Na SAT Morogoro
Mfugaji ambaye hajaweza kuchagua eneo na kulitunza kwa ajili ya baadae kukata nyasi, anaweza kutafuta eneo la kuvuna malisho ya mifugo
Malisho asilia ni uoto unaoota katika mazingira ambayo hayajaandaliwa rasmi kwa upandaji wa mbegu., zaidi tu ya usimamizi na kuzuia uvamizi wa mifugo kwenye eneo hilo wakati wa uotaji na ukuaji wake.
Uchaguzi wa eneo
Chagua eneo lenye nyasi nzuri na kiwango kikubwa cha malisho, usiruhusu uchungaji wa mifugo katika eneo hilo. Eneo hilo linaweza kurutubishwa kwa kuweka/ kusambaza samadi ili kuongeza virutubisho kwenye udongo, hivyo kupata nyasi bora na zilizokua vizuri.
Kwa mfugaji ambaye hajaweza kuchagua eneo na kulitunza kwa ajili ya baadae kukata nyasi, anaweza
kutafuta eneo la kuvuna malisho ya mifugo kwa kuzungukia maeneo yote yenye majani na kuchagua majani yanayofaa.
Aina ya majani yanayofaa kuchaguliwa kwa malisho
Majani jamii ya nyasi yasiyo na asili ya ugumu yakikauka, na yasiyo na kijimti kikubwa au kirefu ndio bora kwa mifugo. Mfano wa majani yanayofaa ni nyasi jamii ya Mbudu, na mengineyo ya aina hiyo.
Wakati wa uvunaji
Ili kupata malisho bora ya mifugo nyasi zinatakiwa kuvunwa wakati wa ukuaji (siku chache kabla ya kuanza kutoa maua). Huu ni wakati ambao malisho yanakuwa na virutubisho muhimu kwa afya na ukuaji wa mifugo.
Nyasi zinapoanza kutoa maua virutubisho vingi hupotea, hivyo inatakiwa uanze kuvuna kabla hayajaanza kutoa maua. Kwa mfugaji aliyechelewa kuandaa na kutafuta eneo la kuvuna malisho, avune wakati wowote ila ahakikishe malisho hayajakauka yenyewe kabla ya kukatwa.
Vifaa vya kukatia nyasi
Kuna vifaa vinavyotumika katika uvunaji wa malisho asilia kulingana na uwezo wa mfugaji mwenyewe. Vifaa vinavyotumika ni mundu uliopindwa (Sickle) kwa ajili ya kukata nyasi, kisu kwa ajili ya kukata kamba ya kufunga majani na panga kwa ajili ya kuondoa vichaka kabla ya kukata majani.
Ukaushaji
Malisho hukatwa na kuachwa juani kwa muda wa siku mbili, baada ya hapo huwekwa kivulini chini ya mti tayari kwa ajili ya utengenezaji wa marobota(belo).
Ubora wa malisho yaliyokaushwa
Malisho yaliyokaushwa vizuri hayana fangasi. Dalili za kuharibika kwa nyasi ni pamoja na kuwa na fangasi wa rangi ya kijivu, kijani au nyeusi. Majani yakiwa katika hali hii hayatakiwi katika malisho. Fangasi husababisha madhara mbalimbali ikiwamo mifugo kujaa matumbo.
Ufungaji wa malisho yaliyokaushwa
Kifaa kinachotumika kwa ajili ya malisho yaliyokaushwa ni boksi lenye ukubwa wa urefu inchi 30, upana inchi 17 na kina cha boksi inchi 10.5. Boksi linatakiwa kuwa na uwezo wa kukunjuka katika pembe/kona tatu ili kurahisisha utoaji wa balo la nyasi zilizokaushwa.
Namna ya kufunga
Utatakiwa kukunja boksi na kutengeneza mstatili, huku komeo lake likiwa imefungwa vizuri. Baada ya hapo, jaza nyasi ndani ya boksi na shindilia vizuri kwa kutumia miguu ukiwa umevaa kiatu kisafi. Balo moja lililojazwa na kushindiliwa vizuri inaweza kuwa na uzito wa kilo 15 na kuendelea kufuatana na aina ya nyasi, ukaushaji na ushindiliaji mzuri.
Namna ya uhifadhi wa malisho yaliyokaushwa
Malisho huhifadhiwa kwenye eneo ambalo hakuna jua la moja kwa moja, mbali na mvua ili kutunza ubora wake. Matumizi ya kichanja ni muhimu kwa sababu nyasi haitakiwi kuwekwa juu ya ardhi/sakafu ili kutoruhusu uotaji wa fangasi na kusababisha kuharibika kwa malisho.
Malisho yaliyokaushwa huweza kuhifadhiwa kwa zaidi ya miaka mitatu kama yamehifadhiwa vizuri, mbali na unyevu pia sehemu inayopitisha hewa ya kutosha wakati wote.
Ulishaji
Malisho yaliyokaushwa hulishwa kwa kufungua kamba, kutoa nyasi na kumpatia ng’ombe au mifugo mingine.
Belo moja linaweza kukidhi mahitaji ya ng’ombe mmoja au zaidi kwa siku
kulingana na ukubwa wa ng’ombe. Kwa nyasi zilizokaushwa hula wastani wa asilimia 3 hadi 5 ya uzito
wa mwili wake, pia atatakiwa kunywa maji lita 10 hadi 15 baada ya kula.
Makala hii imeandaliwa na Shirika la
Kilimo Endelevu Tanzania (SAT).