Chakula bora na nafuu cha samaki ni suluhisho la uhakika kwa maendeleo ya ufugaji samaki tanzania

Ufugaji wa kambale kwenye mabwawaChakula samakiUfugaji wa kambale kwenye mabwawa

Na Mtafiti

Chakula cha samaki ni tatizo kubwa katika maendeleo ya ufugaji wa samaki hapa nchini. Wengi wa wafugaji wadogo wa samaki hutegemea kurutubisha bwawa kwa kutumia chakula kisichokuwa na ubora kulisha samaki. Matumizi ya chakula duni husababisha kudumaa na kupungua kwa thamani ya samaki ambapo hukatisha tamaa watu wengi kuweza kujitosa katika kazi hii ya ufugaji wa samaki. Juhudi za kuendeleza chakula cha asili cha samaki ni muhimu sana kwani chakula bora na nafuu husaidia kupunguza gharama za uzalishaji, na hivyo kuvutia wawekezaji binafsi na wa kibiashara katika ufugaji na hatimaye kuongeza uzalishaji wa samaki. Iwapo chakula cha samaki chenye kiwango kinachokubalika kitapatikana kwa urahisi katika jamii, wanakaya wanaweza kukipata kwa gharama ndogo, na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kuongeza kipato cha mfugaji. Hii itatatua si tu tatizo la upatikanaji wa chakula lakini pia ufugaji wa samaki utakuwa chanzo cha kuaminika kwa shughuli za kuongeza kipato kwa wafugaji na pia kwa wazalishaji wa chakula cha samaki. Kwa kuongezea, mfumo wa ufugaji utaimarisha uwezeshwaji wa wanawake na kutoa fursa ya ushiriki wao kiuchumi kwanipamoja na kazi nyingine za nyumbani, wanawake huwajibika siku hadi siku katika mabwawa yaliyopo kwenye makazi yao.
Hivi sasa kuna Mradi unaotekelezwa kwa pamoja na watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA). Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Lengo kuu la Mradi ni kutengeneza chakula cha samaki chenye ubora na nafuu kwa kutumia bidhaa zinazopatikana katika maeneo waliko wafugaji. Utafiti wa awali uliofanyika ulikuwa na lengo la kupata maarifa na maoni ya watu wa vijijini katika masuala ya kulisha samaki na usimamizi wa bwawa, kuweka kumbukumbu ya ulishaji wa chakula katika mabwawa,desturi ya kulisha samaki katika maeneo husika pamoja na kutambua mazao  yanayopatikana katika maeneo hayo. Utafiti ulifanywa katika wilaya tatu ambazo ni Songea, Mufindi, na Mvomero. Malighafi zilikusanywa na kufanyiwa tathmini ya lishe na kutengenezewa mkokotoo wa chakula cha samaki kule Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro. Katika malighafi hizo palikuwepo na majani ya mihogo, maharage, nazi, samaki, damu ya mifugo, mbegu za keki ya alizeti, karanga, mahindi, mchele, majani ya maboga, unga wa mihogo, moringa, majani ya mipapai pamoja na viazi vikuu. Malighafi hizo ambazo hupatikana kwa urahisi katika wilaya hizo zilitumika kutengenezea aina saba za vyakula vilivyotumika kwa majaribio kwa miezi sita kuangalia ukuaji wa samaki na kubainisha ufanisi na unafuu wa gharama za chakula kulingana na malighafi zilizotumika.

Jumla ya vifaranga 250 vya samaki vilifugwa katika ndoo ishirini (20) kwa ajili ya majaribio na samaki wakubwa waliwekwa kwenye visiba kumi na viwili (12) vya saruji TAFIRI Dar es Salaam kwa ajili ya kuangalia ukuaji wa muda mrefu kama sehemu ya kwanza ya majaribio. Sehemu ya pili ya majaribio itafanyika katika mashamba ya wafugaji wa samaki waliochaguliwa kutoka Wilaya za Songea na Mufindi. Wafugaji wa samaki waliochaguliwa kutoka katika wilaya hizi mbili tayari wameshapata mafunzo kwa ajili ya kulisha samaki na usimamizi wa mabwawa. Majaribio yote yatafanyika kwa usimamizi wa karibu wa Maafisa Uvuvi wa Wilaya ili kuhakikisha kwamba panakuwa na usimamizi mzuri. Baada ya kukamilika kwa mradi inatarajiwa kwamba kutakuwa na ubora wa hali ya juu wa chakula cha samaki chenye unafuu kwa ajili ya ufugaji endelevu wa Perege katika nchi yetu. Kwa hiyo utafiti huu utachangia katika kutatua tatizo la upatikanaji wa chakula bora  na nafuu cha samaki na hivyo kuchangia katika maendeleo ya ufugaji wa samaki pamoja na kuongeza usalama wa chakula na kipato kwa jamii.

 

CHANZO: Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI)

Leave a Reply