Na Augustino Chengula
Avian leukosis unaojulikana kama kansa ya kuku unasababishwa na virusi walioko kwenye kundi moja na virusi vya ukimwi kisayansi linaitwa retroviruses (family retroviridae). Hawa virusi wa kuku wanaitwa kitaalamu Avian leukosis virus. Ugonjwa huu huenea kutoka kuku wakubwa kwenda kwa vifaranga kupitia mayai (yaani viranga vinazaliwa vikiwa na wadudu). Hivyo unaweza kuwa umenunua vifaranga wakiwa na wadudu wa ugonjwa. Njia kuu ya ueneaji ni kupitia kugusana kati ya kuku na kuku (virusi hupitia kwenye ngozi) au wanaambukizwa na virusi walioko kwenye mazingira (kula kwenye chakula au kwa hewa kupitia kwenye macho na pua).
Ugonjwa huu huwapata kuku wa kuanzia wiki ya 14 na kuendelea. Virusi wa ugonjwa wanaanza kushambulia basa tangu wakiwa na wiki ya 4-8, lakini wakati huu si rahisi kutambua. Ugonjwa huu hujitokeza taratibu ukiwa na vifo kwa mbali. Dalili zikiwa ni kukosa hamu ya kula, udhaifu, kuharisha, kupungukiwa maji na kukonda/kupungua uzito. Ukiwabonyeza eneo la basa na ina huonekana kuwa zimevimba. Kabla ya kufa kuku huwa wamenyong’onyea/waliodhoofika. Si mara zote kuku wenye virusi hivi waonyeshe ugonjwa, kwa wale wanaotaga utagaji wao hushuka.
Ukimpasua kuku aliyekufa utaona ini likiwa limevimba sana (kubwa), lakini viuongo vingine kama bandama/wengu na basa navyo huwa na uvimbe. Kuvimba kwa ini kuliko pitiliza ni dalili ya kutambulisha ugonjwa huu. Kuvimba huku ndiko kunatokana na seli kubadilika kuwa za kansa (seli kugawanyika kwa wingi bila mpangilio). Kwa kuku ambao bado wana basa huwa nayo imevimba.
Kuzuia: Njia ya muafaka ya kuzuia ugonjwa huu kwa kuku ni kuzuia maambuki ya vifaranga hasa kwa wanaozalisha vifaranga. Hawa ndio wanapaswa kuhakikisha wanatoa vifaranga visivyo na ugonjwa huu.