Uandaaji wa nyumba ya kuku wa mayai

Uandaaji wa nyumba ya kuku wa mayai ni jambo la kutilia kipau mbele maana nyumba iliyobora inawafanya kuku wafurahi na kukupa matokeo unayotaraji ya ukuaji na utagaji wa mayai. Nyumba iliyo bora kwa ajili ya ufugaji wa kuku wa mayai inatakiwa iwe na

 1. Iwe na uwezo wa kupitisha hewa na mwanga wa kutosha
 2. Ijengwe kwa uelekeo wa mashariki-kaskazini kwa urefu ili kuwapa kuku mwanga wa asili na jua
 3. Nyumba iwe na joto kati ya nyuzi joto 20-25 ºC
 4. Sakafu ijengwe kwa simenti, paa lisiruhusu mvua wala unyevu, kusiwe na nyufa kwenye sakafu au ukuta, isiruhusu panya kuingia na iwe rahisi kuisafisha.

Mfumo wa ufugaji ndani ya nyumba ya kuku wa mayai unaweza kuwa wa aina mbili:

 1. Ufugaji wa kutumia vizimba (cages)
 2. Ufugaji wa wa chini sakafuni: Katika mfumo huu taka raini huwekwa kwenye sakafu mfano maranda ya mbao na pumba ya mpunga.

Uandaaji wa sehemu ya kulelea vifaranga

Kabla ya kuagiza vifaranga wa kuku wa mayai, hakikisha sehemu ya kutunzia vifaranga imeandaliwa. Vifaranga wanaweza kutunzwa kwenye vizimba (cages), kwenye kingengunengu (Brooder) au kwenye sakafu iliyowekewa taka raini kama pumba ya mpunga.

Kinengunengu (Brooder) kilichogunduliwa na Mtanzania Lohan Manga (technolojia rahisi) kama njia ya kupambana na vifo vya vifaranga.

Kinengunengu hiki hutengenezwa kwa mbao, magunia, ceiling board na takataka za mbao au pumba za mpunga. Chombo hiki cha kulelea vifaranga hakitumii nishati ya joto kama umeme, jiko la mkaa na zinginezo na hivyo ni kifaa rafiki cha kupunguza gharama. Vifaranga hulala katika mduara ambao hufunikwa na hujitengenezea joto wenyewe, wakati wa mchana hukaa sehemu hiyo ya pembe nne, kwa ajili ya chakula na maji, utengenezaji wa aina hii ya kinengunengu huitaji utaalamu kidogo.

Kwa mfumo wowote utakaoamua kuutumia zingatia mambo yafuatayo kabla ya kuingiza vifaranga:

 1. Kabla ya kuleta vifaranga ni muhimu kufanya usafi na kupulizia dawa nyumba ya kuku. Kizimba au kinengunengu kama si vipya navyo vifanyiwe usafi na kupuliziwa dawa.
 2. Hakikisha unapasha joto nyumba ya vifaranga kufikia nyuzi joto 35-36 za sentigredi na liendelee kuwepo kwa kipindi cha masaa 48 hadi 72 tangu kuingiza vifaranga.
 3. Unyevu nyevu (humuidity) iwe asilimia 60
 4. Chakula cha vifaranga kiwepo ndani ya chumba cha kulelea (kinengunengu au kizimba). Kama unatumia kizimba tandika karatasi kisha kiweke chakula juu ya karatasi.
 5. Hakikisha maji ya kunywa vifaranga yanapatikana na siku za mwanzo ikiwezekana wafundishe kunywa maji kwa kutumia vifaa vya maji ulivyo navyo. Hakikisha joto la maji lipo kati ya nyuzi joto 20-25 za sentigredi.
 6. Ingiza vifaranga wako kwa kuwaweka karibu na maji na chakula ila hakikisha umevisambaza kwa uwiano sawa ndani ya nyumba ya kuku.
 7. Wachunguze vifaranga mara kwa mara usiku na mchana ili kubaini kama kuna tatizo lolote.
 8. Hakikisha huweki vifaranga wengi sana ndani ya nyumba ya kulelea, usizidishe vifaranga 25 kwa kila mita moja ya mraba. Hii itasaidia vifaranga kusambaa haraka ndani ya nyumba yote ndani ya siku saba.

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!