Na Farida Mkongwe     

Farida MkongweUfugaji upo wa aina nyingi, katika mfululizo wa makala hizi tutaangalia ufugaji wa samaki na kwa kuanzia tutaangalia mbinu muhimu za kuzingatia wakati wa kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki kwani mkulima au mfugaji iwapo hatazingatia hatua hizi basi ni vigumu kwake kuweza kufanikiwa.

Dr.Berno Mnembuka ni Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Sayansi ya Wanyama katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), pia ni mtaalam wa lishe ya samaki na uzalishaji anaelezea Mbinu 6 muhimu ambazo iwapo mkulima atazizingatia wakati wa kuanzisha mradi wake wa ufugaji wa samaki basi kwa hakika ataweza kujikwamua na umaskini sambamba na kuongeza idadi ya ajira binafsi kwa watanzania.

Mbinu ya kwanza ni kuwa “mfugaji anatakiwa awe na shauku na dhamira ya kweli ya ufugaji”. Ni wazi kuwa dhamira ya kweli ni kitu muhimu sana unapotaka kufanya jambo lolote kwani bila kudhamiria basi huwezi kufanikiwa, matokeo ya kutokuwa na dhamira ni kukata tamaa pindi utakapokutana na changamoto ya aina yoyote lakini ukiwa umedhamiria utakuwa na uwezo wa kuzikabili changamoto na hivyo kujikuta ukifika mwisho wa safari yako huku ukiwa na mafanikio.

Katika hili Dr. Mnembuka anawataka wafugaji watarajiwa wasikurupuke badala yake wafuate maelekezo na hilo linawezekana tu iwapo wafugaji watakuwa na dhamira ya kweli kinyume cha hapo hata yale maelekezo ya ufugaji yatakuwa ni kero kwao hali itakayowafanya washindwe kutoa huduma sahihi za ufugaji na hivyo kupata hasara.

Mbinu ya pili ni mkulima “kufanya tathmini ya rasilimali alizonazo kwa ajili ya mradi wa ufugaji wa samaki”. Tathmini hii inahusisha nguvukazi, rasilimali pesa, pamoja na umiliki wa eneo. Mkulima akiweza kujitambua na kutambua uwezo wa nguvukazi aliyonayo itakuwa ni rahisi kwake kuyamudu majukumu mbalimbali yaliyopo katika ufugaji, pia katika suala la kutambua ukubwa wa ardhi aliyonayo litamsaidia kujua idadi ya samaki anaoweza kufuga pamoja na kiasi cha fedha kinachohitajika.

Mbinu nyingine ambayo ni muhimu kuitambua ni “chanzo endelevu cha mtaji kwa ajili ya mradi”. Mfugaji anatakiwa kuwa na chanzo cha uhakika cha kujipatia mtaji wake ambacho kitakuwa ni endelevu ili asije akajikuta anakwama kupata pesa ya kununulia mahitaji pindi yanapohitajika na hivyo kumpunguzia ubora katika ufugaji wake. Hapa mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka anawashauri wakulima wajiunge katika vyama mbalimbali vya kuweka akiba na kukopa (SACCOS) ikiwa ni pamoja na vikoba  ambavyo hutoa mikopo kwa riba nafuu na taratibu zake za marejesho hazina masharti magumu hivyo kumwezesha mfugaji kukopa kwa urahisi wakati wowote  anapokuwa na mahitaji ya fedha.

“Hulka ya uvumilivu na kuthubutu”, hii ni mbinu ya nne anayopaswa kuwa nayo mfugaji. Mfugaji mtarajiwa wa samaki anapaswa aelewe kuwa ufugaji wa samaki ni mradi kama ilivyo miradi mingine ambayo unaweza kuwekeza lakini faida yake isiweze kuonekana mara moja. Hapa mfugaji anatakiwa awe mvumilivu katika kipindi chote cha mwanzo cha ufugaji kwani hiki ni kipindi cha mpito ambacho kinaweza kumfanya asipate faida lakini akiwa mvumilivu baada ya mradi kukomaa basi atapata faida na inashauriwa mfugaji kutumia rasilimali za kifamilia katika hatua za awali ili kuepuka madeni katika kipindi cha mpito.

Mbinu ya tano ambayo ni muhimu unapotaka kuanza ufugaji wa samaki ni “tathmini ya soko la bidhaa za samaki”.  Soko ni jambo muhimu sana katika suala la biashara kwani hilo ndilo litakalokuongoza na kukuwezesha kujua mahitaji ya watu pamoja na kupanga bei. Mfugaji hana budi kufanya utafiti na kuelewa ni kwa kiasi gani biashara anayotaka kuifanya inakubalika katika jamii aliyopo kinyume cha hapo anaweza asifanikiwe, kutokana na biashara anayoifanya kutokuwa na soko au kutokubalika katika jamii inayomzunguka, kwa mfano unapoamua kufuga samaki kwenye jamii ya wamasai ni wazi kuwa soko lako litakuwa ni dogo kutokana na wamasai wengi kupendelea kula nyama zaidi kuliko samaki.

Mbinu ya sita na ya mwisho ni “kujipatia maarifa ya msingi ya ufugaji wa samaki”.  Kitu chochote ili uweze kukifanya kwa ufanisi ni lazima uwe na elimu au maarifa ambayo yatakuongoza katika utekelezaji. Ni ukweli usiopingika kuwa mtu mwenye elimu au maarifa juu ya biashara anayofanya anapata faida zaidi ukilinganisha na yule anayefanya kienyeji bila ya kuwa na mwongozo. Katika ufugaji wa samaki vyanzo vya maarifa vinaweza kuwa ni majirani zako ambao ni wafugaji, taasisi za dini zenye miradi kama hiyo, ofisi za serikali zinazojihusisha na mambo ya uvuvi, bila kukisahau Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo mjini Morogoro hususan Idara ya Sayansi ya Wanyama ambayo ina wataalamu waliobobea katika suala la ufugaji samaki.

Ni matumaini yangu kuwa wewe mfugaji mtarajiwa hata wewe ambaye tayari umeshaanza kufuga umeweza kufaidika na kujifunza mbinu muhimu unazopaswa kuzitambua kabla ya kuanza mradi wa kufuga samaki, ukiweza kuzizingatia mbinu hizo utaweza kujikomboa wewe na familia yako lakini pia utawakomboa watanzania katika suala la ajira. Usikose kuungana na mwandishi wa makala hii katika sehemu ya pili ambayo itazungumzia “tofauti ya ufugaji samaki wakati wa kiangazi na wakati wa masika”.

 

Source: SUAMEDIA

 

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!