Watu wengi wamekuwa wakiogopa kufuga vifaranga vya umri wa siku moja kwa kuogopa kwamba vifaranga vinakufa sana.

Kuna sababu nyingi zinazofanya vifaranga wafe. Kubwa kati ya hizo ni:

 

  1. WANAPOTOTOLESHWA.
  2. UANGALIZI / USIMAMIZI.
  3. LISHE.
  4. MAGONJWA.

 

  1. WANAPOTOTOLESHWA.

Watotoleshaji wanatakiwa kuuza vifaranga vyenye ubora. Kifaranga bora ni yule aliyechangamka, mwenye maji ya kutosha mwilini, asiye na magonjwa na asiye na ulemavu.

Utafiti uliofanywa kwenye shamba la kuku wa nyama, kwa vifaranga vilivyoanguliwa katika kipindi cha saa 48 ulionyesha kwamba: Vifo vya vifaranga katika siku 10 za mwanzo ilikuwa, 3.2% ya wale walioanguliwa mwanzoni, 1.2% ya wale walioanguliwa wakati wa kilele cha kuangua (siku ya 21), na 52.9% ya wale walioanguliwa mwishoni.

Vifaranga vya mwanzo walikuwa na matatizo ya kupungukiwa maji mwilini, ambapo wale wa mwisho walikuwa na udhaifu wa miguu.

Ni muhimu Watotoleshaji kuchagua vifaranga bora na visivyo na matatizo kwa ajili ya wafugaji (wateja wao).

 

  1. UANGALIZI / USIMAMIZI.

* Joto kali sehemu ya kulelea vifaranga. Joto kali husababisha vifaranga kukosa maji mwilini. 70% ya miili ya vifaranga ni maji. Joto likiwa kubwa muda wote, miili yao hupoteza maji, na ikifikia 10% ya maji yamepungua mwilini, vifaranga hufa.

* Ubaridi sehemu ya kutunzia vifaranga. Hali ya ubaridi huwafanya vifaranga wapate vichomi (pneumonia), ambapo maini yao hugeuka kuwa ya blue. Pia vifaranga hujikusanya sehemu moja ili kupata joto, matokeo yake vifaranga hufa kwa kukosa hewa.

* Vifo kutokana na sumu.

– Chakula kisichokuwa safi na ambacho hakikuchanganywa vizuri kinakuwa ni sumu kwa vifaranga.

– Chumvi inaweza kuua vifaranga kama ikizidishwa kwenye chakula.

– Hewa chafu kwenye sehemu ya vifaranga husababisha vifo. Hewa za carbon monoxide na carbon dioxide ikiwa zaidi ya 30% inasababisha vifo.

– Uchafu na mbolea pia husababisha vifo vya vifaranga.

* Majeraha. Kama vifaranga hawashikwi vizuri wakati wa kuwapa huduma mbalimbali kama chanjo au kuwapunguza midomo, wanaweza kupata majeraha ambayo yanaweza kusababisha vifo.

* Njaa. Vifaranga vichanga havina mafuta ya kutosha mwilini kama hifadhi ya chakula wakati wa njaa, kwa hivyo vinakufa.

* Kutokuwa na nafasi ya kutosha. Nafasi finyu ni kiini kingine cha vifo vya vifaranga. Vifaranga wanasongamana na kusababisha unyevu kwenye kinyesi na uchafu mwingineo na hivyo kuleta madhara kwa vifaranga vyenyewe. Sehemu finyu ya kulishia na kunywea maji, inafanya vifaranga kushinda na njaa na hatimaye kufa.

* Hali ya unyevunyevu. Hali hii kwenye mabanda haifai kwa vile inaweza kupelekea kuzuka kwa bacteria ambao wanaweza kuleta madhara kwa vifaranga.

* Wanyama.  Kama mabanda hayakujengwa imara kuzuia wanyama kama panya, paka au mbwa wanaweza kuwa ni maangamizi kwa vifaranga.

 

  1. LISHE.

* Maji ni muhimu sana kwa afya na utendaji wa vifaranga. Yanatumika kama chombo cha kusafirisha virutubisho mwilini mwa vifaranga na kuweka sawa joto la mwili wakati wa joto kali.

* Vifaranga wakikosa vitamin muhimu (A, D, E Na K) wanakufa. Pia wakipata vitamin kidogo huwafanya kupunguza ukuaji wao.

* Kukosekana kabisa kwa vitamin B-Complex na C kunasababisha vifo. Na kupungua kwa vitamin kunasababisha kupungua uzito, manyoya kutoota sawasawa, ukuaji duni na upungufu wa damu.

 

  1. MAGONJWA.

Kama vifaranga wadogo hawafugwi kwa uangalifu na umakini mkubwa, kuna hatari ya kupata magonjwa kwa kuwa vifaranga hawana kinga. Yapo magonjwa mbalimbali kama kuhara nyeupe na kuhara damu, ambapo yanaweza kuwapata vifaranga na kusababisha vifo.

 

Imeandaliwa na

Aquinus Poultry Farm.

0655347932

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!