Na Mkulima Mbunifu

Ni rahisi sana kukuta mfugaji anapotaka kuanza mradi wa ufugaji akiwaza kupata pesa za kununua ng’ombe, kujenga banda na kisha kutafuta ng’ombe aliye bora na kumnunua akiamini kuwa kilichobakia ni malisho tu kisha kufikia mafanikio.

Kwa kuwaza hivyo tu, ni wazi kuwa kama mfugaji unajitengenezea hasara wewe mwenyewe. Ni muhimu sana kukumbuka na kuzingatia kuwa ili ng’ombe wako wawe na afya nzuri itakayowezesha kufikia mafanikio mazuri, wanahitaji kupata dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu, hali kadhalika chanjo kwa ajili ya kuzui magonjwa ya aina mbalimbali yanayoweza kusababisha hasara endapo ng’ombe wako hawatapata chanjo.

Inashauriwa kuwasiliana na wataalamu wa mifugo walio katika eneo lako mara kwa mara ili kufahamu aina ya chanjo ambayo inafaa kutolewa kwa mifugo yako kwa kipindi hicho na kwa muda muafaka.

Kamwe usikae bila kuwachanja ng’ombe wako katika kipindi muafaka.

Aina za chanjo

Kuna aina nyingi za chanjo, na chanjo hizo zimegawanyika katika makundi mawili, chanjo hai na chanjo mfu.

Chanjo mfu inabidi irudiwe kila mwaka au zaidi kulingana na aina ya ugonjwa. Chanjo hai huchomwa mara moja kwa mwaka au miaka mitatu kisha kurudiwa tena.

Chanjo hizi hutolewa kwa ajili ya magonjwa yanayosababishwa na bakteria na virusi.

Magonjwa yanayosababishwa na virusi hayana tiba maalumu.

Kinachotibiwa ni magonjwa yanayosababishwa na matokeo ya kudhuriwa na virusi, mfano vidonda.  Ni muhimu kuchanja ng’ombe na mifugo wengine kabla ya aina flani ya ugonjwa kusambaa.

Mambo ya kuzingatia kwenye ulishaji wa ng’ombe

Mwanzo wa kuzalisha maziwa

Wakati huu lisha ng’ombe kwa mfumo ambao, atazalisha kiasi kikubwa cha maziwa bila kupoteza uzito kwa kiasi kikubwa.

Utaratibu wa kulisha unatakiwa kuwa ongezeko la virutubisho taratibu kwa kiwango cha kilo 0.5 – 1 kwa siku, kuanzia kilo 2.5 kwa siku, huku uzalishaji wa maziwa ukiongezeka.

Simamisha ongezeko la kulisha virutubisho endapo hakutakuwa na ongezeko la maziwa.  Kulisha ng’ombe kwa kiwango cha chini wakati anapoanza kukamuliwa itasababisha uzalishaji mdogo wa maziwa, na pia atakuwa na dalili hafifu anapofikia wakati wa kuwa kwenye joto.

Endapo hauna kipato cha kutosha kumlisha ng’ombe virutubisho wakati wote, ni bora ukamlisha wakati wa kuanza uzalishaji wa maziwa tu na kuacha anapoelekea mwishoni.

Kipindi cha kati na mwisho

Wakati ng’ombe anapofikia kipindi cha mwisho uzalishaji wa maziwa hupungua kwa haraka sana.

Katika kipindi hiki, ng’ombe ni lazima alishwe kufuatana na kiwango cha maziwa anachozalisha. Kiwango cha malisho kinaweza kutolewa kulingana na aina ya malisho.

Kwa wastani, mfugaji anashauriwa kulisha kiwango cha kilo 1, ya chakula cha kuongeza maziwa kwa kila kilo 1½ ya maziwa yanayozalishwa kwa zaidi ya kilo 7 kwa siku.

 

Chanzo: Mkulima Mbunifu

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!