Ujue ugonjwa wa homa ya bonde la ufa (hbu)

Na Mwandish wetu

Augustino Chengula

Utangulizi

Waliokuwepo mwaka 2007 nchini wakiwa na umri wa kuelewa mambo bila shaka watakuwa hawajasahau ugonjwa uliopelekea kuzuliwa kula nyama maeneo mengi ya nchi. Hofu ilitanda kwa walaji wote wa nyama ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Hii ilitokana na uwepo wanugonjwa wa homa ya bonde la ufa (HBU). HBU ilianza kwa kushambulia mifugo kukiwepo na utupaji mimba usiokuwa wa kawaida. Wafugaji hawakujua nini na hivyo hawakuchukua tahadhari yeyote ya kupambana nao. Ugonjwanukavamia maeneo mengi ukianzia mikoa ya kaskazini mwa nchi (Arusha, Simanjiro, Babati na Ngorongoro). Maeneo haya yamekuwa yakiripoti kila unapotokea ugonjwa huu. Ugonjwa wa HBU hutokea kila baada ya miaka kati ya 10-20 na hapa Tanzania umetokea miaka ifuatayo: 1947, 1957, 1977, 1997 na 2007. Hii ya mwisho ya 2007 ndiyo iliyoripotiwa kuwa kubwa kuliko zote, ugonjwa ukiikumba mikoa 10 kati ya 21 na wilaya 25 kati ya 126. Watu 144 walipoteza maisha kati ya watu 511 waliodhaniwa kuwa na ugonjwa. Kati ya hao 186 walithibitika kuwa na ugonjwa huku 124 wakitengwa kama wagonjwa wenye dalili za HBU. Madhara ya HBU kwa mifugo ilikuwa ni vifo vya ng’ombe (16 973), mbuzi (20 913) na kondoo (12 124) pamoja na utupaji mimba kwa ng’ombe (15 726), mbuzi (19 199) na kondoo (11 085). Hasara ya kiuchumi iliyotokana vifo vya mifugo inakadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni sita.

 

Kwanini uijue elimu hii sasa?

Kinga ni bora kuliko tiba! Usemi huu ni maarufu lakini pia umesadia sana kuoa maisha ya watu au kuwafanya watu wapate maendeleo pale wanapoamua kuuishi kwa vitendo. Tahadhari za mapema za viashiria vya kuwepo kwa ugonjwa huu nchini na duniani kote zimekwisha kutolewa na FAO pamoja na vyombo vingine vinatoa taarifa za hali ya hewa vikiwemo vya hapa nchini kuwa kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa mvua kubwa mithili ya El Nino. Mvua hizi zinazosabisha mafuriko na kuongezeka kwa ukijani vinavyotengeneza mazingira ya rafiki kwa mbu wanaosambaza virusi vya HBU na kupelekea mlipuko wa HBU. Uwepo wa virusi vya ugonjwa huu kwa wanyama na binadamu kwa kiwango cha chini kwa kipidi kisicho na ugonjwa katika maeneo kadhaa hapa nchini umethibitishwa na wataamu wa HBU.

 

HBU ni nini?

Homa ya Bonde la Ufa (HBU) (Rift valley fever) ni ugonjwa wa kirusi unaojitokeza kwa dharula ukishambulia  hasa wanyama wanaocheua (ngo’mbe, mbuzi, kondoo), lakini wanyama wengine pia hupata kama punda, ngamia na wanyama pori mfano nyati, nyumbu na swala . Mwanadamu pia hupata ugojwa huu kutoka kwa wanyama walio na ugonjwa huu kwa kula nyama isiyopimwa na kupikwa vizuri au kwa kushika mazao ya wanyama wenye ugonjwa . Ugonjwa unasababishwa na virusi vya homa ya bonde la ufa homa (VHBU) vinavyo sambazwa na mbu aina ya Aedes. HBU huleta madhara makubwa sana kiuchumi na kijamii pale unapotokea na hasa hatua za makusudi za kuzuia kuenea kwake zisipo chukuliwa. Kuwepo kwa wanyama wanao tupa mimba kwa wingi kati ya kondoo, mbuzi, ng’ombe na ngamia na vifo vya wanyama wadondo (watoto wa mbuzi, kondoo, na ndama) kwa karibu asilimia mia moja na uwepo wa dalili zinazofanana na mafua ya ndege ni viashilia tosha vya kuwepo kwa HBU. Historia ya kuwepo kwa mvua nyingi kiasi cha kutengeneza mafuriko pamoja na ongezeko la mbu wanaoeneza ugonjwa huu ni kiashiria cha kuanzia kufanya uchunguzi wa kina ili hatua mahususi ziweze kuchukuliwa.

UGONJWA wa homa ya bonde la ufa (Rift Valley Fever) umefahamika kwa zaidi ya miaka 60 nchini Kenya.

Lakini miaka mitatu iliyopita ulipiga hodi hapa nchini na kuua watu katika mikoa ambayo Bonde la Ufa linapita hasa maeneo ya Arusha na Manyara, Kanda ya Kaskazini mwa Tanzania.

Ugonjwa wa homa ya bonde la ufa ulioonekana kwa mara ya kwanza Kenya, matukio yake makubwa yameonekana katika nchi nyingi za Bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na Misri, Sudan, Somalia, Kenya, Msumbiji, Nigeria, Senegal, Tanzania, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini.

Nchi ya Misri ilikumbwa na ugonjwa huu mwaka 1977 na 1978 ambapo watu wapatao 18,000 waliugua na 598 walikufa. Nchi ambazo taarifa zilitolewa za matukio ya ugonjwa huu nje ya Bara la Afrika ni pamoja na Yemen na Saudi Arabia.

Kwa hapa Tanzania ugonjwa huu ulionekana mwaka 1979 na 1998 katika mikoa ya Mara, Arusha na Kilimanjaro ambapo ng’ombe, mbuzi, kondoo na ngamia waliathirika.

 

Nini kinasababisha HBU?

HBU ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vijulikanvyo kama virusi vya homa ya bonde la ufa (VHBU) vilivyopo kwenye familia ya virusi ya Bunya (Bunyaviridae). VHBU vimekuepo tangu zamani sana na viligunduliwa kitaalamu kwa mara ya kwanza nchini Kenya mnamo mwaka 1931 katika bonde la ufa (Rift Vlley), kiini cha jina la ugonjwa. Vinasaba vya kirusi hiki ni vya aina ya RNA na ina vipingili vitatu ambavyo husaidia kirusi huyu kutengeneza aina nyingine ya kirusi yuleyule na kumfanya asishambuliwe na kinga ya mwili ya mnyama.

 

HBU inaenezwa na nini?

HBU inasambazwa kutoka kwa mnyama mmoja kwenda kwa mwingine na hata kwenda kwa binadamu kwa njia ya Mbu. Wapo mbu wengi waliokwisha tambuliwa kusambaza ugonjwa huu lakini msambazaji mkuu ni mbu aina ya Aedes na unasemekana uwepo wake miaka na miaka unategemea kupitia mayai ya Aedes yanayotagwa kwenye madimbwi wakati wa mafuriko yajulikanayo kama ‘madambo’. Mbu aina nyingine kama vile jamii ya Culex na Anopheles wanaweza kusambaza virusi vya ugonjwa kati ya wanyama na wanyama na kati ya wanyama na binadamu. Lakini zaidi ya kupata ugonjwa moja kwa moja toka kwenye mbu, binadamu wanaweza kupata ugonjwa kupitia kugusa damu au majimaji ya aina nyingine ya wanyama wakati wa kuchinja, kuzalisha wanyama wagonjwa, kushika vitoto vya mbuzi au kondoo vilivyokufa.

Aidha, binadamu wanaweza kupata ugonjwa kutokana na kula vyakula visivyopikwa vizuri vitokanavyo na wanyama wagonjwa au wenye virusi. Kati ya mlipuko na mlipuko, VHBU huwepo kwenye baadhgi ya wanyama au wanadamu kwa kiasi cha chini sana kiasi cha kutoonyesha dalili zozote.

HBU1
Mzunguko ya uambukizaji na ukuzaji wa virusi vya HBU

 

Dalili za HBU ni zipi?

Dalili za jumla

Kutambuliwa kwa ugonjwa huu na wafugaji au wataalamu katika maeneo ambako hakuna maabara au vifaa vya kufanyia uchunguzi unategema dalili ambazo zitajionyesha kwa mnyama mara apatapo ugonjwa huu. Dalili hizi zitaonekana kwa mnyama anayetembea au kwa uchunguzi mara baada ya kufa na kupasuliwa ili kuona viuongo vya ndani vilivyo athirika vikiambatana na historia ya mvua nyingi kiasi cha kuwepo mafuriko. Kuwepo kwa utupaji wa mimba kusikoelezeka kunako karibia asilimia 100 kwa kondoo na ng’ombe katika eneo kubwa lakini kiasi kidogo kwa mbuzi pamoja na wanyama wengine wanaocheua ni ishara muhimu ya kuhisi uwepo wa huu ugonjwa.

Dalili nyingine zaweza kuwa vifo vya gafla na ugonjwa wenye vifo vingi kwa aina nyingi za wanyama (ikikaribia asilimia 100 kwa kondoo wadogo na ndama chini ya siku 7 na vifo vichache kwa wanyama wakubwa), Homa kali, kutokwa na machozi na makasi kwa wanyama wakubwa, kuharisha damu, kuvimba tezi, kutapika, maumivu ya tumbo, na kukosa hamu ya kula.  Kwa upande wa mwanadamu dalili zinazofanana na mafua ya ndege zitaonekana kwa mgonjwa na vifo ni chini ya asilimia mbili. Dalilizote hizi zilizotajwa zikitumiwa kwa umakini zitasaidia sana kuhisi uwepo wa ugonjwa na kufanya tahadhari za haraka zichukuliwe. Hata hivyo mawasiliano ya haraka yanahitajika na wadau wengine ili kubaini ugonjwa huu kwa haraka.

 

Dalili za HBU kwa wanyama wadogo wanaocheua

Kondoo na mbuzi wanaonyesha dalili zinazofanana lakini kondoo ndiye anayeoneka kuathirika na ugonjwa kwa asilimia kubwa. Kondoo mweye ugonjwa huwa na homa, hukosa hamu ya kula, hutoa makamasi mazito, na  huharisha damu. Asilimia 90 hadi 100 ya kondoo wenye mimba hutupa mimba, na kasi ya kufa huwa ni kuanzia asilimia 90 kwa watoto na asilimia 20 hadi 60 kwa wakubwa. Watoto wa kondoo wanaozaliwa au walio chini ya wiki mbili wanauwezekano mubwa wa kupata HBU wakipata homa kati ya nyuzi 40–42 za sentigredi ambalo hupungua wanapo karibia kufa, kutokula kwa sababu ya kushindwa kutembea na udhaifu, maumivu ya tumbo. Kifo hutokea ndani ya masaa 24 hadi 36. Wale walio zaidi ya wiki mbili pia wananafasi kubwa lakini hufa bila ya kuonyesha dalili za uhakika ndani ya masaa 24 hadi 96 wakiwa na joto la nyuzi 41 hadi 42 za sentigredi. Wakubwa hutupa mimba kwa asilimia karibu 100 wakiwa na dalili za kutokula, udhaifu, kunyong’onyea, kupmua kwa kasi, kutapika, kuharisha damu, na makamasi mazito.

 

Dalili za HBU kwa wanyama wakubwa wanaocheua

Hapa nazungumzia ng’ombe, nyumbu, ngamia na nyati ambao dalili zake hazitishi kama za wanyama wadogo, ndama wao hufa kwa asilimia 10 hadi 30 laikin utupaji wa mimba huwa kati asilimia 90 hadi 100. Ndama ndiyo wanuwezekano mubwa wa kupata ugonjwa wakiwa na homa kati ya nyuzi 40 hadi 41, kukosa hamu ya kula, udhaifu na kunyong’onyea, na kuharisha damu. Wakubwa huugua kwa kiasi kidogo mara nyingi wakiwa hawaonyeshi dalili lakini wengine wakiwa na homa inayoisha kati ya masaa 24 hadi 96, ngozi kavu, kutoa machozi na makamasi, kutoa udenda kwa wingi mdomoni, kukosa hamu ya kula, udhaifu, kuharisha damu, na kupungua kwa maziwa. Kwa maeneo wanayofuga ngamia dallili huwa hazionekani kwa macho lakini kutupa mimba hufikia asilimia 70 na waoto hufa kuanzia wadogo hadi miezi 4. Wanyama pori wanaocheua kama nyati na nyumbu hawaonyeshi dalili zozote hata wakati wa mlipuko. Hivyo wanauwezo wa kusambaza kwa mifugo hasa inayokula ndani au mipakani mwa hifadhi au maeneo ambayo wanyama pori hukutana na mifugo.

 

Dalili za HBU kwa mwanadamu

HBU huwapata pia wanadamu na ripoti zinaonyesha kuwa mwanadamu huambukizwa toka kwa wanyama na haijaonekana kama mwanadamu anaweza kumuambukiza mwanadmu mwenzake. Hivyo mwanadamu ataupata kwa kula au kunywa mazao ya wanyama wenye ugonjwa, kuwa karibu au kuhudmia wanyama wenye ugonjwa. Mwanadamu akishapatwa na VHBU huanza kuonyesha dalili ndani ya siku mbili hadi sita na dalili huisha ndani ya siku 4 hadi 7 na kasha kupona au kufa (ambako ni chini ya asilimia mbili).

Dalili ni homa (nyuzi 37.8 hadi 40), maumivu makali ya kichwa, kuumia macho waangaliapo mwanga mkali wa jua, mafua, mgongo, kuharisha, kutapika, na kuvuja damu. Asilimia ndogo wanaweza kuwa na ugonjwa mkali zaidi wakiwa na numonia yenye damu, homa kali, tumbo kuuma, kutapika damu, upofu wa macho na maumivu ya uti wa mgongo na kufa ni aslimia 1 hadi 2.

 

Dalili za HBU kwa wanyama wengine

Wanyama wengine ambao wameripotiwa kupata ugonjwa ni mbwa nap aka ambapo ugonjwa unaweza kuwa mkali wenye vifo kwa watoto na kutupa mimba kwa mbwa wakubwa. Nguruwe na kuku hawapati ugonjwa huu kabisa.

 

Dalili za HBU mnyama akifa na kufanyiwa uchunguzi

Dalili kubwa za ugonjwa huu huonekana kwenye ini ambalo seli zake huwa zimeshambuliwa sana na kuonyesha vijialama vyeupe vyenye kipenyo cha karibu milimita 1, ini kujaa damu na kuvimba likionyesha rangi ya kahawia yenye unjano has kwenye ini la mimba iliyotolewa na ugonjwa. Damu nyingi ilisambaa ndani ya ngozi, vitone vidogo na makubwa nje ya viungo vya tumboni, kujaa maji, kuvimba na kuwa na damu kwenye tezi mbalimbali, kuwepo kwa damu kwenye figo na ini ni dalili nyingine zinazoweza kuonekana. Kwa watakao salimika kufa, kupona ni haraka na hutengeneza kinga inayodumu kwa muda mrefu.

 

Utautambuaje ugonjwa  wa HBU? 

Nci nyingi za afrika ambapo ugonjwa upo siku zote kwa wanyama na maeneo ambapo hutokea kama mlipuko kwa wanyama wanaocheua na wanadamu, huwa hakuna vifaa vinavyojitosheleza kupambana na ugonjwa. Hivyo ugonjwa huchukua muda mrefu kabla ya kufanikiwa kuutokomeza au kabla haujapotea wenyewe.

Dalili zilizotajwa hapo juu ni hatua ya awali nay a muhimu kwa utambuzi wa HBU na kuchukua hatua mahususi za kupambana nao kabla ya sampuli kupelekwa maabara kwa uchunguzi wa kina. Maabara uchunguzi waweza kuwa wa kuotesha virusi kwenye seli na kuangalia mdhara anayosababisha, kutumia vipimo kama ELISA, kubaini vinasaba vyake na vingine vingi.

 

Namna gani unaweza kuzuia HBU isitokee kwenye mifugo yako au ikitokea ufanye nini? 

Kama ilivyo kwa magonjwa yote ya virusi kutokuwa na tiba maalumu, hata HBU haina tiba maalumu na matibabu yake iwe kwa wanadamu au wanyama yanatemea dalili ili kuzuia wadudu wengine kama bacteria wasishambulie. Ili kuzuia usitokee, chanjo ndiyo njia pekee nay a kuaminika hadi sasa. Pia kwa vile umbu ndo waenezaji wakubwa wa mifugo, kuogesha mifugo kulingana na maelezo ya mtengeneza itasaidia sana. Matumizi ya vyandarua kwa binadamu yanasaia pamoja kuepuka kutembea kwenye maeneo yenye mbu wanaosambaza ugonjwa huu.  Lakini ukisha tokea, kuzuia wanyama wasitembee ovyo kutoka sehemu moja hadi nyingine ili ugonjwa ubaki eneo moja. Uangamizaji wa mbu ungesaidia sana lakini ngumu kufanya kazi hiyo ya kuwatokomeza hao mbu. Uchinjaji wa ng’ombe wenye ugonjwa haishauriwi kabisa kuepuka kuambukizwa, na wala kula nyama isiyopimwa au kunywa maziwa yasiyochemshwa vizuri. Changamoto ziko nyingi hasa kwa nchi kama Tanzania, ikiwemo kupata chanjo inayoendana na virusi tulivyo navyo, wafugaji kutibu mifugo yao wenyewe na kusababisha kuripoti ugonjwa kwa kuchelewa, kasi ya kuagiza chanjo hadi ifike wakati wa mlipuko huwa ndogo ukilinganisha na kasi ya ugonjwa, na ufugaji wa kuhama hama.

 

HITIMISHO

HBU huleta madhara makubwa sana unapojitokeza hapa nchini kwa njia ya mlipuko, kiuchumi na kijamii. Umakini unahitajika hasa kwa wafugaji ili kuweza kuutambua ugonjwa huu kwa wakati na kuripoti kwenye vyombo husika. Lengo la kuandikia juu ya HBU ni kutaka kuwasaidia wafugaji ili waweze kuutambua ugonjwa huu maana tafiti zinaonyesha kuwa wafugaji wengi hawakuujua ugonjwa huu ulipotokea mwaka 2006/07 licha ya kutokea mwaka 1997. Hii inaonyesha kuwa wafugaji wengi huusahau ugonjwa huu kwa vile inachukua muda mrefu kujirudia hata madhara yake husahaurika hata kama ni makubwa ukilingalinisha na mgonjwa kama Ndigana kali ambayo yapo nao kila siku. Hivyo elimu ya mara kwa mara inahitajika ili uwakae masikioni mwao na pengine ingefaa kuwe na vipindi redioni vilivyorekodiwa.

Leave a Reply