Chakula cha samaki: njia bora ya kudhibiti ubora wake

Na Mtafiti

Utafiti wa awali na Utengenezaji wa Chakula

Utafiti wa viungo mchanganyiko vinavyotumika na wakulima  kulishia samaki, na unaofaa ulifanyika katika mikoa ya Arusha na Mbeya. Lengo la utafiti huu lilikuwa ni kupata uelewa, na kuweka kumbukumbu za aina ya vyakula ambavyo wafugaji wa samaki wanatumia kuwanalisha samaki wao, upatikanaji wake, utunzaji wa mabwawa, changamoto wanazokutana nazo, motisha ya kufanya kazi ya ufugaji wa samaki kibiashara, na kukusanya aina mbali mbali za malighafi za vyakula kwa ajili ya utambuzi wa viinilishe ambavyo baadae vilitumika kutengenezea chakula cha majaribio ikiwa ni jitihada ya kupata chakula kinachofaa. Dodoso lilitumika kufanya mahojiano kwa wakulima katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Arumeru  mkoani Arusha na Wilaya ya Tukuyu mkoani Mbeya

Jumla ya wafugaji wa samaki wapatao 49 walihojiwa kutoka kwenye vijiji 10 wilayani Arumeru, na wengine 3 kutoka Manispaa ya Arusha, wakati wakulima 48 walihojiwa katika vijiji 8 wilayani Tukuyu. Vijiji vilivyotembelewa Wilaya ya Arumeru ni pamoja na Kimnyaki, Olmotonyi, Kimandolu, Nambala, Meru, Manyata, Midawe, Ndatu, Magadini, Lekitatu, Njiro, Makumbusho ya Taifa (Arusha Mjini), na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha eneo la Sekei. Kwa upande mwingine, vijiji vilivyotembelewa wilayani Tukuyu ni Kyimo, Mpuguso, Syukula, Ilolo, Ilundo (Buswema), Bujinga, Nkalisi na Matamba.

Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba, isipokuwa kwa wakulima wachache tu, wakulima walio wengi wanalisha samaki wao vyakula mbali mbali vya ziada. Kuna tofauti inayoonekana wazi kati ya Mbeya na Arusha. Wakati wakulima wengi wa Arusha wanatumia pumba za mahindi (zaidi ya 40%), Pumba za mchele (20%), Mashudu ya pamba na mashudu ya alizeti, Dagaa na Uduvi (maji baridi), pamoja na mbogamboga (kama vile matembele, spinachi, majani ya mihogo, ‘majani ya sungura’, ‘mashona nguo’) na mabaki ya matunda (mfano: maparachichi, ndizi); kwa Mkoa wa Mbeya wakulima wanalisha samaki wao hasa kwa kutumia mboga za majani (mfano: Majani ya Mihogo, spinachi, majani ya migomba, majani ya maboga, kabichi), mabaki ya vyakula na mara chache pumba za mahindi na mpunga, na alizeti wakati kipato kinaporuhusu kufanya hivyo.

Ilionekana wazi pia kuwa, japokuwa wakulima wanawalisha samaki chakula cha ziada, wakulima hawana uelewa wa kutosha wa jinsi inavyotakiwa kufanyika; na hakuna ukaribu kiutendaji kati ya wakulima na maafisa wa uvuvi ambao  wanapaswa kusambaza utaalamu huu. Sababu kubwa ya msingi juu ya ugumu wa mawasiliano kati ya wakulima na maafisa ugani, hasa kwa Arusha, ni ukubwa wa eneo ambalo wanatakiwa kulihudumia ukilinganisha na uwezeshwaji kidogo wanaoupata kutoka kwenye halmashauri husika. Tena, kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa samaki ikiwa vyakula bora na vya bei nafuu vitakuwepo.

Jumla ya sampuli 17 za malighafi za kutengenezea vyakula zilikusanywa kutoka maeneo ulikofanyika utafiti. Matokeo yalionyesha kwamba Arumeru ina aina nyingi za malighafi za vyakula (aina 13). Malighafi za vyakula zilizokusanywa kutoka maeneo ya utafiti zilitumwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Mkoani Morogoro kwaajili ya uchambuzi wa viini lishe (proximate analysis). Matokeo yanaonesha kwamba damu ilikuwa na kiwango kikubwa cha protini (84%) ikifuatiwa na Dagaa (64%) na maharage ya soya (39.26%).

 

Majaribio ya Ukuaji wa Samaki: Kituoni and Kwenye mashamba ya majaribio

Mwaka wa kwanza wa mradi ambao ulianza Januari 2013, yalijengwa matanki 9 kwa ajili ya majaribio ya kukuza samaki kwa kutumia chakula kinachotokana na malighafi kutoka Arusha. Majaribio hayo yalifanyika katika kituo cha TAFIRI Dar es Salaam. Vyakula vya aina tatu (TAFIRI I, TAFIRI II, na TAFIRI III) vyenye virutubisho mbali mbali vinavyotokana na malighafi ya asili vilitengenezwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya samaki. Hivyo dhumuni kuu lilikuwa kutathimini ubora wa vyakula vilivyotengenezwa ili kuboresha ukuaji wa samaki jamii ya Perege kwa muda wa miezi mitatu.

Matokeo yaliyotokana na jaribio hili yalikuwa ya kutia moyo. Utafiti huu ulianza na samaki wenye uzito wa wastani wa gramu 2.7. Baada ya miezi mitatu ambapo jaribio lilikamilika, samaki walivunwa na kupatikana wenye wastani wa uzito wa gramu 70, hali inayoashiria ubora wa vyakula na hivyo kuleta mapinduzi  katika sekta ya ufugaji wa samaki Tanzania.

Mwaka wa pili wa Mradi huu unahusu ushirikishaji wa wafugaji wadogo wadogo katika maeneo yao ya ufugaji. Majaribio haya yanayofanyika katika Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha yanafanyika katika mabwawa 8 tofauti baada ya kuyatathimini na kukidhi vigezo vilivyohitajika. Lengo hasa la kuwashirikisha moja kwa moja wafugaji kwa kutumia mabwawa yao lilikuwa: kwanza, kuhakikisha yale yote waliyofundishwa na watafiti kutoka TAFIRI wanayazingatia kwa vitendo, pili  kujaribu kulinganisha matokeo yatakayopatikana chini ya usimamizi wao wenyewe na matokeo yaliyopatikana kipindi cha majaribio katika Kituo cha utafiti cha TAFIRI Dar es Salaam kwa kutumia vyakula vile vile.

Shughuli nyingine iliyofanywa katika awamu hii, ilikuwa kutoa mafunzo kwa maafisa uvuvi Wilaya na wafugaji wa samaki juu ya kuchagua, kuandaa na kutengeneza chakula bora cha samaki kwa kutumia malighafi za asili  zinazopatikana kwa urahisi katika maeneo yao ya ufugaji. Mafunzo yalifanyika kwa mafanikio, washiriki ishirini na tisa (29) walishiriki kikamilifu ikiwa ni sawa na asilimia 73 (73%) ya idadi ya washiriki iliyokusudiwa. Majaribio haya litegemewa kufika ukomo mwishoni mwa mwezi wa Oktoba 2014. Tathimini ya Mradi na matokeo juu ya ukuaji wa samaki yatakayopatikana kutokana na majaribio yote mawili yanatarajiwa kusambazwa kwa wafugaji wadogo wadogo na wadau mbali mbali mwanzoni mwa mwaka 2015.

Kwa kumalizia, hadi sasa ufanisi wa vyakula vilivyotumika kwenye utafiti huu ni wa kuridhisha. Tunaamini kwamba majawabu yatakayotokana na majaribio yote mawili (TAFIRI na Arusha) na kwa kuzingatia  ubora wa maji (mazingira ya maji), yatatupa matokeo mazuri zaidi. Tunatarajia matokeo ya utafiti huu pia yatatumika kuhamasisha ufugaji wa samaki katika maeneo mengine ya Tanzania ili kukidhi na kufikia malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) kwa kuongeza uzalishaji, na kupungunza kama si kutokomeza kabisa ukosefu wa lishe bora inayotokana na ukosefu au upungu wa protini na pia kuchangia katika kuboresha maisha ya wafugaji na kuinua uchumi wa Taifa kwa ujumla.

 

CHANZO: Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI)

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!