Ufugaji wa kuku wa kienyeji kama mradi

P1

Na. Ev. Mujaya Mujaya

Simu: +255715678122 au +255768678122

Barua Pepe: ev.mujaya@gmail.com

 

MAHITAJI

 1. Kuku(tetea) 10 na Jogoo 01
 2. Banda bora
 3. Vyombo vya chakula na maji
 4. Chakula bora
 5. Madawa na chanjo kwajili ya magonjwa
 6. Chanzo cha nishati joto na mwanga
 7. Elimu na ujuzi wa malezi bora
 8. Chombo au chumba cha kutunzia vifaranga
 9. Mayai ya kuku wa kisasa/mayai mabovu(ambayo hayakuanguliwa)
 10. Madaftari au kitabu cha kutunzia kumbukumbu

p5

KUKU 10

Wakati wa kuanza mradi wako hakikisha una kuku 10 (matetea) wenye umri sawa na hawajawai kutaga hata mara moja. Chagua kuku wenye rangi nzuri kutoka katika familia bora kutegemea malengo ya mradi wako. Mfano kama lengo lako ni kuzalisha kuku wa kienyeji kwajili ya nyama basi chagua mbegu ambayo inakuwa haraka na yenye uzito mkubwa. Au ikiwa lengo ni mayai basi ni vema kuchagua aina ya kuku yenye kukua haraka na kutaga mayai mengi.

Ili kupunguza gharama za manunuzi ya kuku na hivyo kuongeza faida kwa mfugaji ni vema kununua kuku wadogo ambao wametoka tu kuachishwa kulelewa na mama zao. Kuku hawa utawapata kwa bei ya chini, tena watafaa sana maana watakua na umri mmoja pia.

JOGOO 01

Jogoo mmoja tu anatosha kuwahudumia kuku matetea yote kumi. Hakikisha katika uchaguzi wa jogoo bora lililochangamka, rangi mzuri, upanga umesimama, macho angavu, uzito wa kutosha, rangi nzuri na uwezo mkubwa wa kuzalisha. Ni vema mfugaji akaelewa kwamba kuku wote watakaozalishwa watategemea ubora wa jogoo wake. Uwezo wa kutaga kwa kuku na upatikanaji wa mayai pia hutegemea kwa karibu ubora wa jogoo aliyechaguliwa.

 

BANDA BORA

Miongoni mwa mambo mhimu naya kwanza kuzingatiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji kama mradi ni maandalizi ya banda bora. Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Mfugaji anatakiwa kuandaa banda lenye ukubwa wa mita 10 kwa mita 04. Yani urefu uwe mita 10 na upana upana wa mita 04. Kisha kata vyumba vya mita 2 urefu na upana mita 4 kutoka katika banda lako hivyo utakuwa na jumla ya vyumba vitano vyenye ukubwa unaolingana. Ujenzi uzingatie malighafi na vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira husika. Mfano katika maeneo ambayo fito zinapatikana kwa urahisi banda linaweza kuandaliwa kwa miti na kukandikwa kwa udongo. Au sehemu ambayo mabanzi hupatikana kwa urahisi basi banda laweza kujengwa kwa kutumia mabanzi. Vifaa vya kujengea banda vizingatie pia gharama na upatikanaji wake katika eneo husika.

P2

Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-

 • Sakafu: Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
 • Kuta: Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi,udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
 • Paa: Nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
 • Wigo: Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi, matete, wavu na mabati

Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-

 • Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari.
 • Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.
 • Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.
 • Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala.
 • Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga.
 • Liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka vyombo vya chakula na maji.
 • Kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa. Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga.

 

JINSI YA KUFANYA

Wakuze kuku wako hadi watakapofikia muda wa kutaga. Wakianza kutetea ni kiashiria kwamba wakati wa kutaga umekaribia hivyo andaa viota kwajili ya kutagia.

Viota vinapaswa viwe na ukubwa stahiki ili kumwezesha kuku kuyafunika mayai yote vizuri wakati wa kuetamia, viota viwe vinavyozuia mayai kutawanyika, viwe mahali pakavu na safi.

P3

Hakikisha kuku wote wanataga katika viota tofauti. Kuku anapotaga mayai matatu unapashwa kuchukua mayai mawili na kumwachia yai moja ili kumfanya aendelee kutaga zaidi. Kuku akifikia yai la kumi na mbili anza kumwachia mayai matatu ili kumwandaa kwa kazi ya kuetamia. Kwa kufanya hivi, kuku atataga mayai 15 au zaidi na ikiwa atataga mayai 15 au chini ya hapo nakushauri utafute mayai mengine ujazilizie ili kufikisha mayai 20 kwa kila kuku. Zingatia kwamba mayai unayoyatoa kwa kila kuku, yanatunzwa sehemu salama, mahali pakavu, pasafi na penye joto la wastani.

Kuku wote wanapaswa kuanza kuetamia kwa siku moja. Ili kufanikisha hili inapasa uwe karibu na kuku wako. Kuku mmoja akianza kuetamia mwekee mayai ya kuku wa kisasa au mayai mabovu ya kuku wa kienyeji. Utafanya hivi hadi kuku wako wote watakapoanza kuetamia mayai. Kuweka mayai mabovu au mayai ya kuku yaliyotumika humfanya kuku aendelee kuetamia akijua ni mayai yake.

Baada ya kuona kwamba kuku wako wote wapo tayari kwa kuetamia mayai, waandalie banda maalumu kwajili ya kuetamia yani chumba kimoja katika lile banda letu. Ninashauri kwamba chumba kwajili ya kuetamia kiwe chumba cha kwanza au cha mwisho katika mfuatano wa vyumba vya banda lako. Andaa viota bora vya kuetamia, weka mayai 20 kwa kila kiota, ikiwa hayajatimia unaweza kununua kwa wafugaji wengine ili kuifikia idadi yako.

Waamishe kuku kutoka wanapotagia na kuwaweka katika chumba ulichokiandaa kwajili ya kuetamia. Ili ufanikiwe katika zoezi hili inafaa lifanyike wakati wa usiku na unafanya katika giza. Mweke kuku katika kila kiota na asubuhi wajikute kila mmoja katika kiota chake. Wahudumie kwa chakula na maji ya kutosha. Wakati wa usiku waongezee joto la ziada kwa kuweka jiko au ndoo ya chuma yenye chengachenga za mkaa au kama una umeme weka taa za joto.

Baada ya siku 21-25 kuku wako wataanza kuangua vifaranga. Huu ndio wakati unaotakiwa kuwa karibu sana na kuku wako kuliko wakati wote. Watenge vifaranga mara tu baada ya kuanguliwa; waweke katika chumba chao maalumu mbali na kuku. Kama chumba cha kuetamia kilikuwa cha kwanza basi vifaranga wawe chumba cha mwisho n.k

Ukishawatenga vifaranga mbali na matetea wako, wawekee tena mayai mengine 20 kila tetea, mayai ambayo utayanunua kwa wafigaji wenzako. Hakikisha kuku waliotaga hayo mayai ni wazuri, hawana magonjwa na wanauzito/ukubwa unaofaa. Mayai yote yakaguliwe vizuri ili kujua kwamba yameharibika, yana nyufa au mabovu. Kabla ya kuweka mayai mengine hakikisha chumba chako ni kisafi na viota vimesafishwa, havina wadudu na uchafu wowote. Kuku wako bila kujijua wataanza kuetamia upya mayai uliowawekea.

Ukiwawekea mayai rudia mzunguko kama nilivyokwambia awali. Baada ya siku 21 hadi 25 tena utapata vifaranga wako wengine tena. Fuata kila hatua kama nilivyokwambia hapo awali. Lakini kwa awamu hii nashauri waache matetea wako wapumzike wala usiwapatie mayai mengine tena.

 

JINSI YA KULEA VIFARANGA

Ikikaribia siku ya 20 tangu ulipowawekea matetea wako mayai katika chumba cha kuetamia, andaa chumba kwa ajili ya kulea vifaranga. Safisha kwa kuondoa uchafu na wadudu wote.

p4

Washa taa ya joto au weka chombo cha kutoa joto katika chumba cha vifaranga nusu saa kabla hujaanza kuingiza vifaranga wako. Weka pia chakula na maji ya kutosha katika vyombo vyenye umbile na ukubwa utakaowawezesha vifaranga kuvitumia. Tandaza magazeti, maboksi, makaratasi n.k katika sakafu ya chumba hicho. Hakikisha vifaranga wako hawajikusanyi sehemu moja maana wakifanya hivyo wengi wao watakufa ili ufanikiwe katika jambo hili, banda lako liwe la mduara katika kona zake.

Weka joto la kutosha. Joto la kutosha ni lile linalowafanya vifaranga watawanyike chini ya chanzo cha joto wakati kama joto limezidi vifaranya kukimbia mbali na chanzo cha joto na ikiwa joto halitoshi vifaranga hujukusanya chini ya chanzo cha joto.

Baada ya siku 3 utawapatia chanjo ya Gumboro na siku 7 wapatie chanjo ya New Castle, utarudia tena kuwapa chanjo hii baada ya mwezi mmoja kisha utafanya hivi kila baada ya miezi mitatu mitatu.

MAPATO YA MRADI WAKO

Katika uzazi wa kwanza utapata vifaranga 150 kwa wastani wa vifaranga 15 kwa kila kuku. Tuseme haujazingatia kanuni za ufugaji za makala hii ukapata vifaranga 100 yani wastani wa vifaranga 10 kwa kila kuku. Kisha baadaye wakakua wakafa kuku 50 yani watano kwa kila kuku utakuwa na jumla ya kuku 50.

Baada ya wiki 3 utapata tena kuku tufanye kwa mahesabu kama hayo hapo juu kwa hasara utakuwa na kuku wengine 50, na kufanya jumla ya kuku 100. Ikiwa kuku wako baada ya uzao wa pili uliwapumzisha kwa miezi miwili basi mwezi wa 3 utapata tena kuku vifaranga 100 na wiki 3 baadaye utapata wengine 100. Kwa mahesabu kama hayo awali wakikuwa utakuwa na kuku wengine 100 ambao watakuwa.

Baada ya miezi 6 utakuwa na kuku wakubwa wa uzao wa kwanza 50, uzao wa pili kuku 50 na utakuwa na kuku wenye umri wa miezi mitatu 50 wa uzao wa 3 na kuku wengine 50 wa uzao wa 4.

Katika kuku 100 wa uzao wa kwanza na pili, tufanye kuku 50 wawe matetea ukijumlisha na kuku 10 ulioanza nao mradi utakuwa na matetea 60. Ikiwa kila tetea atatotoa vifaranga 10 na vikakua vitano tu, mwishoni utakuwa na kuku 300 na baada ya miezi mitatu kuku wengine 900 toka katika kutoka kwa uzao wa kwanza, wapili na watatu. Hivyo mwaka wa pili utafunga na kuku si chini ya 1,200/= wanaotaga mayai.

Ukiuza majogoo yote 1,200/= kwa bei ya 8,000/= ili upate pesa ya kujenga miundombinu bora maana sasa utakuwa na kuku wengi wanaoendelea kuzaliana kwa kasi utapata pesa kiasi cha TZS 7,200,000/=. Sasa ongeza kuku wako wa kutaga hadi wafikie kuku 4,000 maana sasa utakuwa na pesa za kutosha kuendesha mradi wako.

Sasa ukiwa na kuku 4000 wa kienyeji wa kutaga mayai, ikiwa kuku 3000 tu watataga ukauza yai moja kwa bei ya haraka haraka ya TZS 250 tu, utapata TZS 750,000/= kwa siku ambayo sawa na TZS 22,500,000/= kwa mwezi na TZS 270,000,000/= kwa mwaka sawa sawa na 128,572 USD. Kumbuka mwamba makadilio haya niya chini sana. Ukifata kanuni zote kwa makini na maombi huku ukimtanguliza Mungu utafikia hata TZS 500,000,000/= kwa mwaka.

Kumbuka unapofanikiwa kupata mapato ya kila aina, umtolee Mungu zaka(x10%) ya mapato yako, pia ukatoe sadaka ambayo ni kubwa kuliko zaka na uwasaidie masikini na wahitaji.

Tunza kumbukumbu zako zote za fedha katika daftari maalumu kuhusu mapato na matumizi ya mradi wako. Pia hali ya kuku wako kuhusu tarehe za chanjo ya mwisho, siku walipoanza kuetamia, magonjwa yanayowasumbua mara kwa mara n.k

 

Chanzo:

 P6

Leave a Reply