila mtu unayemuuliza habari za ufugaji wa samaki, atakuelekeza eneo la mji mdogo wa Muhutwe jirani na wafugaji hao licha ya kwamba wapo wafuagaji wengine wadogo wadogo. Nilipofika mjini Bukoba, katika mazungumzo yangu na wakazi mbalimbali, niliambiwa kuwa wafugaji hao wametembelewa na viongozi wengi wa kitaifa akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda. Nilipitia taarifa mbalimbali za habari za ofisi ya waziri mkuu, nilibaini kuwa alifika eneo hilo Machi 5, 2011. Pinda kwa kuonesha kuvutiwa na ubunifu wa wafugaji hao, aliwaahidi wakazi wa Muleba kuwa atahakikisha wilaya hiyo inakuwa kituo kikuu cha ufugaji wa samaki katika mabwawa ili wilaya nyingine nchini ziweze kujifunza kutoka kwao. Akaongeza kuwa kama juhudi zitafanyika na kuwezesha wavuvi wengi kuingia katika ufugaji wa samaki kwa njia ya mabwawa hakuna mvuvi ambaye atakimbilia tena ziwani kwani atakuwa na uhakika wa kipato kutokana na samaki anaowafuga. Mmoja wa wafugaji hao, Julius Onesmo, alimweleza waziri mkuu kuwa mradi huo ulianzishwa mwaka 2007, ukigharimu sh milioni 58 na hivi sasa anafuga aina mbili za samaki ambazo ni sato na mumi (kambale). Onesmo ambaye zamani alikuwa mvuvi wa ziwani, alisema kuwa alikwenda kujifunza Uganda na aliporudi nchini alianza ufugaji na kwamba wamekwisha kuvuna samaki zaidi ya 13,400 aina ya sato wenye uzito wa kilo zaidi ya 4,414 ambao waliwauza kwa zaidi ya sh milioni 10.6. Katika taarifa yake kwa Pinda, Onesmo alisema mradi huo hivi sasa umefikisha thamani ya sh milioni 390 na hadi kukamilika unahitaji sh bilioni 1.027. Tanzania Daima, kwenye uchunguzi wake ilibaini kuwa ahadi ya waziri mkuu bado haijatelezeka ipasavyo, lakini wafugaji hao wanaendelea kujikongoja wakikabiliana na changamoto kadhaa huku wale wadogo wanaoanza nao wakilalamikia gharama za uendeshaji. Nikiwa eneo la mradi kijijini Ruhanga, mmoja wa wakurugenzi wa mradi huo, Rashid, alinieleza mambo mengi na vilevile aliweka wazi kuwa Tanzania bado ina safari ndefu katika utekelezaji wa kilimo hicho cha ufugaji wa samaki. Walianzaje “Tulikuwa wavuvi wa muda mrefu mimi na mwenzagu zaidi ya miaka 20, na katika kutembea tukafika nchini Uganda ambapo tulikuta wenzetu wanaendesha mradi kama huu tukajifunza na tukaona uwezekano wa kufuga upo,” alisema Rashid. Alisema kuwa baada ya kurudi nchini walianzisha utafiti wao huko eneo la Kimwani na kisha wakaja Ruhanga na kununua eneo tayari kwa kuanza mradi. Mkurugenzi huyo anasema baada ya kuanza utekelezaji wa mradi wao, serikali ya wilaya na mkoa walianza kutembelea kuona na kuwapa mawazo mbalimbali. Rashid alisema kuwa Pinda alipotembea mradi wao, aliwauliza wanahitaji kusaidiwa nini na kutaka kujua ni taasisi zipi zimejitokeza kuwawesha. “Tulimweleza kuwa tunahitaji kupata ujuzi zaidi kwani elimu ya ufugaji huu tuliyokuwa nayo ilikuwa ndogo sana ,” alisema. Alisema kuwa Pinda alikubali ombi lao na kuahidi kumpeleka nchini Vietinam kujifunza, pia kwa vile kituo chao hakina umeme aliwaahidi kupatiwa nishati hiyo na vile vile kukifanya kiwe cha utafiti wa ufugaji samaki. “Juni 16 hadi 22 mwaka 2011, nilikwenda kupata mafunzo Vietnam nikiongozana na Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Uvuvi. Nilijifunza kwa vitendo, nikakutana na wafugaji na wenye viwanda vya samaki,” alibainisha Rashid. Kwamba wakufunzi hao walionesha utayari wa kuisaidia Tanzania, jambo ambalo alimweleza hata waziri mkuu alipompelekea ripoti ya kile alichojifunza huko. Rashid ambaye anasema kuwa ahadi ya umeme inaanza kutekelezeka kutokana na serikali kufunga jenereta tayari lakini anaona changamoto kubwa iko kwenye ukosefu wa vifaa vya kisasa katika uzalishaji. Vitu gani vinahitajika Alisema kuwa ili kufikia ufugaji wa samaki wa kisasa walielezwa kwamba lazima wawe na maji ya uhakika, mashine ya kisasa yenye kutengeneza chakula cha samaki, kuzalisha vifaranga, kupima uzito na urefu, uwezo wa maji, omoni na vituo vya utafiti. “Sasa mashine hii inauzwa bei ghali na haiko hapa nchini, hivyo bila kuwa nayo ni uongo kufanya ufugaji wa kisasa unaotakiwa kwa vile hii inafanya kila kitu yenyewe,” alibainisha. Kukosekana kwa mashine hiyo, kunawafanya samaki walionao kuzaliana hovyo, kutopimwa uzito na urefu, viumbe hivyo hivi sasa vinalishwa pumba na vyakula vingine vya asili. “Sisi tunawalisha pumba tu, na tukiziweka zinazama chini na hivyo baadaye kuwa uchafu, kwa hali hiyo samaki hawezi kukua ipasavyo na kuzaliana,” aliongeza. Rashid alifafanua kuwa kutokana na ujuzi walioupata ni kwamba kitaalamu bwawa moja linapaswa kuwa na samaki 12,000 lakini ukosefu wa mashine hiyo, mabwawa yao wanaweka samaki 3,000. “Samaki anatumia miezi sita kufikia kiwango cha kuvunwa. Lakini utashangaa kutokana na kutokuwa na mashine hiyo, samaki wetu kwenye bwawa wanaweza kuwa zaidi ya idadi tuliyopanda maana wanazaliana bila sisi kujua,” alisema. Mkurugenzi huyo anasema kwa sasa wana mabwawa 11 ambayo yamepndwa samaki zaidi ya 40,000. Malengo yao ni yapi? “Mwanzo wakati tunaanza, malengo yetu yalikuwa ni kuwahudumia jamii inayotuzunguka ili wapate kitoweo hicho kwa bei nafuu, na baada ya kuanza kuvuna tulimudu kuwasambazia na kuwauzia,” alidai. Hata hivyo, alisema kuwa lengo hilo lilififishwa kutokana na ukosefu wa vifaa kama majokofu ya kuhifadhia samaki, magari ya kusambaza na masoko ya kudumu na hivyo wakajikuta wanunuzi wao wakubwa ni wafanyabiashara kutoka Arusha na Dar es Salaam . “Na kadiri tulivyozidi kusonga mbele wanunuzi wetu pia wamebadilika ambapo sasa tunawauzia Wachina, kwa sababu wao wamekuja na teknolojia yao ya mishipi ya kuvulia, hivyo wanavua wenyewe kisha tunapima wanatulipa,” alisema. Kwamba wanauza kilo moja kwa sh 4,000 wakati wananchi wa kawaida walikuwa wakiwauzia kwa mafungu kuanzia sh 1,500 na kuendelea. Alisema kuwa pia mwananchi wa kawaida akiwa na mishipi ya kuvua watamruhusu avue samaki. Na katika kuufanya mradi wao endelevu, tayari wameanza kusomesha wataalamu wao katika Chuo cha Mbegani mkoani Pwani, ambapo mmoja amehitimu kwa ngazi ya diploma (stashahada) na mwingine anaendelea na masomo. Changamoto zinazowakabili Licha ya Rashid kukiri kuwa kilimo hicho cha ufugaji wa samaki kina faida, bado anakiona kina gharama kubwa za uendeshaji na vifaa. Anatolea mfano kuwa kuchimba bwawa moja la kisasa, kunahitaji kati ya sh milioni sita hadi nane. Fedha hizo kwa mwananchi wa kawaida si rahisi kuzimudu. Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, licha ya kituo chao kuteuliwa kuwa cha utafiti lakini mpaka sasa hakina maabara ya kuendeshea mafunzo kwa vitendo. “Mimi hapa hata watu wanapokuja kujifunza, nawapatia tu maelekezo ya mdomo lakini nawashauri wachimbe tu mabwawa yakae tayari ila wasianze ufugaji hadi mashine ya kisasa iwe imepatikana nchini,” aliongeza. Hata hivyo, anashauri kuwa kama kweli serikali inajikita katika kuikuza sekta ya uvuvi katika ufugaji samaki, ni lazima kuwepo na vituo vingi vya utafiti visivyopungua 20. Vile vile anaona katika kuboresha ufugaji huo ni vema wakapatiwa mikopo ya haraka, itakayowawezesha kutimiza malengo yao kama walivyojiwekea. Wafugaji wengine wanasemaje? Kwa mujibu wa Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Muleba, Symphorian Ngaiza, mpaka sasa wapo wafugaji wa samaki 80 binafsi na vikundi wanaotambuliwa. Hata hivyo, bado wafugaji wakubwa mpaka sasa ni J&B na wengine ni wadogo wadogo wanaofuga samaki kwa ajili ya matumizi yao wenyewe. Na katika kuzunguka huku na kule nikagundua kuwa hata baadhi ya wilaya kama Bukoba Vijijini wako wafugaji wengine wadogo. Baadhi yao ni Erick Peter na John Kakizo, hawa maeneo yao ya ufugaji yapo Nkindo, Kata ya Ijuganyondo wilayani Bukoba Vijijini, licha ya kutokuwa na uwekezaji mkubwa ila si haba. Peter anaeleza kuwa alianzisha mradi huo Agosti mwaka 2010 na sasa anayo mabwawa sita, moja akiwa amepanda samaki 1,000 na mengine matano kila moja lina samaki 600. Wasimamizi wa mradi huo, Christian Gabriel na Dismas Ponsian, walisema kuwa bosi wao alipata ujuzi kutoka kituo cha utafiti cha J&B Ruhanga Fish Culture kisha wakaandaa mabwawa na kuanza ufugaji. “Hata vifaranga hawa tuliopanda tumewanunua kwa sh 500 kila kimoja na baadaye nasi tutaanza kuuza vifaranga,” alisema Gabriel. Mbali na samaki, wana miradi mingine ya ufugaji wa kuku, sungura, bata mzinga na nguruwe. “Hapa gharama kubwa iliyopo ni ya uandaaji wa mabwawa, kama unavyoweza kuona kila bwawa hapa limegharimu zaidi ya sh milioni moja,” walibainisha wasimamizi hao. Kwa upande wa vyakula, nao walisema kuwa wanawalisha pumba, majani ya magimbi, magugu na majani ya maboga. Ng’ambo ya mradi huo, nilikutana na mfugaji mwingine, Kakizo mwenye mabwawa manane yenye samaki wengi wakubwa kwa wadogo. Kama ilivyokuwa kwenye mradi wa awali, nako huku nilikutana na wasimamizi watatu, Erick Jason, Pascal Michael na Ladius Adoloph, ambao walinieleza kuwa ufagaji huo ulianza miaka mitatu iliyopita. Walisema kuwa tajiri wao alipata ujuzi kutoka Idara ya Uvuvi ya wilaya na kisha akaandaa mabwawa na kununua vifaranga tayari kuanza ufugaji. Walinieleza kuwa tayari wamevuna mara nyingi na samaki wao wanawauzia wananchi jirani na wenye mahoteli huko mjini. “Kwa wateja wa kawaida inategemeana na ukubwa wa samaki lakini tunauza kati ya sh 1,000 na kuendelea ila wale wanunuzi wa jumla tunawauzia kwa kilo,” alisema Jason. Serikali inasemaje Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Muleba, anasema kuwa Ziwa Victoria ni la kila mtu kuvua na hivyo, ndiyo maana wanawaelekeza wananchi kujiingiza katika ufugaji wa samaki. “Wako wafugaji binafsi na vikundi, hivyo na sisi serikali katika kuhamasisha ufugaji huo, tunajielekeza kuhakikisha wafugaji wanapata mbegu bora za vifaranga pamoja na vyakula vya kisasa,” alisema. Alisema kuwa katika utafiti wao, wamebaini kuwa kambale (mumi) na sato ndiyo wanamudu mazingira ya ufugaji na sato wanazaliana sana kwa njia ya asili wakati kambale wanategemea zaidi njia ya kisasa. Kwamba serikali inakusudia kuanzisha kituo cha kuzalisha vifaranga eneo la Kyamkwikwi ili kuwawezesha wafugaji wa samaki kupata vifaranga bora. “Na katika kuhakikisha hili linatekelezeka katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imetenga sh milioni 20 za kuanzisha mradi huo,” alisema Ngaiza. Alisema ili kukabiliana na tatizo la uhitaji wa mashine ya kisasa kwa ajili ya kutengezea chakula na kuzalisha vifaranga, ni vema wafugaji hao wakajikita kutafuta uzoefu katika nchi jirani ya Uganda ili kupata teknolojia ya bei nafuu. Makala hii ni sehemu ya uchunguzi wa chanzo halisi cha umaskini na maisha duni ya wakazi wa visiwani, mialoni na maeneo ya karibu, kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Muleba na Bukoba. Uchunguzi huu umedhaminiwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF). Mambo usiyoyajua katika ufugaji wa samaki
|