Ufugaji wa samaki hatua kwa hatua: Hatua ya tatu

Farida Mkongwe Ufugaji wa samaki hatua kwa hatua: Hatua ya pili   Na Farida Mkongwe 

HATUA YA 3: UANDAAJI NA UPANDIKIZAJI WA VIFARANGA VYA SAMAKI

Katika  hatua hii ya tatu tutaangalia uandaaji na upandikizaji wa vifaranga au mbegu za samaki katika bwawa.

Dr. Berno Mnembuka ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Wanyama iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) pia ni mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji anasema kabla ya kuvisafirisha vifaranga kutoka kwenye bwawa wanaloishi ni vema vikatolewa na kuwekwa kwenye vibwawa vidogo vidogo kwa muda wa kati ya saa 24 hadi 72 (kutegemeana na umbali wa safari) bila chakula. Hii ni kwa sababu chombo kinachotumika kusafirishia samaki kinakuwa na maji kidogo hivyo vifaranga vikipewa chakula vitachafua maji hayo kwa kinyesi na kubadilisha hewa iliyopo kwenye maji kitu ambacho kinaweza kuleta madhara kwao.

Wakati wa kupandikiza mfugaji anatakiwa akifika asivimwage vifaranga kwenye bwawa bali anatakiwa kuyaruhusu maji yaliyobeba vifaranga yabadilishane ujoto na maji yatakayopokea vifaranga. Hapa mfugaji anatakiwa kuliweka kontena au chombo alichobebea vifaranga kielee kwenye maji anayotaka kufugia kwa muda wa dakika kati ya 30 hadi 35, baada ya hapo chombo kilicho na vifaranga kifunguliwe na kiinamishwe ili maji hayo yaweze kukutana na yale yaliyoandaliwa kwa ajili ya kufugia na hapo ataruhusu vifaranga kuingia wenyewe kwenye bwawa husika.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka iwapo utafika na kuvimwaga vifaranga kwenye bwawa jipya bila kufuata utaratibu huo wa kitaalamu basi tofauti ya ujoto wa maji kati ya chombo kilichosafirishiwa vifaranga na bwawa unaweza kusababisha vifaranga wote kufa kwa muda mfupi, kitaalamu wanasema kuwa vifo vya vifaranga hivyo vinasababishwa na mshituko wa joto.

Jambo lingine la kuzingatia ni kuwa uandaaji na usafirishaji wa vifaranga ni vizuri ukafanywa muda ambao hali ya hewa inakuwa na ubaridi. Muda unaopendekezwa zaidi na wataalamu ni asubuhi au jioni kwa sababu muda huo samaki wanakuwa na uwezo wa kuhimili misukosuko ya safari tofauti na hali ya hewa inapokuwa ya joto.

Kufikia hapo tumekamilisha hatua ya 3 kuhusu uandaaji na upandikizaji wa vifaranga au mbegu za samaki katika bwawa, kitu muhimu kinachosisitizwa ni kufuata taratibu za kitaalamu katika upandikizaji wa samaki ili kuzuia vifo vinavyotokana na mshituko wa joto.

Usikose kufuatilia hatua ya 4 ya ufugaji wa samaki ambapo tutaangalia ulishaji na utunzaji wa samaki bwawani.

 

CHANZO: SUAMEDIA

Leave a Reply