PATA ELIMU HII KUPITIA APP MPYA ILIYOPORESHWA HAPA
Bakteria ni nini?
Bila shaka swali hili kila mfugaji anaweza kulijibu kwa ukamilifu maana mifugo yake kwa wakati mmoja au mwingine imeugua na kuambiwa ugonjwa una sababishwa na bakteria. Hata uhakika ni kuwa hawajawahi kuona backteria kwa macho yao kwa vile ni vimelea wadogo sana wasioonekana kwa macho. Ni wadudu wenye seli hai moja na wanapatikana kila mahali, kwa Wanyama na mazingira. Bakteria hawa si wote wanamadhara kwa binadamu na Wanyama, wengine wanafaida. Mada hii itajikita kwa bakteria wenye madhara kwa mifugo yetu.
Madawa ya mifugo ni nini?
Swali hili kila mfugaji pia anauwezo wa kulijibu kwa ufasaha kabisa maana anatumia au ametumia madawa ya mifugo kutibu mifugo yake ilipopatwa na magonjwa. Kwa ufupi “madawa ya mifugo” ni kemikali zenye uwezo wa kuua au kuzuia ukuuaji wa vimelea kama bakteria, virusi, fangasi, na minyoo au protozoa. Dawa hizi zinaweza kutumika kwa malengo mbalimbali ikiwemo kutibu wanyama au binadamu wenye maambukizi au ugonjwa, kusafishia mazingira na kuta za mabanda ya mifugo, kutakasia vifaa kwenye maabara, kliniki na hospitali. Hivyo haya madawa yanasaidia kuwafanya wanyama na binadamu waishi wakiwa na afya. Yanatumika kutibu na kuzuia magonjwa yasitokee.
Usugu wa dawa/madawa ni nini?
Hili ndo swali la msingi linalobeba mada ya leo. Nina hakika wafugaji wengi hatujui maana ya usugu wa dawa na namna unavyotokea. Fuatana nami itakusaidia sana na hasa katika kupambana na tatizo hili. Usugu wa dawa ni upungufu wa uwezo wa dawa kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuua au kuzuia vimelea vya magonjwa visikue au kuongezeka. Usugu wa dawa hutokea pale ambapo vimelea vya magonjwa huendelea kuishi hata baada ya kutumia dawa. Vimelea hivi vinavyoendelea kuishi hata baada ya kutumia dawa vinakuwa vimetengeneza usugu kwenye dawa na vinajulikana kama vimelea sugu mfano Bakteria sugu.
Zipo njia nyingi ambazo bakteria sugu wanaweza kujilinda wenyewe kutoka kwenye madawa yaliyotumika kutibu wanyama. Kwa mfano bakteria naweza kuharibu dawa ili isimuue au bakteria sugu wanaweza kuzuia dawa isiwaingie na kuwadhuru. Mara bakteria wawapo sugu kwenye dawa fulani, kuendelea kutumia dawa hiyo kunafanya idadi ya bakteria sugu kuongezeka na kupelekea mifugo yako kuendelea kuugua hata kama unatumia dawa.
Kwa hiyo, matumizi yote ya Madawa ikiwemo kwa binadamu na wanyama yanaweza kuongeza kuibuka kwa usugu wa madawa. Na bakteria sugu wanaweza kusambaa toka sehemu moja au nyingine ikwemo toka kwenye mazingira kwenda kwa watu, toka kwa watu kwenda kwenye mazingira, toka kwa watu kwenda kwa wanyama na kutoka kwa wanyama kwenda kwa watu.
Kwa nini dunia nzima ihofie usugu wa dawa?
Vimelea hawa wamekuwa wakibadilisha maeneo ambayo dawa za kuua au kuzuia kuzaliana kwao na vimelea hawa sugu wanajitokeza na kusambaa dunia nzima. Hii inatishia uwezo wa wetu wa kutibu magonjwa ambukizi yaliyokuwa yanatibika na dawa hizi na kupelekea kwenye magonjwa sugu na vifo. Hofu kubwa pia ni kuwa Madawa tunayotumia sasa kwa binadamu na wanyama yote yanaweza kushindwa kufanya kazi siku za mbeleni.
Kutakuwa kumeibuka vimelea vipya visivyotibika kabisa na kuongeza vifo miongoni mwa binadamu na wayama. Si hayo tu lakini matibabum engine kama ya kubadilishiwa viungo, matibabu ya kanza na kisukari au upasuaji mkubwa utakuwa katika hatari kubwa dhidi ya bakteria sugu wasiouawa na dawa yeyote. Gharama ya matibabu itaongezeka kwa kuuguza kwa muda mrefu mifugo yako au binadamu.
Nini kinapelekea kujitokeza na kusambaa kwa usugu wa madwa?
Ndugu mfugaji hapa unatakiwa kufuatana nami kwa umakini ili ujue mchango wako kwenye usugu wa Madawa. Kwa kawaida usugu wa dawa hutokea kwa njia ya asili kadiri muda unavyokwenda. Lakini madiliko haya huwa ya taratibu na huchukua muda mrefu kusababisha usugu wa Madawa.
Kwa sasa kikubwa kinachochangia ni matumizi mabovu ya Madawa kwa binadamu na mifugo. Ninaposema matumizi mabovu namanisha matumizi ya dawa bila kufuata maelekezo yad awa kutoka kwa wataalamu waliokidhi vigezo vya kuoa maelekezo ya matumizi. Hii inapelekea matumizi yad awa chini ya kiwango au juu ya kiwango. Maelekezo ya matumi yad awa yoyote ile yamefanyiwa utafiti wa kina kuwa kwa kufuata dozi hiyo kimelea kitauawa au kuziliwa kuzaliana kwake.
Matumizi mabaya ya Madawa kwa mifugo na binadamu Tanzania imekuwa kitu cha kawaida sana. Kwa kujua ama kutokujua kila mtu anapenda kuwa daktari kwa kutibu mifugo yake, ya jirani yake au kujitibu mwenyewe na jirani zake. Kwa sababu hiyo usugu wa madawa unaendelea kujitokeza na kusambaa kwa kasi. Wafugaji wamekuwa wakilalamika kuwa dawa fulani nimeitumia lakini haifanyi kazi. Hawajui sababu kuwa ni wao wenyewe wanaosababisha haya yote.
Mambo yanayoweza kuchangia kwa haya yote ni pamoja na uduni wa elimu ya usugu wad awa kwa wafugaji wetu, Udhaifu katika usimamiaji wa sharia na kanuni za matumizi ya madawa kwa wanyama na binadamu, mifumo dhaifu ya ufuatiliaji wa matumizi ya Madawa kwa mifugo na binadamu na ukosefu wa miongozo mipya juu matumizi ya dawa za mifugo na binadamu.
Mambo mengine ni pamoja na ukosefu wa mwendelezo wa elimu ya matumizi ya dawa kwa watoa maelekezo, tabia ya wafugaji kuhifadhi dawa na kutumia watu wasio na utaalamu (vishoka) kutibu wanyama wao, kiwango kikubwa cha matumizi mabovu ya dawa na wafugaji na utupaji taka usiosahihi kwenye maeneo ya kutupa taka.
Matumizi ya dawa kwa wafugaji hapa nchini kwenye mifugo ni asilimia 100%. Matumizi makubwa yapo kwa kuku. Hiki ni kiashiria kuwa wafugaji wengi wanatazama kutibu Zaidi punge mfugo wake akiugua badala ya kuchukua tahadhari. Usemi wa “kinga ni bora kuliko tiba” umepuuzwa kwa kutokujua au kwa kujua. Bado lisingekuwa tatizo kama wataalamu wangekuwa wanatumika.
Tafiti mbalimbali zimeshafanyika kuonyesha namna ambavyo wafugaji wamekuwa wakitibu mifugo yao wenyewe. Ulitafiti nilioufanya mwaka 2013 (Chengula et al. 2013) maeneo ya Arusha, Manyara na Morogoro ulibaini wafugaji wakitibu mifugo yao wenyewe. Sababu kubwa waliyoitoa ni gharama kubwa ya kuwaita wataalamu wa mifugo ikijumuisha mafuta ya usafiri, na madawa. Hivyo kwao ilikuwa rahisi kununua dawa na kutibu wenyewe bila hata ya kuwa na utaalamu. Matibabu waliyafanya kwa kurithi toka kwa wakubwa zao au kwa majirani.
Utaona ni namna gani madawa ya mifugo yamekuwa yakitumika hovyo. Bila hata kuangalia tafiti za kisanyansi, kama ni mtu wa mitandao mfano facebook na whatsapp, utakubaliana nami kuwa kuna matumizi ya mabayay a dawa. Jaribu kujiunga na makundi ya mitandaoni utaona namna ambavyo kila mfugaji ni daktari. Kuna mambo mengi yanaweza kuwa yamepelekea hili lakini kikubwa ni elimu na ukwepaji wa gharama ambapo bila kujua kuwa inawapelekea kwenye hasara kubwa.
Mfugaji ataambiwa dawa na mfugaji mwenzake ataenda kunnua na kutibu mifugo yake. Hivyo anaweza kutumia chini ya kiwango au akatumia dawa isiyo yenyewe kwa ugonjwa ulipo kwa kifugo yake. Hapa matumizi mabovu yanaonekana dhahiri. Vishoka huko mitaani ndo usiseme, hawana utaalamu lakini ndo madaktari wa kuaminiwa na sababu kubwa ni kuwa wanatibu kwa bei rahisi na wala hakuna anayewabaini ili wachukuliwe sharia. Nao wanachangia kwenye usugu wad awa.
Eneo jingine ambalo lingependa kulisema ni la uuzaji wa dawa holela. Upatikanaji wad awa kiholela unamchango mkubwa sana kwa wafugaji na vishoka kutibu wenyewe. Kila mtu anauwezo wa kununua dawa na nyingine zimekuwa zikipata kwenye minada tena zikiwa juani. Maduka ya madawa yanamchango mkubwa sana kwenye usugu wa madawa. Hawa wamekuwa wakitoa maelekezo ya namna ya kutibu mifugo kwa wafugaji. Wafugaji wanakuwa madaktari kwa njia hii, nafasi ya daktari ya kutibu mifugo inakuwa haipo. Wengi wa wamiliki wa maduka wanatumia Madaktari kama wasimamizi wa maduka yao (ipo kisheria) lakini je wanatenda kazi yao sawa sawa? Mfano daktari yupo Morogoro anasimamia duka Kibaha au Moshi, hapo anasimamia nini? Duka halina mtaalamu lakini wafugaji wanapewa maelekezo ya kutibu mifugo yao. Tatizo hili kwa uelewa wangu ni kubwa sana kwa wafugaji wa kuku. Akienda dukani akiwa na maelekezo ya wafugaji wenzake ananunua dawa anaenda kutibu kuku wake. USUGU UTAENDELEA KUKUA HADI TUBADILI NAMNA TUNAVYOFANYA MAMBO YETU.
Ewe mfugaji, muuza daw ana wataalamu wote tubadili namna tunavyotumia dawa za mifugo. Daktari wa kweli hatibu kwa njia ya mitandao, yaani unakuwa sehemu ya kutoa maelekezo ya namna ya kutibu mifugo kwa nja ya mtandao.
IMEANDALIWA NA DR. AUGUSTINO A. CHENGULA
source https://ufugajiapp.blogspot.com/2020/07/matumizi-ya-madawa-ya-mifugo.html