Mojawapo ya maswali yanaulizwa na wafugaji wengi wa samaki ni pamoja na swala la maji yaliyomo ndani ya bwawa. Maswali yanayoulizwa ni kama yafuatayo
- Maji yanayofaa kwa ufugaji wa samaki yawe na sifa zipi?
Maji yanayofaa kwa ufugaji wa samaki ni maji nyasiyo na Klorini na ammonia ambayo ni sumu kwa ufugaji wa samaki. Maji ya bomba mara nyingi huwekwe Klorini na ammonia ili kuua vijidudu vya magonjwa kwa binadamu au mifugo. Hivyo hayana usalama sana kwa matumizi ya samaki hasa yakitumiwa moja kwa moja.
Je, yanaweza kutumika kwa ufugaji wa samaki?
Jibu ni ndiyo. Nini cha kufanya? Maji haya yanaweza kuondolewa Klorini na yakatumika kwa ufugaji wa samaki. Klorini na ammonia zinaweza kuondolewa kwa njia mbili: moja kwa kutumia dawa za kuondoa Klorini na ammonia zilizotengenezwa viwandani, mbili kwa kuyaweka maji kwenye chombo kikubwa cha waza kwa muda huku ukiyakoroga au kuyajaza kwenye bwawa kuyaacha siku kadhaa huku ukiyakoroga. Kama unabadilisha kiasi tu, basi yaweke kwenye chombo kwa siku mbili au tatu kabla hujaweka ndani ya bwawa.
- Nikisha weka maji kwenye bwawa la samaki nahitaji kubadilisha?
Jibu rahisi ni ndiyo. Wafugaji wengi wamekuwa wakifuga samaki kwa muda mrefu sana bila kubadilisha hii kwa kutojua umuhimu wa kubadilisha maji kwenye bwawa la samaki. Kwanini nibadilishe maji kwenye bwawa la samaki? Tambua kwamba maisha ya samaki ni kwenye maji na kwakuwa samaki watumia virubisho asili vilivyomo ndani ya maji mfano madini na hewa hivyo ni muhimu kubadili maji yaliyomo ndani ya bwawa. Lakini pia maji yanachafuliwa na vitu kama fosifeti, hewa ya kabondaoksaidi, ammonia, naitraiti na protini zinazokusanyika kidogo kidogo ndani ya maji na kuathiri ukuaji wa samaki. Maji hupotea taratibu kadiri siku zinavyoenda kama mvuke.
- Najuaje kama nahitaji kubadilisha maji na ni baada ya muda gani?
Unaweza kubadilisha maji mara baada ya kupima kwa kutumia vipimo maalumu vinavyoweza kubaini kiasi cha oksijeni iliyomo, uchafu wa maji, PH, ammonia n.k. Hivi vikiwa kaitka viwango visivyokubalika basi unabadilisha maji ya bwawa lako. Kwa kawaida unaweza kubadilisha maji kwa utaratibu huu (siyo msahafu):
-Unaweza kubadili maji asilimia kumi (10%) tu endapo unabadili kila wiki, yaani unapunguza na kuongeza maji asilimia 10 tu ya maji yanayotakiwa kuwemo ndani ya bwawa.
-Kama unataka kubadili maji kila baada ya wiki mbili basi punguza na kuongeza asilimia 20 tu ya maji yanayotakiwa kuwemo ndani ya bwawa.
-Kama unachagua kubadilisha kila baada ya wiki tatu, basi punguza na kuongeza asilimia 30 ya maji yanayotakiwa kuwemo ndani ya bwawa la samaki.
Kumbuka: Ni vizuri kubadili maji kidogo kidogo kwenye bwawa lako ili kuto athiri afya ya samaki wako kwa kusababisha mshtuko. Aidha haijalishi utaratibu upi utachagua hapo juu wa kubadilisha maji, ni LAZIMA ubadilishe maji kwa kupunguza na kuongeza asilimia 60-70 ya maji yanayotakiwa kuwa ndani ya bwawa lako mara tatu kwa mwaka. Kwa maeneo ya baridi madiliko haya makubwa ya maji yafanyike kipindi cha joto ili kuepuka kuongeza maji ya baridi kwenye bwawa lako. Aidha kubadilisha maji mengi mara kwa mar ahata kama una maji ya kutosha haishauriwi kwani pia huathiri samaki kwa mshtuko.
Utoaji wa maji yote huku samaki wakiwa ndani ya bwawa haushauriwi kwa namna yeyote ile, huu ufanyike tu pale ambapo unataka kuwavuna samaki wote bwawani.